Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ameeleza kuwa zabuni ya vitalu vya utafiti wa
mafuta na gesi asilia vilivyo bahari kuu na ziwa Tanganyika kaskazini itafungwa
tarehe 15 mwezi wa tano mwaka huu.
Waziri Muhongo
alisema hayo wakati alipofanya mazungumzo na Waziri mstaafu wa Nishati na
Viwanda kutoka nchini ufaransa Bw.Erick Besson aliyemtembelea wizarani ili
kufahamu fursa za uwekezaji zilizo katika sekta za Nishati na Madini
akiiwakilisha kampuni ya GDF Suez ya Ufaransa.
“Kampuni
unayoiwakilisha ni kubwa, yenye teknolojia ya kisasa na inafanya uwekezaji
mkubwa duniani hivyo kama mna nia ya kuwekeza katika uendelezaji wa vitalu vya
gesi mnaweza kuingia katika ushindani wa kumiliki vitalu hivyo kwani muda bado
unaruhusu”. Alisema Profesa Muhongo.
Waziri Muhongo
alimweleza Bw. Besson kwamba Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) linamiliki
vitalu viwili vya gesi karibu na mpaka wa Msumbiji lakini linahitaji mbia mwenye
nia ya dhati watakayeshirikiana naye katika hatua zote za uendelezaji wa vitalu,
kwa sababu TPDC bado inakua, alitoa changamoto kwa kampuni hiyo ya GDF Suez
kuingia katika ushindani huo.
Katika suala la
usimamizi wa bomba la gesi asilia, Profesa Muhongo alimweleza Bw. Besson kuwa
TPDC pia itahitaji kupata uzoefu na pengine mbia aliyebobea katika usimamizi wa
bomba hilo atakayeshirikiana na TPDC katika usimamizi wa bomba la gesi nchini.
Profesa Muhongo alisema Serikali itasambaza
gesi katika makazi ya watu ili kupunguza uharibifu wa mazingira huku akitoa
mfano kuwa jiji la Dar es Salaam pekee linatumia si chini ya magunia 50 ya mkaa
kwa siku hivyo gesi itapunguza uharibifu wa mazingira.
Alisema huo ni mpango
endelevu kwani tayari kuna bomba la urefu wa la 6.3 kilometa kutoka Ubungo hadi
Mikocheni linalotoa gesi majumbani na bei yake haizidi shilingi 12,500 kwa
mwezi.
Alisema kuwa TPDC
itahitaji mbia katika utekelezaji wa mpango huo wa usambazaji gesi majumbani na
katika sehemu ambazo bomba la gesi haliwezi kupita kutahitajika mitungi ya gesi
ili wananchi wote wafaidi gesi hiyo.
Kuhusu umeme, Waziri
Muhongo alimweleza Waziri mstaafu huyo wa Ufaransa kwamba serikali inajikita
katika miradi ya usambazaji umeme kwa utaratibu wa ubia au mikopo ya bei nafuu na
ina mpango wa kujenga njia ya umeme ya msongo wa 400kv kuelekea ziwa Tanganyika
hivyo aliikaribisha kampuni ya GD Suez kuwekeza katika miradi hiyo ya
usambazaji umeme.
“Tunatafuta pia
wawekezaji katika suala la usambazaji umeme na ujengaji wa vituo vya kupooza
umeme na transfoma kubwa kwani tumeamua kufanya uwekezaji mkubwa katika eneo
hili mf. jijini Dar es Salaam tulikuwa
na vituo vitano tu vya kupoozea umeme lakini sasa tunajenga vingine vitano
vikubwa na vidogo 15 ili kutatua tatizo la umeme jijini Dar es Salaam hivyo
unakaribishwa kuwekeza katika eneo hili pia”. Alisema Profesa Muhongo
Aidha Profesa Muhongo
alimweleza Bw. Besson kuwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) linatafuta mbia
watakayeshirikiana naye katika kuendesha mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia
makaa ya mawe Kiwira mkoani Mbeya hivyo kama wana nia ya kuwekeza katika eneo
hilo pia wanakaribishwa kuingia katika ushindani wa kupata nafasi hiyo.
Naye Waziri mstaafu
wa Viwanda na Nishati kutoka nchini Ufaransa, Bw. Besson alimshukuru Profesa
Muhongo kwa taarifa nzuri kuhusu fursa
za uwekezaji nchini na ameahidi kupata taarifa zaidi za uwekezaji katika
mashirika ya TPDC, STAMICO na TANESCO ili kuona jinsi kampuni ya Suez
itakavyoshirikiana na mashirika hayo katika kuendeleza sekta za Nishati na Madini.
PICHANI JUU:
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akiwa
pamoja na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Marcel Escure (kulia kwa Waziri) pamoja
na Waziri Mstaafu wa Viwanda na Nishati wa Ufaransa Bw. Eric Besson (kulia kwa
Balozi), pamoja na watendaji kutoka Ubalozi wa Ufaransa na Wizara ya
Nishati na Madini, wakati walipomtembelea wizarani ili kufahamu fursa za
uwekezaji katika sekta za Nishati na Madini..