TAN

TAN

Bayport

Bayport

Kikoa

Kikoa

Myway entertainment

Myway entertainment

FORE PLAN CLINIC

FORE PLAN CLINIC

MPINGA CUP 2016

MPINGA CUP 2016

Mashujaa Fm 89.3, Lindi

Wednesday, June 13, 2012

KUTOKA KATIKA MITANDAO MBALIMBALI YA MAGAZETI YA MAJIRA

Posted: 28 May 2012 01:01 AM PDT
Diwani wa kata ya msongola ambaye pia ni Mwenyekiti wa Huduma za Uchumi za Jamii wa Manispaa ya Ilala, Bi.Angelina Malembeka (katikati) akipiga makofi pamoja na Mratibu wa Benki za Wananchi Vijijini (VICOBA) Tanzania, Bw.Aldo Mfinde, kulia na Mwenyekiti wa kikundi cha Mlimani Vicoba cha Ukonga jeshini, Bi.Shia Simba, wakati wa uzinduzi wa kikundi hicho, Dar es Salaam juzi. (Picha na Charles Lucasa)


Na Amina Athumani

LIGI ya Taifa inayoshirikisha mabingwa wa mikoa inaanza kutimua vumbi leo kwenye vituo vya Kigoma, Musoma na Mtwara.

Akitoa ratiba hiyo Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma, Flamingo ya Arusha itacheza na Forest ya Kilimanjaro saa 8 mchana wakati saa 10 jioni ni Ashanti United ya Ilala na Polisi ya Mara.

Alisema kituo cha Kigoma leo kina mechi moja  kati ya Mwadui ya Shinyanga na JKT Kanembwa ya Kigoma itakayochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika kuanzia saa 10 kamili jioni.

Alisema Tenende ya Mbeya na Kurugenzi ya Iringa ndizo zitakazoanza saa 8 mchana kwenye Kituo cha Mtwara na kufuatia na mechi kati ya Mpanda Stars ya Rukwa na Ndani ya Mtwara kuanzia saa 10 kamili jioni ambapo mechi hizo zinachezwa katika Uwanja wa Umoja.



Msanii AT kutoka Zanzibar akitumbuiza jukwaani wakati wa shoo maalum ya Washindi wa Tuzo za Kili Music zilizofanyika juzi kwenye Uwanja wa Umoja,Mtwara.


Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Ndege nchini ATCL Bw. Paul Chizi amesema idadi ya abiria wa shirika  hilo imezidi kuongezeka baada ya wananchi kuonesha uzalendo na imani kwa kampuni hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi huyo ilieleza hatua hiyo inatokana na mpango walionao wa kujizatiti  ili kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya usafiri wa anga kupitia mpango wa maendeleo wa miaka mitano wa shirika hilo.

Bw. Chizi alisema tangu uzinduzi wa safari za Dar es Salaam-Kilimanjaro-Mwanza wiki moja iliyopita kwa kutumia ndege ya aina ya Boeing 737-500, kampuni yake imekuwa ikijaza abiria takribani 106 katika kila safari kwa siku tatu mfulilizo hali ambayo inaashiria kuwa wananchi wameanza kuwa na imani na huduma zinazotolewa na shirika lake.

 “Ndege yetu kwa takribani siku tatu zilizopita imekuwa ikijaza abiria  katika safari zote za Dar es Salaam-Kilimanjaro-Mwanza . Sikujua kuwa tutakuwa na uwezo wa kurejea na kupata mapokezi ya namna hii kwa haraka kutokana na kuwa kuna watoa huduma wengine katika njia hii,"alisema Bw.Chizi.

“Baada ya wananchi kuonesha imani na uzalendo,tutaendelea na kuongeza nguvu zetu katika kutoa huduma zetu kwa wakati na kwa bei nafuu. Nawaomba wananchi kuendelea na uzalendo wanaouonesha kwa faida ya kampuni yetu na nchi nzima kwa ujumla,” aliongeza.

Bw. Chiza alisema kuwa kurudi kwa huduma za ndege ya ATCL kumeanzisha  vita ya viwango vya bei za usafiri wa anga baada ya ATCL kutoza bei ya chini kwa safari zake kunadaiwa kusababisha watoa huduma wengine wakiwemo Precision Air nao kupunguza gharama zao ili kukabiliana na ATCL.


Na Mwandishi Wetu

MECHI ya kirafiki ya kimataifa kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Malawi (The Flames), imeingiza sh. 40,980,000 kutokana na mashabiki 9,365 walioingia uwanjani.

Mechi hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya kujiandaa na mechi zao za kuwania kucheza Kombe la Dunia 2014 ambapo Stars itacheza na Ivory Coast Juni 2, mwaka huu na Malawi itaumana na Uganda.
Timu hizo ziliumana juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo zilishindwa kutambiana baada ya kutoka suluhu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema mapato hayo yametokana na hao waliokata tiketi kwa viingilio vya sh. 3,000, sh. 5,000, sh. 51,000 na sh. 20,000.

Alisema asilimia 18 ya mapato hayo ambayo ni sh. 6,251,186 ilikwenda kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) wakati gharama kabla ya mgawo zilikuwa tiketi (sh. 4,999,800), waamuzi (sh.,105,000), usafi na ulinzi (sh. 2,350,000), maandalizi ya uwanja (sh. 400,000), Wachina (sh. 2,000,000) na umeme (sh. 300,000).

Aliongeza kwa upande wa mgawo asilimia 20 ya gharama za mechi ni sh. 4,714,803, asilimia 10 ya uwanja sh. 2,357,401, asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 1,178,701, asilimia 20 ya Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 4,714,803 na asilimia 45 ya TFF (sh. 10,608,306).

Wasanii wa kikundi cha Kinoko kutoka Dar es Salaam,wakilishambulia jukwaa wakati wa promosheni ya Airtel Jiunge na Supa 5 katika Uwanja waJamuhuri,mkoani Dodoma jana.Uzinduzi rasmi ulifanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Na Pendo Mtibuche, Dodoma

UCHUMI wa Tanzania umekua kwa asilimia 6.4 mwaka 2011 ambapo katika sekta ya usafirishaji na mawasiliano, ukuaji huo upo asilimia 11.3.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Beno Ndulu aliyasema hayo mjini Dodoma mwishoni mwa wiki wakati akitoa mada katika mafunzo elekezi yanayoshirikisha wakuu wa mikoa, wilaya na makatibu tawala wa mikoa.

Alisema, uchumi katika sekta ya fedha umekua kwa asilimia 10.7, ujenzi 9.0, biashara 8.1 na uzalishaji 7.8 ambapo hadi sasa, Tanzania inakopesheka kinyume na taarifa zinazotolewa ambazo si rasmi.

Alisema, sekta ya kilimo bado inaongoza katika kuliingizia Taifa ikifuatiwa na biashara, uzalishaji na ujenzi.

Pia Gavana huyo aliishauri Hifadhi ya Taifa ya Chakula kuanza kuwa na mkakati wa kuhifadhi mpunga badala ya mahindi pekee ili kupunguza mfumuko wa bei kwani mchele ni nafaka inayotumiwa sana na kaya mbalimbali.

Hata hivyo Prof. Ndulu alisema kushuka kwa thamani ya fedha nchini kumepungua kutoka asilimia 19.7 hadi 19.0 mwaka 2002.

“Kushuka kwa thamani ya fedha, kumetokana na kushuka kwa bei ya bidhaa hasa katika eneo la nishati na mafuta hadi sasa asilimia 75 ya Watanzania wanategemea kilimo hivyo ili Tanzania iweze kupiga hatua katika maendeleo, sekta hii inatakiwa kutiliwa mkazo,” alisema Prof. Ndulu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Tume ya Mipango Dkt. Phillip Mpango aliwataka viongozi kuongoza kwa mifano badala ya nadharia ili kujua changamoto zinazowapata wale wanaowaongoza.

Aliwataka viongozi kuwa na uchungu na uduni wa maisha ya wananchi wengi wanaowaongoza, kuangalia namna ya kuwasaidia ili waweze kuondokana na matatizo yanayowakabili.

Mafunzo hayo yanahudhuriwa na Wakuu wa Mikoa 24, Makatibu Tawala wa Mikoa 25 na Wakuu wa Wilaya 133

Askari polisi akipita kando ya uzio ulioangushwa na upepo kwenye eneo la ujenzi wa Barabara ya Mtaa wa Manfierd na kusababisha usumbufu kwa watumiaji wa barabara hiyo, Dar es salaam jana.Picha na Prona Mumwi.

Na Mwandishi Wetu, Mtwara

MWENYEKITI wa Chama cha NCCR-Mageuzi Bw. James Mbatia amesema bei ya zao la korosho imepanda kutokana na jitihada za chama chake na kuahidi kuendelea kuwapigania wakulima.

Bw. Mbatia alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti juzi mkoani Mtwara alipokuwa akifungua matawi ya chama hicho katika Jimbo la Mtwara Mjini.
Aliongeza kuwa, baadhi ya watu wanaweza wasikubaline na hilo, lakini ukweli ni kwamba wakulima wa zao hilo katika mikoa ya Mtwara na Lindi wanalipwa sh. 1,200 kwa kilo kutokana na jinsi chama hicho kilivyokuwa kikiwatetea kwa nguvu wakulima hao.

Alisema, wananchi wa Mtwara wamesahaulika wakati wanalima korosho na ufuta kwa kuwa fedha wanazolipwa ni kidogo.
Aliongeza kuwa Machi, mwaka huu, alikuwa mkoani humo, ambapo  alishangaa kusikia wapata hasara. "Niliposikia hivyo, nikachachamaa, hadi bei ya zao la korosho ikapanda," alisema.
“Pamoja na kuandika barua kwa rais, tuliendelea kupiga kelele kila siku na hatimaye kelele zetu zimekuwa mkombozi kwa wana Mtwara na Lindi kwa sababu sasa naambiwa mnalipwa sh. 1,200 kwa kilo moja ya korosho," alisema.
Alisisitiza kuwa fedha hizo bado hazitoshi, wanataka walipwe zaidi ya kiasi hicho kwa sababu maisha ni magumu.
Katika ziara yake hiyo, Bw. Mbatia alifungua tawi katika Kijiji cha Namayanga pamoja na matawi mawili katika Kata ya Likombe likiwamo Tawi la Likombe na Tumaini Jema.
Pia alifungua Ofisi ya Kata ya Majengo, alifungua Tawi la Mbatia, lililoko Kata ya Ufukoni, alifungua Tawi la Uledi lililoko Kata ya Chikongola na pia mwanasiasa huyo alifungua Tawi la Harakati lililoko Chikongora.


Na Amina Athumani

ZANZIBAR imefanikiwa kutetea ubingwa wake wa Judo katika michuano ya Taifa ya mchezo huo iliyomalizika jana katika Ukumbi wa Land Mark Hotel, Dar es Salaam.

Zanzibar ambao pia ni mabingwa wa Afrika Mashariki katika mchezo huo wamefanikiwa kutwaa ushindi wa jumla katika michuano hiyo iliyoandaliwa na Chama cha Judo Tanzania Bara (JATA).

Michuano hiyo ambayo imeanza juzi ilishirikisha wachezaji kutoka Zanzibar na Tanzania Bara ambayo ilikuwa ikiwakilishwa na timu kutoka mikoa na klabu mbalimbali.

Kwa upande wa washindi mmoja mmoja, Ahmed Magongo kutoka Korogwe, Tanga amenyakua ubingwa wa jumla na kufanikiwa kupata kitita cha dola za marekani 1,000 zilizotolewa na mdhamini Gemin.

Pia kwa upande wa washindi wa uzito wa juu mchezaji Masoud Amour kutoka Zanzibar  anayecheza uzito wa kilo 100 amefanikiwa kukaa kileleni katika uzito huo.

Mohamed Hamis kutoka Zanzibar aliyepigana katika uzito wa kilo 81, amefanikiwa kukaa kileleni ambapo kwa upande wa wanawake mchezaji Matilda Mgasi anayecheza kilo 63 ameshika nafasi ya kwanza katika uzito wake.

Akizungumzia mashindano hayo, Mwenyekiti WA JATA, Chief Kiumbe alisema mashindano hayo ni mara ya kwanza kufanyika kwa wachezaji kupewa fedha taslim.

Alisema kupitia mdhamini wao Genim wamefanikiwa kuyafanya mashindano kuwa katika ubora wa hali ya juu na kuomba wadau, Kampuni na taasisi binfsi kuunga mkono maendeleo ya mchezo huo kwa kutoa sapoti katika mashindano mbalimbali watakayoyaandaa.

Alisema changamoto kubwa inayoikabili JATA hadi sasa ni kukosekana kwa ukumbi wa kudumu wa kuchezewa mchezo huo na kwamba Zanzibar wamekuwa wakifanya vema katika mashindano mbalimbali ya Afrika kutokana na kuwa na ukumbi mkubwa kwa ajili ya mchezo huo.

Baadhi ya wakazi wa jiji wakijitolea damu kwa hiari katika kituo cha Huduma na Ushauri Nasaha cha FEMINA (HIP) wakati wa maadhimisho ya Siku ya UKIMWI ya Chuo cha Mwalimu Nyerere Kigamboni, Dar es salaam juzi, ambayo huadhimishwa kila mwaka.


Na Speciroza Joseph

NAIBU wa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Fedha ya Klabu ya Simba, amewataka wana-Simba kuendeleza umoja na mshikamano ili waendelee kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali.

Mbali na hilo, pia wafanye haraka kuwa na uwanja wao wenyewe wa kisasa zaidi ya ule unaomilikiwa na timu ya Azam FC kwani timu hiyo ina historia kubwa nchini.

Kauli hiyo aliitoa jana jioni wakati wa sherehe za kusherehekea ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambao timu hiyo uliupata zilizofanyika katika Ukumbi wa Dar Live, Dar es Salaam.

Akizungumza na wanachama na mashabiki wa Simba waliojitokeza katika sherehe hizo, Makalla alisema Simba ni timu kubwa na inatakiwa kupiga hatua kubwa tofauti na ilivyo hivi sasa.

"Simba ina historia kubwa haikutakiwa kuwa katika hali hiyo, Serikali inajikita kukuza michezo kwa kuongeza walimu wa ndani wa kuendeleza mchezo huo uwe na mafanikio zaidi kwa wachezaji wa ndani," alisema Makalla.
Kabla ya Makalla kuzungumza, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Godfrey Nyange 'Kaburu' aalisema ubingwa wao umetokana na ushirikiano wa wapenzi, wanachama na kuahidi watatengeneza timu bora zaidi ushindani ligi kuu na Klabu Bingwa.

Alisema baada ya arobaini ya aliyekuwa mchezaji wao, Patrick Mafisango kupita watafanya sherehe kubwa Watanzania wote.
Naye aliyekuwa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Mwina Kaduguda alisema mwezi ujao anatarajia kutoa kitabu maalum kitakachoelezea historia ya Simba tangu ilivyoanzishwa na mafanikio iliyopata.
Alisema kitabu hicho kimechapishwa nje ya nchi ili kiwe na ubora zaidi ambapo anawaomba wanachama wao wakae mkao wa kula kusubili kitabu hicho.
Sherehe hizo zilipambwa na burudani mbalimbali ambapo Bendi ya Msondo Ngoma ndio ilikuwa ya kwanza kupanda jukwaani baada ya michezo ya watoto kumalizika na burudani zingine ziliendelea.

Vikundi mbalimbali vya ngoma na wasanii wa bongofleva walitoa burudani ya aina yake lakini iliyokonga nyoyo za watu wengi ni burudani kutoka kwa Bendi ya Taarab ya Mashauzi Classis iliyo chini ya msaniii, Isha Mashauzi.

 
Amina Athuman na Zahoro Mlanzi

KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imeitaka Kamati ya Uchaguzi ya Klabu ya Yanga, ianze mchakato wa kujaza nafasi zilizo wazi kuanzia Juni Mosi, mwaka huu na Julai 15 ifanye uchaguzi wa viongozi wapya.

Hatua hiyo ya Kamati ya Uchaguzi imekuja baada ya kujadili kwa kina mustakabali wa uongozi ndani ya klabu hiyo pamoja na kupokea ushauri kutoka kwa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi kwa Wachezaji ya shirikisho hilo kutokana na kujiuzulu kwa Wajumbe nane na kifo cha Mjumbe mmoja wa Kamati ya Utendaji.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na kusainiwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Deogratias Lyatto alieleza kwamba katika kikao chao kilichofanyika jana jioni kiliamua Kamati ya Uchaguzi Yanga ifanye mambo matano muhimu.

Taarifa hiyo iliainisha mambo hayo ni kwamba kamati hiyo ianze mara moja mchakato wa kujaza nafasi zilizo wazi kwa wajumbe wa kuchaguliwa waliojiuzulu kwa mujibu wa ibara ya 28 ya katiba ya Yanga.
"Mchakato huo uanze Juni Mosi kwa kuzingatia kikamilifu kanuni za uchaguzi wa uanachama wa TFF na uchaguzi wenyewe ufanyike Julai 15, mwaka huu mahali patakapopangwa na kamati hiyo na Sektetarieti ya klabu hiyo," ilieleza sehemu ya taariaf hiyo.

Ilifafanua zaidi kwamba Mkutano Mkuu utakuwa na agenda moja ambayo ni kujaza nafasi za viongozi hao wa kuchaguliwa na pia kamati hiyo iandae na kusimamia shughuli za uchaguzi kwa kuishirikisha sekretarieti chini ya kanuni za wanachama wa TFF kwa mujibu wa katiba ya TFF ibara ya 49(1) na katiba ya Yanga ibara ya 45(1) na (2).
Wakati huohuo, Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imekabidhi shughuli zote za Klabu ya Yanga kufanywa na Sekretarieti ya Yanga chini ya Katibu Mkuu, Celestine Mwesigwa.

Kamati hiyo pia imewataka wajumbe wote wa klabu hiyo ambao hawajajiuzulu kutofanya shughuli zozote za klabu hadi  nafasi za viongozi wa klabu hiyo waliojiuzulu zitakapozibwa.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo,  Alex Mgongolwa, alisema nafasi za viongozi waliojiuzulu zitajazwa katika mkutano wa kawaida wa Yanga.
Alisema maamuzi hayo yamefanywa na kamati hiyo baada ya kukaa kikao na Kamati ya Utendaji Mei 26, mwaka huu na kutoa mwongozo kwa Yanga  baada ya Kamati ya Uchaguzi Yanga kuomba mwongozo huo.
Alisema baada ya kupata taarifa rasmi kutoka Yanga, Kamati imebaini kuwa Kamati ya Utendaji ya Yanga imekosa akidhi baada ya wajumbe wake wengi kujiuzulu hivyo kutokuwa na uwezo wa kufanya uamuzi kwa mujibu wa Ibara ya 32(1) ya Katiba ya klabu hiyo.

No comments:

Post a Comment