Na Ali Mohamed
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Mali Asili Zanzibar Juma
Ali Juma amesema serikali haipo tayari kuona Karafuu ya Zanzibar
inapoteza hadhi na ubora wake wa asili kutokana na kuchafuliwa na baadhi
ya watu wasiokuwa waaminifu.
Akizungumza katika semina ya ubora wa zao la karafuu kwa
maendeleo ya Zanzibar katika Ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo Pemba alisema
hatua zitachukuliwa kudhibiti hali hiyo.
Kauli hiyo imekuja baada ya kuwepo malalamiko ya wateja na
matukio ya kupungua uzito wa karafuu zinazosafirishwa nje ya nchi ambapo
sababu hizo zinasababishwa na karafuu kutokauka vizuri na kuchanganywa
na vitu visivyohitajika.
Alisema Wakaguzi na wapasishaji katika vituo vya manunuzi ndio
dhamana na wanawajibika kisheria juu ya kulinda ubora wa karafuu hivyo
hawatakiwi kupasisha karafuu zisizokuwa na ubora unaotakiwa.
Alisema kuwa kutakuwa na utaratibu wa kufatilia karafuu
zinazonunuliwa vituoni ili kuwajua wapasishaji wanaozembea ama kula
njama katika kutekeleza wajibu huo na hatua za kisheria zitachukuliwa
kwa watakao bainika.
Nae Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Biashara la Taifa
Zanzibar ZSTC Mwanahija Almas Ali alisema Shirika limeingiza mashine ya
kupima ubora wa karafuu kwa majaribio na endapo ikifaa zitawekwa katika
vituo vyote vya manunuzi.
Alisema dhamira ya Shirika ni kusafirisha karafuu zenye ubora
maalumu na kusisitiza kuwa ni lazima yawepo mashirikiano kati ya wadau
wote wa zao la karafuu juu ya kulinda ubora unaotakiwa.
Akiwasilisha mada ya ubora wa karafuu Mkurugenzi Masoko wa ZSTC
Abdlla Salum Kibe alisema karafuu bora zinatakiwa ziwe safi, zimekauka
vizuri, ziwe na rangi ya dhahabu na zilizoanikwa kwa kutumia jua.
Alizitaja sifa nyengine kuwa ni Karafuu zisizochanganywa na aina
yo yote ya taka, zilizoanikwa kwa mpangilio unaokubalika wenye
kupitisha hewa na zenye unyevu wa kiwango kinachokubalika cha 14%.
Kwa upande wao Wakaguzi na Wapasishaji wamesikitishwa na matukio
hayo ya kununuliwa karafuu chini ya kiwango cha ubora na kudai kuwa wao
wanajitahidi kwa kila hali kutekeleza kazi zao kwa uadilifu.
Aidha waliahidi kuwa wataendelea kuwa waadilifu na makini zaidi
katika utendaji kazi na waliiomba serikali kuendelea kuwapatia mafunzu
maalumu na vifaa vya kisasa ili kuongeza ufanisi wa kazi hiyo muhimu.
No comments:
Post a Comment