Pages

Monday, February 6, 2012

Profesa Makame Mnyaa Mbarawa amnadi Mohamedraza Hassanal Dharamsi mgombea wa CCM Uzini Zanzibar

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kinajiendesha kwa kuheshimu maoni, maamuzi na ushauri unaotolewa na wananchama wake katika ngazi mbalimbali.
Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Profesa Makame Mnyaa Mbarawa wakati akimnadi mgombea wa CCM Jimbo la Uzini Mohamedraza Hassanal Dharamsi katika shehia ya Mchangani Mkoa Kusini Unguja.
Profesa Mbarawa amesema Kamati Kuu ya Taifa ya CCM hufanya uchambuzi, kupima mambo kwa vigezo husika hatimaye huzingatia maamuzi na ushauri wa wananchama wake.
Amesema CCM si chama kinachochakachua, kubadili au kupuuzia maoni na maamuzi ya wanachama wake kwa kufanya upendeleo.
Ameeleza kuwa CCM ni taasisi ya kisiasa yenye uzoefu mkubwa Barani Afrika, viongozi wake ni mahiri, wajuzi na wenye uwezo wa kupima mwenendo ulivyo.
Aidha Mjumbe huyo Kamati Kuu ya CCM amesisitiza kuwa CCM huongozwa na mwelekeo wa Katiba na Kanuni zake bila ya kufanya ubaguzi, upendeleo na maonevu.
Akizungumzia mchakato wa kumpata mgombea wa Uzini, Profesa Mbarawa amesema Kamati Kuu ya CCM imefanya tafakuri pana, uchambuzi wa kutosha na kukusanya vielelezo vilivyomthibitisha kuwa Raza anatosha kuwa mgombea.
Amewataka wananchi wa Uzini kujipanga na kuhakikisha Mgombea huyo wa CCM anashinda katika uchaguzi wa Februari 12 mwaka huu, ili ashirikiane na wananchi wenzake kuleta maendeleo.

No comments:

Post a Comment