Posted: 12 Mar 2013 12:12 AM PDT
Rehema Mohamed na Rehema Maigala WASHTAKIWA wa kesi ya wizi na uchochezi inamkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Shekhe Issa Ponda na wenzake, jana waliendelea kujitetea baadhi yao wakikana maelezo ya awali waliyotoa katika Kituoa cha Polisi Mabatini, Kijitonyama. Katika kesi hiyo, washtakiwa hao wametoa utetezi wao kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, mbele ya Hakimu Victoria Nongwa wakiongozwa na wakili wao, Bw.Juma Nassoro. Mshtakiwa Alawi Musa, alikana maelezo yake na kudai kuwa, alikwenda katika Msikiti wa Changombe Markaz, kwenye ibada ya Itikafu kwa ajili ya kukomboa eneo la Waislamu lililouzwa. Alawi alikana maelezo ya kuhusika kujenga Msikiti wa muda katika eneo la Markaz, linalomilikiwa na Kampuni ya Agritanza Ltd, wakati wakati akihojiwa na wakili wa Serikali Tumaini Kweka. Katika maelezo aliyotoa polisi, mshtakiwa huyo alidai yeye ni mzaliwa wa Zanzibar, Kijiji cha Ole na alikuja Dar es Salaam mwaka 2008, lakini wakili huyo alipomuhoji kuhusu maelezo hayo pia aliyakana. Kwa upande wake, mshtakiwa Ramadhani Rashidi katika maelezo aliyotoa polisi, alidai kuwa yeye ni mkazi wa Mlandizi na alipata taarifa za kusaidia ujenzi wa Msikiti katika kiwanja cha Chang'ombe Markaz kutoka kwa imamu wake wa Msikiti wa Nuruh. Katika maelezo hayo, alidaikuwa baada ya kupata taarifa hizo alikuja Dar es Salaam na kwenda Chang'ombe Markaz, Oktoba 15,2012 na walikamatwa na polisi Oktoba 16 mwaka huo usiku. Hata hivyo, mshtakiwa huyo alikana maelezo hayo na kudai polisi walimuhoji jina lake, umri na anapoishi ambapo suala la kwenda Chang'ombe Markaz, kujenga msikiti halijui hivyo huenda polisi wamejiandikia. Shekhe Ponda na wenzake wanakabiliwa na makosa matano ambapo Oktoba 12 ,2012 wanadaiwa kula njama na kuvamia kiwanja kinachomilikiwa na Kampuni ya Agritaza Ltd kwa nia ya kujimilikisha isivyo halali. Katika kosa la uchochezi, inadaiwa Shekhe Ponda na Salehe Mkadam wakiwa katika eneo la Chang'ombe Markaz na viongozi wa taasisi hiyo, waliwashawishi wafuasi wao ambao ni washtakiwa katika kesi hiyo kutenda makosa hayo. |
Posted: 12 Mar 2013 12:11 AM PDT
Na Yusuph Mussa, Korogwe MKUU wa Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, Bw. Mrisho Gambo, ameungana na vyama vya upinzani kuikataa taarifa ya Kaimu Ofisa Elimu Sekondari wilayani humo Bw. Shabaan Shemzigwa, kuhusu chanzo cha kufeli kwa wanafunzi wa kidato cha nne mwaka 2012 na kudai haina mashiko. Akizungumza mwishoni mwa wiki kwenye Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC), Kaimu Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF), wilayani humo, Bw. Ibrahim Abdillah, alisema taarifa hiyo haioneshi matatizo yaliyochangia wanafunzi kufanya vibaya zaidi. “Mwenyekiti (DC), naomba tuikatae taarifa ya Ofisa Elimu kwani haioneshi tatizo lililofanya wanafunzi kufeli zaidi ya kuja na asilimia ya watoto waliopata sifuri, pia hawaoneshi ni jitihada gani ambazo watafanya ili kumaliza tatizo hili,” alisema Bw. Abdillah. Kwa upande wake, Bw. Shemzigwa alijitetea na kudai kuwa, alipata taarifa kikao hicho siku moja kabla hivyo ameshindwa kuingiza vitu vingi kwenye ripoti yake na kukiri kasoro hizo lakini alimtibua Bw. Gambo baada ya kusema kuwa, tatizo la kufeli ni la kitaifa. Bw. Gambo alimwambia Bw. Shemzigwa kuwa, asilete taarifa ambazo zinazungumzia Taifa katika kikao hicho bali yeye anapaswa kusema ni nambna gani wataweza kumaliza tatizo la watoto kufeli wilayani humo. “Taarifa iliyotolewa na Ofisa Elimu inaonesha kama funika kombe mwanaharamu apite, haioneshi mkakati au jitihada gani zitafanyika kupunguza matokeo mabaya kwa wanafunzi... taarifa hii ni sawa na utani, dharau na mazoea. “Acha kusema wanafunzi kupata sifuri ni tatizo la Taifa, kwani mimi, mke wangu na mtoto wangu tumepata zero...zungumzia nini kifanyike ili kuondoa tatizo hili, kama ningekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ningemuandikia barua Ofisa Elimu ya kujieleza kwa nini asishushwe cheo,” alisema Bw. Gambo. Aliongeza kuwa, anaungana mkono msimamo wa vyama vya upinzani kuikataa taarifa hiyo na kumtaka Bw. Shemzigwa aiondoe kwenye kumbukumbu za DCC na kuiwasilisha wakati ujao. Alisema kama Watanzania tunataka ufaulu mzuri kwa watoto wao, wanapaswa kuacha kuingiza siasa na haki za binadamu kwenye masuala ya elimu kwani kuacha kuwachapa viboko wanafunzi kupunguza nidhamu shuleni ambayo ndio msingi wa mafanikio. taarifa hiyo ilisema wanafunzi 1,727 waliomaliza kidato cha nne wilayani humo mwaka 2012, walipata sifuri sawa na asilimia 83.269. Akizungumza na gazeti hili baada ya kikao hicho, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wilayani humo, Dunstan Mdoe, alisema kuwe na masharti magumu kwa wakuu wa shule za sekondari kuwa atakayeshindwa kufikia kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wake afukuzwe. |
Posted: 12 Mar 2013 12:10 AM PDT
Na Kassim Mahege
SIKU moja baada ya Waziri wa Mambo ya ndani Dkt.Emmanuel Nchimbi kuwasimamisha kazi maofisa wa Jeshi la Polisi kwa tuhuma mbalimbali, Mwenyekiti wa Chama Cha Democratic Party(DP) Mchungaji Christopha Mtikila amempongeza kwa hatua hiyo na kumtaka asiishie hapo. Akizungumza na gazeti hili jana alisema kuwa hatua hiyo inaonyesha ishara nzuri kwa Jeshi la polisi lakini Dkt Nchimbi anatakiwa achimbuwe mizizi ya uhalifu kwa jeshi hilo na hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa watakaobainika. "Kuwasimamisha kazi pekeyake haitoshi tunataka ukweli ukibainika kwa maofisa hao hatua kali sana za kisheria zifanyike dhidi yao,maana hao ndio wanaolipaka matope Jeshi la Polisi."na kuongeza kuwa hao ndio wanaowaumiza wananchi."alisema Mtikila. Akitolea mfano wa aliyekuwa waziri wa fedha Basil Mramba,Amatus Liyumba na Yona wa benki kuu mahakama yenyewe ilithibitisha kuwa hakuna makosa yoyote ya wizi walioyafanya ispokuwa makosa yao yalikuwa ni kutumia vibaya madaraka yao na kuongeza kuwa leo hii watu hao wanasota kisutu,hivyo anataka na maofisa hao pia wapelekwe mahakamani ili iwe fundisho kwa wengine. Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dkt.Wilbroad Slaa alisema haoni kama kuna jipya kutokana na hatua hiyo. "Mimi sitaki kuzungumzia uamuzi huo wa Dkt.Nchimbi kwa sababu ni dhahiri kuwa kuna double standard,Nchimbi aliwahi kuunda tume kwa ajili ya kufuatilia mauaji ya Mwangosi lakini hakuna hatua yoyote alioichukua mimi sioni kama kuna jambo jipya."alisema Slaa. Alisema hatua hiyo imechelewa kutokana na kukithiri kwa vitendo vya uhalifu kwa jeshi la polisi na kutolea mfano kuwa Dkt.Nchimbi aliwahi kuunda tume yake kwa ajili ya kuchunguza mauaji ya mwangosi,Ripoti zote zilizotolewa zilionyesha kuwa Jeshi la polisi lilitumia nguvu isio ya lazima na kuongeza kuwa mpaka hivi leo Nchimbi hajasema chochote. |
Posted: 12 Mar 2013 12:09 AM PDT
Na David John MWENYEKITI wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Bw. James Mbatia, amemshauri aliyekuwa mgombea urais nchini Kenya kwa tiketi ya Chama cha Muungano CORD, Bw. Raila Odinga kuheshimu matokeo ambayo ndio maamuzi ya wananchi. Alisema kinachohitajika baada ya Bw. Uhuru Kenyatta kushinda nafasi ya urais nchini humo kwa tiketi ya Chama cha Muungano wa Jubilee ni kukaa mezani ili kuijenga nchi hiyo kwa pamoja. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es salaam jana, Bw. Mbatia alimpongeza Bw. Kenyatta kwa ushindi alioupata na kusisitiza kuwa, Wakenya wamefanya uamuzi mgumu ambao haukutarajiwa na watu wengi. “Hali nii inatokana na ukweli kwamba, Bw. Kenyatta anakabiliwa na kesi mahakamani lakini bado wananchi wameendelea kumuamini na kumpa nchi ili aweze kuwaongoza kama rais wao. “Ni vyema Bw. Odinga akaachana na nia yake ya kutaka kwenda mahakamani kuweka pingamizi la matokeo yaliyotangazwa badala yake aheshimu maamuzi ya Wakenya ambayo wameyafanya kwa kumchagua Bw. Kenyatta,” alisema. Alisema Wakenya wameandika historia mpya duniani hasa katika Bara la Afrika inayopaswa kuigwa na mataifa mengine na kufafanua kuwa, kama Bw. Odinga atakwenda mahakamani kuweka pingamizi ajue wazi huko ni kutaka kuwagawa Wakenya, kuhatarisha amani ambayo tayari wameionyesha, kusababisha machafuko na chuki. Bw. Mbatia aliongeza kuwa, ushindi wa Bw. Kenyatta ni kielelezo kuwa si kila kitu watakacho wazungu, waafrika wakifanye lakini ufike wakatiAfrika iweze kufanya maamuzi yake wenyewe bila kuingiliwa na taifa lolote duniani. “Namuomba Bw. Odinga na wagombea wengine walioshindwa katika uchaguzi huu waheshimu makubaliano ya kulinda amani ambayo walikubaliana ili kuivusha Kenya kwenye demokrasia ya ukomavu,” alisema Bw. Mbatia. Katika hatua nyingi, Bw. Mbatia alizungumzia mchakato wa Katiba Mpya unaondelea nchini na kusisitiza nchi inapaswa kujifunza kwa yale mazuri ambayo Wakenya wameweza kuyatumia katika Katiba yao ambayo wameipata miaka michache iliyopita. |
Posted: 12 Mar 2013 12:06 AM PDT
KUJIAJIRI ni suala linalopewa kipaumbele na mamlaka mbalimbali nchini pamoja na mataifa yaliyoendelea. Mabadiliko makubwa katika mifumo ya uchumi, yamechangia wananchi wengi kukosa kazi za kuajiriwa ambapo ajira binafsi ndizo zinazoonekana kushika kasi katika maeneo mengi. Nchini Tanzania, idadi kubwa ya wananchi wameamua kujiajiri wenyewe wakiwemo wastaafu kwa kufungua vitega uchumi mbalimbali pamoja na kufanya biashara ndogondogo ili waweze kujipatia kipato. Cha kukidhi mahitaji yao. Kujiajiri katika biashara ni jambo jema lakini sisi tunaona kuwa, tatizo kubwa linalowasibu wadau wengi wanaofanya shughuli hizo ni kukosa mafunzo ambayo yatawawezesha kuendesha biashara pamoja na kukuza mitaji yao. Wafanyabiashara wengi nchini hawabadiliki kwa sababu shughuli wanazofanya ni zile za mazoea bila kuwa na ujuzi wa namna ya kuziendesha hivyo upo umuhimu wa Serikali, kubeba jukumu hilo ili kuwawekea msingi mzuri wa maisha. Baadhi ya wastaafu waliopewa viinua mgongo na kuwekeza kwenye biashara, wanakabiliwa na wakati mgumu wa kutafuna mitaji yao kwa sababu ya kufanya biashara zisizoendelea. Wanaofanya biashara ya kuuza maandazi na vitumbua, hawana mtazamo wa kutunza ziada wanazopata kwa kufungua akaunti bali wanachokipata kinakwenda tumboni bila kujua senti 50 inayobaki, ilipaswa kuwekwa akiba ili kuendeleza biashara zao. Hili ni jambo hatari sana, wafanyabiashara kama hawa mbali ya kufanya biashara hizo kila siku, bado wataendelea kubaki maskini bila mafanikio yoyopte kama Serikali haitachukua hatua za haraka kuwasaidia kwa kuwapatia mafunzo ya kuendesha biashara zao. Ni wajibu wa Serikali na wadau wengine, kutambua kundi hili ni watu wenye vipato vidogo na vile vya kati ambao hawawezi kulipa maelfu ya pesa kugharamia mafunzo ya uendeshaji biashara. Wito wetu kwa Serikali ibuni mkakati wa kushirikisha wadau wengine na kuandaa mpango maalumu wa kutoa mafunzo ya usimamizi na uendeshaji shughuli za ujasiriamali bure kwa wananchi waishio mijini na vijijini. Kwa kufanya hivyo, italeta mwamko kwa wajasiriamali kujua namna ya kuendesha shughuli zao na kuwapa ubunifu zaidi wa biashara mpya tofauti na sasa. Hivi sasa, wajasiriamali wengi wanafanya biashara kwa kumwiga mwenzake, utakuta kila mahali biashara ni saloon, grosari, maduka ya dawa, chakula na nguo. Je, hivi hizi ndio huduma pekee wanazohitaji wananchi? |
TAN
Bayport
Kikoa
Myway entertainment
FORE PLAN CLINIC
MPINGA CUP 2016
Mashujaa Fm 89.3, Lindi
Wednesday, March 13, 2013
Washtakiwa kesi ya uchochezi, wizi wakana waelezo ya awali
Subscribe to:
Posts (Atom)