TAN
Bayport
Kikoa
Myway entertainment
FORE PLAN CLINIC
MPINGA CUP 2016
Mashujaa Fm 89.3, Lindi
Thursday, March 12, 2015
Mwarobaini wa utoroshwaji wa madini ya tanzanite nchini kupatikana
Kamishna wa Madini Nchini Mhandisi
Paul Masanja amesema kuwa Serikali imejipanga kuimarisha ulinzi ndani
ya machimbo ya tanzanite ya Mirerani yaliyopo katika wilaya ya
Simanjiro, mkoani Manyara
Mhandisi Masanja aliyasema hayo mbele ya Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Nishati na Madini kwenye kikao chake na watendaji wa Wizara ya
Nishati na Madini wanaosimamia sekta za madini kilichofanyika jijini
Arusha jana. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ipo mkoani
Arusha kwa ajili ya kutembelea miradi mbalimbali ya umeme pamoja na
kuzungumza na watendaji.
Aidha kamati hiyo, ilikutana na watendaji kutoka Shirika la
Umeme Nchini (TANESCO), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Wakala wa
Ukaguzi wa Madini Nchini (TMAA) na Wakala wa Udhibiti wa Huduma za
Nishati na Maji (EWURA) kwa ajili ya kupokea taarifa mbalimbali za
utekelezaji wa miradi na kutoa maazimio na mapendekezo mbalimbambali.
Mhandisi Masanja alisema kuwa Serikali ilijenga uzio wenye urefu
wa kilomita 10 kwa gharama ya shilingi milioni 300 na kuongeza kuwa
bado serikali ina mpango wa kujenga vibanda kwa ajili ya walinzi ili
kupunguza wachimbaji haramu kuingia ndani ya maeneo ya uchimbaji wa
madini hayo na kutoroka na tanzanite.
Alisema pamoja na kuimarisha ulinzi kwenye maeneo ya mgodi,
Serikali imepanga kujenga kituo kikubwa kwa ajili ya biashara ya madini
aina ya vito kitakachojulikana kwa jina la “Madini House” ambapo
kutafanyika biashara ya madini hali itakayopunguza utoroshwaji wa madini
yanayopelekwa nje ya nchi.
Aliongeza kuwa uanzishwaji wa kamati ya usalama kwa kushirikiana
na mkuu wa wilaya, kituo cha polisi umechangia kuimarishwa kwa ulinzi
katika eneo la mgodi na kusisitiza kuwa bado serikali inabuni njia
nyinyine zaidi za kisasa kwa ajili ya kudhibiti utoroshwaji wa madini ya
tanzanite nje ya nchi.
Akielezea changamoto katika eneo ya Mirerani Mhandisi Masanja
alisema kumekuwepo na migogoro ya wachimbaji wenyewe kwa wenyewe
kugombea ardhi na kutokuzingatia sheria na kanuni za uchimbaji madini
hali inayopelekea ajali za mara kwa mara mgodini.
“ Kule kwenye eneo la mgodi kuna uchimbaji hatari unaofanyika
chini kwa chini ambapo wamejiwekea utaratibu wa kuwa, mchimbaji
anapokutana na mwenzake kwenye mkondo wa madini chini ya ardhi,
anatakiwa kurudi nyuma hatua kumi lakini bado kumekuwepo na changamoto
ya wachimbaji kuvamia maeneo wanayohisi madini yapo bila kuzingatia
kanuni za uchimbaji madini,” alisisitiza Mhandisi Masanja
Aliongeza kuwa changamoto nyingine ni pamoja na maeneo ya
uchimbaji kuwa madogo na kuongeza kuwa ili kukabiliana na changamoto ya
migogoro aliwashauri wachimbaji wadogo kuunda umoja kwa kuunganisha
maeneo yao na kuomba leseni ya pamoja hali itakayowaongezea kipato huku
ikipunguza migogoro isiyo ya lazima.
“ Kwa mfano iwapo wachimbaji wataungana ya kuomba leseni ya
pamoja na kuchimba madini, kila mchimbaji ana uhakika wa kupata faida ya
shilingi milioni 500 kwa mwaka,” alisema Mahandisi Masanja
Wakichangia kwa nyakati tofauti wajumbe kutoka Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Nishati na Madini waliitaka Serikali kuongeza juhudi zaidi
katika usimamizi wa sekta ya madini ikiwa ni pamoja na suala la ulinzi
kwenye migodi hususan katika eneo la Mirerani
Akichangia hoja katika kikao hicho mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Nishati na Madini ambaye ni Mbunge wa Singida (Viti Maalum)
Martha Mlata alisema kuwa mbali na kuimarisha ulinzi katika eneo la
Mirerani kwa kuweka uzio na vibanda kwa ajili ya walinzi, vitambulisho
kwa ajili ya wachimbaji wa mgodini vinatakiwa kutengenezwa vikiwa na
majina ya makampuni yanayochimba madini.
Alisema kufanya hivyo, kutapunguza wimbi la wachimbaji haramu na
wahamiaji wanaoingia katika maeneo hayo na kutoroka na madini hayo.
Mlata alisisitiza kuwa makampuni yanayoshindwa kulipa kodi kwa
kisingizio cha kupata hasara yasivumiliwe kamwe , ikiwezekana
yanyang’anywe leseni za madini.
Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Richard Ndassa alisema kuwa
muarobaini wa utoroshwaji wa madini ya tanzanite unaweza kupatikana kwa
kujenga ukuta mkubwa imara na kuitaka Serikali kuwa na mikakati zaidi
kwa ajili ya kuimarisha ulinzi katika eneo la Mirerani.
Ndassa alisema kuwa suala la usimamizi wa sekta ya madini
halihitaji siasa, na kuwataka wajumbe wa kamati hiyo kuwa wazalendo
badala ya kuweka siasa zaidi kwenye usimamizi wa sekta ya madini.
“Madini ya tanzanite yanapatikana Tanzania pekee duniani, hivyo ni vyema kuhakikisha madini haya yanalindwa kwa nguvu zote pamoja na usimamizi wake bila kuongozwa na siasa,” alisema Ndassa
Wizara ya vipatia vijiji 10 umeme jua katika Wilaya za Kongwa
Jumla ya Vijiji 10 katika Wilaya za Kongwa, Mlele na Uyui
vimeunganishiwa umeme kupitia Mradi wa makontena ya kuzalisha umeme
kutokana na jua.
Mradi huo unatekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Nishati na
Madini, ambapo upo katika hatua ya majaribio na unalenga kuvipatia umeme
vijiji vilivyo mbali na mfumo wa gridi ya Taifa.
Wizara ya Nishati na Madini wiki hii, ilisaini makubaliano ya
kukamilika kwa awamu ya kwanza ya Mradi na Kampuni ya Elektro-Merl ya
nchini Austria ambayo ndiyo ilileta na kufunga makontena 14 ya umeme wa
jua pamoja na mfumo wa usambazaji umeme kwa nyumba zilizoko katika
vijiji husika.
Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo, Mwakilishi
kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Styden Rwebangira alisema
wananchi waliounganishiwa umeme huo wa jua, watapata huduma hiyo bure
kwa kipindi cha miaka miwili ya mwanzo ambayo ni ya matazamio.
Alisema kuwa, baada ya miaka miwili, kuanzia tarehe waliyosaini
makubaliano, wananchi wa vijiji husika wataanza kuchangia fedha kidogo
kwa ajili ya ununuzi wa vifaa mbalimbali kama betri na paneli
vinavyotumika katika mradi huo, ambavyo vina ukomo wa kutumika.
“Vifaa hivi vina gharama kubwa sana, hivyo inabidi kuwa na
utaratibu wa kukusanya fedha za kutosha ili kuweza kununua vifaa vingine
pindi vilivyopo vinapofikia ukomo wake wa kutumika. Hivyo kila
mwananchi anayetumia huduma hii inabidi achangie gharama,” alisema
Mhandisi Rwebangira.
Aidha, aliongeza kuwa, ili kuhakikisha mradi unatoa matokeo
yaliyotarajiwa, inabidi uendeshwe na mtu au kampuni yenye utaalamu wa
masuala ya umeme, mitambo ya umeme jua pamoja na uzoefu na ufahamu wa
kutosha kuhusu mitambo ya aina hiyo.
“Hivyo, kila baada ya miaka miwili, ukiacha kipindi cha
majaribio ambapo mradi utakuwa chini ya Wizara, atachaguliwa mtaalamu au
kampuni kupitia njia ya ushindani ambaye atalipwa kwa utaratibu
utakaokubaliwa katika mkataba,” alisema Rwebangira.
Kwa upande wake, Ofisa wa Wizara aliyefika kushuhudia utiaji
saini makubaliano ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi, Paul
Kiwele alisema Wizara ilifanya tathmini ya kuchagua vijiji kwa ajili ya
majaribio ya mradi huo ambapo vigezo mbalimbali vilitumika.
Kiwele alivitaja vigezo hivyo kuwa ni pamoja na Kijiji husika
kuwa mbali na gridi ya Taifa, kutokuwa katika mpango wa kufikiwa na
miradi ya umeme ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco) hivi karibuni.
Alitaja vigezo vingine kuwa ni nyumba za Kijiji husika kuwa
karibu pamoja na uwepo wa matumizi ya kiwango cha umeme utakaozalishwa.
“Aidha, kwa kuwa mradi huu ni wa majaribio, ililengwa kupata
mikoa mitatu tofauti ili uzoefu utakaopatikana utumike katika
uendelezaji teknolojia hii katika maeneo mengine ya nchi,” alisema.
Naye, Mtaalam kutoka Kampuni ya Elektro Merl, Mhandisi Hannes
Merl akizungumzia mkataba uliosainiwa na Wizara pamoja na Kampuni yake,
Januari mwaka jana kuhusu utekelezaji wa mradi husika, alisema mbali na
kufunga makontena 14 ya umeme wa jua pamoja na mfumo wa usambazaji
umeme, mkataba pia ulihusisha ufungaji wa waya, taa, swichi na soketi
moja kwa kila nyumba iliyofikiwa.
Mhandisi Merl alisema kila kontena lina uwezo wa kuzalisha kWp
13.75 ambapo kila nyumba ya makazi na huduma za biashara zimetengewa W
250 na taasisi za kijamii zimetengewa W 500.
Aliongeza kuwa, wananchi wanaweza kuunganisha mashine ndogo
ndogo za kusaga, kuchomelea, kuranda na kuchana mbao pamoja na
nyinginezo kutoka katika makontena hayo hivyo kunufaika na shughuli za
kiuchumi.
Pia, Mhandisi Merl alisema mradi umetoa jokofu kwa kila zahanati
na vituo vya afya vilivyopo katika vijiji vinavyonufaika na mradi huu.
Aidha, alisema kuwa mradi umefunga taa za mitaani kwa kila kijiji
kitakachonufaika na mradi husika.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi katika vijiji vilivyonufaika
na mradi huo wa makontena ya umeme wa jua, waliishukuru na kuipongeza
Serikali kwa wazo zuri la kuwapelekea wananchi hao umeme wa jua ili nao
waweze kunufaika kwa namna mbalimbali kutokana na uwepo wa nishati hiyo
muhimu.
“Ninaishukuru sana Wizara ya Nishati na Madini kuona matatizo
yetu na kusikia kilio chetu. Imekuwa kama ndoto. Umeme huu umeniwezesha
kuendesha biashara ya saluni kwa njia ya kisasa kabisa. Situmii tena
Mkasi kunyoa wateja wangu kama hapo awali. Sasa ninatumia mashine za
kunyolea na ninapata wateja wengi, hivyo kuboresha kipato changu na
maisha yangu kwa ujumla,” alisema Lazaro Kutamika, mkazi wa Kijiji cha
Lobilo, Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma.
Wizara ya Nishati na Madini imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali
katika jitihada za kuwafikishia wananchi huduma ya umeme. Kwa kupitia
mradi huo wa makontena ya kuzalisha umeme kutokana na jua, Serikali
inafanya majaribio ya kuvipatia umeme vijiji vilivyo mbali na mfumo wa
gridi ya Taifa kwa kutumia teknolojia husika.
Vijiji vilivyonufaika na mradi huo kwa awamu ya kwanza ni pamoja na Lobilo, Leganga, Ngutoto na Silale vya mkoa wa Dodoma. Vingine ni Tura, Loya na Lutende vilivyoko mkoa wa Tabora. Aidha, kwa mkoa wa Katavi, vijiji vilivyonufaika ni Nsenkwa, Mapili na Ilunde.
Mgodi wa Dhahabu Chunya wahesabiwa siku
Baraza la Taifa la Hifadhi
naUsimamizi wa Mazingira na Wataalam wa Mazingira wameagizwa kutoa elimu
ya mazingira kwa wawekezaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Sunshine uliyopo
Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya .
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais
Mazingira, Injinia Binilith Mahenge jana alipotembelea machimbo ya
Mgodi huo nakubaini kuwa unaendeshwa bila kuzingatia Kanuni za
Mazingira.
Katika ziara hiyo Mh. Mahenge alibaini kuwa mgodi huo hauna
mtambo wa kutibu maji-taka yake kabla ya kuyatiririsha katika mazingira
pia bwawa linalotumika kuhifadhi maji-taka hayo halikidhi viwango vya
Kanuni za Mazingira pamoja na kuzibwa kwa mfereji wa asili hivyo kuzuia
mkondo wa mvua.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Mahenge alitoa siku 30 kwa
wataalam wake kuwapatia elimu ya Kanuni za Mazingira wawekezaji wa Mgodi
wa Sunshine ikiwa ni pamoja na kuwataka wawekezaji hao kutekeleza
kanuni hizo ndani ya siku 30 kuanzia jana.
Wakati huo huo Mh. Mahenge alitembelea Machimbo ya Dhaabu ya
Mek na Mgodi wa Shanta Wilayani Chunya ambapo Wataalam wake Mazingira
walibainisha kuwa wawekezaji wa migodi hiyo wametiza kanuni za
mazingira.
Sanjari na hayo Injiania Mahenge alikutana na Watendaji wa
Halmashauri ya Chunya na kukabidhiwa Mapendekezo ya Mradi Maalumu wa
kulinusuru Ziwa Rukwa ili lisitoweke kutokana na kilimo holela,
uchimbaji wa madini na utirirshwaji wa maji-taka kwenye vyanzo vya Ziwa
hilo.
Katika makabidhiano ya Mapendekezo hayo Mh. Mahenge aliwaahidi Watendaji wa Halmashauri ya Chunya kuwa atayafanyia kazi Mapendekezo yao lakini pia aliwaomba na wao kuishauri Wilaya waingize Mazingira katika bajeti zao .
Subscribe to:
Posts (Atom)