…………………………………………………………………………………………..
Na Concilia Niyibitanga
Vijana wanatakiwa kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa bidii kama njia pekee ya kujikwamua na umasikini.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya
Jamii, Mhe. Said Mtanda (Mb.) jana wakati kamati hiyo ilipokuwa ikikagua
miradi inayoendeshwa na vikundi vya vijana katika Halmashauri ya
Manispaa ya Temeke vilivyopata mikopo kutoka katika Mfuko wa Maendeleo
ya Vijana unaoratibiwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo.
Mhe. Mtanda alisema kuwa ajira za maofisini haziwezi kutosheleza
kila kijana kutokana na ukweli huo ni wakati wa vijana kupambana na
hiyo changamoto kwa njia ya kujiajiri kwa kubuni miradi ya
kuwatengenezea kipato hali itakayowakwamua katika umaskini.
“vijana msiogope kuthubutu siyo lazima kuanza na mradi mkubwa
anza na huo huo mdogo ipo siku utakuwa mradi mkubwa hata mbuyu ulianza
kama mchicha”. Alisema Mhe. Mtanda.
Miradi iliyokaguliwa na Kamati hiyo ni pamoja na mradi wa kilimo
cha matikitimaji, mapesheni na ufugaji kuku unaoendeshwa na Kikundi cha
Vijana kijulikanacho kama Sokoine Youth Development kilichopo kata ya
Somangila, Kigamboni.
Kikundi kingine kilichokaguliwa ni kikundi cha vijana
waliohitimu na walioko vyuo vikuu kijulikanacho kama African Legends
kilichopo Kigamboni; kikundi hiki kinachojishughulisha na mgahawa pamoja
na maswala ya teknolojia ya habari na mawasiliano.
Aidha, Kamati hiyo ilikagua kikundi cha Vijana cha Waungwana
Youth Family kinachojishughulisha na kazi za saluni pamoja na muziki;
kikundi hiki kiko katika kata ya Sandali.
Mhe. Mtanda aliwakumbusha vijana umuhimu wa kujiunga katika
vikundi vya vijana ili watambulike na wajiunge katika SACCOS za vijana
katika Halmashauri wazoishi ili iwe rahisi kukopa katika Mfuko wa
Maendeleo ya Vijana.
Naye Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe.
Juma Nkamia (Mb.) alisema kuwa Wizara imejipanga kuwawezesha vijana
kujikwamua kiuchumi na imekuwa ikitoa elimu ya ujasiriamali na stadi za
maisha zoezi ambalo ni endelevu kwani hadi sasa wataalamu wanazunguka
katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya kazi hiyo.
Mhe. Nkamia alisema kuwa Wizara itaendelea kuwezesha vikundi vya
vijana ambavyo tayari vina miradi ili iweze kukua zaidi na kuwa miradi
mikubwa yenye uwezo wa kutengeneza ajira kwa vijana wengine.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa SACCOS ya Vijana ya Temeke, Bw
Swaka Abbas ambapo ndiko mikopo ya vikundi hivyo ilikopitishiwa
aliishukuru Kamati hiyo kwa kuwatembelea na kuwatia moyo. Pia
aliishukuru Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na
Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kwa ushirikiano wanaoupata katika kazi
zao za kutokomeza umaskini.
No comments:
Post a Comment