TAN

TAN

Bayport

Bayport

Kikoa

Kikoa

Myway entertainment

Myway entertainment

FORE PLAN CLINIC

FORE PLAN CLINIC

MPINGA CUP 2016

MPINGA CUP 2016

Mashujaa Fm 89.3, Lindi

Monday, March 13, 2017

Karibu katika Adithi hii ya Kusisimua- Usikose


NJAMA

DIBAJI

Dunia yote ilitingishika zilipopatikana habari kuwa silaha kali na za kisasa zilizokuwa zimetolewa na Urusi kwa wapigania Uhuru wa Afrka Kusini, zimeibiwa bandarini Dar es Salaam.

Habari hizi zilileta utata mwingi, baadhi ya nchi zikisema ni njama za makaburu na nyingine zikisema ni njama za Tanzania.

Katika kiza kinene kilichozunguka suala hili serikali ya Tanzania ilimtuma Willy Gamba, Mpelelezi mashuhuri Ulimwenguni, kutafuta ukweli ulipo. Hapo ndipo patashika zikaanza na Jiji la Dar es Salaam likakumbwa na wimbi la msukosuko wa uhaini, usaliti na mauaji ya kutisha.


SURA YA KWANZA

LIKIZONI

Nilipoamka ilikuwa yapata saa tatu za asubuhi. Kuchelewa kwangu kuamka si kwa sababu mimi ni mtu mvivu wa kuamka, kama ambavyo ungefikiri, ila ilikuwa kwa sababu ya kuchelewa kulala. Nilikuwa nimewasili kwenye uwanja wa ndege wa mjini Freetown; sierra Leone, mnamo saa sita za usiku.

Kutokana na pilikapilika za tangu kutoka uwanjani mpaka kumaliza taratibu, nilijikuta ninaingia kitandani mnamo saa tisa la alfajiri, ukifikiria uchovu wa safari ndefu toka Dar es Salaam, Tanzania, hadi hapa utaona kuwa nina haki ya kuchelewa kuamka kama kweli wewe ni mtu mwenye kufikiria shida za binadamu wenzako.

Nilikuwa nimefika mjini hapa kwa likizo ya wiki mbili ambayo nilikuwa nimepewa na wakubwa wangu wa kazi baada ya kutekeleza kikamilifu kazi moja nzuri na kuwafanya wafurahi sana na kupendekeza nipate likizo.

Hapa mjini freetown nilikuwa nimefikia kwenye hoteli moja maarufu sana iitwayo LIIm Bin Tumaini, hoteli ambayo ilikuwa imependekezwa kwangu na abiria mwenzangu msichana ambaye yeye ni mwenyeji wa mjini Freetown.

Huenda litakuwa jambo la busara nikikusimulia jinsi tulivyoonana na msichana huyu, ambaye kama nitakavyokueleza, utaona kwamba alinifaa sana. Msichana huyu tulikuwa tumeonana kwa nasibu sana. Mimi ilikuwa inanibidi nibadili ndege mjini Roma, Italia. wakati nakuja toka Dar es Salaam kwa ndege ya shirika la ndege la Uingereza (BOAC) ambayo ilikuwa inaelekea moja kwa moja London.

Hivyo nilipofika Roma ilibidi nibadilishe ndege na kwa vile mipango ilikuwa imetayarishwa tayari na wakala ulioshughulikia safari yangu. nilikuta tayari ipo ndege ya shirika la ndegee liitwalo British caledonian, ikiwa inatokea London ikielekea Freetown. Kwa hiyo baada ya kutelemka toka katika ndege iliyotutoa Dar es Salaam, tulipanda ndege hii iliyokuwa ikielekea Freetown tayari kuendelea na safari yetu.

Mimi ndiye nilikuwa abiria wa mwisho kuingia ndani ya ndege maana mambo ya kujitangulizatanguliza mbele, rafiki yangu, mara nyingi yanaweza kukuletea kidamisi. Nilipoingia nilianza kuangaza mahali pa kukaa maana vile vile lazima unaposafiri usikae na watu hovyo hovyo tu kwani wengine wana mikosi. Kama wewe hujui namna ya kuwatambua watu wenye mikosi basi nitafute siku moja nitakunong'oneza.

Mara mbele kidogo nikaona kiti akiwa amekaa mtoto wa kike, nilimwangalia roho yangu ikaridhika.

"Samahani binti, sijui naweza kukaa?".

Aligeuka akaniangalia. Lo msichana huyu alikuwa na macho ya kuvutia sana. Kule kuniangalia tu nilihisi mwili wangu wote ukisisimka. Utafikiri macho yake yalikuwa yanaweza kuona ndani ya moyo wako. Kusema kweli nimeona wasichana wengi wenye macho ya kusisimua maisha mwangu, lakini huyu alitia fora. Macho haya yalikuwa hedaya aliyopewa na Mwenyezi Mungu.

"Bila ya wasiwasi", alijibu kwa sauti ya uchovu. Akagauka akaendelea kuangalia mbele.

Niliketi na muda si mrefu tukaombwa tufunge mikanda tayari kwa ndege kuondoka.

Baada ya kupaa juu na kuruhusiwa kufungua mikanda, nikapata kishawishi cha kuzungumza na huyu binti mwenye macho ya kusisimua.

"Samahani binti", nilimtaka radhi kabla ya kumpa ya kutoka rohoni mwangu.

"Unasemaje?".

"Unajuwa binadamu wanafahamiana kwa kukutana, wengine wanafahamiana kwa kukutana mashuleni, kazini, kwenye starehe na wengine safarini kama hivi na kadhalika. Kwa hiyo binti, mimi ningeonelea vizuri kama tungefahamiana".

Nilimuona akitabasamu.

Mimi naitwa Willy Gamba, sijui wewe mwenzangu unaitwa nani?".

"Mimi naitwa Veronica Amadu".

"Unatoka wapi na unakwenda wapi?".

Aligeuka na kunitazama huku macho yake makali yakionesha mshangao.

Usinielewe vibaya . Kama nilivyokuelza hapo awali, nia yangu ni kufahamiana tu. Nilimuonesha tabasamu la kumlainisha.

Hili tabasamu huwa nimeliweka kwa wakati kama huu tu na huwa silitoi ovyo ovyo. Na kama nilivyotegemea lilimlainisha.

"Mimi natoka mjini London na ninaelekea Freetown ambako ndiko makazi yangu, Je wewe?".

Mimi natokea Dar es Salaam, Tanzania na ninaelekea Freetown vile vile. Niko likizo.

"Yaani kwenu ni Tanzania?".

"Ndio" Akashangaa

"Na ni likizo tu inakuleta Freetown?".

"Ndio".

"Karibu kwetu maana mimi ni mzaliwa wa Sierra Leone 

"Sawa".

"Hivi ninayo furaha kupata mwenyeji, ama siyo?".

"Usiwe na wasiwasi mwenyeji umepata". Alitabasamu tena.

Nakuambia mimi nilizaliwa na bahati ya kuelwana na hawa watoto wa kike maana ni mara chache sana kunichenga. Sijui wewe mwenzangu vipi?".

"London ulienda kimatembezi au kikazi?". Kutokana na mazungumzo nilishakidhi kuwa huyu msichana ni msomi.

"Nilienda kikazi. Kusema kweli mimi ninafanya kazi ya uandishi. Mimi ni mwandishi wa habari za siasa na uchumi za Afrika Magharibi katika gazeti la Afrika".

"Oh, nimekumbuka sasa hata jina lake. Ama kweli nina bahati ya kukutana nawe, maana mimi ni mfanyabiashara huko Afrika Mashariki na nimekuwa natafuta njia ya kuwekeza kupata mipango ya kuwa na uhusiano wa kibiashara na nchi za huku, hivyo nafikiri kama utakuwa na muda utaweza kunielekeza katika mambo haya kwa vizuri".

"Na mimi nitafurahi kufanya hivyo".

"Hata hivyo nami nitapata wasaa wa kujua mambo mbali mengi kutoka Afrika Mashariki kwani sijawahi kufika, utafikia hoteli gani sijui?".

"Sijui mpaka sasa, maana kama nilivyokwambia mimi ni mgeni kabisa sehemu hizi, sijui wewe  utanishauri nifikie hoteli gani?, nataka hoteli yenye wasifa mzuri, tulivu na isiyo na matatizo madogo madogo.

"Nafikiri Bintumaini Hoteli itakufaa sana, ndio hoteli maarufu hapa mjini Freetown".

"Asante, nitafuata ushauri wako".

Tulipokuwa tunatua kwenye uwanja wa ndege wa Freetown msichana huyu aliniahidi kuwa angefika kesho yake saa nne hoteli kwangu na akaahidi kuwa angenipeleka kuogelea kwenye ufuko mmoja maarufu sana uitwao Lumley Beach.

Hivi ndivyo nilivyofahamiana na msichana huyu ambaye asubuhi hii nilijua atakuja kunichukua kunipeleka kuogelea. Hivyo nilipoamka niliagiza chemsha kinywa, hakafu nikaingia maliwatoni nipate kuoga.

Baada ya kuog nilisnza kustaftahi, maana tayari chemsha kinywa ilikuwa imefika. Nilipomaliza kustaftah ilikuwa inakaribia saa nne, hivyo nilijiandaa na kujiweka katika mavazi kuogelea, maana niliamini Veronica alikuwa mtu wa kutimiza ahadi zake.

Wakati najitayarisha, kengele ya simu ililia. Nikaiendea kuijibu.

"Hallo, chumba namba 305 hapa".

"Samahani kwa kukuhatiki, kuna mgeni wako hapa mapokezi", mfanyakazi wa mapokezi alinieleza.

"Hebu nizungumze naye".

"Subiri".

Hallo".

Hallo, Vero. njoo huku chumbani".

"Nakuja".

Tukakata simu. Punde si punde Veronica aligonga mlangoni, nikamfungulia. Harufu nzuri ya uturi wa ghali sana ilijaza chumba, macho yetu yalionana na woga tukapigwa na butwaa, hali iliyotokea sina maneno ya kuielezea. Msisimko uliokuwa ukitolewa na macho yake uliniingia tena, na ni baada ya kujikaza kisabuni ndipo nilipoweza kuongea.

"Vero, habari za toka jana?".

"Ni nzuri. Je, vipi wewe umelala salama?".

"Salama kabisa, karibu uketi".

"Wapi?".

"Hapa kitandani".

Vero akitabasamu akaketi. alikuwa amevalia suruali ya aina ya dengirizi na fulana nyeupe yenye matundu makubwa iliyoonyesha umbo la matiti yake yaliyokuwa yameshikiliwa na kanchiri moja safi sana. Mvao huo ulinipa umbo ambalo liliweza kunisihiri kabisa.

"Uko tayari twende kuogelea?", aliniuliza.

"Niko tayari".

"Kabla hatujaondoka twende hapo nje kwenye rosheni ya chumba hiki nikuonyesha jinsi ukiwa kwenye hoteli hii uwezavyo kuona mandhari ya kupendeza sana". akaongoza roshenini.

"Hoteli hii imejengwa kwenye kilima kama unavyoona", alianza kueleza huku tukiwa tumesimama tukiangalia mandari nzuri mbele yetu.

"Kilima hiki kinaitwa Bintumaini, na hoteli inarithi jina la kilima hiki", alionesha kidole na kuendelea. "Ile bahari ya Antlantic na ule ufuko unaouona ndio ufuko maarufu uitwao Lumley Beach, na ile ghuba inayoonekana vizuri kabisa kutoka hapa inaitwa Ghuba ya mtu wa vita (Man-of-war)".

Nilianza kumpenda huyu msichana kwa mambo yake, kwani alikuwa anachukua jukumu la kunionyesha vizuri mandhari ya mji huu, kitu ambacho sikukitegemea kabisa.

"Lo. hii ghuba inaonesha picha nzuri sana".

"Zamani kabla hoteli hii haijajengwa hapa, watalii wengi walikuwa wanakuja kwenye kilima hiki ili kuchukua picha ya sehemu yote ya pwani na ukanda huu.

"Zile nyumba pale ufukoni ni hoteli?". kulikuwa na majengo mazuri ufukoni na vile vile kati ya hoteli hii na ufukoni kwenye barabara iliyotelemka kutoka hotelini.

"Ile ni Lumley Beach Hoteli, na haya majengo hapa katikati ni Freetown Casino ambayo kila siku iko tayari kumeza na kutoa mamilioni ya pesa". Veronica alimwemwesa.

"Je una swali zaidi?".

"La hasha, mpaka hapa nimekidhi. na ni lazima nikubali kabisa kuwa nimepata mwenyeji wa kunifaa. Tokea sasa nimepata imani kuwa likizo yangu itafana sana.

"Haya sasa twende zetu tukaogelee", Veronica aliniambia huku akinivuta mkono.

Nilifunga mlango wa chumba tukatelemka mpaka mapokezi. Tulipofika mapokezi nikaomba karatasi ili kuwajulisha Dar es Salaam kuwa nimefika salama na mahali gani nilipokuwa nimefikia.

"Tuna habari hizi kwa njia ya Teleksi", nilimwambia kijana wa mapokezi. Alichukua hiyo karatasi akaisoma, nilikuwa nimeandika: DADA MASELINA, NIMEFIKA SALAMA HAPA FREETOWN, NIPO NINASTAREHE HOTELI BINTUMAINI. WILLY".


Aliangalia namba za teleksi nilizokuwa nimeandika akaridhika.

"Sawa nitaipeleka sasa hivi".

"Asante".

Kisha nikamfuata Veronica aliyekuwa akinisubiri nje kwenye gari lake aina ya Peogeot 204 Coupe lililokuwa wazi juu.

"Gari lako zuri sana, mimi nahusudu magari haya ya kimichezo".

"Asante".

Tulipanda ndani ya gari, akalipiga moto tutaondoka kueleka Lumley Beach.

Tulikuwa tumeogelea kwa muda mwingi, tukawa tunajisikia kuchoka. Watu walikuwa wengi sana, sura nyingi zikiwa ni za watalii kutoka Ulaya. Tulitoka ndani ya maji tukaenda kujilaza kwenye mchanga chini ya mwamvuli mmoja mkubwa kati ya miamvuli mingi iliyokuwepo hapo kwa madhumuni ya kutoa kivuli kwa waogeleaji waliochoka na kutaka kupumzika.

"Ngoja niendee vinywaji", Veronica alisema.

"Hapana ngoja mimi ndiye niendee".

"Usiwe na wasi wasi, wewe ni mgeni wangu, sina budi kukushughulikia", alitabasamu na kuelekea baa, punde akarudi akiwa na makopo mawili ya bia aina ya Amstel.

"Hizi pombe mnatengeneza hapa?".

"Hapana, tunaagiza toka ughaibuni".

Tulianza kunywa huku tukiwa kimya kwa muda mfupi kisha Veronica akainuka na kujilaza kifuani pangu.

"Unajua Willy, mimi nilikuwa najiuliza kwa nini umechagua kuja Sierra Leon mapumziko na usiende Ulaya au Marekani kama vijana wengi wa Afrika wenye uwezo kifedha kama wewe wangefanya?".

Sikujua nia hasa ya msichana huyu kuuliza swali kama hili, lakini unapokuwa unazungmza na mtu msomi na hasa mwandishi wa magazeti, kazima uwe macho na majibu yako maana siku zote wana vidadisi vyenye lengo maalum.

"Swali ulilouliza Vero ni swali la kimsingi sana. Kusema kweli vijana wengi wa Kiafrika wamekuwa na kasumba moja mbaya sana, na kasumba hiyo ndiyo ambayo umeizungumzia, maana wanaamini kuwa mtu kabla hajafika Ulaya basi hajaendelea. Pili kama akitembelea nchi nyingine ya Kiafrika hakuna lolote la kujifunza. Yaani ka kifupi wanadharau utamaduni wa Kiafrika na kuheshimu utamaduni wa kizungu. Kwa mawazo yao maendeleo na ustaarabu vinapatikana Ulaya. Hili ni tatizo tuliloachiwa na ukoloni".

"Wakoloni waliotutawala walituachia kasumba kali ya kwamba kwa Mwafrika hakuna chochote kizuri kinachoweza kupatikana ila mazuri yote yanatokana na Mzungu", nilinyamaza kupitisha mate.

"Ni jambo la soni kuona kuwa baada ya miaka mingi ya nchi nyingi za Kiafrika kujitawala bado kasumba hii inaendelea tu, kwa hiyo Vero, sisi vijana wa Afrika hatuna budi kufanya mapinduzi katika fikira zetu na kutambua kuwa kuna mengi ya kujifunza katika nchi zetu za Kiafika, ambayo yatatusaidia katika maendeleo ya Afrika".

"Kwa kujibu swali lako Vero, mimi nimeanza mapinduzi ya kufuta kasumba hiyo na ndio sababu nimekuja Sierra Leon kwa mapumziko badala ya kwenda Ufaransa au nchi nyingine yoyote nje ya bara hili".

"Kwa hiyo una maana kwamba Ulaya kwa sasa hivi hakuna tunayoweza kujifunza kwa ajili ya maendeleo nyetu?".

"Sina maana hiyo, yako mengi tunayoweza kujifunza kutoka ng'ambo, kwa ajili ya maendeleo yetu. Na vile vile kuna mengi yanatubidi kujifunza katika bara hili kwa maendeleo ya bara zima. Kitu ninachopinga hasa mimi ni kule kudharau katakata kuwa hakuna cha kujifunza katika bara hili.

"Kwa hiyo una maana kuwa kuna umuhimu wa sisi vijana wa Kiafrika kutembeleana ili tuweze kujifunza mengi kati yetu na kuelewana?".

"Sawa kabisa Vero, Sasa hivi viongozi wetu chini ya OAU wanapigania Umoja wa Afrika, Umoja huu hauwezi kupatikana kwa maneno tu ila kwa vitendo pia. Na mimi naamini kuwa Umoja utaletwa na sisi vijana na wala si wazee. Ndio sababu unaona kuna chama cha vijana cha Afrika 'PVM'hivyo kwa kutembeleana na kujua jinsi wenzetu wanavyoishi nchini kwao kutaleta uelewano kati ya vijana katika fani mbali mbali na hata katika utamaduni wa nchi hadi nchi. Kwa kutokana na uelewano huu umoja wa Afrika utafikiwa kwa urahisi.

"Nafikiri nimekuelewa, yaani una maana kuwa kama wewe ni mfanyabiashara na umekuja Sierra Leon na kuonana na vijana wenzako wafanyabiashara, mkazungumza mambo ya kibiashara, utakaporudi kwenu kama mtakuwa mmeelewana, unaweza kuanza kufanya ushirikiano wa kibiashara kati yao na wewe".

Anaendelea "Hii haitakuwa na maana kwamba ni biashara kati ya Tanzania na Sierra Leon, hivyo kutakuwa na ushirikiano wa kibiashara katika nchi zetu. Jambo kama hili likiishaanza kati ya nchi na nchi katika fani mbali mbali, kutafikia wakati ambapo nchi za kiafrika zitashirikiana sana. Hivyo lazima uelewano utakuwepo wa hali ya juu na kwa hivyo umoja unaweza kupatikana bila bila jasho. Nafikiri ndio maana uliyokuwa nayo".

"Hasa ndio maana yangu Vero, umenipata vizuri sana,".

"Kuna neno moja uligusia, yaani jambo la utamaduni. Mimi nafikiri kiutamaduni na kiitikadi Afrika haina tofauti kati ya nchi na nchi. Maana Mwafrika ni Mwafrika tu, awe wa Tanzania au wa Sierra Leon utamaduni wake ni sawasawa tu. Sijui wewe unafikiriaje?".

Nakwambia mtu mara akisha kuwa mwandishi basi siku zote yu mwandishi, msichana huyu alikuwa ananitoa jasho kwa maswali, lakini mimi Willy mambo kama haya ninayapenda maana yananipanua mawazo hivyo nilimjibu.

"Kusema kweli utamaduni wa mwafrika haupitani sana lakini tofauti zipo. Tofauti hizi zinatokana na mazingira ya nchi na nchi, kwa mfano nchi zilizotawaliwa na Mfaransa zitakuwa na tofauti kidogo na zile zilizotawaliwa na Mwingereza. Nchi zenye mazingira ya dini ya Kikristo utakuta zinatofautiana kidogo na nchi zenye mazingira ya nchi za Kiislamu".

"Vile vile mazingira na maendeleo ya kiuchumi na kisiasa ambayo yanatofautiana kati ya nchi hizo. Kwa hiyo ingawaje kimsingi utamaduni wa kiafrika ni sawa lakini kuna vipengele vingi vinavyoleta tofauti kati ya utamaduni wa nchi na nchi".

"Kuna vijana wengi wa kiafrika ambao wanasema utamaduni wa kiafrika haufaina ndio maana wengi wao wanaingia mambo chungu nzima toka ng'ambo, wewe unafikiriaje?".

"Hao wanaosema kuwa haufai sikubaliani nao kabisa, mimi kwa upande wangu naamini utamaduni wa mwafrika ni sawa kabisa na hatuna budi kuuendeleza. Ila kusema kweli lazima ufanyiwe marekebisho kutokana na maendeleo ya nchi ili ufuate misingi ya kisiasa na kiuchumi kwa kufuatana na msimamo wa kisiasa na kiuchumi wa kila nchi.

"Vile vile utamaduni unanyumbulika wenyewe kutoka karne hadi karne, hivyo utakuta katika karne hii ambayo teknolojia imeendelea sana na kuingia hata Afrika, utamaduni unabidi kunyumbulika na kufuata hali hii".

Nilitua kidogo kisha nikaendelea

"Juu ya kuiga utamaduni wa kutoka ng'ambo lazima jambo hili liangaliwe kwa makini sana lisije likatupoteza kabisa. jambo hili lazima liangaliwe kama tatizo na liweze kutatuliwa. Nikirudia usemi wangu wa nyuma hii tabia ya kuiga mambo toka ng'ambo inatokana na kasumba ya kufikiri kuwa kila kutu ili mradi kimetoka ng'ambo ni kizuri hata kama hakilingani na matakwa ya utamaduni wetu. Hii yote ni shida ya kutawaliwa.

"Mimi nakubali kuwa kuna mambo ambayo tunaweza kuyaiga toka ng'ambo ili mradi tu yanaweza kulingana na matakwa ya utamaduni wetu na kama ni mambo mazuri yanayolingana na misingi yetu ya kisiasa na kiuchumi. Hivyo mambo ambayo yataweza kuleta maendeleo katika mabadiliko ya utamaduni wet ili yaweze kulingana na hali ya maendeleo ya nchi zetu itabidi tuyaieege.

"Lakini yale ambayo tutaona yanatuletea madhara lazima tuyapige vita. Kwa ufupi Vero, utamaduni wa mwafrika kimsingi lazima uendelee daima dumu".

"Katika kabila langu wa Wamembe ambao tunatoa katika Jumbo la Kusibi, kitendo kama hiki cha kuogelea kwa pamoja wanawake na wanaume hadi sasa kinaonekana ni kitendo cha aibu, kilichoigwa kutoka kwa Wazungu kinyume na utamaduni wetu wa kiafrika.

"Kama wazee wangu watanikuta sasa hivi watasikitika sana, wataniona nimepotea kabisa. Je Willy unamtazamo gani kwa kitendo hiki ukikiangalia na mtamo wa utamaduni wa kiafrika?", alitoa tabasamu la kuonesha kuwa swali langu lilikuwa tamu sana.

"Kwa upande wangu binafsi nafikiri kitendo kama hiki ni kati ya vitendo ambavyo vinabidi vikubalike kutokana na hali ya kimaendeleo iliyofikiwa sasa na nchi zetu. Wakati wa mwanzo na katikati ya karne hii jambo hili lingeonekana kuwa baya. Na kwa vile wazee wetu wamekuwa wakati huu, lazima mtazamo wao uwe hivyo. Lakini sisi pamoja na watoto wetu ambao tumekua mwishoni mwa karne hii jambo hili ni lazima likubalike maana tunajua faida yake".

"Au unajitetea", alitania Veronika.

"Pamoja na hayo".

"Lo, Willy, kwa mfanyabiashara, wewe ni mtu unayejua mambo ya maana sana. nafikiri uandishi ungekufaa sana. Vijana wengi wa kiafrika wangekuwa na mwamko kama wako Afrika ingepiga hatua haraka haraka sana, maana nimekuona kuwa una fikira za kimapinduzi. Haya mazungumzo yetu nitayatafutia nafasi katika gazeti la "Afrika" ili tujue vijana wenzetu nao wanafikiriaje".

"Ukifanya hivyo utakuwa umefanya jambo la maana, hasa ukitaka lipate usikivu na ubishani sana, jaribu kukilaumu Chama cha vijana wa Afrika (PYM) kuwa hakijawa na msimamo imara wa kuwaeleza vijana wa Afrika, ni vipi kijana wa Afrika yampasa awe kifikira".

"Basi niache mimi nitajua jinsi ya kuwakoroga".

"Naamini baada ya wewe kukubali kuwa kuna haja ya sisi vijana wa kiafrika kutembeleana, utakuwa mtu wa kwanza kuitikia mwito wa kuja kututembelea Tanzania, uwezen kuonana na vijana wa huko!".

"Bila shaka. Ninakuahidi mara tu utakaporudi mimi nitakuja huko. Tutapanga zaidi baadae".

"Karibu Tanzania kwa mikono miwili".

"Umeoa?", aliuliza ghafla.

"Bado".

"Una mchumba?".

"Ndio".

"Lini mnatarajia kuoana?".

"Yuko Ulaya kwa masomo ya miaka mitatu. Sasa amebakiza miaka miwili, kwa hiyo mipango ya kuoana bado iko mbali; tuseme miaka mitatu toka sasa".

"Muda mrefu huo, chochote kinaweza kutokea".

"Mungu atasaidia yasitokee mabaya".

Mazunguzo haya ya mwisho yalileta kimya kati yetu, sijui Veronika alikuwa akifikiri nini baada ya kuniuliza swali hilo.

Macho yake haya ya kusisima yalizidi kunisisimua, zaidi nilipoona yanaingiwa na wingi la jitimai. Mara nikana kivuli cha mtu kimesimama karibu yetu. Veronika naye alikuwa amekiona. Akainuka kutoka kifuani na kugeuka kuangalia.

"Hallo Vero, habari yako".

Kijana mmoja hirimu yangu alikuwa amesimama karibu na mwavuli wetu.

"Hallo Sharrif, nzuri".

Kijana huyu alikuwa amevaa fulana nzuri iliyokuwa na picha ya hayati Komredi Che Guevara. Nilipomwangalia vizuri mara moja nikatambua kuwa nimeonana tena na mtu mwenye fikra za kimapinduzi".

Veronika alisimama na mimi ikanibidi nisimame ili tusalimiane.

"Sherrif, huyu ni rafiki yangu, Willy Gamba, kutoka Tanzania. Yeye ni mfanyabishara na yuko hapa kwa mapumziko". Kisha akamfahamisha Sharrif kangu.

"Huyu ni Ahmed Sharrif. Ni mwandishi mwenzangu katika gazeti la Afrika. Yeye anashughulikia habari za Ukombozi Kusini mwa Afrika", tukapeana mikono.

"Mimi hufika Tanzania mara nyingi sana. Hasa wakati wa mikutano ya kamati ya Ukombozi na mikutano ya Nchi zilizo Mstari wa mbele wa Ukombozi".

Nikajua kwamba kubuni kwangu kulikuwa sawa. Kijana huyu alikuwa mwanamapinduzi.

"Ahaa, vizuri. Nafurahi kusikia unajua nchi yangu".

"Vipi Vero, hamuwezi kuwa na muda tukaonana baadaye jioni nipate mumkaribisha huyu komredi hapa kwetu,; unajua hawa kwao ni wakarimu sana".

"Hamna taabu, au unasemaje Willy?".

"Mimi sina maneno, uamuzi unao wewe mwenyeji wangu".

"Basi tutaonana saa hizo", Sharrif aliaga akaondoka.

Tuliingia ndani ya maji mara ya mwisho kabla ya kwenda kupata chakula cha mchana.

Niliingia ndani ya baa hii ya III Bintumaini kiasi cha saa moja za jioni kama miadi yetu ilivyokuwa. Niliangaza kuona kama Sherrif alikuwa amefika lakini alikuwa hajafika. Veronika ambaye tulikuwa tumeachana baada ya chakula cha mchana tukiwa tumeahidiana kuonana ndani ya baa hii saa moja hivi naye alikuwa hajawasili.

Nilichagua meza moja iliyokuwa kwenye kona kushoto ya mlango wa kuingilia. Halafu nikaagiza bia moja baridi. Bado baa ilikuwa haijaa watu. Kulikuwa na watu wasiozidi kumi hivi baa ilikuwa kimya mbali na mabishano ya watu watatu waliokuwa wamekaa kaunta wakibisha juu ya mpira wa fainali za klabu bingwa ya Afrika kati ya timu ya Hafia kutoka Guinea na Canon kutoka Cameroon.

Muda si mrefu Veronika, Sharrif na msichana mwingine wakaingia. Waliponiona wakanijia. Sharrif alipungiana mikono na hao watu waliokuwa wakibishana juu ya mpira pamoja na mwuza baa aliyekuwa amekaa nyuma ya kaunta. Walipofika nikasisima kuwakaribisha.

"Karibuni".

"Asante", walijibu kwa pamoja. wakavuta viti na kukaa.

Mfanyakazi alifika tayari kwa kuwahudumia.

"Mtakunywa nini?", niliwauliza.

Wote walijibu kuwa wataanza na bia ili kukata kiu. Hivyo niliagiza bia nne maana na mimi nilikuwa nimemaliza yangu.

"Samahani sana kwa kukuweka ukisubiri". Veronika alitoa udhuru.

"Kwa mwafrika mmewahi sana", nilimjibu. Wote tukacheka.

"Willy usianze tena siasa yako", alionya Veronika. Halafu kama ameshituka akasema "Kumradhi

Willy nimesahau kukufahamisha kwa mgeni wetu. Huyu dada anaitwa Khadija na ni mchumba wake Sharrif".

"Oh. nafurahi kukutana naye. Mimi naitwa Willy Gamba, habari yako?".

"Habari yangu ni nzuri, na mimi nimefurahi kukutana nawe". Tukapeana mikono.

Khadija alikuwa msichana mwenye uzuri wa kutosheleza kabisa. Ingawa uzuri wake huwezi kuulinganisha na ule wa Veronika. Maana Veronika alikuwa na uzuri wa peke yake usio wa kawaida, yaani si kwamba alikuwa mzuri sana wa sura ila tu macho yake na umbo lake lilileta

msisimko wa pekee kwa mwanamume.Sujui kama wewe nawe umewahi kuona msichana wa aina hii?,

Kama hujawahi bahati yako mbaya, afadhali fanya kila njia usafiri uone mengi. Kwa hiyo Khadija alikuwa na uzuri wa kufaa. Kwa sura na umbo lake Sharrif alikuwa amejipatia mchumba mrembo.

"Hongera Sharrif, kwa kuwa na mchumba mrembo namana hii, hakika unajua kuchagua.

"Asante. Ninapochagua msichana ili awe mama watoto wangu baadae, ninahakikisha sifanyi kosa".

Veronika alimwemwesa na Khadija akabinua mdomo kutokana na usemi wa Sharrif. Vinywaji vilifika, kwa muda tukanywa kwa ukimya.

"Dar es Salaam unakaa upande gani?", Sharrif alivunja ukimya.

"Nakaa sehemu inayoitwa Upanga".

"Upanga naifahamu sana. Kuna jamaa mmoja wa hapa kwetu anaitwa Kamara Frank yuko kwenye ofisi za Kamati ya Ukombozi ya OAU. Sijui kama unamfahamu?", Ingawaje nilikuwa namfahamu lakini kwa sababu ambazo sijawahi kuzieleza nilibana.

"Simfahamu".

"Dar es Salaam napapenda sana mimi, safari nyingine nikienda huko lazima twende wote na Khadija, unasemaje".

"Nitafurahi ile mbaya".

"Na mimi nina mipango ya kutembelea huko baada ya Willy kurudi Dar es Salaam. Mnaonaje kama tukifanya safari moja?", Veronika aliwauliza.

"Kama hatutakuwa mzigo kwa Willy litakuwa jambo la maana", alijubu Sharrif.

"Mimi ninawakaribisheni nyote kwa mikono miwili. Hamna taabu kabisa kwangu".

"Hapa utakuwepo kwa muda gani?", Khadija aliuliza kwa shauku.

"Si zaidi ya wiki mbili".

"Mpaka utakapoondoka tutakuwa tumeshapanga lini tutakuja, au siyo Ahmed?", aliuliza Khadija.

"Bila shaka mpenzi".

Nilitambua kuwa Khadija alikuwa na shauku kubwa ya kuja Dar es Salaam maana tabasamu haikutoka tulipokuwa tukizungumza jambo hili.

"Ni leo asubuhi tulipokuwa tunazungumza juu ya haja iliyopo kwa vijana wa Afrika kutembeleana ili wapate kujifunza mengi kati yao. Kwa hiyo Willy inaonekana kampeni yako imeshika moto mara moja", alidakiza Veronika.

"Na kweli", nilijibu.

Mazungumzo yaliendelea huku vinywaji vikimiminika. Ilipofika saa mbili unusu tulikwenda hotelini tukala chakula cha jioni. Kisha tukarudi kwenye meza yetu tukaendelea na vinywaji na mazungumzo. Sharrif ndiye alikuwa akitawala mazungumzo akieleza mambo aliyoyaina na kuyasikia wakati akisafiri Afrika Kusini na kuandika habari za huko. Alitueleza kwa kinaganaga jinsi ubaguzi wa rangi unavyoendeshwa huko Afrika ya Kusini.

Mimi ni mtu mwenye roho ngumu isiyojali, lakini maneno aliyoeleza Sharrif ylinitia uchungu mno. Wote watatu tulibaki tumebung'aa tu huku tukimsikiliza Sharrif akitueleza habari hizi za kutisha na kusikitisha sana. Mawazo yangu yalikumbuka safari zangu nilizofanya katika kusaidia ukombozi na nikaona nina haki kabisa ya kusaidia ukombozi bila hata kulipwa.  

"Ngoja nikukate kauri Sharrif", alidakia Veronika.

"Umetueleza mengi juu ya unyama unaofanywa na makaburu katika siasa yao ya ubaguzi wa rangi, na tumesoma na kusikia mengi ya kutisha vile vile. Ukiwa mwandishi wa habari na ukiwa mtu ambaye umefanya utafiti mwingi juu ya siasa na nafikiri historia ya sehemu hiyo  ni matumaini yangu kuwa utaweza kunijibu maswali yangufulani fulani ambayo huwa yananipa dukuduku juu ya Afrika Kusini.

"Bila wasiwasi nitajitahidi kujibu yake nitakayoweza, maana nyinyi waandishi maswali yenu ni ya kijanja sana", alijibu Sharrif akitania. Mimi na Khadija tulikaa kimya kufaidi kutoka kwa waandishi hawa wa gazeti maarufu la Afrika juu ya sehemu hii yenye matata mengi, yaani Kusini mwa Afrika.

"Huu ubaguzi ulianzaanzaje?, nikifanua zaidi ningependa unipe historia jinsi hawa watu weupe walivyofika Kusini mwa Afrika mpaka wakafikia kiasu cha kuwafukuza wakazi wa asili wa sehemu hiyo na kutawala sehemu hiyo. maana mimi naamini kuwa watu hawa weupe si wazaliwa wa huko", aliuliza Veronika.

"Swali lako ni zuri sana. Kihistoria ubaguzi wa rangi uliota mizizi yake tangu zamani wakati wazungu walipokuwa wakitafuta njia ya maisha ya kikoloni. Mnamo majira ya machipuko ya mwaka  1652 kikundi kidogo cha meli tatu za Kidachi kilitia nanga katika Ghuba ya Meza (Table Bay), karibu kabisa na ncha ya kusini mwa bara hili la Afrika. Tokea  muda huo watu hao walianzisha koloni dogo katika sehemu hiyo, ambalo ndilo likawa kiini cha kuanzishwa kwa makazi ya Wazungu kusini mwa Afrika". Sharrif alilegeza koo kwa kinywaji kisha akaendelea.

"Baada ya muda si mrefu wakoloni hawa wa Kidachi, walianza kupora maeneo bora ya ardhi na sehemu zenye rutuba na wakati huo huo wakiwapiga vita wakazi wa asili wa sehemu hiyo na kuwaondoa katika sehemu zao. Wakishirikiana na wakoloni wa Kijerumani. Walitumia silaha kali dhidi ya wenyeji wa sehemu hii na kuweza kuwashinda. Mapambano makali yalitokea na kuwafukuzia mbali wakazi wa asili wa sehemu hiyo. Hivi ndivyo ilivyotokea mpaka kuwepo Wazungu kusini mwa Afrika.

"Umetueleza kwa ufasaha sana jinsi wazungu wacheche walivyoweza kufika kusini mwa Afrika. Lakini bado hujaeleza jinsi ubaguzi ulivyoanza", Veronika alikumbusha.

"Swali hilo ndilo naendea. Wazungu hawa walipoweza kuwafukuza wakazi wa asili katika maeneo yao bora ya ardhi, walihitaji watu wa kuja kuwatumikia katika mashamba yao. Hivyo walileta watumwa hasa kutoka Madagascar ili watumike katika kazi za malipo ya chini. Kutokana na hayo, utumwa ukaingia kusini mwa Afrika. Kwa bahati mbaya watu waliotumiwa kama watumwa katika mashamba ya wakoloni hawa walikuwa watu weusi. Hivyo uhusiano kati ya watu hawa weusi na wakoloni ukawa wa utwana na mwinyi. Wazungu walianza kuwabagua watu weusi kwa kuwaona kuwa ni watumwa wao, kwa hivyo watu wa hali ya chini sana kwao".

"Ilipo karne ya ishirini ambapo utumwa ulipigwa vita usionekane mahali popote duniani. wazungu hawa ndipo wakaanzisha siasa ya ubaguzi wa rangi ambayo kimsingi unaendeleza uhusiano ule ule uliokuwepo wakati wa utumwa. Kwa hiyo ndugu zangu, ubaguzi wa rangi ni utumwa wa karne ya ishirini. hivi ndivyo ubaguzi wa rangi ulivyoanzishwa.

"Kwa hiyo siasa ya ubaguzi wa rangi ulikuwepo hata kabla ya kujitawala kwao mwaka 1948?", Veronika aliuliza

"Ndio; hii siasa ilikuwepo ila tu tunaweza kusema walipojitawaka siasa hii iliinuliwa hadhi yake kwa kuitungia sheria chungu nzima za kuilinda. Kwa mfano ukifanya kosa lolote dogo la kuvunja sheria hii utahukumiwa kama umefanya kosa la jinai. Siasa hii ya ubaguzi ina sheria na amri nyingi za ukandamizaji ambazo hutawala maisha ya kila siku ya Waafrika, machotara na watu wengine wasiokuwa wazungu zaidi ya milioni ishirini walioko Afrika Kusini. KWa kifupi sheria hizi huwanyima haki za kibinadamu".

Mazungumzo haya yalizidi kunigusa sana.

"Nasikia kutokana na siasa hiyo ya kibaguzi mamilioni hayo ya watu yamezuiwa maendeleo bali huteswa na kunyimwa haki zote za msingi za kisiasa, kijamii na kiuchumi. Na vile vile huwafanya waafrika wa huko wasitambuliwe kama binadamu. Ni jambo la kutia uchungu sana',
nilidakiza.

"Ni la kutia uchungu sana Willy", Sherrif alisisitiza.

"Fikiri wewe uambiwe kuwa hufai kuitwa binadamu, sijui utajisikiaje".

"Utajisikia afadhali kufa", nilijibu.

"Na ndio maana jumuia ya ulimwengu inapiga kelele juu ya siasa hii. Na sisi, wale wakiwa ndugu zetu, hatuna budi kuwaunga mkono katika harakati zao za kujikomboa kutoka katika balaa la siasa hii", Sherrif alisisitiza.

"Hivi hawa wazungu wa huko hawana dini?", Khadija aliuliza kwa mara ya kwanza.

"Kwanini?, Wana dini karibu wote kwani dini huko imekomaa kabisa", Sherrif alijibu.

"Basi ni jambo la kushangaza kwa mambo wanayoyafanya na hali wao ni wacha Mungu. Maana imeandikwa katika Biblia katika kitabu cha Mathayo Mt: 22:37-40, nalo neno lasema kuwa Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndio amri iliyo kuu tena ni ya kwanza; na ya pili ifanane nayo, nayo ni hii Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati na manabii. Hawa Waafrika wanaokaa nao ndio majirani zao, sasa kama wanawanyanyasa hivi hawana haja ya kujiita wenye dini, maana amri hii ilinenwa na Yesu Kristo mwenyewe", Khadija alinena.

Wote tulishangazwa busara ya maneno ya michana huyu. Tulipigwa bumbuazi tukawa kimya kwa muda.

"Mungu atawasaidia wa Wafrika wa huko Khadija. Maelezo yako yanaonyesha kuwa hata Mungu hayuko pamoja na hao Makaburu", nilijibu.

Baada ya kupita kipindi kingine cha ukimya kila mtu akiwa anayatafakari yaliyosemwa, Veronika alivunja tena ukimya.

"Harakati za kujikomboa zilianza lini huko Afrika Kusini?".

"Wazalendo wa Afrika Kusini walianza harakati za kupinga utawala huu wa kikandamizaji siku nyingi sana. Lakini tukio ambalo lilileta sura nzima ya jinsi wazalendo walivyokuwa wameingiwa na mwamko ni lile tukio la Shapeville mnamo mwaka 1960. Katika tukio hilo ambapo wazalendo walijitokeza waziwazi kupigaba na Makaburu, Serikali ya Makaburu ilifanya mauaji ambayo yalisababisha chuki kubwa kuhusiana na utawala huo wa Makaburu. Hata Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilistushwa na tukio na likapitisha azimio la kusisitiza kwamba siasa ya ubaguzi wa rangi inaweza kuhatarisha amani na usalama wa ulimwengu".

"Tokea hapo Baraza la Usalama na Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kila mara yamerudia kulaani kwa nguvu na kuipinga siasa ya ubaguzi wa rangi, na makazi ya vitongoji vya Bantustan na kuunga mkono kanuni za kujitawala kwa walio wengi Afrika Kusini. Lakini ukweli ni kwamba utawala wa kibaguzi wa Pretoria unapuuza maazimio haya ya umoja wa Mataifa. Na utawaka huo unazidi kuota mizizi mirefu zaidi nchini humo", Sherrif alieleza kwa sauti ya jitimai. Baada ya kunywa kinywaji chake na kulegeza koo aliendelea.

"Baada ya kuuawa kwa Waafrika katika kitongoji cha Soweto mnamo mwaka 1976, Baraza la Usalama lilisisitiza tena kutambua kwa uhalali harakati zinazofanywa na wazalendo wa Afrika Kusini dhini ya ubaguzi wa rangi".

"Nakumbuka nimewahi kusoma kuwa mbamo Agosti mwaka 1963 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio maarufu la 181 ambalo ambalo lilizitaka nchi zote zilizo wanachama wa Umoja huo kukomesha kuuza na kupeleka zana za aina zote za kivita na magari ya kijeshi kwa Afrika Kusini. Nasikia kuwa nchi za Magharibi ambazo ndizo zaidi zinahusika na upelekaji wa zana hizi hazilitekelezi ombi hili. Jambo hili ni la kweli?", Veronika aliuliza.

"Jambo hili ni kweli kabisa na limeleta utata mwingi katika mikutano mingi ya kimataifa. Nchi za Magharibi kama vile Uingereza, Marekani Ujerumani Magharibi, Japan, Italia na Uyahudi bado zinaendelea kupeleka silaha Afrika Kusini, pamoja na kuwapatia wabaguzi hao utaalamu na hati kwa ajili ya utengenezaji wa aina mbali mbali ya silaha. Nafikiri unakumbuka kashfa ya mafuta ambayo yamekuwa yakipelekwa Rhodesia na Afrika kusini na Kampuni za mafuta za Shell na BP za Uingereza na huku serikali yao ikiwa na habari kamili", Sherrif alieleza.

"Na Jumuia ya Ulimwengu imefanya nini", Veronika aliendelea kuuliza. "Jumuia ya Ulimwengu imebaki kupiga makelele mengi na kulaani ushiriano huu. Kwani matokeo ya ushirikiano huo yamekuwa ni kuanzisha kwa viwanda vya kijeshi vya Afrika Kusini vyenye uwezo wa kujitegemea katika utengenezaji wa sikaha za kisasa ambazo wabaguzi huzitumia kuendeshea vitendo vya kikatili dhidi ya wakazi wazalendo wa Afrika Kusini na nchi jirani. Hii inaonesha waziwazi kuwa utawala wa Makaburu hautavunjwa iwapo utaendelea kupata misaada mikubwa kiufundi kutoka nchi hizi za Magharibi. Lililopo sasa ni kwa nchi za Kiafrika na nchi rafiki zilizo tayari kusaidia kuzidisha harakati za ukombozi dhidi ya hawa wabaguzi wa rangi si kwa maneno ila kwa vitendo", Sherrif alisisitiza.

"Wewe unadhani ni vitendo gani vinaweza kusaidia kwani  nchi zetu za Kiafrika kisilaha bado tuko nyuma sana, hivyo kuamua vita dhidi ya Afrika Kusini , yaani vita ya kijeshi kama ulivyosema itakuwa vita dhidi ya nchi za Magharibi vilevile", Veronika aliyasema.

"Kitu muhimu mbali na harakati za kijeshi zinazochukuliwa na wapigania uhuru dhidi ya majeshi ya Makaburu na Rhodesia ni lazima kwa nchi zote za Kiafrika zionyeshe mfano wa kukomesha ushirikiano wa kiuchumi na tawala hizo dhalimu na kuziba njia zote za kuweka raslimali katika uchumi wake. Hii ina maana hata kupiga marufuku makampuni ya kibepari yanayoendesha biashara katika nchi za Kiafrika, lakini vilevile yanaendesha biashara na tawala hizi dhalimu. Kwa kufanya hivi hata nchi za Magharibi zitaelewa msisimamo wetu na ni imani yangu kuwa zitaliangalia suala lote upya na kuweza kuzingatia Azimio la 181".

"Naamini mnaelewa vizuri kabisa kuwa kiuchumi nchini za Magharibi zinatutegemea sana hata kuliko sisi tunavyoweza kuzitegemea. Hivyo jambo lolote la kuwapiga vita kiuchumi lazima itabidi waliangalie kikamilifu", Sherrif alifafanua.

Maudhi yaliyokuwa yameendelea yalizidi kunigisa sana roho. Ilionekana Sherrif alikuwa anaelewa hali halisi ilivyo Kusini mwa Afrika kuliko nilivyomtegemea. Nilifurahi kuwa nilikuwa nimeanza likizo yangu vizuri kwa kuonana na hawa vijana wa Kiafrika wenye fikira za ki maendeleo na kimapinduzi.

Ili kuzidi kupanua mawazo nilimweleza Sherrif, "Katika shughuli zangu za kibiashara hukutana na watu ambao wanatetea kuwa biashara na Afrika Kusini na Rhodesia iendelee. Watu hawa wanabisha wakisema makampuni ya nchi za Magharibi yanayoendesha shughuli zake Afrika Kusini na Rhodesia husaidia kuinua hali ya kazi na maisha ya Waafrika wa nchi hizo. Aijui wewe una maoni gani juu ya sababu hizo?".

"Ndugu Willy madai ya namna hiyo ni bure. Nia ya madai kama hayo ni kuhalalisha vitendo vya uhusiano wake na siasa na siasa ya ubaguzi wa rangi. Hali yote hii inaonyesha jinsi ulivyo unafiki wa siasa ya nchi za Magharibi ya kujishughulisha na haki za binadamu. Lakini kufuatana na mienendo ya kisiasa na kiuchumi utaona waziwazi kuwa siasa yao halisi kwa Afrika ni kinyume na ile wanayoitangaza".

"Jambo hili linathibitishwa na tabia za nchi za Magharibi kutochukua hatua yoyote kali dhidi ya wabaguzi wa rangi. Zaidi ya tote sijui maisha ya watu wanaokandamizwa, kunyanyaswa na kutendewa vitendo vya kikatili yanaweza kuinuliwa namna gani na watu hao hao wanaowakandamiza. Mimi nina imani kuwa ni mara mia uwe huru na masikini kuliko kuwa tajiri na mtumwa", Sherrif alisema na huzuni.

"Baada ya kutembelea sana sehemu hii na kufanya uchunguzi mwingi kama ulivyotueleza hapa, wewe  unahisi hali ya baadaye ya Afrika Kusini itakuwaje?", nilimwuliza.

"Ukweli ni kwamba ufungamano wa walimwengu na watu wa Kusini mwa Afrika unazidi kukua. Watu wa asili wa Afrika Kusini wamefikia hali ya kutovumilia kabisa siasa hiyo ya ubaguzi wa rangi. Jumuia ya ulimwengu kila siku inapiga kelele aina zote za ubaguzi wa rangi zitokomwezwe. Hivyo mgogoro wa kijamii Kusini mwa Afrika ulio juu ya msingi wa tofauti ya kijamii ambao unawanyima walio wengi haki zake, umefikia kiwango cha hatari. Kwa hiyo kwa maoni yangu muda wa tawala hizi dhalimu umebaki mfupi.

Khadija aliyekuwa amenyamaza kwa muda mrefu alimwuliza Sherrif. "Umeeleza maneno yanayotia uchungu sana, kama maneno haya ni kweli, huoni kuwa litakuwa jambo la adhimu kwa nchi huru za Afrika kuungana na kuziangusha tawala hizi dhalimu. Kwanini jambo hili halifanyiki?".

"Kama nilivyokwisha kusema mpenzi, jambo kama hilo si rahisi ingawaje ndio njia pekee ya kuweza kuleta mafanikio haraka. Nitakueleza kwa nini si rahisi. Unyonge wa nchi za Kiafrika unatokana na mgawanyiko wetu. Na mgawanyiko huu umetokana na tofauti zilizopo miongoni mwa nchi za Kiafrika. Nchi hizi zinahitilafiana katika kutafasiri historia, kisiasa na vile vile zinahitilafiana katika viwango na ukubwa wa maeneo ya uchumi. Na sumu kubwa inayoimalisha mgawanyo huu ni ukoloni mamboleo unaoendelea katika nchi nyingi huru za Afrika. Mimi nakubaliana nawe kabisa kuwa tukizingatia umoja, na tushirikiane katika kuwasaidia wapigania uhuru Kusini mwa Afrika kwa hali na mali, na halafu tushirikiane kuzipiga sehemu hizo vita vya kiuchumi, hakika ushindi hauko mbali. Lakini kama nilivyokwisha sema ushindi Kusini mwa Afrika ni dhahiri, na ni jukumu letu sote vijana wa Afrika kujizatiti katika umoja. Na jukumu letu liwe ni kuhskikidha kuwa uhuru Kusini mwa Afrika unakuja upesi".

"Wewe Sherriff, ukiombwa ushike silaha uende ukapigane bega kwa bega na wapigania uhuru utakwenda ?", Veronika alimwuliza.

"Mimi nitakuwa tayari kabisa kwenda. Lakini naamini kushika silaha siyo njia pekee ya kusaidia vita vya ukombozi. Kwa taarifa yako sasa hivi nitaongeza safari zangu Kusini mwa Afrika na kwa kufanya hivi nitaweza kuandika mengi juu ya harakati za ukombozi. Kitu ambacho kitawafumbua wengi macho na kuona haja iliyopo katika kusaidia harakati hizi".

Mara kengele ikalia. Wote tukaangalia saa zetu na kuona kuwa ilikuwa sata kasoro robo. Kwa muda wote huo wa mazungumzo vinywaji vilikuwa vinamiminika sana, hivyo hata mimi nilijisikia napata nishai.

"Hiyo kengele ina maana kuwa tuagize duru ya mwisho ya vinywaji", Veronika alikumbusha.

"Lo, mimi nafikiri siwezi kuchukua zaidi ya hapa, nasikia nishai ya hali ya juu sana", Khadija alilalamika.

Wote tulikubaliana naye kwa kuwa vinywaji vilikuwa vimetuishia na kukubaliana zilikuwa saa za kuondoka.

"Kusema kweli kwa namna fulani tumemdhulumu Willy muda wake mzuri wa kupumzika kwa mazungumzo yasiyo ya kimapumziko. Unajua mtu akiwa katika likizo ya mbali namna hii anahitaji starehe na mazungumzo ya kistarehe. Lakini tumejikuta katika mazungumzo makali sana utafikiri Kamati ya Ukombozi ya OAU. Kwa niaba ya wenyeji wenzangu nakuomba radhi".

"La hasha, Sherriff. Mimi binafsi nimefurahia sana mazungumzo haya. Na kwa muda mrefu nadhani sijakaa na kundi la kufurahisha namna hii. Ni lazima nikiri kuwa nina bahati kubwa kuweza kufahamiana na Vero, na kuwa na urafiki wa haraka namna hii. Na ni matumaini yangu makubwa kwamba likizo yangu itakuwa ya mafanikio sana. Maelezo uliyoeleza hapa ni ya faida sana kwangu kama kijana wa Kiafrika. Kwa taarifa yako hata mimi fikra zangu ni za kimaendeleo na kimapinduzi. Kwa vile na nyinyi nimetambua kuwa mna mawazo ya namna hiyo hiyo, naamini likizo yangu itakuwa ya faida katika kila nyanja".

"Vero, una mpango gani kwa kesho juu ya matembezi ya mgeni wetu?" Sherriff aliuliza.

"Bado, tulikuwa hatujapanga kitu maalum. Lakini ninafikiri kwa kesho itabidi tumtembeze aone mji kwa ujumla. Mipango kamili tutapanga".

"Katika mipango yenu, mimi nitawakaribisha kwa chakula cha mchana nyumbani kwangu", Khadija alisema.

"Na mimi kwa kesho jioni nawakaribisha kwenye tafrija ya karusi ya rafiki yangu. Tafrija itaanza saa moja jioni. Kutakuwa na bendi maarufu kutoka Nigeria, itakuwa tafrija kubwa", Sherriff naye alituambia.

"Msiwe na wasiwasi mipango yote itapangwa", Veronika alijibu.

"Ndiyo sababu sikuchukii Vero, maana kila wakati mambo yako ni chapuchapu. Willy, kweli umepata mwenyeji halisi, nadhani atakuwa mwenyeji wako kwa kila kitu", Sherriff alitania huku akicheka.

"Wewe na maneno yako!" Vero alijibu.

"Kwani si ya ukweli?" Sherriff aliendelea kutania.

"Basi, basi baba imetosha", Veronika alikatisha, wote tukacheka.

Tulimaliza vinywaji, Sherriff na Khadija akasimama ili tuagane.

"Oke Willy, mimi nitakuja kiasi cha saa nne, au itakuwa mapema sana, Vero?".

"Wee, acha utundu wako. Wewe njoo tu utanikuta nami nimefika", Vero alilalamika.

"Sema nitakukuta", alisema Sherriff na kabla Vero hajasema alichotaka kusema akaendelea. "Willy hebu tuongee faragha kidogo".

Tuliondoka tukasimama pembeni kidogo.

"Unajua jila lako nimewahi kulisikia katika mambo ya ukombozi nafikiri, sijui kama unaweza kuwa wewe?".

"La hasha, nafikiri umechanganya majina. Mimi sijawahi kabisa kuhusika na mambo ya ukombozi, siku zote mimi ni mfanyabiashara tu".

"Samahani, ni hilo tu nilitaka kuhakikisha".

Tulirudi hapo mezani tukawapitia wasichana wetu, tukaondoka na kuwasindikiza akiana Sherriff mpaka kwenye gari lao, wakaondoka. Moyoni nilijisikia mtu mwenye bahati sana kwa kujikuta nimepata marafiki wa hali hii katika muda mfupi namna hii, Lakini ni lazima utambue Willy ni mtu mwenye bahati siku zote. Hii ndiyo inaitwa bahati ya kuzaliwa. Na ndiyo Mama Willy alinitoa nayo tumboni.

Tulibaki tumeshikana tukiangalia taa za nyuma za gari yao ikipotea kwenye mtelemko wa mlima Bintumain ikielekea mjini. Wakati wote huo nilikuwa nimeushikilia mkono wa Veronika. Nilikuta nikiuminyaminya lakini yeye alitulia tu kama hasikii.

"Willy na mimi naona niende sasa, saa zimepita sana".

Aliniangalia na macho yake yakamelemeta kwenye taa hafifu zilizokuwa zinatumulika. Kwa mara nyingine nikasikia misisiko ndani ya mwili wangu.

"Sidhani litakuwa jambo la busara kwako kuendesha saa hizi za usiku baada ya kuwa tumekunywa pombe nyingi kiasi hiki".

"Basi nitaacha gari langu hapa nitaagiza teksi".

"Kwani ni lazima uende nyumbani?".

"Wewe unafikiriaje?",

"Mimi naona lingekuwa jambo la maana kama tukikaa pamoja usiku huu tuweze kuelewana zaidi".

"Bado upo siku nyingi hivyo tutapata muda mwingi wa kukaa pamoja na kuelewana zaidi kama unavyoita", Vero alijibu kwa sauti ya mahaba ya kupendeza.

Si kawaida yangu Willy kubembeleza sana msichana hasa akiwa msichana mwenye msimamo kama huyu. Kwani kwa kufanya hivyo unaweza ukaleta kutoelewana naye bure. Ingawaje roho yangu ilikuwa inang'wenya nilijikaza.

"Kama utakavyopenda mama, lakini ningefurahi sana kama ungebaki".

"Hapana Willy, ngoja niende. Nitaendesha tu usiwe na wasiwasi mimi ni mjuzi sana katika udereva. Samahani kama kwa kufanya hivi nitakuwa nimekuudhi".

"Si kitu, unavyopenda wewe mimi nitaridhika.

Niliona hakuna njia zaidi ila kumwacha aende. Nilijua siku zilizokuwa zinakuja urafiki wetu ungekuwa wa kukata na shoka, miye Willy nawajulia sana binadamu hawa.

Nilimsindikiza mpaka kwenye gari lake. Tulipofika tukaegemea kwenye gari kisha tukasimama tumeangaliana. Mara nikashitukia amepitisha mikono yake juu ya shingo yangu. Midomo yetu ikakutana. Ulimi wake wa moto ulipenya mdomoni mwangu na mara tukawa tumeingia katika ulimwengu wa peke yetu. Tulikaa tukibusiana kwa muda kama wa dakika moja, halafu ghafla akaniachia. Akaingia ndani ya gari lake.

"Willy mpenzi, nitakuja kesho asubuhi. Kiasi cha saa mbili, nitakuwa hapa".

"Asante", nilijibu bado nikiwa nimeshikwa na butwaa.

Aliwasha gari moto, akanirushia busu, nami nikalijibu halafu akaondoa gari kwa kasi sana utafikiri anaanza mbio za magari za East African Safari.

Nilisimama hapo nikiliangalia gari mpaka lilipopotea. Kisha niligeuka kuelekea ndani ya hoteli kulala, huku nikijua siku hii sintaisahau maisha mwangu.

Kesho yake niliamka yapata saa moja ya asubuhi. Usiku huo nilikuwa nimelala fofofo shauri ya pombe nilizokuwa nimekunywa.

Nilipoamka nilikwenda maliwatoni halafu nikavaa nguo safi.

Nikatelemka chini ili nikapate kifungua kinywa kwenye chumba cha chakula. Veronika alifika saa mbili kama alivyokuwa ameahidi. Alikuja moja kwa moja chumbani ambako alikuta ninamsubiri.

"Itabidi tumsubiri Sherriff. Isingekuwa hivyo tungeondoka sasa hivi tukaanza matembezi ya mjini", Veronika alinena.

"Hamna tabu, tumsubiri tu".

Tulikaa tukisimuliana maisha yetu ya kazi huku tukimsubiri Sherriff. Naye akawasili hapo saa tatu kama alivyokuwa ameahidi.

"Mbona umekuja peke yako, wapi Khadija?", nilimuuliza.

"Khadija amekwenda kazini, tutaonana mchana, unakumbuka ametukaribisha chakula cha mchana nyumbani kwake?"

"Nafikiri tuondoke sasa", Veronika alishauri.

"Yaa, nafikiri twende. Naona tutumie gari lako maana ni wazi hivyo litatufaa sana kwa kumuonyesha Willy sehemu mbalimbali".

"Hamna tabu".

Wote tulisimama ili tutoke chumbani kuelekea matembezini. Kabla hatujaanza kuondoka mfanyakazi mmoja wa hotelini alibisha hodi kwenye chumba changu. Nilimkaribisha, akaingia ndani maana mlango wa chumba ulikuwa wazi. Alikuwa ameshika bahasha ndogo mkononi mwake.

"Kuna ujumbe wako uliofika sasa hivi kwa njia ya teleksi kutoka Dar es Salaam".

"Asante".

Nilipokea na yeye akaondoka. Nilifungua bahasha nikatoa kikaratasi chenye ujumbe huku Sherriff na Veronika wanikiangalia kwa shauku kutaka kujua ulikuwa ujumbe gani. Ujumbe ulisema.

"MAMA MGONJWA SANA, RUDI HARAKA, FIKA MOJA KWA MOJA HOSPITALI. MASELINA"

Nilihisi jasho jembamba likinitoka maana ujumbe huu ulikuwa na maana kuwa limetokea jambo la haraka ofisini kwetu na nilitakiwa nifike kwa Chifu haraka iwezekanavyo. Nilipitisha karatasi kwa Veronika na Sherriff ambao walisoma na kuonyesha nyuso za huzuni sana.

"Inaonekana sina bahati. Mama yangu anaumwa. Inabidi niondoke leo hii hii kurudi Dar es Salaam.

"Lo, masikini Willy, kwanini Mungu anaruhusu vitu vya huzuni vitokee wakati watu wako katikati ya raha!", Veronika alilalamika.

"Ndivyo maisha yalivyo", Sherriff alijibu kwa sauti kunjufu.

"Itabidi sasa tuache kila mipango. Mnipeleke kwenye ofisi ya ndege nikatayarishe safari.

"Jambo kama hili ni muhimu, hatuna budi kufanya hivyo. Veronika atakupeleka, mimi itabidi nikamweleze Khadija mambo yalivyo halafu tuonane hapa saa tano, maana najua kuna ndege ya saa kumi iendayo London kupitia Roma, Kama una bahati unaweza kupata kiti katika ndege hiyo.

"Bila ya shaka nitapata, maana kwa ajili ya safari zangu mhimu za kibiashara huwa nimenunua tiketi maalum. Kwa hiyo dakika yoyote nikitaka kusafiri lazima nipatiwe nafasi"'

"Basi kumbe hamna tabu", Sherriff alisema.

Tuliondoka, Veronika na mimi tukaelekea ofisi za ndege ya Shirika la ndege la British Caledonian, na Sherrif akaenda ofisini kwa Khadija. Mambo yote yalifanikiwa, Nilipata kiti kwenye ndege ya saa kumi kama Sherriff alivyokuwa amebashiri.

Mnamo saa tano kasoro robo tulikuwa tumerudi hotelini. Nilikwenda mapokezi na kuwashauri kuwa nilikuwa naondoka siku hiyo hiyo kwa hivyo ilinibidi nilipe deni la hoteli kwa siku nilizokuwa nimekaa. Baada ya kulipa deni la hoteli, mimi na Veronika tuliingia baa na kuacha ujumbe mapokezi kuwa Sherriff akija atukute huko.

Sherriff hakufika saa tano kama alivyoahidi, bali alitokea mnamo saa sita, akiwa na uso wenye furaha furaha. Hata kabla hajasema neno nikahisi alikuwa na habari za kumfurahisha.

"Mungu kweli anafanya mambo ya ajabu", Sherrif alisema huku akivuta kiti na kuketi. "Toka hapa nilikwenda ofisini kwa Khadija ili nimweleze mambo yalivyokuwa. Baada ya kufika na kumweleza na yeye kusikitika sana, aliniambia alikuwa amepata simu kutoka kwenye ofisi yetu hapa mjini ikinitafuta kutaka kujua niko wapi maana kulikuwa na ujumbe wangu kutoka kwenye ofisi yetu kuu mjini London. Hivyo alinishauri niende hapo ofisini kwetu. Ofisi yetu ni ndogo sana, ina mfanyakazi mmoja ambaye ni opereta wa teleksi ambayo inaatuwasilisha na ofisi yetu London. Basi aliponieleza hivyo Khadija nikapita ofisini kwetu. Lo, nikakuta ujumbe kuwa ninatakiwa kuondoka kwenda London kwenye ofisi yatu kuu kwani kumetokea kazi mhimu jiji Dar es salaam ambako baada ya kupata maagizo huko London nitatakuwa kwenda Dar es Salaam. Basi mnaona mambo yalivyo!", kinywaji chake kilifika akanywa kidogo kidogo.

"Nilipoona nafasi ya kwenda Dar es Salaam itamfaa Veronika vile vile, nikatuma ujumbe hapo hapo niliruhusiwe kuandamana na Veronika. Jibu nililojibiwa ni "ok" baada ya kupata jibu nimekwenda ofisi ya ndege nikakuta nyingi zimeshaondoka. Kwa bahati na sisi tumepata nafasi kwenye ndege hiyo hiyo Willy atakayoondoka nayo. Kwa hiyo Veronika uko safarini kuelekea London, halafu Dar es Salaam. Mnasemaje?"

Mimi nilichoka kabisa kwa maneno haya.

"Lo, ni furaha iliyoje!", Veronika alijibu kwa furaha isiyo kifani.

Karibu sana Dar es Salaam, maana likizo yetu imeanza upya, sasa si Freetown bali Dar es Salaam. Ninawahakikishia kuwa mtafurahia kazi yenu Dar es Salaam maana itakuwa kazi na dawa.

"Ngoja niende nikajitayarishe basi, tutaonana uwanja wa ndege saa tisa mchana", Veronika aliomba huku akiwa hana hamu na kinywaji tena, maana aliacha bia yake nusu.

Veronika na Sherriff waliondoka kwenda kujitayarisha tukiwa tumekubaliana kuonana uwanja wa ndege saa tisa za mchana.

Ndege iliondoka Freetown saa kumi juu ya alama. Veronika, Sherriff na mimi tulikaa karibu karibu. Niliwapa simu yangu kusudi wafikapo Dar es Salaam wanijulishe, maana mimi nilikuwa nawahi kufika kabla yao. Wao walikuwa wanaeleka kwanza London.

Nilitoa kadi yangu ya kazi nikampa Veronika tulipokuwa karibu kutua mjini Roma, ambapo mimi nilikuwa natelemka na kupanda ndege ya kuelekea Dar es Salaam.

"Ofisi yetu hii" 'African International Agencies' masaa ishirini na nne kuna mtu. Kwa hiyo muda wowote mkitua pigeni simu ofini hapo, mimi nitapata habari mara moja", na tulipotua Roma niliagana nao. Veronika alinisindikiza nje na kunipa busu.

"Dar es Salaam tutafahamiana zaidi", aliniahidi kwa kuninong'oneza.

**************************************************

No comments:

Post a Comment