Sisi
 Wawakilishi wa Jumuiya na Taasisi za Dini, tuliopendekezwa na Taasisi 
zetu na baadaye kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 
baada ya kushauriana na Rais wa Zanzibar kuwa Wajumbe wa Bunge Maalum la
 Katiba, na kula kiapo cha utekelezaji wa jukumu hili kubwa.
Tukiamini
 kuandaa Katiba Mpya kwa maridhiano ya Kitaifa kwa wananchi wote, 
tulipokea jukumu hili kama wajibu wetu Kitaifa.  Aidha tunaamini kwamba 
katika kupata maridhiano ya Kitaifa ni muhimu kuheshimu kila wazo na 
fikra inayotolewa na kuunganisha fikra hizo kwa usahihi, kwa njia ya 
kidemokrasia kwa kupiga kura na kukubaliana na matokeo ya wengi.
Kama 
ilivyoelezwa hapo awali, kabla ya kuanza shughuli za Bunge Maalum, kila 
mjumbe alikula kiapo cha kuwa mwaminifu na mtiifu kwa Jamhuri ya 
Muungano wa Tanzania na kwa kadiri ya uwezo wake na ufahamu wake, 
kufanya kazi zinazomhusu, bila upendeleo na kumuomba Mwenyezi Mungu 
amsaidie. 
Tumeshangazwa
 na kusikitishwa sana kuona kwamba mchakato wa kutayarisha Katiba 
itakayopendekezwa na Bunge hili kwa wananchi, unachafuliwa taswira 
yake.  Bunge Maalum la Katiba linachafuliwa na, shughuli zake kuingiliwa
 na kupotoshwa na wajumbe wenzetu walio nje ya Bunge, Makundi, Taasisi 
na Vyombo mbali mbali vya habari, uhalali na ukweli wa shughuli za 
BungeMaalum la Katiba unapotoshwa.  Wananchi wanaaminishwa yasiyo na 
ukweli.
Upotoshwaji huu umezua mijadala mbali mbali katika jamii ya Watanzania na bado linaendelezwa kama ifuatavyo:
1.   Kwamba
 Bunge Maalum la Katiba halina uhalali kwa kuwa hao wajumbe wenzetu 
walioondoka wameliondolea uhalali wake kwa vile hwapo, wakiwepo Bungeni 
basi uhalalai wake utakuwepo - utapatikana;
2.   Inadaiwa kwamba Kanuni za Bunge Maalum la Katiba zinavunjwa ovyo ovyo;
3.   Inadaiwa
 pia, kwamba kinachojadiliwa sasa katika Bunge hili ni Waraka mwingine 
na si Rasimu iliyotayarishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, 
iliyowasilishwa rasmi Bungeni na kuanza kujadiliwa na wajumbe;
4.   Inadaiwa
 na watu na Taasisi mbali mbali, kwamba viongozi wa dini, wajumbe wa 
Bunge Maalum la Katiba, na wajumbe wa Kundi la 201, wanapewa rushwa. 
Isitoshe Vyombo vya habari vimeandika tuhuma kama hizi.
5.   Inadaiwa pia kwamba wajumbe waliomo katika Bunge hili ni wachache, ukilinganisha na hao walioko nje ya Bunge hilo;
6.   Bunge hili, kwa tuhuma hizo, lazima lisitishwe au livunjwe na Mhe. Rais.
Kabla 
ya kuanza kuusahihisha upotoshwaji huo, sisi Wawakilishi wa Taasisi za 
Dini mbali mbali na Wajumbe wa Kundi la 201 katika Bunge Maalum la 
Katiba, tunapenda kufahamisha umma wa Tanzania mchakato wa kutayarisha 
Katiba Mpya ulivyo kisheria.
Tunapenda
 kuwafahamisha Watanzania wenzetu kwamba mchakato huu una hatua tatu kwa
 mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.  Mpaka hivi sasa ni hatua 
moja imekamilika.  Hatua ya pili ndiyo inayoendelea, na hatua ya tatu 
bado haijaanza.
Hatua 
ya kwanza ni ile ya uandaaji wa Rasimu. Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, 
Sura ya 83 iliunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba, chini ya kifungu cha 
tano cha sheria hiyo.  Tume hii ilipewa jukumu la kuratibu na kukusanya 
maoni ya wananchi juu ya Katiba, kuanisha na kuchambua maoni ya wananchi
 na kisha kuandaa rasimu ya Katiba.  Kazi hiyo ilifanyika kwa kipindi 
cha takriban miaka miwili na hatimaye Rasimu ya Katiba ilikamilika.
Hatua 
ya pili ilikuwa ni kuipeleka Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalum la 
Katiba, ambalo liliundwa kwa shughuli maalum ya kuandika Katiba 
inayopendekezwa, ili ifikishwe kwa wananchi ambao wataamua waikubali au 
waikatae kwa kuwa wao ndio wenye maamuzi ya mwisho.  Hawa ni Watanzania 
wote wenye uwezo wa kupiga kura kwa kutoa maoni yao.  Hoja ya Mamlaka ya
 Bunge hili hatujazungumzia kwa vile imefikishwa Mahakama Kuu ya 
Tanzania ili kupata tafsiri sahihi ya mamlaka ya Bunge hili.  
Tunachoweza kusema ni kwamba jukumu kuu la Bunge hili ni kutengeneza 
Katiba inayopendekezwa na Bunge ili ifikishwe kwa wananchi  waipigie 
kura ya maoni.  Hatua hii ya pili bado inaendelea.
Hatua 
ya tatu ni pale Bunge Maalum la Katiba tutamkabidhi Mhe. Rais Katiba 
inayopendekezwa ambayo itafikishwa kwa wananchi ili waikubali kama 
wataridhika nayo au kuikataa kama haikidhi matarajio yao.
Hatua hii ni ya mwisho wananchi wakiikubali tunapata Katiba Mpya wakiikataa, tunaendelea na Katiba tuliyonayo.
Kilichotokea
 ni kwamba, wajumbe wenzetu walio nje ya Bunge hili wameamua kuukiuka 
utaratibu uliowekwa kisheria.  Badala yake wamepeleka Rasimu ya Katiba 
kwa wananchi wakati mchakato wa kutayarisha Katiba inayopendekezwa bado 
haujakamilika.
Sisi 
Wawakilishi wa Taasisi za Dini, ambao kuuhubiri, kuutangaza na 
kuusimamia ukweli ni moja ya majukumu yetu katika jamii, tumesikitishwa 
sana na taarifa potofu zinazosambazwa kwa makusudi na makundi, taasisi 
na vyombo vya habari mbali mbali na tukiwa wajumbe wa Bunge hili ambao 
tunafahamu kwa kina na tunaridhika na kila hatua ya mchakato huu.  Tuna 
wajibu wa kusahihisha upotofu huu, unaoendeshwa kwa makusudi na hivi 
kuwaeleza Watanzania ukweli na hali halisi inayojiri hapa Bungeni.  
Watanzania msifadhaishwe na wala msibabaishwe.  Hali ni shwari.  
Mchakato unaendelea kwa amani na utulivu.
Katika
 kusahihisha upotofu unaozungumzwa kupitia mijadala na midahalo mbali 
mbali katika jamii, tunaomba kufafanua hali ilivyo kama ifuatavyo:-
TUHUMA KWAMBA BUNGE MAALUM LA KATIBA KUKOSA UHALALI
Jambo 
hili si kweli hata kidogo kwani kuna wajumbe wa aina tatu Bungeni ambao 
wamewekwa na kutambuliwa kisheria.  Hawa ni kama wafuatao:
1.   Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
2.   Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
3.   Wajumbe 201 walioteuliwa na Mhe. Rais, baada ya kupendekezwa na Taasisi, Mashirika na makundi mbali mbali nchini,
Uhalali
 wa Bunge unakuwapo wakati wajumbe kutoka makundi hayo matatu wapo 
Bungeni, na si Vyama vya Siasa pekee.  Iwapo kwa mfano wajumbe wa 201 
wakiamua kutoshiriki katika shughuli za Bunge, basi sehemu moja muhimu 
ya Bunge haitakuwapo na uhalali wa Bunge hautakuwepo.
Hata 
hivyo, Kanuni za Bunge Maalum la Katiba zimeweka idadi ya akidi ambayo 
ni nusu ya wajumbe wote wa Bunge Maalum.  Akidi hii ikifikiwa Bunge 
huendelea na shughuli zake.  Akidi hii hufikiwa kila wakati BungeMaalum 
linapokutana.  Hii inamaanisha kwamba Bunge Maalum la Katiba linaendesha
 shughuli zake kwa misingi ya sheria na taratibu zilizojiwekea.  Bunge 
lina uhalali wa kufanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria.
TUHUMA KWAMBA KANUNI ZA BUNGE MAALUM LA KATIBA ZINAVUNJWA
Suala 
hilo halijawahi kutokea.  Kanuni za Bunge Maalum la Katiba zilipitishwa 
na wajumbe wote kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sheria 
Namba 83.  Vile vile uendeshaji wote wa shughuli za Bunge zinafanywa kwa
 mujibu wa Kanuni za Bunge Maalum.  Kanuni hizo zinatoa fursa ya Bunge 
Maalum kuzirekebisha pindi inapobainika ipo haja ya kufanya hivyo kwa 
mujibu wa kanuni Namba 87.  
WARAKA MWINGINE UNAJADILIWA NA SI RASIMU YA TUME
Hili 
nalo si kweli.  Tunawahakikishia Watanzania wote kwamba sisi kama 
Wawakilishi wa Taasisi za Dini miongoni mwa wajumbe wa Kundi la 201, kwa
 ujumla tunasema hii si kweli.  Ni upotoshaji wa makusudi.  Tunaijadili 
Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ibara kwa ibara.  Ibara nyingi 
zimeachwa kama zilivyo.  Kuna ibara ambazo zimeboreshwa au kurekebishwa,
 kuna ambazo zimeondolewa na kuna nyingine mpya ambazo zimewekwa ili 
kuweka mambo ya msingi ambayo Rasimu haikuyazingatia au haikuyaona.
WAWAKILISHI WA TAASISI ZA DINI, WAJUMBE WA KUNDI LA 201 WA BUNGE LA KATIBA KUPEWA AU KUPOKEA RUSHWA
Sisi 
Wawakilishi wa Taasisi za Dini na Wajumbe wa Kundi la 201 wa Bunge hili 
tumesikitishwa sana na taarifa hii iliyosambazwa na baadhi ya watu, na 
kukaririwa na baadhi ya vyombo vya habari aidha kupitia kwenye mijadala,
 midahalo na makongamano  mbali mbali.  Baadhi yetu sisi Viongozi wa 
Kiroho tumeapishwa viapo vya uadilifu katika uongozi wetu wa kiroho na 
tuko mstari wa mbele kuongoza waumini wetu kuepuka dhambi ya tamaa ya 
fedha, na kusema uongo.  Taarifa kama hizo hazionyeshi heshima kwa dini 
au nafasi zetu za kipekee katika uongozi wa kiroho.  Taarifa hizi 
zinatangazwa kwa makusudi na watu mbali mbali  kupita vyombo vya habari 
kwa malengo ya kisiasa na kutudhalilisha sisi Viongozi wa kiroho mbele 
ya umma.  Tunaomba tabia hii ikomeshwe.
TUHUMA KWAMBA BUNGE KUWA NA WAJUMBE WACHACHE
Hili nalo si kweli.  Wajumbe wanaohudhuria Bunge wanakidhi akidi inayohitajika kwa mujibu wa kanuni.
HOJA YA KUSITISHWA AU KUVUNJWA KWA BUNGE MAALUM
Hii ni
 hoja inayozungumzwa katika mijadala mbali mbali katika jamii.  Msingi 
wa hoja hiyo ni kutokuueleza umma ukweli ulioko Bungeni kwa kupeleka 
taarifa potofu kwa wananchi kwamba Bunge Maalum limekosa mwelekeo.  
Hatuoni sababu za hoja hii kutiliwa maanani kwa kuwa hakuna sababu za 
msingi na za kisheria za kufanya hivyo. 
HITIMISHO
Kumekuwa
 na taarifa mbali mbali zenye malengo ya ama kuingilia shughuli za Bunge
 hili au kutudhalilisha sisi wajumbe ambao si Wabunge au Wawakilishi.  
Wajumbe 201, ambao mchango wao katika mijadala ya Kamati mbali mbali 
umekuwa na uzito wa pekee, hautambuliki katika taarifa hizo ambazo 
zimejaa malengo ya kisiasa zaidi kuliko ukamilishaji wa shughuli za 
Bunge Maalum.
Kuna 
taarifa nyingine zimesambazwa zikiwa na upotoshaji mkubwa, licha ya 
kwamba Taasisi zinazosambaza taarifa hizo zina wajumbe wake katika Bunge
 Maalum.  Wajumbe hao wangeweza kuzielimisha Taasisi zao ukweli ulipo 
hapa Bungeni, na hivyo kuwafikishia wasomaji wao taarifa zilizo za kweli
 na ili kulijengea Bunge hili heshima machoni pa umma wa Tanzania na 
Kimataifa.   Udhalilishaji kama huu unatuumiza hata sisi wajumbe ambao 
kwa hiari yetu tuliamua kubaki Bungeni na kuyatimiza hayo ambayo 
tulitumwa tuje tuyakamilishe.
Kama 
tulivyosema hapo awali ni wajibu wetu kama Viongozi wa Dini na Wajumbe 
wa Bunge hili kuutaarifu umma hali halisi katika shughuli za Bunge 
Maalum na kuwasihi wapotoshaji kwamba wauheshimu ukweli na wawaheshimu 
watanzania kwa kuwaeleza ukweli.
Ahsanteni sana.  
No comments:
Post a Comment