………………………………………………………………………………………..
Na Veronica Kazimoto
Morogoro
Wito umetolewa kwa Maafisa wa
Ngazi za Juu wa Jeshi la Magereza kutoka vitengo mbalimbali vya Makao
Makuu ya Jeshi hilo kuwahimiza maofisa waliopo chini yao kutumia takwimu
mbalimbali zinazozalishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu ili zisaidie
katika kuandaa mipango na kutoa maamuzi mbalimbali ya kazi zinazofanywa
na jeshi hilo.
Wito huo umetolewa leo na Meneja
Tawala wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Gabriel Madembwe wakati
akifungua Mafunzo ya Takwimu Rasmi kwa Maafisa wa Ngazi za Juu wa Jeshi
hilo yaliyofanyika katika ukumbi wa Amabilisi uliopo mkoani Morogoro.
Madembwe amesema kuwa maafisa
wengi katika Jeshi la Magereza wakijua umuhimu wa matumizi ya takwimu
itasaidia kuleta mabadiliko hasa katika kupanga mipango yao kwenye
maeneo yao ya kazi.
“Napenda kusisitiza kuwa ili
mabadiliko yatokee sehemu yoyote ile; iwe nyumbani, kazini au katika
jamii, ni lazima kuwepo na kichocheo cha mabadiliko hayo, hivyo ninyi
mtakuwa kiungo muhimu katika kuleta mabadiliko yenye kutoa maamuzi kwa
kuzingatia matumizi ya takwimu rasmi”, amesema Madembwe.
Nae Kamishna Msaidizi Mwandamizi
wa Jeshi la Magereza kutoka Makao Makuu Dar es Salaam Bw. Edward Kaluvya
amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka ambapo kwa sasa wamekuwa
wakitumia sana takwimu katika maeneo mengi ya kazi zao.
“Mafunzo haya yatatusaidia kujenga
uelewa wa pamoja na kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali
yanayohusiana na uzalishaji, uhifadhi na utumiaji wa takwimu kwa usahihi
katika kutoa maamuzi na kupanga mipango endelevu katika Jeshi letu la
Magereza”, amefafanua Kaluvya.
Mafunzo haya ya siku tatu
yanatolewa na Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika kilichopo jijini Dar
es Salaam na yamefadhiliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kupia Mpango
Kabambe wa Kitaifa wa Kuboresha na Kuimarisha Takwimu Tanzania (TSMP).
Lengo kuu la Mpango huu ni
kuhakikisha Tanzania inakuwa na mfumo imara wa kitaifa wa kuratibu,
kukusanya, kuhifadhi na kusambaza takwimu nchini.
No comments:
Post a Comment