TAN

TAN

Bayport

Bayport

Kikoa

Kikoa

Myway entertainment

Myway entertainment

FORE PLAN CLINIC

FORE PLAN CLINIC

MPINGA CUP 2016

MPINGA CUP 2016

Mashujaa Fm 89.3, Lindi

Tuesday, March 13, 2012

Lipumba arejea kuinusuru CUF



*Apata mapokezi ya kihistoria akitokea Marekani
*Adai Tanzania hakuna utawala wa kidemokrasia
*Wanafunzi 808 Dodoma wakihama chama hicho


Na Peter Mwenda
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amewasili jana akitokea nchini Marekani na kupata mapokezi ya kihistoria.

Wachambuzi wa mambo ya siasa wanasema kuwa, kurejea kwa kiongozi huyo kutasaidia kukinusuru chama hicho ambacho hivi sasa kimekubwa na jinamizi la kuondokewa na wanachama wake.

Profesa Lipumba aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere saa 9:20 alasiri ambapo viongozi mbalimbali wa chama hicho walijitokeza kumpokea wakiwemo wabunge na wanachama wakiongozwa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad.

Baada ya kushuka kwenye ndege, Prof. Lipumba alifanya mazungumzo na baadhi ya viongozi wa CUF katika chumba maalumu cha mapumziko.

Baada ya kumaliza mazungumzo, Prof. Lipumba alitoka nje na kuvalishwa shada la maua huku vigelegele na nderemo zikitawala katika maeneo mbalimbali ya uwanja huo.

Eneo la uwaja lilijaa wafuasi wa CUF waliokuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za kumpongeza Prof. Lipumba kwa kuwa mwafrika pekee kuchaguliwa kwenye kamati ya kuchunguza chanzo cha mdororo wa uchumi duniani.

Kutokana na wingi wa watu walijitokeza kumpokea, Maofisa Usalama walimzuia Prof. Lipumba na Maalim Seif, kuhutubia wananchi katika uwanja huo.

Maofisa hao walishauri viongozi hao waondoke ndipo Prof. Lipumba aliamua kuzungumza na waadishi wa habari na kusema kuwa, kazi anyoifanya nchini Marekani angeweza kuifanya Tanzania kama mchumi aliyebobea lakini hapati ushirikiano.

“Nipo tayari kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Tanzania kuhusu masuala ya uchumi, hii itatokana na utawala na demokrasia ambao kwa sasa haupo nchini Tanzania,” alisema.

Aliwashukuru Watanzania na wafuasi wa CUF kwa kujitokeza kumpokea na kudhihilisha kuwa, wananchi wana imani na chama hicho.

Kwa upande wake, Shekhe Issa Ponda, akiongoza mashekhe wenzake 20 kutoka misikiti mbalimbali jijini Dar es Salaam, alisema mchango wa Prof. Lipumba ni heshima kubwa kwa Tanzania.

Ofisa Mawasiliano wa CUF, Bw. Salium Biman, alisema chama hicho kitachukua dola mwaka 2015 kutokana na umati mkubwa wa watu waliojitokeza uwanjani wenye imani na Prof. Lipumba.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu CUF Zanzibar, Bw. Ismail Jussa Ladhu, alisema umati uliojitokeza kumlaki Mwenyekiti huyo ni salamu tosha kwa mbunge wa Wawi, Bw. Hamad Rashid Mohammed kuwa chama hicho bado kina nguvu.

“CUF imeanza kazi rasmi ya kuimarisha chama ili 2015 tuchukue dola kwa kishindo,” alisema, Bw. Jussa.

Baada ya kuzungumza na waandishi wa habari, Prof. Lipumba aliondoka na msafari wa watu walifika kumpokea ukiongozwa na pikipiki, magari na watembea kwa miguu hadi Uwanja wa Karume.

Awali mapokezi hayo yaliingia dosari baada ya gari aina ya Fuso lenye namba za usajili T 854 AMN, lililokuwa limejaza wafuasi wa chama hicho, kupinduka na kusababisha watu 10 kuumia.

Taarifa nyingine zinasema kuwa, gari lingine ambalo lilikuwa likitokea Rufiji mkoani Pwani kupeleka wafuasi wa chama hicho uwanjani hapo, lilimgonga mtembea kwa miguu na kufa papo hapo.

Wakati huo huo, Mwandishi wetu kutoka Dodoma anaripoti kuwa, zaidi ya wanafunzi 808 wa Vyuo Vikuu mkoani hapa ambao ni wananchama wa CUF, wametoa tamko la kujitoa na kurudisha kadi kwa uongozi wa chama hicho kwenye matawi ya vyuo vyao.

Wanafunzi hao walidai kuwa, wamelazimika kujiondoa katika chama hicho kutokana na kitendo cha viongozi wa ngazi ya juu kujali zaidi maslahi binafsi na kukidumaza chama.

Tamko la kujitoa katika chama limetolewa na Mwenyekiti wa Tawi la St. John  Bw. Muhamed Abdullha kwa niaba ya wanafunzi wezake katika kikao kifupi kilichofanyika kwenye Ukumbi wa mikutano chuoni hapo.

Bw. Abdullah alisema wanachama waliojitoa ni wasomi wa elimu ya juu katika vyuo vyote mkoani haapa ambao wamerudisha kadi za chama hicho na kila mmoja atachagua chama cha kwenda ambacho kina mtazamo wa kuleta maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

“Uongozi wa CUF kimsingi umetuchosha, hatujui unajali maslahi ya nani, inaonesha wazi kuwa viongozi wachache wa juu wanalinda maslahi binafsi na ndiyo maana chama hakikui.

“Kutokana na hali hiyo, wanafunzi ambao ni wanachana wa CUF tumelazimika kurudisha kadi, kila mmoja atachagua cham cha kwenda chenye mwelekeo wa kusaidia wananchi,” alisema.

Walisema Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Bw. Ismail Jussa Ladhu, amekuwa akitumia madaraka yake vibaya na kukiuka katiba ya chama hicho jambo ambalo limekuwa kilichangia kuwepo matakaba kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Katika tamko lao, wanafunzi hao walidai kuchoshwa na tabia za viongozi wa chama kuingiza udini kwa kuwabagua Wakristo na Waislamu na kujenga ukuta kati ya Wazanzibari na wenzao wa bara jambo ambalo ni kinyume na katiba yao.
Posted: 11 Mar 2012 11:49 PM PDT
Maelfu ya wanachama na wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) wakiwa wamejaa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA) kumpokea Mwenyekiti wao Profesa Ibrahim Lipumba aliyewasili jana alasiri akitokea Marekani, picha ndogo ni Profesa Lipumba na Katibu Mkuu  wake, Maalim Seif Sharif Hamad wakisalimia wananchi. (Picha na Peter Mwenda)
Posted: 11 Mar 2012 11:30 PM PDT
*Ataka mafisadi watoswe katika chaguzi za chama hicho
Na Mwandishi Wetu, Mwanza

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Samuel Sitta, amewapa mtihani mzito wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Mwanza na mikoa mingine nchini kuweka historia katika chaguzi mbalimbali ndani ya chama hicho kwa kukisaficha chama na kuwatosa wagombea wanaotaka uongozi kwa maslahi binafsi kwani wanachangia kukishushia hadhi chama hicho.

Alisema kama mafisadi na makundi yao yatapewa nafasi za uongozi ndani ya chama, watajuta kupoteza nafasi muhimu ambazo zinapaswa kufanyiwa mabadiliko ya kihistoria na watakuwa wameshiriki kuisaliti CCM na kuiweka pabaya chaguzi zijazo.

Bw. Sitta aliyasema hayo juzi katika mkutano wa hadhara ambao ulihudhuriwa na maelfu ya wana CCM pamoja na waananchi katika Uwanja wa Magomeni, uliopo Kata ya Kilumba, jijini Mwanza.

Alisema njia pekee ya kuinusuru CCM ni wanachama kuhakikisha wanachagua viongozi waadilifu kuanzia ngazi ya shina hadi Taifa.

Aliongeza kuwa, wananchi wengi bado wana imani na chama hicho lakini wanalalamikia mwenendo wa baadhi ya viongozi hivyo uchaguzi wa mwaka huu lazima uwe wa kihistoria.

“Hii ndio fursa ya kukinga’risha chama chaetu, wana CCM tumieni uchaguzi huu kuchagua viongozi wanaopinga aina zote za ubaguzi ukiwemo wa kipato, tuchague viongzoi wenye huruma na wanaotetea wanyonge ambao ndio wengi.

“Tusipofanya hivyo na kuwaachia wenye uchu na matajiri, tutakuwa hatujaitendea haki imani yetu, itikadi yetu na misingi yetu, tuweke historia katika uchaguzi huu kwa kuwaenzi waasisi wetu wa Taifa.

“Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, alituachia msingi wa CCM kutetea wanyonge na huu umedhihirika, tumekuwa wakombozi hadi nje ya nchi, ukombozi huo ndio aliomnfanya Mzee wetu Karume kuwajengea maghorofa wanyonge hivyo lazima turudi katika misingi hiyo,” alisema Bw. Sitta.

Bw. Sitta ambaye alialikwa na Kamati ya Siasa Wilaya ya Ilemela na Kata ya Kirumba kuzindua kampeni za kumnadi mgombea udiwani wa kata hiyo, alisema CCM imekuwa ikilaumiwa na Watanzania kwa kupoteza uelekeo, kushindwa kuendeleza sera na itikadi iliyomo ndani ya katiba yake.

“Imani yetu rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa, huu ndio wakati wa kurudisha chama chetu katika njia yake na kusafisha vumbi la kila aina ili CCM ing'ae mbele ya jamii, tusipofanya hivyo, tutakua hatukitakii mema,” alisema.

Akimnadi mgombea udiwani wa kata hiyo, Bw. Jackson Robert, maarufu kama 'Masamaki', Bw. Sitta alisema mgombea huyo anastahili kuchaguliwa kutokana na uadilifu na msimamo wake thabiti katika kusimamia sera za CCM.

Alisema ushindi alioupata wa asilimia 70 ndani ya chama hicho ni dalili ya ushindi wake katika uchaguzi huo.

Bw. Robert atachuana wagombea wengine wa vyama mbalimbali huku mpinzani wake mkuu akitarajiwa kutoka chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Posted: 11 Mar 2012 11:28 PM PDT
Pamela Mollel na Queen Lema, Arusha

RAIS mstaafu wa Awamu ya Tatu, Bw. Benjamin Mkapa, leo anatarajia kuzindua kampeni za mgombea ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha, kwa tiketi Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Sioi Sumari.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa CCM mkoani hapa, Bi. Mary Chatanda, alisema kampeni hizo zitahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho.

Alisema uzinduzi huo utakuwa tofauti na vyama vingine vya siasa ambavyo vinakodisha watu kutoka nje ya jimbo hilo.

“Tutazindua kampeni kwa kishindo ili kuwapa wananchi fursa ya kuona jinsi tulivyojipanga kushinda, kampeni zetu zitafunguliwa na Rais mstaafu, Bw. Benjamin Mkapa na viongozi wengine wa kitaifa watakuwepo ila tumeojipanga kupambana,” alisema Bi. Chatanda.

Katika hatua nyingine, Bi. Chatanda alisema wananchi wanapaswa kutokubali kudanganywa na aina yoyote ya propaganda kuhusu madai ya mgawanyiko wa wanachama ndani ya CCM.

Alisema wanachama wote wapo katika kundi moja jambo ambalo linawapa matumaini ya ushindi. Akizungumzia pingamizi lilowekwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), dhidi ya mgombea wao, Bi. Chatanda alisema pingamizi hilo limefutwa.

Bw. Sumari alikuwa amewekewa pingamizi na CHADEMA kwa madai kuwa hajawahi kukana uraia wa nje.
Posted: 11 Mar 2012 11:24 PM PDT
FEBRUARI 2009, Rais Jakaya Kikwete alimvua madaraka na kumfukuza kazi aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, mkoani Kagera, Bw. Albert Mnali, kutokana na kitendo cha kuwacharaza bakora walimu wa shule za msingi wilayani humo.

Hatua hiyo ilitokana na Bw. Mnali kufanya kitendo cha udhalilishaji kisichokubalika katika jamii na kuwavunja moyo walimu.

Bw. Mnali aliamrisha polisi kuwacharaza viboko walimu ambao aliamini wao ndio wamechangia wanafunzi wa shule za msingi wilayani humo kufeli mitihani.

Tukiachana na hilo, wachambuzi wa mambo ya uchumi wanasema ufadhili unaotolewa na wahisani kutoka mataifa mbalimbali duniani una faida na madhara yake.

Mwishoni mwa wiki, gazeti moja linalotoka kila siku liliandika habari inayosema “Mholanzi amchapa vibao Mwalimu Mkuu”. Tukio hili lilitokea katika Shule ya Msingi Marera, iliyopo Kata ya Rhotia, Wilaya ya Karatu, mkoani Arusha.

Mashuhuda wa tukio hilo wanadai kuwa, raia wa Uholanzi, Bi. Marise Koch, ambaye ndiye mfadhili wa shule hiyo kwa kukarabati majengo ya shule, ofisi, nyumba ya walimu na kutoa kompyuta ndogo 'Laptop', alimdhalilisha Mwalimu Mkuu Bw. Emmanuel Ginwe kwa kumpiga vibao mbele ya wanafunzi, walimu wenzake.

Tukio hilo limeripotiwa katika Kituo cha Polisi Karatu na kufunguliwa jalada namba KRT/RB/835/2012. Bi. Koch aliwakuta walimu wa shule hiyo wakipanga ratiba ya shule na kuhoji kwanini hawajaingia darasani.

Walimu hao walijibu tayari wanafunzi wamepewa kazi za kufanya lakini majibu hayo hayakumridhisha. Aliamua kwenda ofisini kwa Bw. Ginwe na kudai yeye anafadhili vitu vingi lakini walimu hawafundishi, kuanza kukusanya kopyuta alizotoa kama msaada shuleni hapo lakini Mwalimu Mkuu alimsihi asifanye hivyo.

Baada ya Bi. Koch kuona anazuiwa, alimpiga Bw. Ginwe vibao na kuendelea kuzikusanya kitendo ambacho kiliwashtua walimu na wanafunzi walioshuhudia tukio hilo.

Sisi tunasema kuwa, tukio hili halikubaliki kwani dhana ya ufadhili si kunyanyasa watu wanaopewa misaada na kuingiza mambo yao katika mitaala ya elimu nchini.

Kimsingi, kilichofanywa na Bi. Koch ni kosa kisheria hivyo tunaliomba Jeshi la Polisi wilayani Karatu, lichukue hatua stahiki za kuhakikisha mfadhili huyo anafikishwa mahakamani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Matatizo yaliyopo katika sekta ya elimu na nyinginezo si kigezo cha kuwafanya Watanzania wanyanyasike na kudhalilishwa ndani ya nchi yao. Tumechoka na manyanyaso ya aina hii, tunataka sheria imuadhibu Bi. Koch kama ilivyofanya kwa Bw. Mnari ambaye alifukuzwa kazi kwa kosa la kudharirisha walimu.

Kama Serikali itashindwa kuchukua hatua stahiki dhidi ya mfadhili huyu, upo uwezekano wa kukwamisha maendeleo ya elimu shuleni hapo kutokana na ukweli kwamba, walimu katika shule husika hawatakuwa na imani na serikali yao kwa sababu haijawali.
Posted: 11 Mar 2012 11:22 PM PDT
Na Pendo Mtibuche, Dodoma
SERIKALI mkoani Dodoma imesema suala la upandaji holela huduma za matibabu ya afya chini ya mifuko ya  afya ya jamii NHIF na CHF limekuwa likiathiri utendaji wa mifuko hiyo.

Hali hiyo imedaiwa kutokana na wauzaji wa dawa na watoa huduma kubadilisha
bei ya dawa wanavyotaka na kwa wakati wowote.

Hayo yalielezwa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt.Rehema Nchimbi wakati akifungua kongamano la siku moja la wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoa wa Dodoma.

Alisema, sekta hiyo ya afya imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi ambazo ambazo zimekuwa kuongeza malalamiko mengi kuhusu ukosefu wa dawa katika vituo vingi vya Serikali na hasa vilivyopo ndani ya Manispaa ya Dodoma na Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa.

Alisema, kutokana na suala hilo kuwa nyeti basi ipo haja ya Serikali
kulitazama kwa makini suala hilo na kulitafutia ufumbuzi.

Mbali na changamoto hiyo ya kupanda kwa bei ya matibabu, lakini pia Mkuu huyo wa mkoa alibainisha kuwa  pia kumekuwepo na vituo vya afya ambavyo  vina uhaba wa watoa huduma wenye sifa hasa vijijini, hivyo suala hilo linasababisha utoaji huduma hafifu zisizokidhi kiwango kinachotakiwa kwa wanachama.

Alisema, hali ya afya katika Mkoa wa Dodoma inahitaji kufanyiwa tathimini ya uhakika ili kuona ni njia zipi zitakazoinua mifuko hiyo miwili ya afya ya jamii yaani NHIF na CHF ili iweze kufanya vizuri.
Posted: 11 Mar 2012 10:59 PM PDT
Na Mkwasi Issa, Pemba
ZAIDI ya miche 15,000 ya mikarafuu inatarajiwa kutolewa kwa wakulima kisiwani Pemba katika kipindi cha mvua za msimu wa masika ambazo zinatarajiwa kuanza kunyesha visiwani humo mwaka huu.

Ofisa wa Mashamba ya Serikali kisiwani Pemba, Bi.Asha Saleh Mbarouk aliyaeleza hayo wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti hili kuhusiana na mikakati ya Serikali ya kuimarisha zao la karafuu katika msimu huu.

Alisema kuwa, ni vema wakulima kuanza kuyatayarisha mashamba yao mapema kabla ya mvua za masika hazijaanza ili kujiweka tayari kwa ajili ya kupanda mikarafuu mipya.

Bi. Mbarouk alisema, kila mkulima anayehitaji kupatiwa miche ya mikarafuu anatakiwa kujaza fomu ambazo zinapatikana kwa maofisa wa kilimo kwa kila shehia, fomu amabazo zitamuwezesha kupatiwa miche hiyo.

Aidha, alisema miche hiyo inapatikana vitalu vilivyoko Weni katika Wilaya  ya Wete, Kicha kwa wilaya ya Micheweni, Kigope Wilaya ya Mkoani pamoja na Kitalu Wilaya ya Chake.

Hata hivyo Ofisa huyo aliwataka wakulima kuwa tayari kwenda kuchukuwa na kujaza fomu ambapo kwa sasa watendaji wa kilimo wameanza kukagua na kupima mashamba operesheni ambayo kwa sasa inaendelea katika shehia ya Mtambwe Kaskazini.
Posted: 11 Mar 2012 10:57 PM PDT
Na Theresia Victor, Dodoma
MHANDISI Deogratius Assey ambaye amejitokeza katika kinyang’anyiro cha kugombea nafasi ya ubunge, Bunge la Afrika Mashariki (EAC) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) amesema tayari amerejesha fomu katika ofisi ya chama hicho mkoani Dodoma kwa ajili ya kugombea nafasi hiyo.

Akizumgumza na Majira baada ya kurudisha fomu hiyo jana, Bw. Assey alisema, alilazimika kuingia katika ushindani huo kwa ajili ya kutaka kutetea maslahi ya vijana kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Bw. Assey alisema, pamoja na kuwepo kwa sera za kuwepo kwa jumuiya hiyo lakini bado haijapata mtu madhubuti ambaye yupo tayari kwa ajili ya kuwatetea na kuwapiagania vijana kuingia katika ushindani wa ajira kupitia EAC.

Alisema, alilazimika kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo kwani alikuwa hajiamini kuwa kama angeweza kupata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wananchi kwa kumuunga mkono kama ambavyo kwa sasa mambo yamekuwa mazuri kwa kupata ushirikianao wa kutosha.

“Lakini cha kushangaza nimeungwa mkono na wanacha wote wa Chadema na hata wale wasiyo kuwa wanachama, hata hivyo wamenichangia hata gharama za kulipia fomu ambayo ilikuwa inagharimu shilingi laki moja...lakini wamenichangia,”alisema Bw.Assey.

Aliongeza kuwa, ikiwa atafanikiwa kuipata nafasi hiyo atahakikisha kuwa vijana wanatetewa zaidi katika masuala ya ajira tofauti na ilivyo sasa ambapo Watanzania bado hawajaweza kunufaika na suala zima la ajira kwa vijana katika jumuiya.

Aidha, kwa upande wake Katibu wa Mkoa wa Dodoma CHADEMA, Bw. Stivine Masawe alisema, ameipokea fomu ya mgombea huyo na kusema kuwa haina makosa yoyote na hivyo iko sawa na ataiwasilisha Makao Makuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo jijini Dar es Salaam.

Bw. Masawe alisema, kujitokeza kwa Mhandisi Assey ambaye ni kijana na mwanachama hai katika chama hicho ni fursa pekee kwa vijana kutatuliwa matatizo yao kama atapata nafasi ya kuchukua nafasi hiyo ya ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki.
Posted: 11 Mar 2012 10:50 PM PDT
Kiungo wa timu ya Simba, Patrick Mafisango (kulia) akijaribu kuwatoka mabeki wa Toto African ya Mwanza wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana.(Picha na Michael Machellah)
Posted: 11 Mar 2012 10:49 PM PDT
*Wadaiwa kumpiga mtoto, mechi yao yaingiza mil. 73/-
Na Zahoro Mlanzi
WACHEZAJI wa Yanga Nurdin Bakari, Athuman Idd 'Chuji' na Jerryson Tegete, wanadaiwa kumpiga mtoto anayeishi Mtaa wa Faru na Swahili, Kariakoo, Dar es Salaam na kumsababishia maumivu.
Tukio hilo lilitokea juzi usiku baada ya mtoto huyo kuwazomea kutokana na kipigo cha bao 3-1 dhidi ya Azam FC ambapo gari la Yanga lililokuwa limebeba wachezaji,  lilisimama na wachezaji hao kwenda kumpiga mtoto huyo ngumi na mateka.

Kwa mujibu wa shuhuda aliyekuwepo eneo la tukio (jina tunalo),  alisema “ Baada ya mtoto huyu kuwazomea, Chuji, Nurdin na Tegete walishuka kwenye gari la kumuadhibu, walipomaliza kiu yao walirudi katika basi lao na kuondoka,” alidai mtoa habari huyo.
Alidai kuwa, walipokwenda kumuangalia mtoto huyo walimkuta katika hali mbaya huku mwili wake ukiwa na majeraha.

Vyanzo mbalimbali vya kuaminika vilidai kuwa, mtoto huyo alikimbizwa hospitali kutokana na hali yake kuwa mbaya.

Alipotafutwa kwa njia ya simu ili aweze kuzungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda Mkoa wa Kipolisi Ilala, Saada Juma, alisema hana  taarifa zozote kwani hadi anaondoka ofisini juzi saa 1:30 usiku, hakuna mtu aliyetoa taarifa ya tukio hilo.

“Leo (jana) Ma-OCD wangu walikuwa wakinipa taarifa za mara kwa mara kuhusiana na tukio la kuwasili kwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Bw. Ibrahim Lipumba lakini taarifa za kupigwa mtoto hadi akafariki dunia au kukamatwa kwa wachezaji wa Yanga hilo sijalipata,” alisema Kamanda Juma.

“Kama lipo nadhani nitapata taarifa ila kinachonishangaza, tutaanzaje kupaata taarifa za kifo kabla ya kuumizwa mtoto husika kwani hizo ndio zingesaidia kupata majibu ya uhakika kwa hicho unachonieleza lakini siwezi kusema uongo ila ukweli ni kwamba sina taarifa na hilo,” alisema.

Majira halikuishia hapo pia lilimtafuta Mwenyekiti wa klabu hiyo, Llody Nchunga ambaye alisema hana taarifa za wachezaji wake kufanya fujo, kukamatwa au kufa kwa mtoto huyo.

“Sijui kama hilo tukio lina ukweli, ninachokiamini mimi ni kwamba, wachezaji wote walirudi klabuni na leo (jana) asubuhi, nilikwenda kuzungumza nao tukaamua kuwapa siku moja ya mapumziko hivyo wamekwenda majumbani kwao,” alisema Nchunga.

Alisema kama tukio hilo lilifanyika, labda ni baada ya kurudi klabuni na baadhi yao kutoka tena kwenda mitaani kufanya fujo lakini walipotoka uwanjani, warurudi klabuni.

Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu timu hiyo, Kostadin Papic atawachukulia hatua wachezaji wote waliomfanyia fujo mwamuzi  Israel Mujuni kutoka Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya mechi iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Papic alisema kitendo kilichofanywa na wachezaji wake hakikuwa kizuri na utovu wa nidhamu hivyo atahakikisha anawachukulia hatua.
Wakati huo huo, mchezo kati ya Yanga na Azam umeingiza sh. milioni 72,731,000.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari Dar es Salaam na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema watazamaji 19,339 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo kwa kiingilio cha sh. 3,000 viti vya bluu na kijani, sh. 5,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C na B wakati kwa VIP A ilikuwa sh. 15,000.

No comments:

Post a Comment