Na: Genofeva Matemu – Maelezo
Vijana kutoka Wilaya ya Mpwapwa na
Kongwa Mkoa wa Dodoma wameshauriwa kutokimbilia mikopo inayotolewa kwa
vijana kabla ya kujipanga na kuwa na malengo ya matumizi ya mikopo hiyo
kwa maendeleo ya Taifa.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Bw. Christopher
Ryoba Kangoye wakati wa ziara ya maafisa kutoka Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo walipomtembelea ofisini kwake na baadae
kukutana na vijana wa wilaya hizo jana Wilaya ya Mpwapwa Mkoa wa Dodoma.
“Vijana wamekua na tabia ya kukimbilia mikopo inayotolewa na
taasisi mbalimbali za serikali na zisizo za serikali kabla ya kujipanga
hivyo kushindwa kutumia fedha hizo kwa uangalifu na hatimaye kushindwa
kurudisha mikopo hiyo kwa wakati”, alisema Bw. Kangoye.
Aidha Bw. Kangoye amesema kuwa vijana ni nguvu kazi ya taifa
hivyo wanapaswa kujitambua na kutumia nguvu hizo zitakazozalisha matunda
mazuri kwani ili mtu aweze kuendelea lazima afanye kazi kwa bidii na
kwa ufanisi.
Akizungumza kwa niaba ya maafisa kutoka Wizarani waliofika
ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mwezeshaji kutoka Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi Ester Riwa amesema kuwa Wizara
inayosimamia masuala ya Vijana imepanga mikakati mingi ya kuwainua
vijana wa taifa hili hivyo kuiomba Wilaya ya Mpwapwa kushirikiana na
Wizara inayosimamia vijana kuwaongoza vijana wa Wilaya yao kuwa lulu ya
taifa itakayomulika vijana wengine kutoka Wilaya zote nchini Tanzania.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Vijana kutoka Wilaya ya
Mpwapwa Bw. Paschal Jeremiah amesema kuwa vikundi vya vijana kutoka
Wilaya ya Mpwapwa vilipatiwa mkopo wa shilingi milioni 10 mnamo mwaka
2009 na urejeshaji wa mkopo huo umefanyika kwa asilimia 90 hali
inayoonyesha kuwa vijana wa Wilaya yake wako makini na wanastahili
kupatiwa mkopo mwingine kuendeleza shughuli walizozianzisha.
Naye kijana Briton Ivan Majele kutoka kikundi cha Umoja wa
Vijana Ng’ambo kilichopo Wilaya ya Mpwapwa kinachofanya kazi ya kufyatua
matofali amewataka vijana wenzake nchini kutobweteka bali wathubutu na
kuamini kuwa mtaji mdogo unaposimamiwa vizuri huzaa na kuwa mkubwa hivyo
kuthamini kile kidogo walichonacho na kukiendeleza.
No comments:
Post a Comment