Na Abdulla Ali Maelezo- Zanzibar
Vitendo vinavyokwenda kinyume na
maadili ya kijamii vimekuwa vikishamiri kwa kasi miongoni mwa vijana wa
Zanzibar licha ya viongozi wa Dini, Wazee na Walimu kuvikemea vitendo
hivyo.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri
Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mhe. Bi Hindi Hamad Khamis wakati
akijibu swali la mwakilishi wa Jimbo la Muyuni Mhe. Jaku Hashim katika
mkutano wa 18 wa Baraza la Wawakilishi ulioanza leo Chukwani Zanzibar.
Amesema kuwa hivi sasa imekuwa ni
jambo la kawaida kwa baadhi ya vijana wa kiume hususan wa Kizaanzibari
kutoboa masikio, kusuka nywele na kujipodoa jambo ambalo ni kinyume cha
sheria, Silka na Utamaduni wa Mzanzibari.
Mhe Bi Hindi amesema Serikali
imechukua hatua mbalimbali katika kupambana na tatizo la uvunjifu wa
Mila, Silka na Desturi ikiwa ni pamoja na kushajihisha kutolewa elimu ya
Dini na Malezi, Kulinda na Kuhimiza uendelezaji wa Utamaduni pamoja na
kusambaza ustaarabu wa Mzanzibari kwa njia ya Sanaa ya Maonyesho, Semina
na Makongamano.
Mhe. Bi Hindi ametanabahisha kuwa
ili kuondokana na vitendo hivyo viovu, Serikali inapitia upya sheria
zilizopo zinazohusiana na mambo ya Mila, Silka na Desturi kwa lengo la
kuzipa nguvu ili kupunguza kasi ya vitendo vinavyoipaka matope Zanzibar
ambavyo kwa kiasi kikubwa vinachangiwa na uwepo wa utandawazi duniani
kote.
Aidha amesema tatizo liliopo sio
kutokuwepo kwa sheria bali ni usimamizi wa sheria hizo na kuthibitishwa
kwa makosa mbele ya vyombo vya sheria ili kuweza kuchukuliwa hatua
zinazofaa.
“Kwa kulipatia ufumbuzi tatizo hili, sisi sote hapa ni viongozi na wananchi kwa ujumla tunatakiwa kushirikiana kupiga vita vitendo hivyo na kutilia nguvu usimamizi wa sheria tunazozitunga”, alieleza Naibu waziri Bi hindi.
“Kwa kulipatia ufumbuzi tatizo hili, sisi sote hapa ni viongozi na wananchi kwa ujumla tunatakiwa kushirikiana kupiga vita vitendo hivyo na kutilia nguvu usimamizi wa sheria tunazozitunga”, alieleza Naibu waziri Bi hindi.
Mhe. Bi Hindi amewataka Viongozi,
Walimu, Viongozi wa Dini na Wananchi kwa ujumla kushirikiana pamoja
katika kupiga vita vitendo hivyo viovu na kutilia mkazo usimamizi wa
sheria ili kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.
No comments:
Post a Comment