…………………………………………………………………….
Hussein Makame, MAELEZO, Lindi
WANANCHI waliopo kwenye maeneo ya
miradi ya maji mkoani Lindi na nchini kwa ujumla wametakiwa kuacha
kuzembea kwenye vikao vya kujadili maendeleo ya miradi hiyo kwani
kufanya hivyo kutachangia kufa kwa miradi hiyo.
Hayo yamesemwa na Kiongozi wa ziara
ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji mkoani Pwani,
Lindi na Mtwara Amina Makilagi (Mb) wakati alipotembelea mradi wa maji
wa Rondo-Mnara uliopo katika kijiji cha Mnara Kata za Mnara na Chiponda
wilaya ya Lindi mkoani Lindi.
Alisema miradi mingi ya maendeleo
imekufa kutokana na wananchi kuzembea kwenye vikao vya kujadili
uendeshaji wa miradi ya maji, hivyo kuwafanya viongozi wasio waaminifu
kutumia vibaya fedha za miradi hiyo.
“Mnachotakiwa msizembee kwenye
vikao vya kujadili miradi ya maji kwani mkifanya hivyo miradi itakufa
kutokana na viongozi kutumia vibaya fedha za miradi hiyo kujinufaisha
wenyewe” alisema Makilagi.
Alisema wanatakiwa kuhakikisha kuwa
wanasimamia utaratibu wa kuingiza fedha za miradi ya maendeleo ya maji
kwenye akaunti kwani kufanya hivyo kutaepusha viongozi wabadhirifu
kuihujumu miradi hiyo.
Akisoma taarifa ya mradi huo mbele
ya wajumbe wa kamati hiyo ya bunge, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya
Lindi Olliver Vavunge alisema mradi wa Rondo-Mnara ulisanifiwa kuhudumia
wakazi 18,000 kwenye vijiji sita.
Alisema mradi huo uliojengwa na
serikali mwaka 1973 una uwezo wa kuzalisha mita za maji zenye ujazo wa
450 kwa siku lakini kutokana na changamoto ya uchakavu wa mitambo na
gharama kubwa za uendheshaji, uzalishaji umepungua hadi mita za ujazo
328 kwa siku.
“Vituo vitatu vya kusukua maji
vilijengwa kutoka kwenye chanzo cha maji kilichopo katika kijiji cha
Chikote.Ambapo kwenye kila kituo ilifungwa mitambo miwili ya kusukuma
maji iliyotumia injini ya diseli.” Alisema Vavunge.
Alisema mradi wa Rondo-Mnara ni
miongoni mwa miradi minne ya maji safi na salama ambayo hadi sasa
imekamilika na inatoa huduma kwa wananchi ikiwemo miradi ya Kiwawa,
Likwaya na Namkongo.
“Miradi hiyo inatoa huduma ya maji
kwa wakazi 5,000 huku halmashauri ikiendelea kutekeleza miradi ya Maji
ya Namangale, Hingawali, Littipu, Nyangamara na Nahukahuka” alisema.
Kwa upande wa mradi wa Ng’apa
unaojulikana kwa jina la 7 Towns Upgrading Program, unaofadhiliwa na
serikali ya Ujerumani na Jumuiya ya Ulaya, una lengo la kuboresha huduma
ya maji katika mji wa Lindi.
Mradi huo unatarajiwa kukamilika
mwezi Machi mwaka huu na kufikisha huduma ya maji safi na salama kwa
wakazi 194,143 wa manispaa ya Lindi na unajenga mtambo wa kusafisha
majitaka yanayozalishwa katika mji wa Lindi.
Awali akiwasilisha taarifa ya
huduma ya maji mkoa wa Lindi kwa wajumbe wa kamati hiyo ya Bunge mkoani
Lindi, Afisa Tawala wa Mkoa wa Lindi Abdallah Chikota alisema hadi
Novemba mwaka 2014 wakazi wa mijini wanaopata maji safi ni asilimia 55.4
ya wakazi wote 162, 049.
Alisema kwa upande wa wakazi wa
vijijini wanaopata huduma ya maji safi na salama wanakadiiriwa kufikia
297,796 kati ya wakazi 702, 603 wa vijijini.
Naye Mkuu wa mkoa wa Lindi Mwantumu
Mahiza alisema pamoja na Serikali kutoa fedha kwa ajili ya kutoa huduma
ya maji safi na salama kwa wakazi wa mkoa huo, lakini huduma hiyo
haipatikani kama inavyotakiwa kutokana na tatizo la kukatika kwa umeme
ambao kwa siku unaweza kukatika kati ya mara 22 hadi 25.
Hata hivyo, alisema amewasilisha
taarifa kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na wanatarajia kukutana
na uongozi wa juu wa shirika hilo hivi karibuni ili kujadili changamoto
hiyo ambayo inategemewa kwa kiasi kikubwa katika upatikanaji wa maji
mkoani humo.
Ziara ya wajumbe wa kamati ya Bunge
ya Kilimo, Mifugo na Maji inaendelea kukagua miradi ya maji katika mkoa
wa Mtwara ambapo inatarajia kukagua miradi ya Nanyamba-Namkuku na
Tandahimba-Matogolo.
No comments:
Post a Comment