WACHEZAJI WAWILI VPL, FDL WAPIGWA FAINI
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imewapiga faini na kuwafungia mechi wachezaji wawili wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa kufanya vitendo kinyume na kanuni zinazotawala ligi hizo.
Mshambuliaji Haruna Chanongo wa
Stand United amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 kwa
kumpiga teke mwamuzi wa mechi dhidi ya Polisi Morogoro iliyochezwa
Januari 3 mwaka huu Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Adhabu hiyo
imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 37(3) ya Ligi Kuu.
Kipa Amani Simba wa Oljoro JKT
amepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kukataa kupeana mkono na viongozi
wakati wa kusalimia kabla ya kuanza mechi kati ya timu yake na Toto
Africans iliyofanyika jijini Mwanza. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa
kanuni ya 14 ya FDL.
Timu ya Polisi Mara imepigwa faini
ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake wakati wa mechi ya
FDL dhidi ya Mwadui ya Shinyanga iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya
Karume mjini Musoma. Pia Polisi Tabora imepigwa faini ya sh. 500,000
kutokana na vurugu za washabiki wake kwenye mechi namba 40 dhidi ya
Geita Gold, adhabu ambazo zimetolewa kwa mujibu wa kanuni ya 41.
12 WAPELEKWA KAMATI YA NIDHAMU YA TFF
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limewapeleka
wanamichezo 12 wakiwemo viongozi, makocha na wachezaji kwenye Kamati ya
Nidhamu kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu kutokana na matukio
mbalimbali kwenye Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na michuano ya Kombe la
Taifa la Wanawake.
Wachezaji Dihe Makonga, Swalehe
Idd Hussein, Ramadhan Mwinyimbegu na Shaibu Nayopa wa Oljoro JKT, na
Nassib Lugusha wa Polisi Dodoma wanalalmikiwa katika Kamati ya Nidhamu
kwa kushambulia waamuzi na kufanya vurugu kwenye benchi la timu pinzani
katika mechi zao za FDL.
Mtunza Vifaa (Kit Manager) wa
Polisi Mara, Clement Kajeri analalamikiwa kwa kuongoza mashambulizi
dhidi ya waamuzi kwenye mechi kati ya timu yake na Mwadui iliyochezwa
Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.
Naye Mtunza Vifaa (Kit Manager) wa
Rhino Rangers, Albert Mbunji anapelekwa katika Kamati hiyo kwa kupinga
maamuzi na kuwatukana waamuzi kwenye mechi dhidi ya Polisi Dodoma
iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Pia Mtunza Vifaa (Kit Manager) wa
Oljoro JKT, Eliud Justine Mjarifu analalamikiwa kwa matukio mawili;
alimpiga Kocha wa Burkina Faso, CR Mwakambaya kwenye mechi ya FDL
iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Pia alimtukana mwamuzi
akiba (fouth official) Mussa Magogo kwenye mechi dhidi ya Toto Africans
iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Kocha wa Polisi Tabora, Kim
Christopher analalamikiwa kwa kumtolea mlugha chafu mwamuzi wa mechi
kati ya timu yake na Panone FC iliyochezwa Uwanja wa Ushirika mjini
Moshi.
Msimamizi wa Kituo cha Musoma,
Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara (FAM), Mugisha Galibona
naye anapelekwa katika Kamati ya Nidhamu kwa tuhuma za kutotoa
ushirikiano kwa maofisa wa mechi na kuchochea maofisa hao (waamuzi)
kupigwa.
Kwa upande wake, Kamati ya Mpira
wa Miguu wa Wanawake ya TFF imependekeza Katibu wa Chama cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Simiyu, Emmanuel Sologo, na Kaimu Katibu wa Chama cha
Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida (SIREFA), Gabriel Gunda kupelekwa kwenye
kamati ya Nidhamu kwa matukio mbalimbali yaliyojitokeza kwenye mechi za
Kombe la Taifa la Wanawake.
Sologo anatuhumiwa kumpiga kibao
mwamuzi wa mechi ya marudiano kati ya timu yake ya Simiyu na Shinyanga
iliyochezwa mjini Shinyanga, tukio ambalo lilimfanya mwamuzi huyo avunje
mchezo.
Naye Gunda analalamikiwa kwa
kushindwa kuhakikisha timu yake ya Singida inaingia uwanjani kwenye
mechi ya marudiano dhidi ya Dodoma iliyokuwa ifanyike kwenye Uwanja wa
Namfua mjini Singida.
SDL KUANZA MZUNGUKO WA PILI JANUARI 31
Mzunguko wa pili wa Ligi Daraja la Pili (SDL) sasa utaanza
Januari 31 mwaka huu, badala ya Januari 24 mwaka huu kama ilivyopangwa
awali ili kutoa fursa kwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia usajili wa dirisha
dogo.
Timu zinazocheza ligi hiyo katika
makundi manne tofauti ni; Milambo FC, Mji Mkuu FC (CDA), Mvuvumwa FC,
Singida United, na Ujenzi Rukwa (Kundi A), Arusha FC, Bulyanhulu FC, JKT
Rwamkoma FC, Mbao FC, na Pamba SC (Kundi B).
Nyingine ni Abajalo FC, Cosmopolitan, Kariakoo Lindi, Kiluvya
United, Mshikamano FC, na Transit Camp (Kundi C), wakati Kundi D ni
Magereza Iringa, Mji Njombe, Mkamba Rangers, Town Small Boys, Volcano
FC, na Wenda FC.
No comments:
Post a Comment