TAN

TAN

Bayport

Bayport

Kikoa

Kikoa

Myway entertainment

Myway entertainment

FORE PLAN CLINIC

FORE PLAN CLINIC

MPINGA CUP 2016

MPINGA CUP 2016

Mashujaa Fm 89.3, Lindi

Monday, March 13, 2017

Karibu katika Adithi hii ya Kusisimua- Usikose


NJAMA

DIBAJI

Dunia yote ilitingishika zilipopatikana habari kuwa silaha kali na za kisasa zilizokuwa zimetolewa na Urusi kwa wapigania Uhuru wa Afrka Kusini, zimeibiwa bandarini Dar es Salaam.

Habari hizi zilileta utata mwingi, baadhi ya nchi zikisema ni njama za makaburu na nyingine zikisema ni njama za Tanzania.

Katika kiza kinene kilichozunguka suala hili serikali ya Tanzania ilimtuma Willy Gamba, Mpelelezi mashuhuri Ulimwenguni, kutafuta ukweli ulipo. Hapo ndipo patashika zikaanza na Jiji la Dar es Salaam likakumbwa na wimbi la msukosuko wa uhaini, usaliti na mauaji ya kutisha.


SURA YA KWANZA

LIKIZONI

Nilipoamka ilikuwa yapata saa tatu za asubuhi. Kuchelewa kwangu kuamka si kwa sababu mimi ni mtu mvivu wa kuamka, kama ambavyo ungefikiri, ila ilikuwa kwa sababu ya kuchelewa kulala. Nilikuwa nimewasili kwenye uwanja wa ndege wa mjini Freetown; sierra Leone, mnamo saa sita za usiku.

Kutokana na pilikapilika za tangu kutoka uwanjani mpaka kumaliza taratibu, nilijikuta ninaingia kitandani mnamo saa tisa la alfajiri, ukifikiria uchovu wa safari ndefu toka Dar es Salaam, Tanzania, hadi hapa utaona kuwa nina haki ya kuchelewa kuamka kama kweli wewe ni mtu mwenye kufikiria shida za binadamu wenzako.

Nilikuwa nimefika mjini hapa kwa likizo ya wiki mbili ambayo nilikuwa nimepewa na wakubwa wangu wa kazi baada ya kutekeleza kikamilifu kazi moja nzuri na kuwafanya wafurahi sana na kupendekeza nipate likizo.

Hapa mjini freetown nilikuwa nimefikia kwenye hoteli moja maarufu sana iitwayo LIIm Bin Tumaini, hoteli ambayo ilikuwa imependekezwa kwangu na abiria mwenzangu msichana ambaye yeye ni mwenyeji wa mjini Freetown.

Huenda litakuwa jambo la busara nikikusimulia jinsi tulivyoonana na msichana huyu, ambaye kama nitakavyokueleza, utaona kwamba alinifaa sana. Msichana huyu tulikuwa tumeonana kwa nasibu sana. Mimi ilikuwa inanibidi nibadili ndege mjini Roma, Italia. wakati nakuja toka Dar es Salaam kwa ndege ya shirika la ndege la Uingereza (BOAC) ambayo ilikuwa inaelekea moja kwa moja London.

Hivyo nilipofika Roma ilibidi nibadilishe ndege na kwa vile mipango ilikuwa imetayarishwa tayari na wakala ulioshughulikia safari yangu. nilikuta tayari ipo ndege ya shirika la ndegee liitwalo British caledonian, ikiwa inatokea London ikielekea Freetown. Kwa hiyo baada ya kutelemka toka katika ndege iliyotutoa Dar es Salaam, tulipanda ndege hii iliyokuwa ikielekea Freetown tayari kuendelea na safari yetu.

Mimi ndiye nilikuwa abiria wa mwisho kuingia ndani ya ndege maana mambo ya kujitangulizatanguliza mbele, rafiki yangu, mara nyingi yanaweza kukuletea kidamisi. Nilipoingia nilianza kuangaza mahali pa kukaa maana vile vile lazima unaposafiri usikae na watu hovyo hovyo tu kwani wengine wana mikosi. Kama wewe hujui namna ya kuwatambua watu wenye mikosi basi nitafute siku moja nitakunong'oneza.

Mara mbele kidogo nikaona kiti akiwa amekaa mtoto wa kike, nilimwangalia roho yangu ikaridhika.

"Samahani binti, sijui naweza kukaa?".

Aligeuka akaniangalia. Lo msichana huyu alikuwa na macho ya kuvutia sana. Kule kuniangalia tu nilihisi mwili wangu wote ukisisimka. Utafikiri macho yake yalikuwa yanaweza kuona ndani ya moyo wako. Kusema kweli nimeona wasichana wengi wenye macho ya kusisimua maisha mwangu, lakini huyu alitia fora. Macho haya yalikuwa hedaya aliyopewa na Mwenyezi Mungu.

"Bila ya wasiwasi", alijibu kwa sauti ya uchovu. Akagauka akaendelea kuangalia mbele.

Niliketi na muda si mrefu tukaombwa tufunge mikanda tayari kwa ndege kuondoka.

Baada ya kupaa juu na kuruhusiwa kufungua mikanda, nikapata kishawishi cha kuzungumza na huyu binti mwenye macho ya kusisimua.

"Samahani binti", nilimtaka radhi kabla ya kumpa ya kutoka rohoni mwangu.

"Unasemaje?".

"Unajuwa binadamu wanafahamiana kwa kukutana, wengine wanafahamiana kwa kukutana mashuleni, kazini, kwenye starehe na wengine safarini kama hivi na kadhalika. Kwa hiyo binti, mimi ningeonelea vizuri kama tungefahamiana".

Nilimuona akitabasamu.

Mimi naitwa Willy Gamba, sijui wewe mwenzangu unaitwa nani?".

"Mimi naitwa Veronica Amadu".

"Unatoka wapi na unakwenda wapi?".

Aligeuka na kunitazama huku macho yake makali yakionesha mshangao.

Usinielewe vibaya . Kama nilivyokuelza hapo awali, nia yangu ni kufahamiana tu. Nilimuonesha tabasamu la kumlainisha.

Hili tabasamu huwa nimeliweka kwa wakati kama huu tu na huwa silitoi ovyo ovyo. Na kama nilivyotegemea lilimlainisha.

"Mimi natoka mjini London na ninaelekea Freetown ambako ndiko makazi yangu, Je wewe?".

Mimi natokea Dar es Salaam, Tanzania na ninaelekea Freetown vile vile. Niko likizo.

"Yaani kwenu ni Tanzania?".

"Ndio" Akashangaa

"Na ni likizo tu inakuleta Freetown?".

"Ndio".

"Karibu kwetu maana mimi ni mzaliwa wa Sierra Leone 

"Sawa".

"Hivi ninayo furaha kupata mwenyeji, ama siyo?".

"Usiwe na wasiwasi mwenyeji umepata". Alitabasamu tena.

Nakuambia mimi nilizaliwa na bahati ya kuelwana na hawa watoto wa kike maana ni mara chache sana kunichenga. Sijui wewe mwenzangu vipi?".

"London ulienda kimatembezi au kikazi?". Kutokana na mazungumzo nilishakidhi kuwa huyu msichana ni msomi.

"Nilienda kikazi. Kusema kweli mimi ninafanya kazi ya uandishi. Mimi ni mwandishi wa habari za siasa na uchumi za Afrika Magharibi katika gazeti la Afrika".

"Oh, nimekumbuka sasa hata jina lake. Ama kweli nina bahati ya kukutana nawe, maana mimi ni mfanyabiashara huko Afrika Mashariki na nimekuwa natafuta njia ya kuwekeza kupata mipango ya kuwa na uhusiano wa kibiashara na nchi za huku, hivyo nafikiri kama utakuwa na muda utaweza kunielekeza katika mambo haya kwa vizuri".

"Na mimi nitafurahi kufanya hivyo".

"Hata hivyo nami nitapata wasaa wa kujua mambo mbali mengi kutoka Afrika Mashariki kwani sijawahi kufika, utafikia hoteli gani sijui?".

"Sijui mpaka sasa, maana kama nilivyokwambia mimi ni mgeni kabisa sehemu hizi, sijui wewe  utanishauri nifikie hoteli gani?, nataka hoteli yenye wasifa mzuri, tulivu na isiyo na matatizo madogo madogo.

"Nafikiri Bintumaini Hoteli itakufaa sana, ndio hoteli maarufu hapa mjini Freetown".

"Asante, nitafuata ushauri wako".

Tulipokuwa tunatua kwenye uwanja wa ndege wa Freetown msichana huyu aliniahidi kuwa angefika kesho yake saa nne hoteli kwangu na akaahidi kuwa angenipeleka kuogelea kwenye ufuko mmoja maarufu sana uitwao Lumley Beach.

Hivi ndivyo nilivyofahamiana na msichana huyu ambaye asubuhi hii nilijua atakuja kunichukua kunipeleka kuogelea. Hivyo nilipoamka niliagiza chemsha kinywa, hakafu nikaingia maliwatoni nipate kuoga.

Baada ya kuog nilisnza kustaftahi, maana tayari chemsha kinywa ilikuwa imefika. Nilipomaliza kustaftah ilikuwa inakaribia saa nne, hivyo nilijiandaa na kujiweka katika mavazi kuogelea, maana niliamini Veronica alikuwa mtu wa kutimiza ahadi zake.

Wakati najitayarisha, kengele ya simu ililia. Nikaiendea kuijibu.

"Hallo, chumba namba 305 hapa".

"Samahani kwa kukuhatiki, kuna mgeni wako hapa mapokezi", mfanyakazi wa mapokezi alinieleza.

"Hebu nizungumze naye".

"Subiri".

Hallo".

Hallo, Vero. njoo huku chumbani".

"Nakuja".

Tukakata simu. Punde si punde Veronica aligonga mlangoni, nikamfungulia. Harufu nzuri ya uturi wa ghali sana ilijaza chumba, macho yetu yalionana na woga tukapigwa na butwaa, hali iliyotokea sina maneno ya kuielezea. Msisimko uliokuwa ukitolewa na macho yake uliniingia tena, na ni baada ya kujikaza kisabuni ndipo nilipoweza kuongea.

"Vero, habari za toka jana?".

"Ni nzuri. Je, vipi wewe umelala salama?".

"Salama kabisa, karibu uketi".

"Wapi?".

"Hapa kitandani".

Vero akitabasamu akaketi. alikuwa amevalia suruali ya aina ya dengirizi na fulana nyeupe yenye matundu makubwa iliyoonyesha umbo la matiti yake yaliyokuwa yameshikiliwa na kanchiri moja safi sana. Mvao huo ulinipa umbo ambalo liliweza kunisihiri kabisa.

"Uko tayari twende kuogelea?", aliniuliza.

"Niko tayari".

"Kabla hatujaondoka twende hapo nje kwenye rosheni ya chumba hiki nikuonyesha jinsi ukiwa kwenye hoteli hii uwezavyo kuona mandhari ya kupendeza sana". akaongoza roshenini.

"Hoteli hii imejengwa kwenye kilima kama unavyoona", alianza kueleza huku tukiwa tumesimama tukiangalia mandari nzuri mbele yetu.

"Kilima hiki kinaitwa Bintumaini, na hoteli inarithi jina la kilima hiki", alionesha kidole na kuendelea. "Ile bahari ya Antlantic na ule ufuko unaouona ndio ufuko maarufu uitwao Lumley Beach, na ile ghuba inayoonekana vizuri kabisa kutoka hapa inaitwa Ghuba ya mtu wa vita (Man-of-war)".

Nilianza kumpenda huyu msichana kwa mambo yake, kwani alikuwa anachukua jukumu la kunionyesha vizuri mandhari ya mji huu, kitu ambacho sikukitegemea kabisa.

"Lo. hii ghuba inaonesha picha nzuri sana".

"Zamani kabla hoteli hii haijajengwa hapa, watalii wengi walikuwa wanakuja kwenye kilima hiki ili kuchukua picha ya sehemu yote ya pwani na ukanda huu.

"Zile nyumba pale ufukoni ni hoteli?". kulikuwa na majengo mazuri ufukoni na vile vile kati ya hoteli hii na ufukoni kwenye barabara iliyotelemka kutoka hotelini.

"Ile ni Lumley Beach Hoteli, na haya majengo hapa katikati ni Freetown Casino ambayo kila siku iko tayari kumeza na kutoa mamilioni ya pesa". Veronica alimwemwesa.

"Je una swali zaidi?".

"La hasha, mpaka hapa nimekidhi. na ni lazima nikubali kabisa kuwa nimepata mwenyeji wa kunifaa. Tokea sasa nimepata imani kuwa likizo yangu itafana sana.

"Haya sasa twende zetu tukaogelee", Veronica aliniambia huku akinivuta mkono.

Nilifunga mlango wa chumba tukatelemka mpaka mapokezi. Tulipofika mapokezi nikaomba karatasi ili kuwajulisha Dar es Salaam kuwa nimefika salama na mahali gani nilipokuwa nimefikia.

"Tuna habari hizi kwa njia ya Teleksi", nilimwambia kijana wa mapokezi. Alichukua hiyo karatasi akaisoma, nilikuwa nimeandika: DADA MASELINA, NIMEFIKA SALAMA HAPA FREETOWN, NIPO NINASTAREHE HOTELI BINTUMAINI. WILLY".