TAN

TAN

Bayport

Bayport

Kikoa

Kikoa

Myway entertainment

Myway entertainment

FORE PLAN CLINIC

FORE PLAN CLINIC

MPINGA CUP 2016

MPINGA CUP 2016

Mashujaa Fm 89.3, Lindi

Saturday, June 16, 2012

Mbunge aibana serikali muswada wa ushauri

Posted: 14 Jun 2012 11:35 PM PDT

Kocha wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Kim Poulsen akizungumza wakati wa hafla ya kuiaga timu hiyo iliyoondoka leo alfajiri kwenda Msumbiji kucheza mechi ya marudiano ya mchujo wa Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani. (Picha na Charles Lucas)
Posted: 14 Jun 2012 11:38 PM PDT

Na Elizabeth Mayemba

TIMU ya Taifa (Taifa Stars) imeondoka nchini leo kwenda Msumbiji kwa ajili ya mechi yao ya marudiano dhidi ya nchi hiyo 'Mambas' kusaka tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
Mechi  hiyo inatarajia kuchezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa ulioko Zampeto nje kidogo ya jiji la Maputo kuanzia saa 9 mchana kwa saa za huko.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ameitakia kila la kheri timu hiyo ili ifanye vizuri, huku akiwapongeza kwa ushindi katika mechi yao iliyopita dhidi ya Gambia, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Akikabidhi bendera ya taifa kwa Stars, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadik, alisema anaimani timu hiyo itaiwakilisha nchi vyema katika michuano hiyo na Watanzania wapo nyuma yao.
"Mkumbuke kuwa mnakwenda Msumbiji kuiwakilisha nchi, hivyo macho na masikio ya Wanzania wote yapo kwenu kuona mtavuna nini huko, kwa mchezo mzuri mliouonesha mechi iliyopita dhidi ya Gambia bila shaka na huko mtatuwakilisha vizuri," alisema.
Alisema matokeo mazuri waliyoonesha katika mchezo uliopita isiwe ni nguvu ya soda na nidhamu, ambayo wanatakiwa kuionesha huko na ushindi kwao uwe wa kwanza.
Pia Mkuu wa Mkoa huyo alisema kuwa Rais Jakaya Kikwete, ameitakia kila la kheri timu hiyo na kuitaka iwakilishe vyema nchi.
"Wakati nakuja kuiaga timu ya taifa, Rais ametoa salamu zake kuwa anawatakia kila la kheri ili mfanye vizuri na matokeo ambayo yalipita dhidi ya Gambia yamemfurahisha na anawapongeza sana," alisema.
Naye Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen alisema ili kuitoa 'Mambas' kwenye michuano ya Afrika ni lazima timu yake ishinde mechi hiyo.
Alisema maandalizi katika kikosi chake yalikwenda vizuri ingawa ana wachezaji watatu ambao ni majeruhi, kipa Mwadini Ali na mabeki Nassoro Masoud 'Cholo' na Waziri Salum.
Iwapo Taifa Stars itaitoa Msumbiji katika raundi ya mwisho itapangiwa moja kati ya timu 16 zilizocheza Fainali za AFCON zilizofanyika Januari mwaka huu katika nchi za Gabon na Equatorial Guinea.
Katika mechi ya kwanza dhidi ya Msumbiji iliyochezwa Dar es Salaam, Februari 29 mwaka huu timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Posted: 14 Jun 2012 11:32 PM PDT

MBUNGE wa Moshi Mjini, mkaoni Kilimanjaro, Bw. Philemon Ndasambulo (CHADEMA), ameitaka Serikali kulieleza Bunge ni lini italeta muswada wa sheria ya Sera ya Taifa ya Ushauri kwenye Viwanda ili iweze kutumika na kuinufaisha nchi kiuchumi.
Bw. Ndesambulo aliuliza swali hilo bungeni mjini Dodoma jana katika kipindi cha maswali na majibu.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Bw. Stephen Wassira, alisema Serikali ilianza kuandaa mchakato wa sera hiyo ili kuwezesha wataalam elekezi kuishauri Serikali mambo ya kiuchumi na kijamii.
Alisema ulijadiliwa na wadau katika hatua mbalimbali na baada ya kukubaliwa, Aprili 2004 ulipelekwa katika Baraza la Mawaziri.
Baraza hilo lilijadili waraka, kukubalina na kumshauri Rais ili aweze kuusaini na kuwa sera rasmi. Ushauri mwingine waliotoa ili kutekeleza sera hiyo, lazima kianzishwe Chama cha Washauri elekezi ili kitumike kama Sekretarieti ya Baraza la Taifa ambapo Ofisi ya Rais, Mipango na Uwezeshaji, ichukue jukumu la kuandaa mpango mkakati wa sera haraka iwezekanavyo na kuhakikisha inatekelezwa kwa faida ya Watanzania.
Alisema kutokana na mabadiliko ya muundo wa Serikali ambao ulitangazwa Februari 2008, baadhi ya majukumu yaliyokuwa yakisimamiwa na kutekelezwa na Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, yalihamishiwa katika Wizara nyingine.
Aliongeza kuwa, hivi sasa utekelezaji wa sera hiyo unaenda sambamba na Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2008, kwa kuhusisha vyombo vya vitatu ambavyo ni Baraza la Ushauri wa Masuala ya Kazi, Uchumi na Jamii.
Mchakato wa kuandaa rasimu ya sheria ya uanzishwaji Baraza la Kitaifa la Huduma na Ushauri, unafanyiwa kazi pamoja na kupata maoni ya wadau mbalimbali chini ya utaratibu wa Wizara ya Kazi na Ajira.
Kwa kuzingatia maoni ya wadau, Serikali itafanya tathmini ya namna kuendelea na utekelezaji wa sera hiyo.
Posted: 14 Jun 2012 11:30 PM PDT
Posted: 14 Jun 2012 11:28 PM PDT


WAMILIKI wa shule binafsi zisizo za Serikali, wanawajibika kutangaza ajira za walimu kwa njia ya matangazo au nyingine wanazoona zinafaa na kuwaajiri katika shule husika.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bw. Philipo Mulugo, aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Bi. Elizabeth Batenga (CCM).
Bi. Batenga alitaka kufahamu kwanini shule na vyuo vya Serikali havina walimu wa kutosha lakini katika shule na vyuo binafsi kuna walimu wa kutosha, je, waanawapata wapi?
Akijibu swali hilo, Bw. Mulugo, alisema sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 1995, inafafanua wazi kuwa utoaji elimu nchini utakuwa kwa ushirikiano wa Serikali na taasisi au watu binafsi.
Alisema shule zisizo za Serikali, zinapata walimu kwa kutangaza ajira kupitia matangazo na kupata walimu kutoka vyuoni au nje ya nchi kwa kuhakikisha wanatimiza masharti ya ajira.
Aliongeza kuwa, baada ya kufungua milango ya ajira kwa nchi za Afrika Mashariki, walimu kutoka nchi jirani watapata ajira katika shule zisizo za Serikali hivyo upo uwezekano mkubwa wa shule za Serikali kupata walimu wa kutosha.
Akizungumzia suala la utoaji na ukaguaji maendeleo ya elimu kwenye shule na vyuo vya Serikali na binafsi, Bw. Mulugo alisema   jambo hilo linasimamiwa na Wizara yake kupitia idara na taasisi zake ikiwemo ya ukaguzi wa shule, Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi pamoaja na Tume ya Vyuo Vikuu.
Posted: 14 Jun 2012 11:27 PM PDT

MBUNGE wa Ole, Zanzibar Bw. Rajabu Mbaruk Mohamed (CUF),  amemtaka Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda kutoa tamkoa la kuunda Tume Huru ambayo itafanya uchunguzi wa kina ili kubaini watu waliosababisha vurugu zilizotokea hivi karibuni visiwani Zanzibar zikihusishwa na kundi la Uamsho.
Bw. Mohamed aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma jana waakati akiuliza swali kwa Bw. Pinda na kudai kuwa yupo tayari kuunda tume huru iweze kufanya kazi na wahusika ili watakaobainika wachukuliwe hatua.
Akijibu swali hilo, Bw. Pinda alisema Mei 26-27 mwaka huu, vurugu kubwa zilitokea Zanzibar zikihusishwa na kikundi kimoja kilichosajiliwa ili kueneza dini ya Kiisilam mwaka 2001 lakini kikaingia katika masuala mengine yasiyohusiana na dini hiyo.
Alisema kikundi hicho kilianza kupinga Muungano baada ya kuanza mchakato wa Katiba Mpya na kufanya maandamano ambayo polisi hawakuwa na taarifa nayo.
Bw. Pinda alisema, kikundi hicho kinapaswa kudhibitiwa ili kutoa fursa ya kufanikisha mchakato wa uandikaji Katiba Mpya kwani Serikali ikiachia jambo hili bila kuchukua hatua, kukundi hicho kinaweza kuleta madhara makubwa.
Aliongeza kuwa, kutokana na vurugu hizo baadhi ya watu waliohusika wamekamatwa akiwemo kiongozi wao mmoja ambaye ni Shekhe Juma Mussa Issa na kudai kuwa taarifa za kiusalama zinasema kikundi hicho hakitaki Muungano uliopo.
Alisema ombi la kuundwa tume hutu ili kuchunguza chanzo cha vurugu hizo ni zuri na kubainisha kuwa, lazima lifikishwe katika Serikali ya Zanzibar ndipo hatua zingine zichukuliwe.
Posted: 14 Jun 2012 11:35 PM PDT
Mchezaji Goodluck Mabiriki wa Ilala (kulia) akigombea mpira na mshambuliaji wa timu ya Lindi, Khalfan Malibiche wakati wa fainali za michuano ya Airtel Rising Stars inayoendelea kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Posted: 14 Jun 2012 11:21 PM PDT

Na Mwandishi Wetu

TIMU za soka za Mkoa wa Mbeya za wanaume na wanawake zimejihakikishia kucheza nusu fainali ya michuano ya kukuza vipaji wenye umri chini ya miaka 17 ya Airtel Rising Stars inayotarajiwa kuanza leo kwenye Uwanja wa Karume, Jijini, Dar es salaam.
Timu hizo zimefuzu kucheza nusu fainali hiyo baada ya kumaliza katika makundi yao zikiwa zinaongoza.
Nayo Arusha imefanikiwa kupitisha timu zake zote za wanaume na wanawake baada ya kushika nafasi ya pili katika kundi A nyuma ya Mbeya.
Mbali na timu hizo, zingine zilizofuzu kwa upande wa wanaume ni Temeke ilioonesha kuwa tishio katika michuano hiyo kwa kufunga idadi kubwa ya mabao.
Ilianza kwa kuisambaratisha Lindi kwa mabao 12-2 kabla ya kuichakaza tena Ilala kwa mabao 3-0. Wakati wanaume wamefuzu, timu yao ya wanawake inasubiri matokeo kati ya Ilala na Lindi zilizotarajiwa kucheza jana.
Hata hivyo, kwa upande wa wanaume timu ya mwisho itakayoungana na timu hizo inategemea matokeo ya mechi za mwisho za makundi zilizotarajiwa kuchezwa baadaye jana, sambamba na kwa upnade wa wanawake.
Katika mechi zilizochezwa juzi asubuhi timu ya wanawake ya Temeke iliichapa Ilala kwa mabao 2-0.
Kwa upande wa wanaume, Temeke iliendeleza mwendo wake wa kugawa dozi baada ya kuibugiza Ilala kwa mabao 3-0. Goli la kwanza la washindi lilifungwa na Khalid Mwenda dakika ya 28, la pili liliwekwa kimiani na Paulo Balama dakika ya 43 na la mwisho lilpatikana dakika ya 87 kupitia kwa mshambuliaji wake hatari, Bakari Ally.
Katika mechi nyingine iliyochezwa jioni, timu ya wanawake ya Arusha iliifunga Kinondoni kwa mabao 2-0, kupitia kwa Anitha Antony dakika za pili na 35. Mechi ya mwisho ilizikutanisha Kinondoni na Arusha ambapo zilitoka sare ya mabao 2-2. Wafungaji wa Arusha  ni Nazir Abdul dakika za 22 na 82, wakati yale ya Kinondoni yaliwekwa kimiani na Omar Ramadhani na Jarufu Lutonga katika dakika ya 55
Posted: 14 Jun 2012 11:20 PM PDT

Na Zahoro Mlanzi

KAMPUNI ya Bantu inatarajia kuandaa tamasha la utoaji tuzo za filamu nchini (Bantu Film Awards), litakalofanyika kwa mara ya kwanza Julai jijini Dar es Salaam likiwa na lengo la kutambua kazi za wasanii na kuzitangaza kimataifa.
Akizungumzia tamasha hilo Dar es Salaam jana, Ofisa wa kampuni hiyo, Stewart Kambona alisema maandalizi ya tamasha hilo yanaendelea vizuri na kwamba wapo katika mazungumzo na wadau mbalimbali wa sanaa, wakiwemo waadhiri wa vituo vya sanaa kutoka katika vyuo vikuu mbalimbali nchini.
Alisema tamasha hilo linatarajiwa kufanyika mwezi ujao Dar es Salaam, ambalo litasaidia kutoa motisha kwa wasanii wanaochipukia na hata wale wakongwe katika fani hiyo kuongeza bidii katika kuandaa kazi zao.
"Unajua hili tamasha litakuwa ni chachu ya wasanii kuzidi kupata mafanikio kwani wakiona mwenzao leo amepewa tuzo kutokana na kazi yake fulani, nina hakika atajipanga ili mwakani naye apewe tuzo, tunatarajia tuzo hizi kufanyika kila mwaka," alisema Kambona.
Alisema kwa kuanzia kutakuwa na kategoria 27 ambazo alizitaja baadhi yake kuwa ni tuzo ya muongozaji bora, mtunzi na mpiga picha ambapo watahakikisha wanatoa fursa kwa wadau kutoa michango yao, ili kusiwepo na maneno ya hapa na pale baada ya kutoa tuzo hizo.
Naye Wasanii Jacob Stephen 'JB' na Irene Uwoya wakizungumza kwa niaba ya wasanii wenzao kwa nyakati tofauti, waliishukuru kampuni hiyo kwa kuwa na wazo hilo ambalo wanaamini litasaidia kuinua tasnia ya filamu hapa nchini ndani na nje ya nchi.
JB alisema wamekuwa wakifanya sanaa kwa muda mrefu, lakini hakukuwa na kitu cha kuwatia moyo ila hivi sasa kila mmoja ataongeza ubunifu wake katika kuandaa kazi ili mwisho wa mwaka wapate tuzo.
Naye Uwoya alisema tuzo hizo kwao ni changamoto ya kuzidi kufanya vitu vizuri zaidi, kwani ana imani tuzo hizo zitawatambulisha kimataifa kupitia kazi zao na mwisho wa siku mafanikio ya fani hiyo yataongezeka.
Posted: 14 Jun 2012 11:36 PM PDT
Wanyange wanaowania taji la Redd's Miss Kigamboni 2012 wakiwa katika mazoezi jana, mashindano hayo yanatarajia kufanyika leo katika Ukumbi wa Navy Beach, Kigamboni. (Picha na Victor Mkumbo)
Posted: 14 Jun 2012 11:17 PM PDT

Na Victor mkumbo

MSHINDI wa kwanza wa taji la urembo la Kitongoji cha Kigamboni mwaka huu 'Redd's Miss Kigamboni City 2012', atazawadiwa sh. 500,000 katika mashindano yatakayofanyika leo katika ukumbi wa Navy Beach, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, mratibu wa mashindano hayo, kutoka kampuni ya K&L Media Solutions, Somoe Ng'itu alisema maandalizi yote yamekamilika  na warembo wote wako tayari kwa kinyang'amyiro hicho.
Mratibu huyo alisema mshindi wa pili atazawadiwa  sh. 350,000, wa tatu sh. 300,000, wa nne na watano wataondoka na cha sh. 200,000 kila mmoja na wengine saba waliobaki watapatiwa kifuta jasho sh. 150,000 kila mmoja.
Alisema mgeni rasmi katika mashindano hayo atakuwa ni diwani wa kata ya Kigamboni, Dotto Mawa ambaye ametoa mchango mkubwa katika kufanikisha kinyang'anyiro hicho.
Aliongeza kuwa ili kuboresha shindano hilo bendi ya muziki wa dansi ya FM Academia maarufu Wazee wa Ngwasuma na msanii na mchekeshaji mahiri hapa nchini, Mpoki watatumbuiza kwenye kinyang'anyiro hicho.
"Tumeboresha zaidi mashindano ya Redd's Miss Kigamboni kwa mwaka huu ambapo warembo wote wana sifa na tunatarajia kuwapata wawakilishi wazuri katika mashindano ya Redd's Miss Temeke pamoja na Redd's Miss Tanzania 2012," alisema.
Aliwataja warembo watakaochuana kuwa ni Susanne Jeremiah, Agness Goodluck, Elizabeth Boniface, Dorothea Kessy, Esther Albert, Edda Silyvester, Sophia Martin, Doreen Kweka, Khadija Kombo, Linnah David, Rosemary Peter na Winnie Karaya.
Aliwashukuru wadhamini ambao wamejitokeza kusaidia mashindano hayo ambao ni Redd's, Dodoma Wine, Hope Country Hotel, Screen Masters, Nobro Collections, Times FM na Kitwe Traders.
Aliongeza kuwa warembo watakaoshika nafasi tatu za juu wataungana na wenzao kutoka vitongoji vya Kurasini na Chang'ombe, ili kuwania taji la Kanda ya Temeke baadaye mwaka huu.
Posted: 14 Jun 2012 11:16 PM PDT

Na Mhaiki Andrew, Songea

SHIRIKA lisilokuwa la Kiserikali la Good Hope Sports Club la mkoani Ruvuma lina mikakati ya kutoa mafunzo ya ukocha na waamuzi kwa wanafunzi wa shule za Sekondari, ikiwa na lengo la kuibua na kuendeleza michezo mkoani hapa.
Akizungumza mjini hapa juzi Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Joseph Mapunda alisema mafunzo hayo yatawalenga wanafunzi wa shule hizo kidato cha kwanza hadi cha tatu ili kuwapatia taaluma ya michezo, badala ya kutegemea makocha kutoka nje ya mkoa kufundisha.
Alisema shirika hilo, limejiwekea malengo endelevu katika kusaidia kuinua michezo ambapo alidai baada ya kukamilika kazi hiyo kwa shule za sekondari pia mafunzo hayo yatatolewa kwa vijana wa shule za msingi kuanzia darasa la tano, ili wajengeke na uelewa kabla ya kuchaguliwa kuanza kidato cha kwanza.
Mapunda alisema kabla ya kuanza kwa utoaji wa mafunzo ya ukocha kwa wanafunzi hao, bodi ya shirika hilo imekutana na kuweka mikakati itakayowezesha kufanikiwa kwa kupendekeza shule za kuanzia, badala ya shule zote kwa pamoja kwa kutumia kanda za kielimu mkoani Ruvuma.
Alisema katika mapendekezo yao, wamekubaliana wataanzia na shule za sekondari katika wilaya mbili za Songea na Namtumbo kabla ya kuamia wilaya nyingine za Nyasa, Mbinga na Tunduru kwa mafunzo hayo ya ukocha na waamuzi ambapo yamelekezwa kutolewa kwa michezo 11 ikiwemo soka, netiboli, ngumi, riadha na mpira wa wavu.
Mkurugenzi huyo alisema programu hiyo ya mafunzo itaanza kutolewa baada ya na kuvutiwa na kituo cha michezo cha Twalipo cha Jijini Dar es Salaam, kilivyofanikiwa kwa kiasi kikubwa kutoa mafunzo ya ukocha na waamuzi kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 20.
Posted: 14 Jun 2012 11:13 PM PDT

Na Victor Mkumbo

MSANII wa muziki wa kizazi kipya nchini Isihaka Nassoro 'Dogo Aslay', anatarajia kuzindua albamu yake ya kwanza Juni 24 mwaka huu katika Ukumbi wa Dar Live, Mbagala.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Meneja wa kundi la TMK Wanaume Family, Said Fella alisema Dogo Aslay anatarajia kuzindua albamu hiyo, kitabu pamoja na filamu ambapo zote amezipa jina la Naenda Kusema.
Alisema albamu hiyo ina jumla ya nyimbo 10 ambayo ameirekodia katika studio ya Poteza Records chini ya mtayarishaji Suresh pamoja na Alow Nem.
Fella alisema katika uzinduzi huo kutakuwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya, ambao watamsindikiza Aslay.
Alisema wasanii watakaoimba jukwaa moja na Aslay ni pamoja na Mh. Temba, Bi. Cheka, TMK Wanaume Family, Ize Man, Ommy Dimpoz na Mwana FA.
"Tumeandaa onesho maalumu kwa ajili ya Aslay kutambulisha albamu, kitabu pamoja na filamu ambapo pia kutakuwa na burudani ya aina yake kutoka kwa wasanii mbalimbali," alisema.
Alizitaja baadhi ya nyimbo zilizopo katika albamu hiyo kuwa ni Nakusemea, Niwe Nawe aliyoimba na Mh. Temba, Kikombe aliyomshirikisha Ferouz, Umbea ambaye amemshirikisha Chege, Utajuta, Mapendo, Nastrago aliyoimba na Mkubwa na Wanawe pamoja na Hawakai.

Bajeti 2012/13 kutabiri mengi *Wengi wahofia utekelezwaji wake *Lipumba alia na ugumu wa maisha

Posted: 14 Jun 2012 01:03 AM PDT
Na Godfrida Jola

WAKATI bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2012/13, ikitarajia kusomwa leo mjini Dodoma, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, amesema bajeti ya mwaka 2011/2012 ambayo ilikuwa sh. trilioni 13.5, haijatekelezwa.
Alisema vipaumbele vya bajeti hiyo, vilikuwa na kasoro nyingi pamoja na wafadhili kutotoa fedha walizoahidi.
Prof. Lipumba aliyasema hayo Dar es Salaam jana alipozungumza na Majira kwa njia ya simu juu ya maoni yake kuhusu bajeti iliyopita na inayotajariwa kusomwa leo.
Alisema bajeti iliyopita imeongeza ukali wa maisha ya Watanzania mara mbili zaidi kutokana na ongezeko la matumizi ya ndani.
Aliongeza kuwa, asilimia 39 ya bajeti yote ilikuwa katika sekta ya maendeleo ambayo hadi kufikia Machi mwaka huu, asilimia 32 pekee ndiyo iliyotekelezwa.
“Bajeti ya kesho (leo), maendeleo yametengewa sh. trilioni 4 na bilioni 500 wakati mwaka 2011, ilikuwa trilioni 4 na bilioni 900 hivyo imepungua na haiwezi kufikia wanapotaka, hii inatokana na Serikali kunyimwa fedha na wafadhili,” alisema.
Alisema bajeti hiyo ilishindwa kumaliza tatizo la ajira kwa vijana kwa kutumia sekta binafsi, kufufua viwanda vilivyopo na kuboresha upatikanaji wa nishati ya umeme ili kuongeza uzalishaji viwandani na kuongeza ajira.
“Bajeti ilishindwa kufanikiwa kutokana na utegemezi wa fedha za wafadhili ambao waligoma kutoa fedha na kuipa Serikali wakati ugumu hivyo kuyumba katika matumizi yake.
“Tatizo la msingi Serikali kutokuwa na dira kwa sababu inafuata malengo ya milenia na utekelezaji wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA 2), ambavyo vyote vimepitwa na wakati, muhimu kubuni njia nyingine ili kupiga hatua ya maendeleo,” alisema Prof. Lipumba.
Alisema Waziri wa Fedha kwa sasa, Dkt. William Mgimwa hajapata muda wa kutosha kuipitia bajeti iliyopita na hana utaalamu kuhusu uongozi hivyo hawezi kubaini kasoro zilizopo.
“Dkt. Mgimwa hana utaalamu wa kutosha wa 'fiscal policy', ni mwezi mmoja tu, toka aingie katika Wizara hii, atawezaje kujua kinachoendelea,” alihoji.
Wakati huo huo, Watanzania wengi wamekuwa na shauku ya kutaka kujua vipaumbele vilivyotolewa katika bajeti iliyopita vimefanyiwa kazi kwa kiwango gani.
Bajeti iliyopita, ilitaja mambo manne ya msingi ili kupunguza makali ya maisha na kutenga asilimia 14 ya bajeti yote kwa ajili ya kulipa deni la Taifa.
Mambo hayo ni pamoja na maboresho ya sheria za kodi,  kuongeza nguvu za uwekezaji katika sekta ya umeme, kupunguza bei ya mafuta ya petroli, matumizi ikiwamo ukubwa wa misafara ya safari za viongozi na kuongeza fedha katika sekta tano.
Pia bajeti hiyo ilitoa vipaumbele katika sekta ya miundombinu ya barabara, reli, bandari na mkongo wa mawasiliano wa Taifa ambao ulitengewa sh. bilioni 2,781.4.
Katika mchanganuo huo, nishati na madini ilitengewa sh. bilioni 539.3 ambayo kwa kiasi kidogo imepunguza tatizo la mgawo wa umeme.
Maji ilitengewa sh. bilioni 621.6  bilioni ikilinganishwa na sh. bilioni 397.6 mwaka 2010/11, sawa na ongezeko la asilimia 56, kilimo na umwagiliaji sh. bilioni 926.2 ikilinganishwa na sh. bilioni  903.8 mwaka 2010/11, sawa na ongezeko la asilimia 2.5.
Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi walisema wanatarajia kupata unafuu wa ukali wa maisha kwa bajeti ya leo kutokana na hali iliyopo kuzididi kupoteza mwelekeo.
Walisema ni muhimu bajeti ya leo ikaweka vipaumbele ambavyo vitatekelezeka ila kuepuka lawama baada ya kuisha kwa mwaka wa fedha.
“Mwaka 2011 Serikali ilisema itasaidia kuweka mikakati ya kupunguza ukali wa maisha lakini imekuwa tofauti maana maisha yamepanda maradufu na kutuacha njia panda,” alisema Bi. Lenarda Christian, mkazi wa Dar es Salaam.
Alisema bajeti ya leo inatakiwa kuonesha namna ya utekelezaji wa malengo yaliyokusudiwa na pia iendane na mipango ya Serikali ya  ukusanyaji wa mapato na matumizi sahihi ya fedha.
Bw. George Martine, mkazi wa Magomeni alisema kutokana na bei ya mafuta na bidhaa kupanda mara kwa mara, imechangia kuongeza ukali wa maisha kwa wananchi.
Alisema Serikali inapaswa kuwaangalia wananchi wake hasa wa kawaida kwa kupunguza bei za nafaka ili kuwanusuru. “Hivi sasa vyakula vimepanda bei maradufu hivyo kusababisha maisha kuwa magumu,” alisema.
Bei za vyakula zilianza kupanda nchini mwishoni mwa 2011 ambavyo ndiyo hutumiwa na watu wengi ukiwemo mchele, maharage, sukari, unga na viungo vya mboga.
Mchele katika masoko ya Dar es Salaam umepanda na kufikia sh.2,300 hadi 2,500 kwa kilo moja, maharage sh. 2,300, 2,500 hadi 2,600 ambapo awali yalipatikana kwa sh.2,000 hadi Sh. 2,200 kwa kilo, unga umefikia sh. 1,000 hadi Sh.1,200 kwa kilo ambapo bei ya awali ilikuwa 800 hadi sh. 900 kwa kilo.
Posted: 14 Jun 2012 01:02 AM PDT 
 Na Peter Mwenda 

MBUNGE wa Mwibara, mkoani Mara, Bw. Kangi Lugola, amemtaka aliyekuwa Waziri wa Fedha, Bw. Mustapha Mkulo, alithibitishie Bunge juu tuhuma alizozielekeza kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), na kudai imehongwa na Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC).
Bw. Lugola aliyasema hayo Bungeni Mjini Dodoma jana baada ya kuomba mwongozo wa spika na kudai kuwa, katika kikao cha Bunge lililopita, alimtaka Bw. Mkulo athibitishe kauli aliyowahi kuitoa bungeni akidai kamati hiyo ilihongwa sh. milioni 60 na CHC ili kupindisha ukweli lakini hakuwepo bungeni.
Alisema katika tuhuma hizo, Bw. Mkulo alimtaja Mwenyekiti wa POAC, Bw. Zitto Kabwe kuwa ameweka rehani ubunge wake kwa ajili ya rushwa hivyo kuishuka hadhi kamati hiyo.
“Kwa vile Bw. Mkulo yupo hapa, naomba Naibu Spika atoe mwongozo ili afute kauli yake ili kuweka kumbukumbu sawa au alete ushahidi bungeni,” alisema.
Katika majibu yake, Naibu Spika Bw. Job Ndugai alisema amepokea jambo hilo na atalitolea mwongozo kwa wakati muafaka.
Posted: 14 Jun 2012 01:10 AM PDT

Naibu Kamishina wa Polisi (DCP), Issaya Mungulu, akiwaonesha waandishi wa habari, picha ya mtuhumiwa wa ugaidi, raia wa Ujerumani, Emrah Erdogan, au kwa jina lingine Abdulrahaman Othman (24), aliyekamatwa nchini akituhumiwa kuwa mpiganaji wa kundi la Al-Qaeda aliyehusika katika matukio mbalimbali ya ugaidi, Dar es Salaam jana. (Picha na Prona Mumwi)
Posted: 14 Jun 2012 12:46 AM PDT

Na Salim Nyomolelo

JESHI la Polisi nchini, linamshikiria raia wa Ujerumani aliyefahamika kwa jina la Bw. Emrah Erdogan, ambaye aliyekamatwa jijini Dar es Salaam, Juni 10 mwaka huu.
Bw. Erdogan ambaye kwa jina lingine anaitwa 'Abdulrahaman Othman', inadaiwa ni mfuasi wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Kamishna wa jeshi hilo, Bw. Isaya Mngulu, alisema kijana huyo ana umri wa miaka 24.
Alisema Bw. Erdogan anadaiwa kushiriki mapambano mbalimbali nchini Afghanistan na hivi karibuni alishirikiana na Kikundi cha Al-Shabab kufanya ugaidi
Aliongeza kuwa, vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kumuhoji wakishirikiana na mataifa mengine.
“Tunashirikiana na nchi za Uganda, Kenya na Ujerumani kumhoji ili kubaini taarida zake, baada ya hapo tutatoa taarifa kwa Watanzania,” alisema Bw. Mngulu.
Hata hivyo, Bw. Mngulu alisema jeshi hilo linatambua mchango wa wananchi ambao ndio uliosaidia kukamatwa kwa mtuhumiwa na kuongeza kuwa, hiyo ndio dhana halisi ya ulinzi shirikishi.
“Jeshi la Polisi linawahakikishia wananchi kuwa, vyombo vya ulinzi na usalama vipo imara kukabiliana na vitisho vyote vya uhalifu na ugaidi, natoa wito kwa wananchi waendelee kutupa ushirikiano katika vyombo vyetu ili kuimarisha amani na utulivu.
Posted: 14 Jun 2012 12:41 AM PDT

Na Mwandishi Wetu

MWENYEKITI wa Muungano wa Vyama vya Wazalishaji na Wachapishaji Maarifa (KOPITAN), Bw. Abdullah Saiwaad, amesema kanuni na muongozo wa tozo kwa kazi zinazorudiwa utasaidia kuliongozea Taifa mapato.
Bw. Saiwaad aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika warsha ya siku moja kuhusu kanuni ya urudufishaji na hakimiliki na kusisitiza kuwa, kanuni hizo zitawasaidia waandishi na wachapishaji wa kazi za maandishi.
“Kanuni hizi zitasaidia ukusanyaji wa kodi kwa Taifa na wenye hakimiliki kunufaika kutokana na kazi zao ambazo muda mrefu zimekuwa zinarudufiwa kinyume na sheria,” alisema.
Katika warsha hiyo, njia mbalimbali za ukusanyaji mapato za kurudufu kazi zenye hakimiliki zilielezwa pamoja na namna ya kutekeleza mifumo hiyo.
Mifumo ya ukusanyaji mirabaha kwa kiasi kikubwa imeletwa ili  kulinda na kuzipa hadhi kazi za wazalishaji ambao ni waandishi na wachapaji mbalimbali.
Aliongeza kuwa, licha ya kuwepo kwa wimbi kubwa la kurudufu kazi za sanaa, Chama cha Hatimiliki nchini COSOTA kinashirikiana beka kwa bega na KOPITAN kuhakikisha mfumo na muongozo wa kanuni hizo ambazo Serikali inatarajia kuzitoa, utakuwa daraja bora la mafanikio ya kuhakikisha kazi za wasanii na waandishi zinalindwa ipasavyo.
“Tuna nia ya kuwa na mfumo bora ambao kila mtu atanufaika, kuja kwa mfumo huu ni mafanikio bora ambayo yatanufaisha watu wote,” alisema Ofisa Mtendaji wa COSOTA, Bw. Yustus Mkinga.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Afrika wa Shirikisho la Kimataifa la Haki za Urudufishaji (IFRRO), Bw. Greenfield Chilongo, aliwataka wamiliki wa haki za kazi mbalimbali za kimaandishi na sanaa nyinginezo, kusimamia haki za umiliki wa kazi zao ili kuzuia urudufishaji wa kazi hizo unaofanyika bila kufuata sheria na kanuni za hakimiliki.
Posted: 14 Jun 2012 01:10 AM PDT

Mbunge wa Tabora Mjini Bw. Aden Rage (kushoto) akimsikiliza Naibu Waziri wa Maji Dkt Binilith Mahenge mara baada ya kipindi cha maswali na majibu Bungeni Mjini Dodoma jana. (Picha na Vicent Tiganya-Maelezo)
Posted: 14 Jun 2012 12:22 AM PDT

Na Willbroad Mathias

TATIZO la ubovu wa miundombinu katika viwanja vya ndege na ukosefu wa mafunzo kwa marubani, linadaiwa kuwa chanzo kikuu cha ajali nyingi za ndege zinazotokea nchini.
Wadau wa sekta ya usafiri wa anga nchini, waliyasema hayo Dar es Salaam jana katika mkutano wao uliolenga kujadili na kutafuta njia mbadala ya kuimarisha usalama wa safari za ndege.
Wakichangia mada inayohusu changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo, wadau hao walisema ajali nyingi za ndege nchini, zinasababishwa na ufinyu wa miundombinu katika viwanja.
Walisema pamoja na kuboreshwa kwa njia za ndege zinazotumika  wakati wa kuruka au kutua, viwanja vingi nchini vimezungukwa na mazingira yasiyo salama.
Akiwasilisha mada katika mkutano huo, Mkaguzi Mkuu wa Ajali za Ndege nchini, kutoka Wizara ya Uchukuzi, Bw. John Nyamwihura, alisema ipo haja ya kuboreshwa miundombinu hiyo ili kuleta ufanisi.
Akizungumzia tatizo la uhaba wa mafunzo ya marumbani nchini Bw. Nyamwihura alisema sekta hiyo kwa sasa inakabiliwa na changamoto hizo baada ya Serikali kujitoa tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Alisema awali Serikali ilikuwa ikibeba jukumu la kugharamia masomo ya marubani tofauti na sasa.
“Hali hii inachangia kuwa na marubani wengi vijana tena wa kigeni tofauti na Tanzania ambayo marubani wengi wazee, enzi ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere, tulikuwa na utaratibu wa kusomesha marubani katika nchi mbalimbali,” alisema Bw.  Nyamwihura.
Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Chama cha Wasafirishaji wa Anga (TAOA), Bw. Eva Jackson, alisema ipo haja ya kuwepo  uwazi katika kuchunguza vyanzo vya ajali za ndege nchini.
“Hivi sasa ukienda katika taarifa za Mamlaka ya Anga (TCAA),  hakuna taarifa za matukio ya ajali au ya usalama licha ya kuripotiwa zaidi ya mara 10,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Bw. Fadhili Manongi, alisema ajali za ndege nchini zimepungua ukilinganisha na miaka ya nyuma.
Alisema mwaka huu kumetokea ajali moja tofauti na miaka iliyopita ambayo zilikuwa zikitokea mara kwa mara.
Posted: 14 Jun 2012 12:21 AM PDT

Na Anneth Kagenda

KAMANDA wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini,  Mohamed Mpinga, amekiri kuwepo vitendo vya uchakachuaji leseni ambavyo ni moja ya sababu inayochangia ongezeko la ajali nchini.
Akizungumza na Majira kwa njia ya simu Dar es Salaam jana, Kamanda Mpinga alisema kuwa madereva wengi wanadanganya kuwa wamesea udereva katika vyuo mbalimbali kikiwemo VETA.
“Kuna matukio ya kufoji vyeti ambayo yamekuwa yakijitokeza katika vyuo mbalimbali kikiwamo VETA, utakuta mtu anafanya udanganyifu na kudai amesema katika chuo hiki wakati katika orodha ya waliohitimu hayumo.
“Tumekuwa tukikemea vitendo hivi na kuvitaka vyuo husika kutuletea orodha ya waliomaliza vyuoni baada ya wanafunzi kumaliza masomo yao ila vitendo hivi vitakoma,” alisema.
Alisema wale wananaondelea na tabia hiyo wakikamatwa sheria itachukua mkondo wake ambapo baadhi ya watu waliozungumza na Majira wakiwamo wamiliki wa vyuo vya udereva, walidai vitendo hivyo bado vinaendelea kwa madereva wengi kupata vyeti bila kuvisomea vyuoni.
Posted: 14 Jun 2012 01:11 AM PDT
Baadhi ya wanahabari wa vyombo mbalimbali kutoka Mikoa ya Iringa,Mbeya na Dar es salaam ambao walishiriki katika utafiti na ukibua kero mbalimbali za wananchi wa kata ya Ijombe wakiwa pamojana Waraghbish wa Mtandao wa Jinsia TGNP hivi karibuni.
Posted: 14 Jun 2012 12:12 AM PDT

Na Kassian Nyandindi, Namtumbo

MADIWANI wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, wametakiwa kuibua miradi ya kimaendeleo ambayo itakuwa na tija kwa wananchi.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Bw. Steven Nana, aliyasema hayo juzi mjini Namtumbo, mkoani hapa wakati akifafanua mambo mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri hiyo.
Alisema hivi sasa halmashauri hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi hivyo ni vyema madiwani wawe na upeo mpana wa kutafuta njia mbadala za kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Bw. Nana aliongeza kuwa, madiwani wana nafasi kubwa katika hilo kama watashirikiana na wananchi kwenye kata zao badala ya kufanya maamuzi mbalimbali bila kuwashirikisha Alisema halmashauri nyingi nchini zinashindwa kujiendesha kwa sababu ya malumbano yasiyo ya lazima miongoni mwao hasa kwa watendaji hivyo kukwamisha maendeleo.
Posted: 14 Jun 2012 01:11 AM PDT
Samaki waliovuliwa katika nyavu sizizoruhusiwa.Utungaji sheria ndogo za kudhibiti uvuvi haramu zitasaidia kustawisha uvuvi endelevu na wenye tija.(Picha na Mtandao wetu).
Posted: 14 Jun 2012 12:05 AM PDT

Na Heckton Chuwa, Same

BENKI ya Ushirika mkoani Kilimanjaro (KCBL), imeanzisha huduma ya akiba kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 18 ili waweze kupata uelewa wa huduma za kibenki.

Meneja Masoko wa benki hiyo Bw. Ahsanterabi Msigomba, aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wa Vyama vya Ushirika vya Msingi na wale wa Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya za Mwanga na Same (VUASU).
“Huduma hii inalenga kuwajengea watoto mazingira ya kuanza kuwa na uelewa wa kujiwekea akiba tangu utotoni,” alisema Bw. Msigomba na kuongeza kuwa, benki hiyo pia imeshirikiana na Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom kwa kuanzisha huduma ya M-PESA na wao kuwa wakala wa huduma hiyo.
“Huduma hizi nyongeza ya huduma zingine tunazozitoa ambazo ni pamoja na zile za Western Money Union Transfer na stakabadhi ya mazao ghalani ambazo zimekuwa na mafaniko makubwa,” alisema.
Bw. Msigomba alisema mpango wa stakabadhi ya mazao ghalani umeendelea kuwa na mafanikio makubwa tangu uanzishwe kutokana na huduma wanazotoa kwa wakulima ambao hawana rasilimali zinazowapa uwezo wa kukopa fedha kwa ajili ya kilimo.
Kwa upande wake, Ofisa Masoko wa benki hiyo Bi. Regina Ndesanjo, alitoa wito kwa wanachama wa benki hiyo kukamilisha hisa zao ili zifikie kiwango cha milioni moja ambacho kimewekwa ili waweze kushiriki Mkutano Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu.

Posted: 14 Jun 2012 01:11 AM PDT
Posted: 13 Jun 2012 11:42 PM PDT


MIGOGORO ya ardhi imekithiri katika maeneo mbalimbali nchini, kusababisha umwagaji damu, kuhatarisha amani na utulivu tulionao kutokana na umuhimu wake.
Ni wazi kuwa migogoro hiyo imegawanyika katika makundi mawili, moja likihusisha wakulima na wafugaji, jingine linahusisha wananchi na wawekezaji.
Kimsingi migogoro inayohusisha wananchi na wawekezaji inachangia wananchi kuichukia Serikali yao na kuharibu mali.
Katika maeneo mengi yaliyohusishwa na migogoro ya ardhi, tayari kumetokea vurugu zilizosababisha uvunjifu wa amani na kusababisha vifo vinavyoweza kuzuilika.
Vurugu hizo pia zimetokea katika maeneo ambayo wananchi walioheshimiana muda mrefu, wameamua kuvunja udugu wao kwa sababu kasi ya Serikali kumaliza migogoro husika haiendani na tatizo lililopo.
Hatua zinazochukuliwa na Serikali ni zile za kujaribu kutuliza hasira za wahusika jambo linaloweza kutuletea maafa makubwa baadaye.
Sisi tunasema kuwa, migogoro mingi ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji inatokana na makundi hayo kutotengewa maeneo.
Mtu akipata eneo mahali popote anajenga, kulima au kufuga kwa sababu Serikali haijachukua hatua stahiki ya kutenga maeneo na matumizi yake.
Ili kuepuka mapigano ya mara kwa mara na kutunza mazingira, umefika wakati wa Serikali kutenga maeneo ya kilimo, ufugaji, makazi ya watu na yale ya wazi.
Maofisa ardhi ni miongoni mwa watu wanaochangia migogoro hiyo kwa kuuza maeneo zaidi ya mara moja hivyo kusababisha jamii kugombana hata kuchukiana.
Sababu kubwa inayochangia maofisa hao kusababisha migogoro hiyo ni tamaa ya fedha mbali ya kujua wazi kuwa wanachokifanya ni kinyume na maadili ya kazi zao.
Ardhi ni mali ya mwananchi na Serikali hivyo kila upande unapaswa kushirikishwa wakati wa kuuza au kumtafuta mwekezaji.
Umefika wakati wa maofisa hao kubadilika na kufanya kazi kwa mujibu wa sheria ili kupunguza migogoro hii ambayo inaweza kuharibu historia ya nchi yetu.
Posted: 14 Jun 2012 01:11 AM PDT

Mfanyabiashara wa kuku (jina halikufahamika) akiwalinda huku akisoma gazeti,kama alivyokutwa katika foleni ya kuingia ndani ya Soko la Kisutu Barabara ya Bibi Titi, Dar es Salaam jana. Kuongezeka kwa wafanyabiashara kwenye soko hilo kunasababisha msongamano. (Picha na Charles Lucas)
Posted: 13 Jun 2012 11:28 PM PDT

Na Suleiman Abeid, Shinyanga

WAKULIMA wa zao la pamba mkoani Shinyanga, wametakiwa kuuza pamba yenye ubora na kushirikisha wadau ili kudhibiti uchafu wa zao hilo unaofanywa kwa makusudi na baadhi ya wakulima wanapokwenda kuiuza sokoni.
Wito huo umetolewa juzi na Meneja Uendeshaji wa Kiwanda cha Kuchambua na Kusindika zao hilo cha Afrisian Ltd, kilichopo mjini hapa, Bw. Hrishikesh Katre, katika hafla fupi ya kukabidhi zawadi kwa vituo vya ununuzi wa pamba vilivyofanya vizuri msimu uliopita.
Alisema kama wakulima na wadau wengine watadhibiti uchafu wa zao hilo unaofanywa kwa makusudi na baadhi ya wakulima ili kuongeza uzito wa pamba wanapokwenda kuiuza sokoni thamani yake katika soko la dunia itaongezeka.
Aliongeza kuwa, baadhi ya wakulima wamekuwa na tabia ya kuweka michanga, maji au magadi katika pamba kabla hawajaenda kuiuza sokoni kitu ambacho mbali ya kushusha ubora wake, pia husababisha hasara kwa kampuni zinazoinunua na serikalini.

“Suala la kurejesha ubora wa pamba yetu lipo mikononi mwetu sisi wenyewe wakulima na wadau wa zao hili, tukidhibiti uchafuzi huu pamba ambayo itanunuliwa itakuwa safi na ubora wake utakuwa mzuri hivyo bei katika soko itapanda na wakulima kufaidika,” alisema Bw. Katre.
Alisema kampuni hiyo imeanzisha utaratibu wa kuvizawadia vituo vyake vya ununuzi ambavyo hununua pamba safi isiyo na uchafu pamoja na kuwapa motisha watu wanaosimamia vituo hivyo kuhakikisha wananunua pamba safi.
Katika hafla iliyofanyika juzi kampuni hiyo ilitoa zawadi mbalimbali kwa wahasibu wa vituo hivyo ikiwemo pikipiki mbili aina ya Toyo, baiskeli mbili aina ya Phoenix, majembe manne ya kukokotwa na ng’ombe na simu tano za mkononi aina ya Nokia vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 4.8.
Bw. Katre alivitaja vigezo vinavyomfanya Mhasibu aweze kushinda na kupewa zawadi kuwa ni pamoja na kufikia lengo la makisio ya ununuzi wa pamba katika kituo chake.
Vigezo vingine ni uaminifu anapokabidhi pamba yake kiwandani na kuhakikisha hanunui pamba iliyochanganywa na mchanga, kokoto au kuwekwa maji ya magadi.
Aliongeza kuwa, kampuni hiyo inanunua pamba katika mikoa ya Tabora, Shinyanga, Simiyu, Mwanza na tayari imeingia mikataba na vikundi 256 vya wakulima ambavyo vitapatiwa pembejeo za kilimo  katika msimu wa mwaka 2012/2013.