Wapima Ardhi na Mipaka
wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi wakiendelea na zoezi la uhakiki wa alama za mipaka kwa kutumia kifaa
kiitwacho Hand Heled GPS kwenye moja ya ramani ya eneo linalopaswa kuwa la
makazi ya watu na taasisi nje kidogo ya mji wa Chalinze,Bagamoyo Pwani.(Picha zote na Aron Msigwa).
===========================================================
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Wizara ya Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi imeto tahadhari kwa Taasisi na wananchi wanaotaka kupimiwa
maeneo yao ya ardhi kuhakikisha kuwa wanafuata sheria, kanuni na taratibu
zinazosimamia masuala ya upimaji wa ardhi ili kuepuka kupata hasara na kuingia
kwenye migogoro ya ardhi isiyo ya lazima kutokana na kutumia watu au makampuni
yasiyosajiliwa kishera.
Hatua hiyo imekuja kufuatia
baadhi ya makampuni yanayojishughulisha na upimaji wa Ardhi na ramani kugundulika
kufanya kazi za wateja wao chini ya viwango kufuatia ramani zilizowasilishwa na
makampuni hayo wizarani hapo kwa ajili ya kuidhinishwa kukosa
sifa pindi zinapofanyiwa uhakiki na wataalam wa wizara hiyo.
Mkurugenzi Msaidizi wa
Upimaji na Ramani vijijini wa wizara hiyo Bw. Huruma Lugalla akizungumza mara
baada ya timu ya wataalam wa wizara hiyo kufanya uhakiki wa moja ya ramani ya eneo
linalopaswa kuwa la makazi ya watu na taasisi nje kidogo ya mji wa Chalinze, Bagamoyo
mkoani Pwani ambalo upimaji wake umekiuka kanuni na taratibu
amesema Serikali haitayafumbia macho makampuni yote yanayochukua fedha za
wananchi na Taasisi na kisha kufanya upimaji usiokidhi viwango vilivyowekwa na
wizara hiyo kwa mujibu wa Sheria.
Amesema wizara hiyo
itaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuyafungia makampuni yote yanayobainika kufanya kazi
chini ya kiwango, kukiuka kwa makusudi taratibu za upimaji wa ardhi na kufanya
uzembe wa kushindwa kuweka mipaka na alama sahihi za maeneo wanayoyapima jambo
linalochangia mivutano na migogoro pindi maeneo husika yanapogawiwa kwa
wananchi.
“Nawaomba wananchi na
Taasisi mbalimbali zinazotaka kupimiwa maeneo yao kwa kutumia makampuni kuwa
makini na kuchukua tahadhari ili kuepuka hasara ya kulipa gharama za upimaji
mara mbili, msichukue watu wa kati au kampuni zisizosajiliwa kisheria ambazo haziko kwenye orodha ya Katibu wa Baraza
la Taifa la Wapima Ardhi” Amesisitiza.
Bw. Lugalla ameeleza
kuwa Kampuni ya Intergrated Property Consultancy and Services (IPCS) kutoka
Morogoro iliyohusika na zoezi la upimaji
na ramani katika eneo hilo haikufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa
kwa mujibu wa sheria kufuatia ramani iliyowasilishwa na Mkurugenzi wake Bw.
Bernard Malugu wizarani hapo kushindwa kukidhi vigezo vya ubora unaotakiwa mara
baada ya kuhakikiwa na wataalam wa Upimaji na ramani wa Wizara.
Amesema wataalam wa upimaji
na ramani wa Wizara hiyo mara baada ya kufanya
uhakiki wa eneo hilo wamebaini
ukosefu wa alama (bikoni) za baadhi viwanja, kukosekana kwa pini za
kugawa viwanja na tofauti umbali wa eneo la kiwanja kimoja hadi kingine
iliyokuwepo kwenye ramani ambayo haikuendana na uhalisia wa eneo husika wakati
wa zoezi la uhakiki.
Aidha, amebainisha kuwa ramani ya eneo hilo
ilisainiwa kimakosa na Mkurugenzi wa Kampuni hiyo kufuatia kampuni yake ambayo imesajiliwa kisheria dhamana kuamua kumtafuta mtu wa kati wa kuifanya kazi
hiyo badala yake na kisha Mkurugenzi wake Bw. Bernard Malugu kuidhinisha ramani
hiyo kwa kuisaini huku ili ipelekwe wizarani kupatiwa kibali huku akijua wazi
kanuni na taratibu zinazosimamia sekta hiyo hazimruhusu kutoa kazi kwa mtu au
kampuni nyingine.
“Ili kuepusha migogoro
ya ardhi inayoweza kutokea katika eneo lile taratibu zitafuatwa ili kampuni
hiyo iifanye kazi ile upya kwa gharama zake na kisha kuwaita wataalam wa wizara
kufanya uhakiki upya ili kujiridhisha kabla ya kutoa kibali cha viwanja hivi,
Sisi kama wizara hatutakubali kuendelea kulaumiwa na wananchi kwa uzembe
unaofanywa na makampuni haya” Amesisitiza.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Kampuni ya IPCS iliyopewa kazi ya kupima eneo hilo akitoa utetezi
kwa kampuni yake mara baada ya kufanyika kwa uhakiki huo alikiri kuwa kampuni
yake imefanya makosa na kukiuka sheria,
miiko na maadili yanayosimamia shughuli za upimaji na ramani nchini.
Amesema yeye kama Mkurugenzi wa kampuni hiyo alisaini
ramani ya eneo hilo Machi 19, 2015 kimakosa hivyo kampuni yake imeonyesha uzembe na udhaifu wa usimamizi
ikiwemo yeye mwenyewe kutomfahamu mtu wa kati aliyeifanya kazi hiyo.
Aidha, amesema
kampuni yake iko tayari kuyabeba mapungufu yote yaliyojitokeza na kukubali
kurudia kazi ya kupima na kuweka mipaka iliyokosekana endapo itaruhusiwa na
wizara hiyo kufanya hivyo
|