Mahmoud Ahmad Arusha
Watu wenye ulemavu nchini wameiomba serikali na taasisi binafsi
zinazotoa huduma za kijamii ikiwemo hospitali,benki na shule kuhakikisha
kuwa wanaweka miundombinu rafiki itakayowawezesha kuzifikia huduma hizo
kwa urahisi.
Katibu wa Shirikisho la Vyama vya
watu wenye Ulemavu Arusha ,Yunusi Urasa amesema kuwa kumekua na tatizo
la la kukosekana kwa miundombinu rafiki kwa walemavu hali
inayowakwamisha kupata huduma hizo muhimu kutokana na ulemavu walionao.
Yunusi aliyasema hayo jana katika
semina ya watu wenye ulemavu iliyofanyika jijini Arusha na kuandaliwa na
Shirikisho la Vyama vya watu wenye ulemavu nchini ,ambapo amesema kuwa
amehimiza serikali kuwakumbuka walemavu katika upangaji wa miji,ujenzi
wa barabara na majengo ili waweze kupata haki zao za msingi za kunufaika
na huduma za jamii.
Katibu huyo amependekeza kuwepo
kwa dawati maalumu la kuwahudumia watu wenye mahitaji maalumu
litakalowasaidia walemavu kupata huduma kwa urahisi.
“Mlemavu asiyeona akienda benki
hawezi kutumia ATM card ni rahisi kuibiwa akikutana na mtu ambaye si
mwaminifu,pegine zitengenezwe ambazo wataweza kuzisoma pia ATM ziko juu
kwa walemavu wanaotambaa ni vigumu kuzifikia” Alisema Yunusi
Naye Katibu wa Chama cha Watu
wenye ulemavu wa ngozi Arusha Happiness Raphael amesema kuwa
wanashangazwa kuona mauaji ya albino yanaendelea huku mashirika ya haki
za binadamu ya kimataifa yakikaa kimya hivyo ameiataka jamii ya
kimataifa kuchukua hatua kukomesha vitendo hivyo.
Mratibu wa Shirikisho la Watu
wenye Ulemavu nchini Francis Mhina amesema kuwa wanafanya juhudi za
kutoa elimu kwa walemavu juu haki zao za msingi na namna ambayo wanaweza
kujikwamua kimaisha ,ameeleza kuwa changamoto kubwa inayowakabili ni
uhaba wa fedha hivyo kushindwa kuwafikia walemavu wengi ambao wako
vijijini na kuishia mijini.
No comments:
Post a Comment