Na Mwandishi Wetu,
Wakazi wa Dar es Salaam wataanza
kupokea huduma zilizoboreshwa zaidi kila watakapotumia mabasi
yanayomilikiwa na Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), hii inatokana
na mafunzo ya mwezi mmoja yanayotolewa na shirika kwa madereva,
makondakta pamoja na wafanyakazi wengine wa shirika hilo.
Akizungumza wakati wa ziara fupi
ya waandishi wa habari katika makao makuu ya UDA jijini Dar es Salaam
Jana, Mkuu wa kitengo cha mahusiano ya umma wa UDA, Bw. George Maziku
alisema kuwa miongoni mwa mambo mengine, kampuni yake imejikita katika
utoaji wa mafunzo madhubuti kwa wafanyakazi wake ili kuboresha huduma
zote zinazotolewa kwa wateja wa UDA.
“Uongozi wa UDA unalichukulia kwa
uzito mkubwa sana suala la usalama. Tumeupitia mtaala wa utoaji elimu
kwa wafanyakazi wetu lengo likiwa ni kuboresha usalama na kufanya wateja
wetu wafurahie huduma zinazotolewa na shirika. Tunatoa mafunzo haya kwa
madereva wetu ili kuinua hali yao ya uzingatiaji wa usalama,” alisema
Maziku.
Mbali na masuala ya usalama, mkuu
huyo wa kitengo cha uhusiano aliahidi uboreshaji wa huduma kwa ujumla
ikiwa ni pamoja na kuwajali wateja, suala ambalo limekua likizua mjadala
mkubwa.
Bw. Maziku alisema kuwa kampuni
yake ina mabasi yapatayo 400 jambo linayoifanya UDA kuwa kampuni ya
kwanza Tanzania kuwa na magari mengi yanayofanya kazi kwa mkupuo, hivyo
kuna uhitaji mkubwa sana wa kuweka viwango thabiti ambavyo vinaweza
kuigwa na makampuni mengine.
“Tunalenga kuwa na mabasi 3000
ifikapo mwakani lakini kikubwa zaidi kabla hata ya kupata idadi hiyo ya
mabasi ni kuwapa mafunzo madereva wetu ili wawe na elimu ya kutosha na
uzoefu wa kutosha katika sekta ya usafirishaji wa umma.
“Kwa kulitambua hili, kampuni
imeajiri wakufunzi kutoka ndani na nje ya nchi, ili kutoa mafunzo kwa
madereva wetu na wafanyakazi wengine wanaojihusisha na usafirishaji,
mafundi na wafanyakazi wote (hasa makondakta) katika kuwajali wateja,”
alisema.
Bw. Maziku alisema kuwa mbali na
mafunzo hayo, kampuni imekuwa ikifuatilia kwa karibu sana tabia na
mienendo ya madereva na makondakta wake mara kwa mara kwa kuwatumia
wasimamizi ambao hupanda mabasi ya kampuni hiyo bila ya makondakta na
madereva kupewa taarifa.
Kwa sasa, mafunzo yaliyokuwa
yakitolewa na kampuni hapo awali, yameonyesha kuzaa matunda
yaliyotarajiwa kwa kuwabadilisha baadhi ya madereva na makondakta wa
kampuni hiyo.
Hii ilibainika baada ya mkazi wa
Dar es Salaam, ambaye amekuwa akitumia huduma za UDA kwa nyakati
tofauti, Bw. Andrew Sanga , kukiri kuwa madereva wa UDA wapo tofauti
ukilinganisha na madereva wengine wa mabasi ya abiria.
“Ilikuwa ni adha kubwa kutumia
usafiri wa umma kutokana na huduma mbovu ambazo abiria tulikua
tukikumbana nazo. Madereva wengi wa abiria hawazingatii suala la usalama
barabarani. Wanaendesha hovyo bila kujali kuwa kuna watumiaji wengine
wa barabara. Lakini nina furaha kusema kuwa madereva wa UDA wapo tofauti
sana na wenzao,” alifafanua.
No comments:
Post a Comment