MIFUKO ya hifadhi ya Jamii ya
NSSF na PSPF imejitokeza kudhamini tuzo za Wanamichezo Bora wa Tanzania
ambazo zitafanyika Desemba 12 mwaka huu ukumbi wa Diamond Jubilee (VIP),
Dar es Salaam, zikiandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo
Tanzania (TASWA).
Udhamini wa PSPF katika tuzo
hizo ni Sh. Milioni tano, wakati NSSF imetoa Sh. Milioni mbili, hivyo
kufanya fedha taslimu ambazo hadi sasa TASWA imepata kufikia Sh. Milioni
37.
Wadhamini wengine ni Kampuni ya
Said Salim Bakhresa (SSB) Group Limited iliyotoa Sh. Milioni 10 na
Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL iliyotoa Sh milioni 20.
Uongozi wa TASWA unaendelea na
mazungumzo na kampuni mbalimbali kwa ajili ya kudhamini tuzo hizo,
ambapo licha ya walioahidi kutoa fedha taslimu, lakini wapo wengine
tunaendelea kuzungumza nao kwa ajili ya kudhamini kwa njia ya huduma
zinazoambatana na tuzo hizo.
Ni imani ya TASWA kwamba hadi
kufikia Novemba 20 mwaka huu kampuni na wadau mbalimbali walioahidi
kutusaidia watakuwa wametekeleza ahadi zao kulingana na mazungumzo
tuliyofanya nao, hivyo kuwatangaza rasmi.
Wanamichezo zaidi ya 100
wanatarajiwa kuwania tuzo kwa michezo mbalimbali, ambapo Kamati ya Tuzo
za Wanamichezo Bora wa TASWA, inatarajiwa kukutana wiki ijayo
kujiridhisha kwa mara ya mwisho orodha ya mapendekezo ya wanamichezo
kutoka vyama mbalimbali vya michezo kwa ajili ya kuwania tuzo hizo.
B; MEDIA DAY BONAZA
TASWA kila mwaka inaandaa
bonanza la vyombo vya habari linalojulikana kama Media Day Bonanza,
ambalo hushirikisha wadau mbalimbali kutoka vyombo vya habari.
Lengo la bonanza hilo ni
kuwaweka pamoja waandishi wote wa habari bila kujali ni wa siasa,
michezo, uchumi, afya na mambo mengine pamoja na wafanyakazi wa vyombo
mbalimbali vya habari, ili kubadilishana mawazo na kufurahi pamoja.
Lakini mwaka huu bonanza hilo
limechelewa kutokana na na suala la wadhamini ambao awali TASWA
ilikubaliana nao, lakini baadaye walisema wamepata matatizo ya kifedha.
Hata hivyo kutokana na umuhimu
wa bonanza hilo, uongozi wa TASWA umezungumza na wadau wengine na
mazungumzo hayo yanaendelea ili Media Day Bonanza ifanyike mwezi ujao
likiwa ni maalum kwa ajili ya kufunga mwaka 2014.
Tunajua maswali kuhusu Media Day
yamekuwa mengi pengine kuliko majibu, pia wasiwasi kwa baadhi yenu ni
mkubwa kuliko uhakika, lakini tunawahakikishia mambo yanaenda vizuri na
ni imani yetu yanakaribia kuiva.
Kwa hili la Media Day, tuliona
ni bora tukawie kuliko kuvurunda. Tusikimbie kwa kasi bila kutazama
tuendako. Tutambae, lakini macho njiani na mbele tunakoelekea na hiyo
ndiyo dhamira yetu.
No comments:
Post a Comment