Akipokea maelezo ya Mwenyekiti wa serikali ya mtaa na baadae kuzungumza
na wananchi wa eneo hilo, mkuu wa wilaya aliambiwa na baadhi ya wakazi
wa asili wa eneo hilo kuwa sehemu hiyo ilikua ni bwawa la maji miaka
yote.
Wakazi hao ambao nyumba zao zimezungukwa na maji walimuomba Mkuu wa
wilaya kusaidiwa pampu kubwa ili maji hayo yavutwe na kupelekwa kwenye
mitaro upande wa pili wa barabara.
Akijibu maombi hayo Mh. Hapi aliwaagiza mainjinia wa manispaa
kuhakikisha kuwa wanafanya utaratibu wa kupata pampu kubwa ya kuvuta
maji hayo. Aidha, Mkuu huyo wa wilaya ya Kinondoni aliwaambia wananchi
kuwa wale wote waliojenga katika eneo hilo ambalo ramani inaonesha kuwa
ni eneo la wazi wajiandae kuondoka.
"Serikali itawasaidia kutoa haya maji kama hatua ya dharura. Lakini
suluhu ya kudumu ni kuwa waliojenga hapa wote wamejenga eneo la wazi
tena ni bwawa. Hivyo lazima wajiandae kuhama.
Serikali kazi yake ni kuwaambia wananchi ukweli, hata kama ukweli huo
utakua na maumivu. Hivyo ukweli wa jambo hili ni kuwa waliojenga hapa
wahame."
Akitoa rai kwa viongozi wa serikali ya mtaa ambao wameshiriki katika
kuuza eneo hilo kinyume na taratibu mh. Mkuu wa Wilaya aliagiza na
kusema
" kila Mwananchi aliyejenga hapa aende ofisi ya mtaa kujisajili akiwa na
vielelezo vyote vya kumiliki eneo hili na alikonunua. Kisha nipewe
taarifa na uhakiki utafanyika. Kama kuna viongozi wa serikali ya mtaa
walishiriki kuuzia watu viwanja hapa kinyume na ramani ambayo wao wana
nakala yao basi wajiandae kuwajibishwa."
Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya alitembelea eneo la Mbweni ambako
Mwananchi asiyefahamika amejenga ukuta kuzunguka eneo la wazi. Hapi
alifika eneo hilo na kujionea ukuta huo kisha akaagiza mtendaji wa mtaa
pamoja na anayejenga ukuta huo kufika ofisini kwake kesho Ijumaa mchana
wakiwa na vielelezo vyote na vibali vya ujenzi kama wanavyo.
Ziara ya mkuu wa wilaya inaendelea muda huu katika maeneo ya barabara za Sinza ambazo wakandarasi walipewa kujenga.