Kaimu
Mkurugenzi wa HakiElimu, Godfrey Boniventura (katikati) akizungumza na
waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam. Wengine kushoto na kulia
ni maofisa wa taasisi ya HakiElimu wakiwa katika mkutano huo.
Kaimu
Mkurugenzi wa HakiElimu, Godfrey Boniventura (katikati) akizungumza na
waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam. Wengine kushoto na kulia
ni maofisa wa taasisi ya HakiElimu wakiwa katika mkutano huo.
Kaimu
Mkurugenzi wa HakiElimu, Godfrey Boniventura (katikati) akizungumza na
waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam. Wengine kushoto na kulia
ni maofisa wa taasisi ya HakiElimu wakiwa katika mkutano huo.
Baadhi
ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari wakifuatilia
mkutano huo uliofanyika katika ofisi za HakiElimu leo jijini Dar es
Salaam.
………………………………………………………………………………………..
Na Joachim Mushi
TAASISI ya HakiElimu imeukosoa
mpango wa Matokeo Makubwa Sasa ‘Big Results Now’ (BRN) unaotekelezwa na
Serikali katika sekta nyeti ikiwemo elimu kwa madai kuwa matokeo yake
kwenye sekta ya elimu sio ya kuridhisha.
Kauli hiyo imetolewa leo na Kaimu
Mkurugenzi wa HakiElimu, Godfrey Boniventura alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam baada ya tathmini ya kitaalamu
iliofanywa katika utekelezaji wa BRN kweye sekta ya elimu.
Boniventura alisema Serikali
isitumie kigezo cha kuongezeka ufaulu kama ishara tosha ya kuimarika kwa
elimu, kwani licha ya ufaulu huu kuonekana kupanda ghafla kuna
changamoto nyingi katika sekta ya elimu ambazo bado hazijatatuliwa na
juhudi kubwa zinahitajika.
“…Mfano migogoro ya mara kwa mara
kati ya walimu na mwajiri, utoro wa walimu, ukosefu wa maabara, vifaa
vya kufundishia na tofauti kubwa iliyopo katika gharama za utoaji elimu
nchini kati ya shule za serikali na shule za binafsi. Mpango wa BRN ni
mzuri lakini muda uliowekwa kutekeleza malengo yake ni mfupi kwa
kuzingatia mazingira ya utoaji elimu na changamoto zake,” alisema
Boniventura.
Kaimu huyo Mkurugenzi alibainisha
kuwa kumekuwepo na mabadiliko ya mara kwa mara katika sekta ya elimu
likiwemo la hivi karibuni la alama za ufaulu na mabadiliko ya viwango
vya upimaji wa matokeo ya wanafunzi ambayo yameleta mabadiliko katika
takwimu za ufaulu lakini yasitumike kama ishara ya kuimarika kwa ubora
wa elimu itolewayo.
Aidha aliongeza kuwa matokeo
mazuri yoyote ya mipango ya maendeleo ikiwemo elimu yanahitaji uwekezaji
wa kutosha, ilhali shule za msingi na sekondari zina changamoto nyingi
za upungufu wa miundombinu jambo ambalo linahitaji kufanyiwa kazi
kiufasaha zaidi tofauti na inavyofanyika sasa.
“…Serikali haina budi kutafakari
na kuona kama uwekezaji uliofanyika mpaka sasa umefanyika kiasi cha
kutosha kuleta matokeo kusudiwa. Hali ya uwekezaji kwenye sekta ya elimu
si nzuri ambapo asilimia 24 tu ya fedha ya bajeti inapangwa kwenye
miradi ya maendeleo inayohusu miundominu ilihali matumizi ya kawaida
yakiwa asilimia 74 ya bajeti ya elimu,” alisema.
Baadhi
ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari wakifuatilia
mkutano huo uliofanyika katika ofisi za HakiElimu leo jijini Dar es
Salaam.
Akifafanua zaidi alisema sekta ya
elimu malengo yaliyopangwa kutekelezwa katika kipindi cha mwaka mmoja
2013/2014, ni pamoja na;- Kuongeza ufaulu kufikia asilimia 70 mwaka
2014; kutoa ruzuku iliyopangwa kwa kila mwanafunzi, kutoa mafunzo ya
uongozi kwa walimu 19,035 kufikia Septemba 2013, lakini kwenye uhalisia
hali hairidhishi.
Alisema BRN ilipanga pia kutoa
mafunzo kwa waalimu 12,300 juu ya ufundishaji wa KKK, kujenga nyumba za
walimu 500 kwa shule za sekondari, kukarabati miundombinu kwa shule
1,200 za sekondari na kuhakikisha kuwa uwino wa mwanafunzi kwa kitabu
unashuka kutoka kitabu kimoja kwa wanafunzi watano hadi vitabu sita kwa
mwanafunzi mmoja lakini hakuna mafanikio ya kuridhisha.
“…HakiElimu imefanya ufuatiliaji
wa utekelezaji wa BRN katika sekta ya elimu kwa karibu sana na kubaini
kuwa hali ya utekelezaji wake bado si ya kuridhisha.
Mathalani, BRN ilipanga kuongeza kiwango cha ufaulu kwa shule
za sekondari na msingi hadi kufikia asilimia 60 mwaka 2013, na asilimia
70 mwaka 2014.”
“Pamoja na matokeo kuonesha
ongezeko la ufaulu, kutoka asilimia 50.6 Mwaka 2012 hadi kufikia
asilimia 58 mwaka 2013 kwa sekondari na kutoka 30.7 mwaka 2012 hadi 50.6
Mwaka 2013 kwa shule za msingi, bado lengo la asilimia 60
halikufikiwa.”
“…Hii inamaanisha lengo la ufaulu
kwa sekondari kufikia asilimia 60 kwa mwaka 2013 limefanikiwa kwa
asilimia karibu 79 na kwa asilimia 42 tu kwa shule za msingi. Hatahivyo
ufaulu wa sekondari si wa kujivunia kwa sababu matokeo ya mtihani wa
mwaka 2013 yametumia viwango vipya vya madaraja, na hivyo hatuwezi
kusema yametokana moja kwa moja na utekelezaji wa BRN,” alieleza
Boniventura kwa wanahabari.
Hata hivyo alishauri ili
kutekeleza Matokeo Makubwa Sasa hatuna budi kujifunza toka kwa nchi
zilizofanikiwa kutekeleza mipango kama Malaysia kwamba; Matokeo Makubwa
Sasa maana yake ni viongozi kufanya tofauti na wafanyavyo sasa,
kuwajibika kwa hali ya juu, viongozi kuwa wabunifu, viongozi kupanga
mipango na kuitafutia fedha za utekelezaji, viongozi kufanya kazi na
kutenda ili kutekeleza ahadi zao ili kupata matokeo ya haraka.
Mwaka 2013 serikali ya Tanzania
ilizindua mpango maalumu wa ufuatiliaji utekelezaji wa mipango na utoaji
huduma kwa umma unaojulikana kama BRN huku lengo la mpango likiwa
kusukuma maendeleo na kuharakisha utekelezaji mipango na kuleta matokeo
yaliyokusuduwa upesi..
*Imeandaliwa na www.thehabari.com