Kamishna wa Madini Nchini Mhandisi
Paul Masanja amesema kuwa Serikali imejipanga kuimarisha ulinzi ndani
ya machimbo ya tanzanite ya Mirerani yaliyopo katika wilaya ya
Simanjiro, mkoani Manyara
Mhandisi Masanja aliyasema hayo mbele ya Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Nishati na Madini kwenye kikao chake na watendaji wa Wizara ya
Nishati na Madini wanaosimamia sekta za madini kilichofanyika jijini
Arusha jana. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ipo mkoani
Arusha kwa ajili ya kutembelea miradi mbalimbali ya umeme pamoja na
kuzungumza na watendaji.
Aidha kamati hiyo, ilikutana na watendaji kutoka Shirika la
Umeme Nchini (TANESCO), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Wakala wa
Ukaguzi wa Madini Nchini (TMAA) na Wakala wa Udhibiti wa Huduma za
Nishati na Maji (EWURA) kwa ajili ya kupokea taarifa mbalimbali za
utekelezaji wa miradi na kutoa maazimio na mapendekezo mbalimbambali.
Mhandisi Masanja alisema kuwa Serikali ilijenga uzio wenye urefu
wa kilomita 10 kwa gharama ya shilingi milioni 300 na kuongeza kuwa
bado serikali ina mpango wa kujenga vibanda kwa ajili ya walinzi ili
kupunguza wachimbaji haramu kuingia ndani ya maeneo ya uchimbaji wa
madini hayo na kutoroka na tanzanite.
Alisema pamoja na kuimarisha ulinzi kwenye maeneo ya mgodi,
Serikali imepanga kujenga kituo kikubwa kwa ajili ya biashara ya madini
aina ya vito kitakachojulikana kwa jina la “Madini House” ambapo
kutafanyika biashara ya madini hali itakayopunguza utoroshwaji wa madini
yanayopelekwa nje ya nchi.
Aliongeza kuwa uanzishwaji wa kamati ya usalama kwa kushirikiana
na mkuu wa wilaya, kituo cha polisi umechangia kuimarishwa kwa ulinzi
katika eneo la mgodi na kusisitiza kuwa bado serikali inabuni njia
nyinyine zaidi za kisasa kwa ajili ya kudhibiti utoroshwaji wa madini ya
tanzanite nje ya nchi.
Akielezea changamoto katika eneo ya Mirerani Mhandisi Masanja
alisema kumekuwepo na migogoro ya wachimbaji wenyewe kwa wenyewe
kugombea ardhi na kutokuzingatia sheria na kanuni za uchimbaji madini
hali inayopelekea ajali za mara kwa mara mgodini.
“ Kule kwenye eneo la mgodi kuna uchimbaji hatari unaofanyika
chini kwa chini ambapo wamejiwekea utaratibu wa kuwa, mchimbaji
anapokutana na mwenzake kwenye mkondo wa madini chini ya ardhi,
anatakiwa kurudi nyuma hatua kumi lakini bado kumekuwepo na changamoto
ya wachimbaji kuvamia maeneo wanayohisi madini yapo bila kuzingatia
kanuni za uchimbaji madini,” alisisitiza Mhandisi Masanja
Aliongeza kuwa changamoto nyingine ni pamoja na maeneo ya
uchimbaji kuwa madogo na kuongeza kuwa ili kukabiliana na changamoto ya
migogoro aliwashauri wachimbaji wadogo kuunda umoja kwa kuunganisha
maeneo yao na kuomba leseni ya pamoja hali itakayowaongezea kipato huku
ikipunguza migogoro isiyo ya lazima.
“ Kwa mfano iwapo wachimbaji wataungana ya kuomba leseni ya
pamoja na kuchimba madini, kila mchimbaji ana uhakika wa kupata faida ya
shilingi milioni 500 kwa mwaka,” alisema Mahandisi Masanja
Wakichangia kwa nyakati tofauti wajumbe kutoka Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Nishati na Madini waliitaka Serikali kuongeza juhudi zaidi
katika usimamizi wa sekta ya madini ikiwa ni pamoja na suala la ulinzi
kwenye migodi hususan katika eneo la Mirerani
Akichangia hoja katika kikao hicho mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Nishati na Madini ambaye ni Mbunge wa Singida (Viti Maalum)
Martha Mlata alisema kuwa mbali na kuimarisha ulinzi katika eneo la
Mirerani kwa kuweka uzio na vibanda kwa ajili ya walinzi, vitambulisho
kwa ajili ya wachimbaji wa mgodini vinatakiwa kutengenezwa vikiwa na
majina ya makampuni yanayochimba madini.
Alisema kufanya hivyo, kutapunguza wimbi la wachimbaji haramu na
wahamiaji wanaoingia katika maeneo hayo na kutoroka na madini hayo.
Mlata alisisitiza kuwa makampuni yanayoshindwa kulipa kodi kwa
kisingizio cha kupata hasara yasivumiliwe kamwe , ikiwezekana
yanyang’anywe leseni za madini.
Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Richard Ndassa alisema kuwa
muarobaini wa utoroshwaji wa madini ya tanzanite unaweza kupatikana kwa
kujenga ukuta mkubwa imara na kuitaka Serikali kuwa na mikakati zaidi
kwa ajili ya kuimarisha ulinzi katika eneo la Mirerani.
Ndassa alisema kuwa suala la usimamizi wa sekta ya madini
halihitaji siasa, na kuwataka wajumbe wa kamati hiyo kuwa wazalendo
badala ya kuweka siasa zaidi kwenye usimamizi wa sekta ya madini.
“Madini ya tanzanite yanapatikana Tanzania pekee duniani, hivyo ni vyema kuhakikisha madini haya yanalindwa kwa nguvu zote pamoja na usimamizi wake bila kuongozwa na siasa,” alisema Ndassa
No comments:
Post a Comment