Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akizungumza kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Prof. Jakaya Mrisho Kikwete kwenye ufunguzi wa mkutano mkubwa wa
kudhibiti ujangili na hifadhi endelevu ya wanyamapori uliofanyika kwenye
ukumbi wa mikutano wa makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini
Arusha. (Picha zote na Zainul Mzige wa MOblog)
Na Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete ameitaka
jumuiya ya kimataifa kushirikiana na Tanzania katika kukabiliana na
majangili wanaomaliza tembo kwa lengo la kupata pembe zao.
Alisema kutokana na biashara nzuri ya pembe hiuzo duniani majangili wamekuwa na soko tayari kiasi cha kuendeleza vitendo vyao.
Alisema mitandao iliyopo
inawezesha kuuawa kwa tembo hao na kufikishwa bidhaa za pembe katika
soko haramu ambalo lipo duniani na hivyo bila ushirikiano wa kimataifa
wanyama hao ambao ni urithi wa dunia watatoweka kabisa katika miaka
ijayo.
Amesema takwimu zilizopo sasa nchini za tembo zinatisha.
Alisema mathalani kwa ujangili
pekee kwenye mfumo wa ekolojia wa Selou-Mikumi tembo waliobaki ni
13,084 kwa mwaka jana kutoka Tembo 109,419 waliokuwepo mwaka 2006.
Alisema mfumo uliopo wa ujangili
na soko la bidhaa hizo unafanya vita inayoendeshwa na Tanzania kuwa
ngumu kama haitapata ushirikiano na mataifa mengine.
Alisema kutokana na ukweli huo
wanataka mataifa jirani na jumuiya ya kimataifa kuingia katika mapambano
ya kudhibiti biashara hiyo na hivyo kuwamaliza majangili na kuendelea
kuhifadhi Tembo.
Katika hotuba yake iliyosomwa kwa
niaba yake na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu kwenye
ufunguzi wa mkutano mkubwa wa kudhibiti ujangili na hifadhi endelevu ya
wanyamapori, alisema serikali ya Tanzania imeanzisha mchakato wa kulinda
wanyama pori.
Baadhi ya wadau kutoka nchi
mbalimbali wanaohudhiria mkutano huo akiwemo Mratibu Mkazi wa mashirika
ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa
Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (wa pili kushoto).
Mchakato huo ni pamoja na kuimarisha doria , kuendesha operesheni za kukabiliana na ujangili.
Alisema pamoja na kuwapo kwa
juhudi za makusudi za kukabiliana na ujangili serikali ya Tanzania
imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za kifedha na
raslimali watu.
Aidha kumekuwepo na ushiriki mdogo kutoka kwa wananchi katika vita dhidi ya ujangili.
Alisema kutokana na haja ya kukabili ujangili na kuwa na hifadhi endelevu, Februari mwaka huu mataifa ya Botswana,
Chad, Garbon na Ethiopia yalitiliana saini mkataba wenye lengo la
kupunguza mahitaji ya bidhaa za wanyamapori, kuimarisha sheria zilizopo
dhidi ya ujangili na pia hifadhi na kusaidia maendeleo ya maeneo
yanayokabiliwa na changamoto ya uwindaji haramu.
Rais Kikwete alisema katika hotuba
yake kwamba kuwepo kwa mataifa hayo katika mkutano huo ni kuendeleza
makubalino ya kutojishughulisha na biashara za bidhaa za wanyamapori kwa
miaka 10 au hadi hapo tembo waliopo bara la Afrika watakapokuwa
wameondoka katika hatari ya kuangamizwa katika uso wa dunia na
majangili.
Mratibu Mkazi wa mashirika ya
Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa
Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez, akizungumza kwenye mkutano
mkubwa wa kudhibiti ujangili na hifadhi endelevu ya wanyamapori
uliofunguliwa rasmi leo jijini Arusha kwenye ukumbi wa mikutano wa makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aidha rais alisema kwamba mkutano
huo wa Arusha unatarajiwa kuona namna ya kuendelea utekelezaji wa
makubaliano ya London, Uingereza ya hifadhi ya wanyamapori walio katika
hatari ya kutoweka akiwemo Tembo.
Alisema kutokana na mfumo wa
ikolojia na hifadhi ya wanyama na majirani zake, Tanzania inataka
majirani kushiriki katika kulinda na kuhifadhi ikolojia hiyo na wanyama
waliopo na sio kuiachia Tanzania pekee.
Tanzania ikiwa na eneo la kilomita
za mraba 943,000 asilimia 30 ya eneo lake na 15 imetumika kwa hifadhi
ya wanyamapori na misitu.
Amesema eneo hilo hutumiwa zaidi
kwa ajili ya utalii wa wanyamapori ambapo asilimia 17 ya pato la taifa
linatokana na utalii huo.
Wakati huo huo Mratibu Mkazi wa
mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la
Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez ,ameipongeza Tanzania
kwa kuitisha kikao cha kujadili ujangili na uhifadhi endelevu wa misitu.
Mwenyekiti wa mkutano mkubwa
wa kudhibiti ujangili na hifadhi endelevu ya wanyamapori ambaye pia ni
Makamu mwenyekiti wa ICCF Group, Dr. Kaush Arha akiwakaribisha wadau
wanaoshiriki mkutano huo kutoa maoni yao katika udhibiti wa ujangili
ulioshika kasi.
Akizungumza kwa niaba ya mashirika
ya Umoja wa Mataifa yaliyopo Kenya na Msumbiji alisema Umoja wa Mataifa
unajisikia furaha kuona mataifa wanachama yanakabilian na changamoto
ya ujangili na uhifadhi wa misitu kwa namna ambavyo itasaidia kizazi
kijacho.
Mratibu huyo alisema kwamba ujangili unatishia maendeleo, mazingira na usalama kitu ambacho Umoja wa Mataifa unakipiga vita.
Anasema biashara ya bidhaa za
wanyamapori zinahatarisha uwepo wa wanyama ambao tayari wapo katika
hatari ya kutoweka, unasababisha rushwa na migogoro ambayo inahatarisha
maihsa ya watu.
Alisema kwa sasa dunia imekuwa
ikipungukiwa na tembo wa Afrika kwa kasi isiyokubalika kutokana na
vitendo vya majangili na hivyo kutaka jamii kushirtikiana kukabiliana na vitendo hivyo.
Mratibu huyo amesema uhalifu unaofanyika kwa wanyamapori na misitu ni lazima ukomeshwe kwa manufaa ya wananchi .
Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Tonia Kandiero akizungumza katika mkutano huo.
Alisema Tanzania inastahili
kupongezwa kwa kuitisha mkutano wa kujadili ujangili Mei mwaka huu na
sasa kuwa mwenyeji wa mkutano wa kikanda wa kukabiliana na ujangili.
Alisema Umoja wa Mataifa
utaendelea kuimarisha ushirikiano wake na mamlaka mbalimbali
zinazoendelea kukabiliana na ujangili na kupotea kwa misitu duniani ili
kuhifadhi urithi wa dunia.
Alisema Umoja huo kupitia
mashirika yake mbalimbali watawezesha mambo mbalimbali ili kukabiliana
na ujangili na uharibifu wa misitu.
Alisema itaendelea kusapoti
programu zinazokuza uchumi wa wananchi waliopo karibu na hifadhi za
wanyamapori na misitu ili waone umuhimu wa kushiriki kuhifadhi wanyama
na misitu husika.
Balozi wa Finland nchini
Tanzania, Mh. Sinikka Antila pamoja na Balozi wa Ujerumani nchini, Egon
Kochanke nao ni miongoni mwa wadau wanaohudhuria mkutano huo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano),Ummy Mwalimu akishiriki mkutano huo.
Mwenyekiti wa mkutano mkubwa
wa kudhibiti ujangili na hifadhi endelevu ya wanyamapori ambaye pia ni
Makamu mwenyekiti wa ICCF Group, Dr. Kaush Arha akiteta jambo na mgeni
rasmi Waziri wa Mali asili na utalii, Mh. Lazaro Nyalandu.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la
Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo (UNDP) Bw. Philippe
Poinsot (katikati) akimsikiliza mdau kutoka AWF akitoa maoni yake kwenye
mkutano huo uliofunguliwa rasmi leo jijini Arusha.
Pichani juu na chini ni
washiriki mbalimbali wa mkutano wa kikanda unaozungumzia ujangili na
hifadhi endelevu uliofunguliwa rasmi leo jijini Arusha.