MKE
WA WAZIRI MKUU, Mama Tunu Pinda amewataka wazazi hapa nchini watoe
kipaumbele kwenye suala la elimu kwa vijana bila ubaguzi wa kijinsia.
Ametoa
wito huo leo mchana (Jumamosi, Machi 8, 2014) wakati akifungua
Kongamano la Wanawake wa Afrika ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya
Wanawake Duniani lililofanyika kwenye ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es
Salaam.
Kongamano
hilo liliandaliwa na Chama cha Walimu Wanawake Tanzania (Tanzania Women
Teachers’ Association – TAWOTEA) kwa kushirikiana na taasisi ya African
Women Charity Organisation ya Oakland, California, Marekani.
Akizungumza
na washiriki wa kongamano hilo, Mama Tunu Pinda alisema: ”Ninawaomba
wazazi wenzangu, wake kwa waume tuungane kwa pamoja kwa kutoa kipaumbele
kwenye suala zima la elimu kwa vijana wetu bila ubaguzi wa kijinsia.
Kwa kufanya hivyo tutawajenga wavulana na wasichana ili wawe na uwezo wa
kiuchumi na uthubutu katika masuala ya uongozi na maisha yao ya
baadaye.”
Akizindua
mfuko wa elimu ulioanzishwa na chama hicho, Mama Pinda alisema ana
imani utakuwa endelevu na utakidhi malengo ya kuazishwa kwake ambayo ni
kuwasaidia watoto wenye uhitaji na waishio kwenye mazingira ili wapate
elimu ya msingi na ya sekondari.
”Mkiwa
ni waalimu wanawake na tena ni walezi wa watoto wetu, mmefanya jambo
kubwa na la kihistoria kwa kuanzisha mfuko wa elimu mlioamua kuuita Tanzania Education Fund (TEF). Nimedokezwa
kwamba malengo ya mfuko huu ni kusaidia gharama za elimu ya msingi na
sekondari kwa watoto wa kike na wa kiume na hasa kwa watoto walio kwenye
mazingira magumu na wenye uhitaji. Ni matumaini yangu kwamba utakuwa
endelevu.”
”Ni
imani yangu kwamba kupitia mfuko huu unaozinduliwa rasmi leo hii,
utaowaongezea vijana wetu wa kike na wa kiume wigo wa kupata elimu
ambapo kama mfuko huu usingekuwepo, isingekuwa rahisi kwao kumudu
gharama za masomo,” aliongeza.
Aliwaomba
wadau wote wa elimu na wananchi kwa ujumla, waunge mkono juhudi za
walimu hao katika kuikomboa nchi hii, hasa katika sekta ya elimu huku
wakiamini elimu ni ufunguo wa maisha.
Mapema,
akisoma risala yao, Mkurugenzi Mtendaji wa TAWOTEA, Mwl. Neema Kabale
alisema asasi hiyo ambayo imesajiliwa tangu mwaka 2008, inajihusisha na
utetezi wa haki za msingi za wanawake, wasichana, vijana na watoto
katika masuala ya elimu, afya, na upatikanaji wa chakula.
Katika
kongamano hilo la siku moja, asasi hiyo iliandaa mada sita zikiwemo za
“Ushiriki wa wanaume katika ukombozi wa mwanamke” na “Majukumu ya Vijana
katika Muungano wa Afrika”.
Akitoa
hitoria fupi ya Kongamano la Wanawake Afrika, Rais wa taasisi ya
African Women Charity Organisation ya Oakland, Marekani, Bi. Rwanda
Saleem, alisema Tanzania ni nchi ya nane kupata fursa ya kuratibu wa
kongamano kama hili.
”Barani
Afrika tayari nchi saba zimekuwa waratibu wa kongamano hili ambazo ni
Ghana, Guinea, Gambia, Senegal, Kenya, Rwanda, na Msumbiji ambayo
ilikuwa mwenyeji mwaka jana. Tanzania imepewa fursa ya kuandaa kongamano
hili mwaka huu,” aliongeza.
Kaulimbiu
ya kongamano hilo ni “Kujenga Muungano wa Afrika kwa Kushirikisha
Wanawake kwenye Uongozi” (The Unification of Africa Through the
Emancipation of Leadership of Women).
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM.
JUMAMOSI, MACHI 8, 2014