Posted: 18 May 2012 01:28 AM PDT

Posted: 18 May 2012 01:14 AM PDT


Gari Toyota Cresta lenye namba T 387 BMZ, likiwa limepondeka baada ya ajali iliyosababisha kifo cha mchezaji soka nyota wa Kimataifa wa Timu ya Taifa ya Rwanda na Simba SC ya Tanzania, marehemu Patrick Mafisango, iliyotokea eneo la VETA, Barabara ya Chang'ombe, juzi usiku. . (Picha zote na Charles Lucas)
Posted: 18 May 2012 12:59 AM PDT

Posted: 18 May 2012 12:48 AM PDT

Na Elizabeth Mayemba

KIFO cha kiungo mshambulaji wa Simba raia wa Rwanda Patrick Mutesa Mafisango, kilichotokea usiku wa kuamkia jana majira ya saa 10 alfajiri, mazingira yake yalikuwa ya kusikitisha sana.
Jana vilio vilitawala nyumbani kwa mchezaji huyo huku kila mmoja asiamini kile kilichotokea hasa kwa wachezaji wenzake ambao walishindwa kujizuia na kuangua vilio.

Akizungumzia mazingira ya ajali hiyo, rafiki wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Olya Ilemba, ambaye alishuhudia kifo cha mchezaji huyo, alisema mauti ilimfika Mafisango wakati wakitokea kujirusha klabu ya Maisha, ambako bendi ya FM Akademia 'Wazee wa Ngwasuma' walikuwa wakipiga siku hiyo.

"Baada ya muziki kumalizika tuliondoka mimi Mafisango na watu wengine watatu, Mafisango ndiye alikuwa akiendesha gari aina ya Toyota Cresta nyeupe, lakini alikuwa akiendesha kwa mwendo wa kasi sana, tulipomuuliza akasema kuwa amechoka anahitaji kupumzika hivyo tumuache," alisema Olya.

Alisema walipofika maeneo ya VETA chuo cha ufundi Chang'ombe eneo ambalo unamalizikia ukuta, walikutana na mwendesha guta hivyo Mafisango akajaribu kumkwepa, lakini akiwa katika harakati hizo ghafla ilitokea pikipiki ambayo ilikuwa mwendo wa kasi sana.

Olya anasema wakati Mafisango anajaribu kumkwepa mwendesha Pikipiki bahati mbaya gari iliacha njia na kuparamia mtaro ambapo mbele yake kulikuwa na miti hivyo akaing'oa.

"Kwakweli ile ajali ilikuwa mbaya sana kwani baada ya gari kusimama tulimfuata Mafisango na kumkuta jicho la upande wa kushoto likiwa limechomoka huku akiwa ameumia vibaya kichwani,  tukajaribu kuondoa kiwiliwili ambacho kilikuwa kimegandamizwa na usukani," alisema

Baada ya kumtoa hapo anasema kuna rafiki yao mwingine Gaspa Karemera alikuwa amechanganyikiwa baada ya kuhisi kuwa Mafisango amefariki, lakini alimwambia wajikaze ili wampeleke hospitali.

Anasema habati nzuri kuna teksi ilikuwa inapita hivyo wakaisimamisha na kumpakia mpaka hospitali ya taifa ya Muhimbili ambapo baadaye walithibitisha kifo chake.

"Inauma sana dada, Mafisango kipenzi chetu ametuacha wakati bado tunamuhitaji, tena ilikuwa jana (leo) aondoke kwenda kwao Rwanda kujiunga na timu ya taifa ya huko, lakini safari yake imekuwa ni kifo," alisema huku akilia Olya.

Msiba wa Mafisango upo Chang'ombe maduka mawili kwenye nyumba wanayoishi wachezaji wenzake, Gervas Kago raia wa Afrika ya Kati na Mganda Derrick Wallulya, inasemekana nyumba anayoishi marehemu nafasi ni finyu hivyo msiba wakahamishia kwa wenzake.

Taarifa ambazo zimelifikia gazeti hili ni kwamba mwili wa marehemu utaagwa leo kwenye viwanja vya TTC  Club Chang'ombe, kuanzia saa nne  asubuhi,kabla ya kusafirishwa saa 10 jioni kwenda kwao Rwanda kwa ajili ya taratibu za mazishi.Marehemu  ameacha mke na mtoto mmoja wa  kiume, Chris Paul, mwenye umri wa miaka mitano

Wakati huo huo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji huyo  wa Simba na timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi), Patrick Mafisango kilichotokea jana  alfajiri kwa ajali ya gari Dar es Salaam.

Katika taarifa iliyotolewa na Ofisa habari wa Shirikisho hilo, Boniface Wambura ilieleza  kuwa, msiba huo ni mkubwa kwa familia ya mpira wa miguu kwani Mafisango kwa kipindi chote alichocheza mpira hapa nchini akiwa na timu za Azam na baadaye Simba, aliifanya kazi yake  kwa bidii.

"Kifo chake ni pigo kubwa si tu kwa familia yake na timu alizochezea, bali ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati ambapo changamoto zake zilikuwa dhahiri uwanjani,"ilieleza sehemu ya taarifa.

"TFF inatoa pole kwa familia ya Mafisango, klabu ya Simba, Shirikisho la Mpira wa Miguu Rwanda (FERWAFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito na Mungu aiweke roho ya marehemu Mafisango mahali pema peponi. Amina,"iliongeza tarifa hiyo.

Pia kiungo wa Yanga Haruna Niyonzima alisema kuwa msiba huo ni mzito sana kwa Mnyarwanda mwenzake, kwani jana saa ambayo Mafisango alipata ajali na kufariki ulikuwa muda wa yeye kuondoka kwenda Rwanda kujiunga na timu ya taifa ya Amavubi.

"Lakini cha kushangaza nilipoondoka nyumbani nilisahau tiketi ya ndege, ile na fika uwanja wa ndege nakumbuka kuwa sikubeba tiketi, wakati narudi nyumbani iliingia simu ya kunitaarifu msiba huo, kwakweli sikuamini mpaka pale nilipoenda Muhimbili," alisema Niyonzima.

Alisema kumbe zote hizo zilikuwa ni dalili kwani haikuwahi hata siku moja akasahau tiketi, lakini jana hali hiyo ilimkuta ambapo anasema siku moja kabla ya kifo chake walizungumza sana.

"Hakusita kunikumbusha kuwa, nitunze jezi yake namba 30 ambayo tulibadilishana wakati tulipocheza nao na sisi kufungwa mabao 5-0, aliniambia  kuwa jezi hiyo nisiigawe kwa mtu yeyote kwani itakuwa ni kumbukumbu yangu, kumbe jamaa kama alijua anakufa, nitamkumbuka daima,"alisema Niyonzima

Nao wachezaji wa timu ya taifa, Taifa Stars' wale wa Simba baada ya kupata taarifa za msiba huo walijikuta wakinyong'onyea na kushindwa kufanya mazoezi kabisa ambayo  yalikuwa yakifanyika Uwanja wa Karume chini ya kocha wao mpya Kim Poulsen.

Wachezaji wa Simba Juma Kaseja na Amir Maftah walishindwa kujizuia na hivyo kuangua vilio ambapo walishindwa kabisa kufanya mazoezi, ambapo daktari wa timu hiyo Mwanandi Mwamkemwa alikuwa akifanya kazi ya ziada ya kuwapa maneno ya kuwafariji.

Hata hivyo mazoezi yalipomalizika, wachezaji wote waliruhusiwa kwenda kwenye msiba wa mchezaji mwenzao, huku Boban akiunganisha moja kwa moja Muhimbili ambako ulihifadhiwa mwili wa marehemu.

Mafisango alikuja nchini mwaka juzi na kujiunga na timu ya Azam FC kabla ya kuhamia Simba mwaka jana, alizaliwa Machi 7, mwaka 1987 mjini Kinshasa, DRC alikoanzia soka kabla ya kuhamia Rwanda, ambako baadaye alichukua uraia wa nchi hiyo.

Kabla ya kuja Tanzania aliichezea timu ya  APR ya Rwanda na  Mechi ya mwisho kuichezea Simba ilikuwa dhidi ya Al Ahly Shandy  yaSudan  iliyofanyika  Jumapili katika hatua ya 16  Bora ya Kombe la Shirikisho, ambayo Simba ilitolewa kwa penalti 9-8, kufuatia sare ya jumla ya 3-3.
Posted: 18 May 2012 12:42 AM PDT
Wachezaji wa timu ya Simba na timu ya taifa, Taifa Stars, Juma Kaseja na Amir Maftah (kulia) wakiwa na huzuni, baada ya kupata taarifa za kifo cha mchezaji mwenzao, Patrick Mafisango, wakati wakiwa mazoezini uwanja wa Karume,Dar es Salaam jana.Wachezaji hao walisitisha mazoezi kutokana mshituko wa kufiwa na mwenzao.(Picha na Rajabu Mhamila)
Posted: 18 May 2012 12:29 AM PDT

Posted: 18 May 2012 12:26 AM PDT

Mgambo wa Manispaa ya Ilala wakisukuma mikokoteni yenye bidhaa mbalimbali za wafanyabiashara ndogondogo baada ya kuwakamata wakifanyabiashara kwenye eneo lisiloruhusiwa Kariakoo Dar es salaam jana. (Picha na Rajabu Mhamila)
Posted: 18 May 2012 12:16 AM PDT

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usajiri wa Kampuni nchini (BRELA), Bw. Esteliano Mahingila, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), Dar es Salaam jana, kuhusu tuzo zilizotolewa na taasisi za kimataifa kwa mamlaka hiyo na Kampuni za BRAVO Logistics Limited, na Kampuni ya Uhandisi ya NEWL, baada ya kufikia vigezo vya utendaji bora wenye kiwango cha kimataifa, kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa NEWL, Bw. Samwel Lema. (Picha na Charles Lucas)
Posted: 18 May 2012 12:08 AM PDT


Mkazi wa jiji mwenye asili ya kimasai alikutwa ameketi kwenye njia ya treni bila kujali usalama wake, kama alivyokutwa na mpigapicha wetu, eneo la Shaurimoyo Ilala, Dar es Salaam jana, haikufahamika tatizo lililosababisha kuketi hapo. (Picha na Charles Lucas)
Posted: 17 May 2012 11:57 PM PDT
Meli ikizama.Ajali za vyombo vya usafiri majini zinaweza kupungua kukiwa na ukaguzi wa vyombo hivyo kabla ya kuanza safari.
Posted: 17 May 2012 11:53 PM PDT


Na Tumaini Maduhu

SEKTA ya usafirishaji  ni moja ya kiunganishi cha maendeleo nchini kutokana na umuhimu wake wa kuunganisha sehemu moja na nyingine.
Sera ya Taifa ya Usafiri ya mwaka 2003 ambayo sasa inafanyiwa maboresho ili iende sambamba na mpango mpya wa serikali wa miaka mitano, yaani 2012/2017 itazingatia maendeleo na teknolojia mpya ijitokeze katika uendeshaji wa sekta ya usafiri wa anga kitaifa na kimatifa.

Sekta hii imekuwa, ikiwakomboa watu kwa kufanikisha majukumu yao kwa kuwarahisishia kubalishana bidhaa mbalimbali na kuwatoa watu sehemu moja kwenda nyingine.
Ni ukweli usiopingika kuwa, nchi yeyote Duniani bila kuwa na usafiri ni sawa usiku wa giza ambao haujui ni lini utapata mwanga wakuangaza.
Hali hii imejidhihirisha, kutokana na watu wengi kukwama katika majukumu yao kutokana na kukosa usafiri.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu Sumatra Bw. Ahmad Kilima anasema, mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Shirika la la usafiri wa baharini Duniani(IMO) wameamdaa warsha  kwa wasafirishaji wa baharini ili kuwajengea ujuzi na weledi wa kudhibiti ajali za baharini.

Anasema kuwa, warsha hiyo imeshirikisha mabaharia, wamiliki wa vyombo vya usafirishaji baharini, chuo cha usafirishaji (DMI).

"Tunaamini mafunzo, haya yatawajengea ujuzi na weledi ambao utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ajali baharini pamoja na namna ya kukagua vyombo vyao kabla ya kusafirisha abiria," anasema Bw Kilima.

Anasema kuwa, kupitia warsha hiyo wanaamini ajali zitapungua baharini kutokana na wadau kutoka sekta mbalimbali za usafirishaji na Wizara husika kutoa mchango wao namna ya kudhibiti ajali za baharini.

Bw.Kilima anasema kuwa, katika kuhakikisha ajali za baharini zinapungua mamlaka hiyo inajitahidi kukagua vyombo vya usafirishaji kabla ya kutoa leseni ili kudhibiti ajali za baharini.

Anasema kuwa, njia nyingine inayotumiwa na mamlaka hiyo katika kuhakikisha wanadhibiti ajali za baharini ni kuvifungia baadhi ya vyombo vinavyosababisha ajali kwa uzembe na kupoteza maisha ya watu.

"Tumeamua kutoa, adhabu hii ikiwa ni moja ya mpango mkakati wetu wa kuhakikisha tunadhibiti ajali zinazosababishwa  na madereva wazembe," anasema, Bw Kilima.

Anatoa mwito kwa vijana kusomea taaluma ya ubaharia ili wapatikane wataalamu wenye mwamko  na wenye tija katika kudhibiti ajali za baharini.

Anasema kuwa, vijana wengi wakiwa na mwamko wa kusomea fani ya ubaharia kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ajali zisizokuwa za lazima.

Hata hivyo anasema kuwa, mamlaka hiyo imekuwa ikikikaa na wamiliki wa vyombo vya usafiri mara kwa mara ili kujengeana ujuzi na uzoefu wa kudhibiti ajali za baharini.

"Tunaamini tukishirikiana na wamiliki wa vyombo vya usafiri  pamoja na mamlaka tutaweza kudhibiti ajali zisizokuwa za lazima zinazopoteza nguvukazi ya taifa," anasema Bw Kilima.

Anasema, wamiliki wa vyombo vya usafiri wanatatakiwa kuwakabidhi watu wenye stahiki katika vyombo vyao ili kudhibiti tatizo la ajali baharini.

"Hili nalo tumaeliangalia, kwa kiasi kikubwa ndiyo maana tumeamua kushirikiana na shirika la usafirishaji duniani ili kuondoa dosari zilizopo baharini," anasema.

Bw. Kilima anasema kuwa, warsha hiyo itakuwa endelevu ili kuileta hamasa katika kubadilishana ujuzi na uzoefu wa kudhibiti ajali zisizo za lazima baharini.

Zimekuwa zikisaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ajali za baharini kutokana na wadau kutoka sehemu mbalimbali za usafirishaji kutoa michango yao ya mawazo ni nini kifanyike ili kuondoa tatizo la ajali za baharini.
Anasema kuwa, mwamko wa watu katika taaluma ya ubaharia majini ni mdogo ndiyo maana kumekuwepo na watu wanaoifanya pasipokuwa na sifa stahiki za fani hiyo.
Anasema, hilo ni tatizo kubwa nchini ndiyo maana kumekuwepo na za baharini mara kwa mara.

Hata hivyo anasema kuwa,  ili kuondoa tatizo hilo kunatakiwa kuwepo na wataalamu wenye sifa stahiki katika fani ili kuondoa ajali zisizokuwa na lazima.
"Ajali kama hizi zinaepukika kama kila mwajiri na mmiliki wa vyombo hivi wataamua kuwajiri watu wenye sifa stahiki za taaluma hii," .

Anatoa wito kwa, vijana kusomea taaluma hiyo ili iwe changamoto kwao katika kuhakikisha wanadhibiti ajali za baharini.
Pia, Desemba 7 ya kila mwaka Tanzania na mataifa 190 duniani ambayo ni wanachama wa Shirika la Kimataifa  la Usafiri wa Anga (ICAO) huungana katika kuadhimisha uwekwaji saini wa mapatano ya kimataifa kuhusu usafiri wa anga ulimwenguni.

Maadhimisho hayo pia yamelenga kuwaongezea ufahamu wananchi wa Tanzania juu ya umuhimu wa sekta ya usafiri wa anga katika kuchochea maendeleo ya jamii, kuimarisha uchumi wa taifa na kuboresha mahusiano kati yao na mataifa mengine.
Wananchi hupata fursa kuelezea shughuli na majukumu waliopewa kisheria katika kusimamia na kuratibu usalama na ufanisi wa usafiri wa anga nchini.


Posted: 17 May 2012 11:49 PM PDT
Mkulima akivuna kahawa. Wakulima wakijiunga katika vikundi watapatiwa mkopo na kuongeza uzalishaji zaidi.
Posted: 17 May 2012 11:09 PM PDT

Na Kassian Nyandindi

SERIKALI imekuwa ikisisitiza wakulima wanaozalisha mazao ya aina mbalimbali kuanzisha vikundi ambavyo wakijiunga kwa pamoja wataweza kuuza mazao yao kwa urahisi bila kurubuniwa na wafanyabiashara wajanja.
Vikundi hivyo ambavyo husisitizwa kuvisajili kisheria ili viweze kutambulika, kuwa na nguvu ya kukopesheka kutoka katika taasisi mbalimbali za kifedha kama vile benki.

Kuwaelimisha wakulima katika hili, ni suala ambalo wataalamu wa sekta husika walipewa kulikeleza kwa vitendo, kuhakikisha kwamba wakulima wanaozalisha mazao ya biashara wanapewa kipaumbele katika kuelimishwa juu ya umuhimu wa kujiunga pamoja ambapo baadaye ni ukombozi mkubwa kwao.

Wakulima wa kahawa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameitikia wito wa kuanzisha vikundi ambavyo sasa vimesajiliwa chini ya wizara ya katiba na sheria (RITA) ili kupata haki zao za msingi.Vikundi 55 wilayani hapa vinavyozalisha kahawa vimekabidhiwa vyeti vya usajili, ili waweze kuuza kahawa yao moja kwa moja mnadani Moshi na hata kwa minada ya nje ya nchi.

Jitihada hizo ni wazo lililotolewa kwa mara ya kwanza na Mbunge wa Mbinga Mashariki Bw. Gaudence Kayombo, kwa lengo la kumwezesha mkulima wa zao hilo, aweze kuuza kahawa yake moja kwa moja mnadani na sio kupitia makampuni binafsi.
Mchango huu uliotolewa na Mbunge huyu ni wa kuungwa mkono kwani utaweza kumsaidia mkulima hata kupata malipo ya kahawa yake kwa bei ya uhakika, sio kama ilivyokuwa kwa miaka nyuma ambapo hakunufaika na chochote katika kilimo cha zao hilo kutokana na wafanyabiashara wajanja kumuibia.

Bw. Kayombo ameviunganisha vikundi hivyo ili viweze kupata mkopo wa fedha kwa kila kikundi, za kununulia kahawa kavu katika msimu wa mavuno ya zao hilo unaotarajiwa kuanza Julai Mosi mwaka  huu.Mikopo hiyo itatolewa kwa vikundi ambavyo vitakidhi vigezo vya kukopesheka kulingana na dhamana walizonazo ambazo benki itaridhia.

Usajili huu unavifanya vikundi viweze kutambulika, kuwa na nguvu ya kisheria katika utendaji wa kazi zao za kila siku, hali ambayo itawafanya waweze kuboresha zao la kahawa na kuongeza thamani ya uzalishaji.

Katika sherehe za kukabidhi vyeti vya usajili kwa vikundi hivyo zilizofanyika hivi karibuni katika kijiji cha Linda kata ya Linda, Ofisa Maendeleo ya Jamii Bw. Paschal Ndunguru ambaye alikuwa akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, anasema ni fursa ya kipekee kwa wanavikundi hao kufanya hivyo kwani kutawawezesha kufanya shughuli zao za uzalishaji kwa viwango vinavyotakiwa.
Bw. Ndunguru anasema, ili waweze kuwa endelevu wanapouza kahawa na kupata malipo, wanakikundi wanatakiwa wawe na nidhamu nzuri katika matumizi ya fedha na sio kuzitumia hovyo katika masuala ya anasa, badala yake wanunue pembejeo za kuendeleza zao hilo na kufanya maendeleo mengine ikiwemo kupeleka watoto shule.

“Ninawasihi tuachane na anasa za dunia hii, tuzingatie kupeleka watoto wetu shule na kufanya mambo mengine ya kimaendeleo katika maisha yetu”, anasisitiza.
Amevishauri, vikundi hivyo kuweka mfumo mzuri wa mapato na matumizi katika kikundi husika, ili kuepukana na malalamiko yasiyo ya lazima miongoni mwao.
“Ndugu zangu tuwe tunajituma katika kazi na kujenga dhana ya kidemokrasia katika kufanya vikao mara kwa mara ndani ya vikundi, hali ya uchumi hivi sasa sio nzuri vijana tuhakikishe tunajituma katika uzalishaji hususani kwenye kilimo”, anasema Bw. Ndunguru.

Anasema, halmashauri ya wilaya hiyo katika bajeti ya mwaka huu, imejiwekea mikakati kuhakikisha kwamba zao la kahawa linaboreshwa kwa kiwango cha juu, ikiwemo kuwaelimisha wakulima juu ya utunzaji na upuliziaji wa madawa ya kuua wadudu aina ya vidung’ata ambavyo vimekuwa vikishambulia zao hilo kwa kasi.

"Maisha bora hayawezi kuja kama watu tunakuwa na umaskini wa mawazo, hivyo binadamu kujituma katika kufanya kazi mbalimbali za kimaendeleo ndio msingi wa kupiga hatua katika maisha" anasema.Pamoja na mambo mengine wakulima hao wameshauriwa kwenda katika vituo vya afya au hospitali kupima afya zao mapema, ili waweze kujitambua kama wana magonjwa watibiwe mapema na hatimaye wasiweze kupoteza nguvu kazi ya taifa hili, katika kuendeleza kilimo cha kahawa.

Wahenga husema kilimo ndio uti wa mgongo, hivyo kinachotakiwa sasa ni kuendelea kujituma ili kuhakikisha wanayafikia malengo waliyojiwekea.Katika maeneo mengi nchini na duniani kilimo, huchangia maendeleo ya mahali husika kwa kiasi kikubwa, endapo tu kanuni bora za kilimo zikifuatwa katika uzalishaji wa mazao mbalimbali.

Sasa yatupasa katika kuyasemea haya tunataka kuone utekelezaji kwa njia ya vitendo, na sio wataalamu kuendelea kukaa maofisini na kufanya kazi kwa mazoea katika mafaili tu, wakati mkulima aliyekuwa kijijini anasubiri  huduma kupitia utaalamu hao.