TAN

TAN

Bayport

Bayport

Kikoa

Kikoa

Myway entertainment

Myway entertainment

FORE PLAN CLINIC

FORE PLAN CLINIC

MPINGA CUP 2016

MPINGA CUP 2016

Mashujaa Fm 89.3, Lindi

Friday, June 15, 2012

Mwanamke auawa katika fumanizi


Posted: 12 Jun 2012 11:48 PM PDT

Na Faida Muyomba, Geita                

MKAZI wa Kijiji cha Mwagimagi, Wilaya ya Geita, mkoani Geita, Bi. Dome Shaban (35), ameuawa kwa kupigwa na mumewe baada ya kumfumania akifanya mapenzi na mwanaume mwingine.

Akizungumza na waandishi wa habati, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Leonard Paulo, alisema tukio hilo lilitokea Juni 11 mwaka huu, saa nane usiku na kumtaja mtuhumiwa wa mauaji hayo kuwa ni Bw. Faida Anthony (45), ambaye ni mume wa mwanamke huyo.

Alisema mwanamke huyo alifumaniwa akiwa na mwanaume mwingine ambaye jina lake halikufahamika wakifanya mapenzi chumbani wakati mumewe hayupo.

“Mtuhumiwa aliporudi nyumbani aligonga mlango na kukuta mkewe akifanya mapenzi na mwanaume mwingine ambaye alifanikiwa kukimbia na hadi sasa hajulikani jina lake na mahali anapoishi,” alisema Kamanda Paulo.

Aliongeza kuwa, mtuhumiwa alichukua kitu chenye ncha kali na kumchoma sehemu ya jicho la kulia la kushoto kabla ya kumpiga sehemu mbalimbali za mwili hadi kusababisha kifo chake.

Alisema mtuhumiwa alitoroka baada ya mauaji hayo ambapo Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka.
Posted: 12 Jun 2012 11:47 PM PDT

Na Salim Nyomolelo

SERIKALI imeanza kuchukulia hatua kwa taasisi, mashirika na watu mbalimbali wanaotumikisha watoto walio chini ya miaka 18 na kuwakosesha haki zao za msingi ikiwemo ya kupata elimu.

Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dkt. Makongoro Mahanga, aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika kilele cha Siku ya Kimataifa ya kupiga vita utumikishwaji watoto iliyoandaliwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO).

Alisema tayari hatua za kisheria zimechukuliwa kwa watu wanaotumikisha watoto walio chini ya miaka 18, ambao  walichukuliwa na kupewa haki zao za msingi ikiwamo elimu.

Aliongeza kuwa, suala la malezi, matunzo na kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vinavyolenga kuhujumu haki zao ni jukumu la wadau wote kutokomeza vitendo hivyo.

“Utumikishwaji watoto katika kazi hatarishi ni hujuma kwa haki za mtoto kuishi, kukosa muda wa kupumzika, malezi bora, kucheza  na kupata elimu,” alisema Bw. Mahanga

Alisema utumikishwaji watoto ni tatizo la kitaifa na kimataifa, ambapo kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na ILO mwaka 2010, zinaonesha watoto milioni 215 wanatumikishwa katika sekta mbalimbali duniani kote.

“Katika Afrika nchi zilizo katika Jangwa la Sahara, zinakadiriwa kuwa na watoto milioni 65 wanaotumikishwa katika kazi za hatari, upande wa Tanzania kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa mwaka 2005/2006, asilimia 18.7 ya watoto wenye umri kati ya miaka mitano hadi 17, wanatumikishwa katika shughuli mbalimbali,” alisema Dkt. Mahanga.

Aliongeza kuwa, Serikali kwa kushirikiana na wadau imeandaa na imeanza kutekeleza mpango kazi wa kitaifa wenye lengo la kutokomeza utumikishwaji watoto.

Mpango huo umelenga kutimiza malengo ya milenia ifikapo mwaka 2015 ambapo Serikali imefanikiwa kuandaa orodha ya kazi hatarishi ambazo hazipaswi kufanywa na watoto chini ya umri wa miaka 18.
Posted: 12 Jun 2012 11:52 PM PDT
Mtoto ambaye jina lake halikupatikana akiangua kilio baada ya karanga na mayai aliyokuwa akiuza kwenye ufukwe wa Bahari ya Hindi eneo la Kawe kumwagika kutokana na upepo makali kama alivypnaswa na kamera yetu.Tukio hilo lilitokea jana ikiwa ni Siku ya Kupinga Utumikishwaji kwa Watoto Duniani yenye kauli mbiu "Haki za binadamu na usawa katika jamii tokomeza utumikishwaji wa watoto". (Picha na Blog ya Immatukio).
Posted: 12 Jun 2012 11:37 PM PDT
Na Godwin Msalichuma, Mtwara

WATUMISHI wawili wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, wamefikishwa mbele ya Hakimu Mkazi, Bi. Agnes Futakamba, wa Mahakama ya Wilaya hiyo wakituhumiwa kwa kosa la ubadhilifu wa sh. milioni 12.32 zilizotolewa kwa ajili ya kuendesha mafunzo ya makuzi na malezi ya mtoto.
Washtakiwa hao ni Bw. Hassan Mwakipa ambaye ni Ofisa Tabibu Msaidizi na Mhasibu Bw. Absolum Ntakandi ambaye hakuwepo mahakamani ambao wankabiliwa na mashtaka 15.

Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. Sospeter Tyeah, alisema washtakiwa wote wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Juni 11-16, 2009.
Alisema makosa hayo yamegawanyika katika maeneo matatu, ambayo ni kula njama za kumdanganya mwajiri wao na kubadilisha matumizi ya fedha kwa manufaa yao binafsi, kugushi nyaraka na kuhujumu uchumi.
Bw. Tyeah alisema katika kosa la kwanza, washtakiwa wanadaiwa
kutengeneza nyaraka za malipo ya washiriki 25 wa mafunzo ya makuzi na malezi ya mtoto Juni 11, 2009 na kila mmoja kulipwa sh. 320,000.
Kosa la pili, katika kipindi hicho washtakiwa wanadaiwa kutumia karatasi zisizo na tarehe kuwalipa washiriki saba sh. 450,000 kila mmoja maelezo ambayo ni ya uongo.
Mashtaka mengine ni kumlipa Bi. Elizabeth Macha, sh. 560,000 kwa madai ya kuhudhuria mafunzo hayo kama mwezeshaji na kuandaa stakabadhi namba R07584 ya Januari, 4, 2010.
Stakabadhi hiyo ilieleza kuwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo alimlipa Mkurugenzi wa Chuo cha Ushirika, tawi la Mtwara, sh. 129,000 kama gharama za ukumbi.
Bw. Tyeah ambaye alitumia zaidi ya dakika 20 kusoma tuhuma hizo, alidai washtakiwa walitumia tiketi ya ndege PW/MQQB7 ya Juni 9, 2009 wakidai ilitumiwa na Bi. Elizaberth Macha kwa ajili ya safari ambayo gharama yake ni sh. 368,000.
Stakabadhi nyingine haikuwa na tarehe ikionesha Mkurugenzi wa halmashauri hiyo alimlipa sh. 750,000, Mkuu wa Chuo cha Ushirika kwa ajili ya ukumbi.

Shtaka lingine ni kuwepo risiti inayoonesha Juni, 12, 2009,
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo amemlipa mtu ambaye hakutajwa jina sh. 320,000 ili kununua karatasi kwa ajili ya kuendesha mafunzo hayo.

Bw.  Tyeah aliieleza mahakama kuwa washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya kugushi nyaraka, kubadilisha matumizi ya fedha na kuisababishia halmashauri hasara ya sh. milioni 12.32.
Posted: 12 Jun 2012 11:35 PM PDT
Rais waZanzibar na Mwenyekiti wa Balaza la Mapinduzi, Dkt.Ali Mohamed Shein, alipokua akizungumza na wahariri na wahandishi wa habari wa vyombo vya habari mbalimbali vya Bara naVisiwani, kuhusu vurugu za kundi la uhamsho zilizotokea visiwani humo kwa siku tatu mfululizo (Juni 26,27 na 28 mwaka huu).Mazungumzo hayo yalifanyika mjini Zanzibar katika ukumbi wa Ikulu hivi karibuni ambapo Serikari ilisisitiza vurugu hizo kusitishwa mara moja.
Posted: 12 Jun 2012 11:26 PM PDT

Na Zahoro Mlanzi

KATIKA kile kinachoonekana kuguswa na sakata la usajili la beki wa timu ya Taifa (Taifa Stars) na Simba, Kelvin Yondani, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga, amesema suala hilo lina mwisho wake kwani chombo husika kitalifanyia kazi pale muda utakapofika.

Beki huyo hivi sasa amekuwa gumza si katika vyombo vya habari hata katika baadhi ya mitaa nchini kutokana na namna ambavyo inadaiwa kusajiliwa na Yanga akitoroshwa kambini usiku.

Kutokana na tukio hilo, uongozi wa Klabu ya Simba, ilitishia kuishtaki Yanga kwa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kutokana na kushindwa kufuata taratibu husika.

Akijibu swali kuhusu sakata hilo Dar es Salaam jana, Tenga alisema Yondani hajatoroshwa kama inavyodaiwa ila anachofahamu ni kwamba beki huyo ni mtu mkubwa ambaye anaweza kuamua lolote, hivyo hakutoroka ila aliondoka kambini.

"Mimi ninadhani tuna mambo mengi ya kufanya kuliko kuanza kuzungumzia hili la Yondani, hiki ni kipindi cha usajili la lolote linaweza kuzungumzwa, si kitu cha ajabu mchezaji kutoka timu moja kwenda nyingine," alisema Tenga na kuongeza;

"Ila hapa tatizo ni kwamba ametokaje kambini, je alipewa ruhusa na viongozi wake au alijiondokea tu na hilo tumewaachia viongozi wake walishughulikie na litakapokamilika watatupa majibu ya hatua gani wamechukua."

Alisema usajili una taratibu zake na muda wake hivyo kama mchezaji akiwa na mkataba atacheza lakini asipokuwa nao hawezi kucheza na kwamba ndio maana suala hilo la usajili lipo mikononi mwa klabu zenyewe.
Alisema ana imani muda ukifika hakuna shaka chombo kinachohusika kitalifanyia kazi na mwisho wa siku itajulikana atachezea klabu ipi lakini yanayoendelea hivi sasa ni 'unazi' wa mashabiki wa klabu hizo.

Aliongeza kutokana na tukio hilo, hivi sasa wameingia mikataba maalum na wachezaji wao ambao utakuwa ukiwaelekeza taratibu za kambi, hivyo mchezaji akienda kinyume na taratibu hizo hatua za kuchukuliwa zitakuwa wazi.
Mbali na hilo, Tenga aliipongeza timu ya Taifa (Taifa Stars) kwa ushindi walioupata wa mabao 2-1 dhidi ya Gambia na kwamba ameomba kikosi hicho kilicho na vijana wengi kilelewe ili baadaye ilete matunda kwa taifa.
Alisema amekoshwa na kiwango kilichooneshwa kwani hakuaimini kama wangeshinda katika mchezo huo lakini kutokana na kujituma katika dakika zote 90 ndivyo zilizosababisha kupata matokeo mazuri.
Posted: 12 Jun 2012 11:25 PM PDT

Na Victor Mkumbo

ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa timu ya Taifa (Taifa Stars),  Marcio Maximo, ameshindwa kuja nchini kama ilivyopangwa kutokana na kumalizia majukumu yake ya kuifundisha Democrata F.C ya Mjini Rio de Jeneiro, Brazil.
Kocha huyo alitarajiwa kutua nchini jana mchana kwa ajili ya kuja kusaini mkataba na mabingwa wa Kombe la Kagame, Yanga.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa timu ya Yanga, Luois Sendeu alisema kocha huyo ameshindwa kuja kama walivyopanga baada ya kutokea dharula na sasa atatua nchini mwishoni mwa wiki hii.
Alisema sababu kubwa iliyomfanya kocha huyo kushindwa kuwasili jana, ni kutokana na timu anayoifundisha kwa sasa ya Democrata F.C kukabiliwa na mchezo mgumu Jumamosi.
"Maximo tayari amekwishatumiwa tiketi ya safari ya kuja hapa nchini, ameshindwa kuwasili leo (jana) kutokana na Klabu yake anayofundisha kukabiliwa na mchezo mgumu,"
Sendeu alisema kuwa Marcio mara baada ya kuwasili nchini atafanya mazungumzo na Uongozi wa Klabu ya Yanga ikiwemo kusaini Mkataba na Klabu ya Yanga kabla ya kuanza kazi ya kukinoa kikosi hicho.
Wakati gazeti hili, likienda mitamboni lilipata taarifa kwamba timu hiyo haipo tayari kumuacha kirahisi kocha huyo, hivyo hawezi kuja nchini mpaka baadhi ya vitu waviweke sawa.
Posted: 12 Jun 2012 11:52 PM PDT
Posted: 12 Jun 2012 11:23 PM PDT

TATIZO la mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini, linachangia kurudisha nyuma maendeleo ya elimu.
Takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi zinathibitisha kuwa tatizo hili limekuwa likiongezeka siku hadi siku hasa baada ya kuanzishwa shule za kata.
Pamoja na shule hizo kupunguza tatizo la wanafunzi kukosa nafasi za masomo, bado zinakabiliwa na changamoto nyingi.
Miongoni mwa changamoto hiyo ni tatizo la mimba kwa wanafunzi ambao wengi wao hulazimika kukatisha masomo, uhaba wa vifaa, vyumba vya madarasa, walimu na madawati.
Tafiti mbalimbali zimebaini kuwa, tatizo la mimba kwa wanafunzi hasa wa sekondari ni kubwa na linagusa hisia za kila mpenda maendeleo  lakini jamii kubwa bado haijahamasika kutoa ushirikiano wa karibu kwa vyombo vya dola ili kuwafichua wahusika wa vitendo hivyo.
Baadhi ya wazazi hupokea rushwa kutoka kwa watuhumiwa ili wasifikishwe katika vyombo vya sheria na kuchukuliwa hatua stahiki ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia za aina hiyo.
Sisi tunasema dhamira yetu ni kuona wazazi wanashirikiana na vyombo hivyo kuhakikisha watuhumiwa wanakamatwa ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Kama jamii itaona umuhimu huu, Tanzania yenye wasomi wazuri waliobobea katika fani mbalimbali itawezekana na maendeleo yatakuwa kwa haraka.
Kitendo cha jamii kuendelea kuwaficha wahusika wa vitendo hivi, kinarudisha nyuma juhudi za Serikali na wadau wa elimu kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu bora.
Imani yetu ni kwamba, uwajibikaji wa viongozi wa vyama na Serikali unahitajika kwa kuhamasisha jamii iboreshe maendeleo ya elimu hasa kwa mtoto wa kike na kukomesha tatizo la mimba.
Umefika wakati wa wanafunzi wetu, kupewa elimu ya kujitambua na kufahamu wajibu walionao kwa jamii na Taifa ili waweze kujithamini na kuepuka vishawishi vinavyoweza kusababisha wapate mimba au kuacha shule.
Elimu ni nyenzo muhimu kwa maendelo ya Taifa lolote Duniani kwani mapinduzi mengi ya maendeleo, hutegemea kiwango cha elimu kwa jamii husika.
Posted: 12 Jun 2012 11:13 PM PDT

Na Sophia Fundi, Ngorongoro

MAMLAKA ya Hifadhi ya Ngorongoro, mkoani Arusha,  imewakamata watu wanne wanaodhaniwa kuwa majangili ambao huwinda wanyama kwa kuwapa sumu katika msitu wa mamalaka hiyo ulioko eneo la Kambi ya Simba, wilayani Karatu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Meneja Huduma za Uhifadhi wa mamlaka hiyo, Bw. Amiyo Amiyo, alisema watu hao walikamatwa juzi, saa ya nne asubuhi katika Msitu wa Sahata.

Alisema watu hao walikuwa na maboga 10 ambayo ndani yake waliyaweka sumu ya kuulia wanyama mbalimbali hasa tembo.

Aliongeza kuwa, hivi sasa majangili wamebadili mbinu ya kuwinda wanyama wakitumia sumu aina ya “aldicarb” ambayo kwa jina jingine hujulikana kama “temk”, kwa mujibu wa uchunguzi wa Mkemia Mkuu wa Serikali.

Bw. Amiyo alisema sumu hiyo ipo kwenye kundi la “Carbametes”, ambayo huathiri mfumo wa ufahamu wa mnyama kama wataila hivyo kusababisha kifo chake.

Katika tukio hilo, majangili hao walikutwa wakilinda maboga waliyotega msituni ili yasiliwe na wanyama wengine zaidi ya tembo ambapo kutokana na hali hiyo, mamlaka imelazimika kuimarisha ulinzi katika misitu.

“Kutokana na doria tunayoifanya kila siku, tumefanikiwa kukamata majangili hawa na kukuta mizoga ya tembo wawili ambao tayari walikuwa wametolewa meno,” alisema.

Alisema majangili hao wanafahamika kwa majina ya Bw. John Lohay (62),  Bw. John Amisi (27), Bw. Isaya Arusha (36), Bw. Roman Amsi (23) wote wakazi wa Kambiya Samba, wilayani Karatu na wamekabidhiwa kwa Jeshi la Polisi.

Aliongeza kuwa, Februali mwaka huu mamlaka hiyo ilifanikiwa kukamata watu wawili katika Msitu wa Mangola Juu wilayani Karatu wakiwa na matikiti maji 60 ndani ya msitu huo.

Alisema matikiti hayo yalikuwa na sumu ya iina hiyo na tayari wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya mjini Karatu.

“Kimsingi majangili wamebuni mbinu mpya ya kuwatega wanyama na kuwaua kwa kutumia sumu, tutahakikisha ulinzi unaimarishwa dani ya misitu yetu ili kupambana na hawa magangili,” alisema.
Posted: 12 Jun 2012 11:12 PM PDT

Na Anneth Kagenda

MAMLAKA ya Usafirishaji wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) inashikilia daladala zaidi ya 126 kwa kukutwa na makosa mbalimbali, yakiwemo ya kutoa lugha ya matusi, kupandisha nauli holela na mengine kutokuwa na leseni.
Taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari Dar es Salaam jana na kusainiwa na Ofisa Uhusiano wa SUMATRA Bw. David Mziray, ilieleza kuwa katika kipindi cha Mei na Juni, 2012 mamlaka ilikamata  ya daladala zenye  makosa mbalimbali, huku wamiliki wa mabasi hayo wakitozwa faini kati ya sh 100,000 na sh 250,000.

Alisema daladala nyingi zilikamatwa kwenye mkosa ya kutokuwa na leseni, kughushi nyaraka za Serikali, kuiba njia, kutokuwa na tiketi kutovaa sale, kupakia eneo ambalo si la kitu na mengine.

Bw. Mziray alisema kutokana na hali hiyo mmiliki ambaye basi lake litabainika na makosa hayo atachukuliwa hatua za kisheria.

"Pamoja na kulipa faini hiyo mmiliki atatakiwa kusitisha mkataba na kumbadilisha dereva wa basi husika ndipo aruhusiwe kuendelea na utoaji huduma ya usafiri," alisema.
Posted: 12 Jun 2012 11:11 PM PDT

Posted: 12 Jun 2012 11:09 PM PDT

Na Victor Mkumbo

MNYANGE atakayeiwakilisha Tanzania katika mashindano ya urembo ya dunia mwaka huu anatarajiwa kupatikana Jumamosi.

Mwakilishi huyo atapatikana katika mashindano yaliyopewa jina la Redd's Miss World Tanzania yatakayofanyika katika Ukumbi wa 327 Club jijini.

Akizungumza na Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Lino Agency ambao ndio waandaaji wa mashindano ya urembo nchini, Hashim Lundenga alisema mashindano hayo yanatarajia kushirikisha jumla ya warembo 10.

Alisema warembo 10 ndio waliothibitisha kushiriki katika mashindano hayo ambaye mmoja wao ndio ataiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Miss World yatakayofanyika Agosti, mwaka huu nchini China.

Lundenga alisema kuwa wameamua kuchukua warembo waliowahi kushiriki katika mashindano ya Miss Tanzania katika miaka iliyopita, kutokana na mabadiliko ya ratiba ya mashindano kwani awali yalikuwa yanafanyika Desemba.

"Tumeamua kuchukua warembo ambao walishawahi kushiriki katika mashindano ya Miss Tanzania miaka iliyopita kwa kuwa mashindano yetu huwa yanaanza Mei na kumalizika Septemba," alisema.

Lundenga alisema mshindi katika mashindano hayo anatarajiwa kuzawadiwa sh. milioni 10 pamoja na kufanyiwa maandalizi yote ya kwa ajili ya matayarisho ya safari.

Naye Meneja wa kinywaji cha Redd's, Victoria Kimaro, alisema wamejiandaa vizuri na mashindano hayo ambapo wanatarajia kuwa watapata mwakilishi mzuri.

Alisema kuwa shindano hilo litakuwa kwa ajili ya watu maalum ambao wataalikwa na kutakuwa na burudani ya aina yake.
Posted: 12 Jun 2012 11:08 PM PDT
Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino Agency, Hashim Lundenga (kushoto), akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) Dar es Salaam jana kuhusu shindano la Redd's Miss World Tanzania litakalofanyika Jumamosi. Kulia ni Meneja wa kinywaji cha Redd's, Victoria Kimaro (Picha na Victor Mkumbo)
Posted: 12 Jun 2012 11:04 PM PDT
Na Daud Magesa, MWANZA

BENDI mbili kongwe za Muziki wa Dansi zenye upinzani wa jadi, DDC Mlimani Park (Sikinde) na Msondo Ngoma, zinatarajia kutoa burudani katika maadhimisho ya sherehe za miaka mitano tangu kuanzishwa kwa  klabu ya starehe ya Villa Park Resort.

Sherehe hizo zitahusisha michezo ya soka, muziki wadansi, taarabu na disco zitafanyika kuanzia Juni 14 hadi 16, mwaka huu jijni.

Akizungumza na gazeti hili jana kuhusu sherehe hizo, Meneja wa hoteli ya Villa Park Resort, Shijani Mtunga, alisema sherehe hizo zimelenga kuwakumbuka wadau wanaofanya nao biashara na kujumuika nao ili kurudisha fadhila kwao.

Alisema kutokana na wadau hao kuwaunga mkono, ili kusherehekea vizuri wamewaandalia burudani mbalimbali za soka, muziki wa dansi, taarabu na disco kwa kila mtu.

Alisema wapenzi wa muziki wa dansi, watapata burudani ya muziki huo kutoka kwa Msondo Ngoma na Sikinde, zitakapopambana Ijumaa, zikisindikizwa na bendi mwenyeji ya Super Kamanyola, ambapo Jumamosi itakuwa ni mapumziko na fainali itafanyika Jumapili.

Alisema ufunguzi wa bonanza hilo utafanyika Alhamisi kwa msanii, Jokha Kassim maarufu kama Kanga Moko, atachengua kwa kutoa burudani ya muziki wa taarabu na Ijumaa kutakuwa na disko.

“Bonanza hili la miaka mitano ya Villa Park, si kucheza tu bali pia kufanya mazoezi ili kujenga afya.Kauli mbiu yake ni kula ni lazima, michezo ni afya," alisema Mtunga.

Posted: 12 Jun 2012 11:03 PM PDT


Na Zahoro Mlanzi

WAREMBO 12 wanaotarajia kuwania taji la kitongoji cha Kigamboni, mwaka huu 'Miss Kigamboni City 2012', leo wanatarajiwa kufanyiwa usaili kwa ajili kumpata mshindi wa shindano hilo litakalofanyika Ijumaa kwenye Ukumbi wa Navy Beach, Dar es Salaam.


Akizungumza Dar es Salaam jana, Mratibu wa shindano hilo, kutoka Kampuni ya K&L Media Solutions, Somoe Ng'itu, alisema maandalizi ya zoezi hilo yamekamilika na wanachosubiri ni siku ya shindano ifike.

Alisema kitongoji hicho kina warembo wenye sifa na wanaojiamini ambao wamepania kurudisha taji la Miss Tanzania kwenye Kanda ya Temeke.

Aliongeza ili kuboresha shindano hilo Bendi ya Muziki wa Dansi ya FM Academia 'Wazee wa Ngwasuma' na msanii na mchekeshaji mahiri hapa nchini, Mpoki watatumbuiza kwenye kinyang'anyiro hicho.

"Tunawaomba wadau wa sanaa ya urembo kufika kushuhudia mrembo wa Kigamboni atakavyopatikana, ni Kitongoji kilichoko sehemu pekee hapa nchini, hivyo ni vizuru kushuhudia shindano hilo," alisema Somoe.

Aliwataja warembo watakaochuana ni Susanne Jeremiah, Agness Goodluck, Elizabeth Boniface, Dorothea Kessy, Esther Albert, Edda Silyvester, Sophia Martin, Doreen Kweka, Khadija Kombo, Linnah David, Rosemary Peter na Winnie Karaya.

Aliwashukuru wadhamini ambao wamejitokeza kusaidia shindano hilo ambao ni Redd's, Dodoma Wine, hoteli ya Hope Country, Screen Masters, Global Publishers, Nobro Collections, Times FM na Clouds FM.

Aliongeza kuwa warembo watakaoshika nafasi tatu za juu kutoka katika shindano hilo wataungana na wenzao kutoka vitongoji vya Kurasini na Chang'ombe ili kuwania taji la Kanda ya Temeke baadaye mwaka huu.

No comments:

Post a Comment