Jeshi la Polisi Kanda Maalum
ya Dar es Salaam limewaachia huru Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (Tanzania Petroleum Development
Corporation – TPDC) Mh. MICHAEL PETRO MWANDA na Kaimu Mkurugenzi Mkuu
wa shirika hilo JAMES ANDILILE kusubiri ufafanuzi wa Bunge kutokana na
tuhuma zinazowakabili. Awali, jana tarehe 03/10/2014 saa tano asubuhi
katika ukumbi wa Bunge uliopo jijini Dar es Salaam katika chumba cha
mikutano kulikuwa na kikao
cha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, Mwenyekiti akiwa ni Mh.
ZITTO ZUBERY KABWE (MB) na makamu wake ni Mh. DEO FILIKUNJOMBE (MB).
Katika kikao hicho agenda ya
mkutano ilikuwa ni kuwasilisha mahesabu ya Shirika la Maendeleo ya
Petroli Tanzania (TPDC) katika kipindi kinachoishia tarehe 30 June,
2013. Baada ya majadiliano ya muda kuhusu hati mbalimbali zilizotakiwa
na Kamati hiyo ya Bunge hatimaye Mwenyekiti wa Kamati Mh. Zitto Zubery
Kabwe alitoa maagizo kwa askari wa Polisi waliokuwepo katika eneo hilo
kwa masuala ya ulinzi kuwa Mwenyekiti wa bodi ya TPDC na Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wafikishwe kituo cha polisi Kati.
Kutokana na maelezo ya mashahidi waliokuwepo kwenye tukio hilo katika ukumbi wa Bunge Mwenyekiti Zitto alisema wapelekwe
Polisi waende kusubiri mwongozo wa Mhe. Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ambaye atawasiliana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali
kwa maagizo ya mwisho. Mara baada ya agizo hilo watu hao walifikishwa
kituo cha Polisi Kati chini ya ulinzi.
Uongozi wa Jeshi la Polisi
Kanda Maalum ya Dar es Salaam ulishindwa kuchukua hatua zaidi ya hapo
kwani shauri hilo halikuwa na mlalamikaji aliyekuja kufungua jalada na
kutoa ufafanuzi kuhusu mashtaka yanayowakabili viongozi wa TPDC. Aidha,
maafisa wawili wa secretarieti ya Bunge waliitwa Polisi kutoa ufafanuzi
kuhusu kadhia hii wakiwepo pia mawakili wa watuhumiwa na hatimaye
kilifanyika kikao cha dharura ili kupata ufafanuzi wa kisheria.
Hatimaye iligundulika
kwamba katika sheria ya HAKI, KINGA na MADARAKA ya Bunge sura ya 296 Kif
12 (3) kinaonyesha kwamba mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali alitakiwa kwanza apendekeze kwa Mhe. Spika wa Bunge juu ya
jambo lolote aliloliona kama ni kosa.
Mhe. Spika akisharidhika kuhusu tuhuma zozote zilizoletwa mezani kwake na Mwenyekiti wa Kamati
ya Bunge, ndipo anamwandikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili suala
hilo lipate ufafanuzi wa kisheria ikiwa ni pamoja na hatua za kisheria
zinazostahili kuchukuliwa.
Katika kikao hicho na jopo la wanasheria iligundulika kwamba katika sheria
ya Haki, Kinga na Madaraka ya bunge, agizo la kukamatwa watu hao
lililotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge lilihita kuzingatiwa kwa
taratibu tajwa hapo juu kwanza kabla ya utekelezaji wake.
Hatimaye ilionekana
hakuna sababu ya kuendelea kuwashikilia viongozi hao na badala yake
wameachiwa huru tukisubiri taratibu na sheria kama ilivyoelezwa hapo
juu.
No comments:
Post a Comment