Na Saidi Mkabakuli
Serikali imesema kuwa ipo
katika hatua za mwisho za kukamilisha miradi ya kitaifa ya kimkakati
iliyoibuliwa katika Mpango wa Kwanza wa Maendeleo unaofikia kikomo mwaka ujao
wa fedha wa serikali.
Hayo
yalisemwa na Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt.
Mary Nagu wakati akiwasilisha Mpango wa
Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2015/16 katika Kamati ya Mpango ya Bunge Zima
kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es
Salaam.
Dkt.
Nagu alisema kuwa mpaka kufikia mwezi machi mwaka huu, serikali imefanikiwa
kutandika reli za uzito wa ratili 56.12 kwa yadi kwa umbali wa km 9 kati ya
stesheni za Lumbe, Mto Ugalla na Katumba; kukamilisha malipo ya ununuzi wa
mabehewa 274 ya mizigo ambapo mabehewa yameshaanza kupokelewa Novemba 2014;
kukamilika kwa matengenezo ya njia ya reli iliyoharibiwa na mafuriko katika
maeneo ya Ruvu – njia panda ya Mruazi.
Waziri Nagu
aliongeza kuwa kwa upande wa Barabara hatua iliyofikiwa ni pamoja na kukamilika
kwa ujenzi wa kilometa 502.6 za barabara kuu kwa kiwango cha lami dhidi ya
lengo la kilomita 560, na ukarabati wa kilomita 78.8 za barabara kuu kwa
kiwango cha lami dhidi ya lengo la kukarabati kilomita 131.5. Kwa
upande wa madaraja hatua iliyofikiwa ni: kuendelea na ujenzi wa madaraja ambapo
daraja la Kigamboni limefikia asilimia 75, Sibiti asilimia 22, Kilombero
asilimia 26, Mbutu asilimia 99, Lukuledi II asilimia 25 na Kavuu asilimia 36.
Katika sekta ya Uchukuzi, Dkt. Nagu aliyataja mafanikio yaliyopatikana ni
pamoja na kuongezeka kwa shehena iliyohudumiwa katika bandari ya Dar es Salaam
kufikia tani milioni 14.3 Machi 2015 dhidi ya lengo la tani milioni 13.0 kwa
mwaka 2014/15; kuongezeka kwa ufanisi wa bandari katika kupakua magari kwa kila
shifti moja ya saa 8 kufikia magari 886 kwa shifti kufikia Machi 2015
ikilinganishwa na lengo la magari 600 kwa shifti katika mwaka 2014/15; kupungua
kwa muda wa meli kupakia na kupakua mizigo bandarini kutoka lengo la wastani wa
siku 5 mwaka 2013/14 hadi wastani wa siku 3.7 kufikia Machi 2015; kuanza kwa
utekelezaji wa mradi wa malipo kwa njia ya mtandao mwezi Julai, 2014; na
kuanza kutoa huduma katika bandari ya
Dar es Salaam kwa masaa 24 kwa siku zote za juma. Aidha, kwa upande wa bandari ya Bagamoyo,
hatua iliyofikiwa ni kusainiwa kwa makubaliano ya ujenzi wa bandari; na
kutangazwa kwa zabuni kwa ajili ya kupata wawekezaji katika bandari za Mtwara
na Mwambani -Tanga.
“Katika sekta ya nishati,
hatua iliyofikiwa ni pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa bomba la gesi kutoka
Mtwara hadi Dar es Salaam (km 542) Machi 2015, na ujenzi wa mitambo ya
kusafisha gesi Madimba (Mtwara) na Songosongo (Lindi) umefikia asilimia 86.9
ambapo unatarajiwa kukamilika Juni 2015. Kwa upande wa usambazaji wa umeme
vijijini, wateja wapya 2,602 wameunganishiwa umeme katika mikoa ya Simiyu,
Singida, Kagera, Tanga, Ruvuma, na Iringa,” alisema Dkt. Nagu.
Kwa mujibu wa Waziri Nagu, shughuli
nyingine zilizotekelezwa nia katika sekta ya nishati, ni pamoja na
kukamilika kwa usimikaji wa mitambo 4 ya kufua umeme yenye uwezo wa jumla ya MW
150, kuendelea na ujenzi wa vituo vya
kupoza na njia za kusafirisha umeme, na kuendelea na ujenzi wa karakana, majengo ya utawala, na barabara za
ndani katika mradi wa Kinyerezi I; kukamilisha ulipaji fidia kwa eneo la
Makambako katika mradi wa usafirishaji umeme wa Makambako - Songea; na kuanza ujenzi wa nguzo za njia ya umeme
katika mradi wa msongo wa kV 400 wa Iringa – Shinyanga.
Akiwasilisha
kazi zilizotekelezwa katika sekta
ya Maji, Dkt. Nagu alisema kuwa ulazaji wa mabomba katika
mradi wa maji Ruvu Chini kutoka Bagamoyo hadi Dar es Salaam kazi ambayo
imekamilika kwa kilomita 52.43 kati ya kilomita 55.93 za mradi sawa na asilimia
93.8; kwa upande wa mradi wa maji Ruvu Juu: mkandarasi amekamilisha utafiti wa
udongo na uchunguzi wa awali wa mahali yatakapojengwa matanki Kibamba na
Kimara; na kwa upande wa mradi wa Bwawa la Kidunda, wananchi wamelipwa fidia ya shilingi bilioni
7 kupisha ujenzi wa barabara na eneo litakapojengwa bwawa.
“Kwa upande wa miradi ya
maji vijijini, jumla
ya miradi 123 ya maji ilijengwa na kukamilika. Idadi hii imenufaisha wananchi
wapatao 463,750 na kuongezeka kwa ufanisi katika masuala ya ununuzi wa huduma
katika mikataba kutoka siku 265 hadi siku 90. Aidha, Serikali imeendelea na
ujenzi wa mabwawa ambapo bwawa la Iguluba (Iringa) na Wegero (Mara)
yamekamilika. Vile vile, ujenzi wa bwawa la Kawa (Rukwa) umefikia asilimia 95,
bwawa la Sasajila (Dodoma) asilimia 66.09 na Mwanjoro (Shinyanga) asilimia
45.4,” aliongeza Waziri Nagu.
Katika sekta ya kilimo, Dkt. Nagu aliyataja mafanikio
yaliyopatikana ni pamoja na: kupatikana kwa hati za mashamba mawili ya Bagamoyo
na Mkulazi; maghala 30 yamekarabatiwa na kupatiwa watoa huduma binafsi katika
Wilaya za Mbozi na Momba. Vile vile,
skimu 30 za umwagiliaji zimepatiwa watoa huduma binafsi katika Wilaya za
Mbarali, Kyela na Iringa; na mafunzo juu ya kubaini na kudhibiti visumbufu,
matumizi bora ya maji, utunzaji na matengenezo ya miundombinu ya umwagiliaji na
kutumia mwongozo wa uendeshaji skimu za umwagiliaji yametolewa. Aidha, ujenzi wa maghala 2 katika Wilaya ya Mlele umekamilika.
Vile vile katika sekta ya viwanda, Waziri
Nagu alizitaja kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kukamilika kwa ukarabati wa
barabara ya Itoni - Mkiu - Liganga na Mchuchuma kwa kiwango cha changarawe ili
kuwezesha mitambo kufika maeneo ya Mchuchuma na Liganga; na kuanza uthamini wa
mali za wananchi watakaohama eneo la Mchuchuma. Vile vile, fidia shilingi
bilioni 53 imelipwa katika eneo la kujenga kituo cha Biashara na Huduma
Kurasini; na fidia ya shilingi bilioni 7 imelipwa katika eneo la uwekezaji
Bagamoyo na Serikali imesaini mkataba na kampuni ya China Mechants Holding International kwa ajili ya kujenga bandari
na eneo la viwanda. Aidha, katika kiwanda cha kuzalisha dawa ya kuua viluwiluwi
wa mbu, Kibaha, kazi ya ufungaji wa mitambo na ujenzi wa miundombinu inaendelea
na inatarajiwa kukamilika kabla ya Julai, 2015.
Akizungumzia upande wa maendeleo ya rasilimali watu, Dkt. Nagu
alisema kuwa kazi zilizofanyika ni pamoja na kuendelea kugharamia
wanafunzi 159 wanaoendelea na mafunzo katika fani za mafuta na gesi kwa ngazi
mbalimbali za mafunzo ndani na nje ya nchi ambapo wanafunzi 124 wanagharamiwa
na Serikali na wanafunzi 35 wanagharamiwa na nchi wahisani; na kuendelea na
ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika vyuo vikuu na vyuo vya ualimu, ufundi
na ustawi wa jamii.
Kwa
upande wa utafutaji wa rasilimali
fedha, Waziri Nagu alisema kuwa Mamlaka
ya Mapato Tanzania inatumia kanzidata bora inayohifadhi taarifa inayoweza
kuthaminisha bidhaa na hivyo kutoa makadirio bora zaidi ya viwango vya kodi.
Vilevile, alisema kuwa tozo kwa ajili ya uwekezaji katika elimu umeanza Julai 2013
ikiwa asilimia 2.5 ya mapato ghafi ya kampuni za simu.
“Katika
sekta ya fedha, kazi
zilizotekelezwa ni pamoja na kuongezea Benki ya Maendeleo ya Kilimo mtaji wa
shilingi bilioni 60; kuendelea kuongeza mtaji wa Benki ya Rasilimali kufikia
shilingi bilioni 212 ambapo mtaji kutoka Serikalini ni shilingi bilioni 152.2
na shilingi bilioni 59.8 zimetokana na malimbikizo ya faida; na mali za Benki ya Maendeleo ya Wanawake
Tanzania ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 26.5 mwaka 2013 hadi shilingi
bilioni 34.8 mwaka 2014,” alisema Dk. Nagu.
Kuhusu eneo la huduma za utalii, Dkt. Nagu aliongeza kuwa kazi zilizofanyika ni pamoja
na usanifu wa ujenzi wa Utalii House awamu ya pili na kuboreshwa kwa mfumo wa
ukusanyaji mapato (utalii, uwindaji na upigaji picha). Aidha, idadi ya watalii
kutoka nje iliongezeka kutoka watalii 1,090,905 mwaka 2013 hadi watalii
1,102,026 mwaka 2014. Vile vile mapato yatokanayo na utalii yaliongezeka kutoka
dola za Marekani bilioni 1.81 mwaka 2013 hadi dola za Marekani bilioni 1.98
mwaka 2014.
“Kwa
upande wa Biashara, hatua
iliyofikiwa ni kurekebisha
sheria ya mfumo wa stakabadhi ghalani na kutoa
elimu kwa wadau mbalimbali kuhusu mfumo huo; kuanzishwa kwa kampuni
ijulikanayo kama Tanzania Mechantile
Exchange plc kusimamia na kuendesha soko la mazao ya bidhaa na kuhamasisha
matumizi ya fursa za masoko ya mipakani, Kikanda na Kimataifa,” aliongeza.
Kwa
mujibu wa Dkt. Nagu maandalizi ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2015/16 yamezingatia maeneo ya kipaumbele yaliyoainishwa katika
malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Mpango wa Maendeleo wa Miaka
Mitano (2011/12 – 2015/16). Aidha, Mpango huu umezingatia Mkakati wa Kukuza
Uchumi na Kupunguza Umaskini – MKUKUTA II (2010/11 – 2014/15), Malengo ya
Milenia, Mwongozo wa Mpango na Bajeti
kwa mwaka 2014/15; Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo 2014/15
yaliyojadiliwa na Bunge Novemba, 2014; Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi
(2010 – 2015); na sera na mikakati ya kisekta.
====================================================
Waziri
wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu
akiwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka
2015/16 Katika Kamati ya
Mpango ya Bunge Zima kwenye Ukumbi wa Mikutano wa
Kimataifa wa Mwalimu Nyerere.
|
Sehemu ya Wabunge waliohudhuria uwasilishaji wa Mpango wa
Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2015/16 Katika Kamati ya Mpango ya Bunge Zima
wakimsikiliza Waziri wa nchi
(Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu,
Mhe. Dkt. Mary Nagu kwenye Ukumbi wa
Mikutano
wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere.
|
|
Baadhi ya Wabunge wakifuatilia kwa makini hotuba ya uwasilishaji wa Mpango wa
Maendeleo wa Taifa
wa Mwaka 2015/16 Katika Kamati ya Mpango ya Bunge Zima.
|
|
Baadhi ya wataalam kutoka
Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakifuatilia kwa makini uwasilishaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa
wa Mwaka 2015/16.
|
|
Katibu
Mtendaji wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Dkt. Philip Mpango (Kulia)
akimpongeza Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe.
Dkt. Mary
Nagu (Kushoto) mara baada ya kuwasilisha
Mpango wa Maendeleo wa
Taifa wa Mwaka 2015/16 Katika Kamati ya Mpango ya Bunge
Zima.
|
|
Naibu Katibu Mtendaji (Sekta za Uzalishaji) kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya
Mipango, Bw. Maduka Kessy (Kulia) akimpongeza Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais)
Mahusiano na Uratibu,
Mhe. Dkt. Mary Nagu (Kushoto) mara baada ya kuwasilisha Mpango wa Maendeleo wa
Taifa wa Mwaka 2015/16
Katika Kamati ya Mpango ya Bunge Zima.
|
|
Naibu Katibu Mtendaji (Huduma za Jamii na Idadi ya Watu),
Bibi Florence Mwanri (Kushoto) akiongea na Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas
Kashilila (Kulia) mara baada ya uwasilishaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa
Mwaka 2015/16 Katika Kamati ya Mpango ya Bunge Zima. Anayewasikiliza ni Naibu
Katibu Mtendaji (Sekta za Uzalishaji) kutoka
Ofisi
ya Rais, Tume ya Mipango, Bw. Maduka Kessy.
|
|
Katibu
Mtendaji wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Dkt. Philip Mpango (Kushoto)
akiongea na viongozi waandamizi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango mara baada ya
uwasilishaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka
2015/16 Katika Kamati ya Mpango ya Bunge Zima.
|
|
viongozi
waandamizi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakifuatilia uwasilishaji wa
Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka
2015/16 uliokuwa ukifanywa na Waziri wa
nchi (Ofisi ya Rais)
Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu katika Kamati ya Mpango
ya Bunge Zima.
|