Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa
Pili wa Rais Mhe. Mohamed Aboud Mohamed amesema Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar imeshatayarisha kanuni za usalama wa barabarani za kutoza
faini za papo kwa papo kama ilivyo sasa kwa upande wa Tanzania Bara.
Hayo ameyaeleza katika ukumbi wa
Baraza la Wawakilishi Chukwani Zanzibar wakati akijibu swali la
mwakilishi wa Jimbo la Kwahani Mhe. Ali Salum Haji.
Waziri Mohamed amesema kuwa kanuni
za sheria ya usalama barabarani kwa upande wa Zanzibar zipo kwa
Mwanasheria Mkuu kwa hatua za mwisho na zitaanza kutumiwa na Jeshi la
Polisi mara baada ya kukamilika rasmi kwa kutoza faini ya papo kwa papo
kwa wote watakaofanya makosa ya usalama wa barabarani.
Waziri Aboud ametanabahisha kuwa
kwa sasa Zanzibar Sheria Nambari 7 ya Mwaka 2003 (R.E 2006) ndio
inayosimamia masuala ya usalama barabarani na kwa mujibu wa sheria hiyo
kifungu namabari 180 hadi 184 vimeelezea kuhusiana na utaratibu wa faini
ya papo kwa papo kwa vyombo vya moto vinavyovunja sheria za usalama wa
barabarani Nchini.
Aidha amesema Jeshi la Polisi lina
jukumu la kusimamia na kutekeleza Sheria zilizotungwa na Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar
ambapo kwa upande wa Tanzania Bara Sheria inayohusika na usalama wa
barabarani ni Sheria nambari 168 ya Mwaka 2002.
“Miongoni mwa majukumu ya Jeshi la
Polisi ni kusimamia na kutekeleza Sheria zilizotungwa na Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar”,
alieleza waziri Mohamed.
Hivyo ameeleza kuwa kupitia Sheria
hiyo Jeshi la Polisi hutekeleza sheria za faini ya papo kwa papo kwa
vyombo vya moto vinavyovunja sheria za usalama barabarani na kusaidia
Serikali kukusanya fedha nyingi zinazotokana na makosa hayo.
Jeshi la polisi ni Jeshi la
Jamhuri ya muungano wa Tanzania na limeundwa kwa mujibu wa katiba ya
Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 chini ya ibara ya 147 ya kuanzishwa
kisheria chini ya kifungu nambari 3 cha sheria ya polisi na polisi
wasaidizi Cap.322 R.E ya mwaka 2002.
No comments:
Post a Comment