Na Jacquiline Mrisho-MAELEZO-Dar es salaam
Jumla
ya wagonjwa 267 wa mkoani Njombe wamenufaika na huduma za matibabu za
madaktari bingwa kutoka hospitali mbalimbali za hapa nchini.
Takwimu
hizo zimetolewa leo mkoani Njombe na Afisa Mawasiliano Mkuu wa Mfuko wa
Taifa wa Bima ya Afya, Luhende Singu wakati akitoa taarifa za maendeleo
ya zoezi la utoaji wa huduma za afya kwa wananchi chini ya ufadhili wa
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Amesema
kuwa kati ya wagonjwa hao, 13 wamepatiwa huduma ya upasuaji kutoka kwa
madaktari bingwa pia huduma hizo zinaendelea kutolewa katika Hospitali
ya Kibena mkoani humo.
"Tunawashukuru
sana wananchi wa Mkoa wa Njombe kwa kuitikia wito wetu, leo ni siku ya
tatu lakini tumeshawapatia matibabu jumla ya wananchi 267 kati ya hao
wagonjwa 13 wamepatiwa huduma ya upasuaji, tunawasihi waendelee kuja
kwakua bado tuna siku mbili za kuendelea kuwapatia huduma za
afya"alisema Singu.
Amefafanua
kuwa asilimia kubwa ya wagonjwa waliopatiwa matibabu mkoani hapo ni
wanawake ambao wengi wao wanasumbuliwa na magonjwa ya moyo pamoja na
mfumo wa mkojo.
Lengo
wa mpango huu wa kutumia madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili na Hospitali za Rufaa za Kanda ni kuhakikisha kuwa huduma za
matibabu kutoka kwa madaktari bingwa zinawafikia wanachama wa Mfuko huo
na Watanzania kwa ujumla popote walipo.
Mpaka
sasa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umepeleka huduma ya madaktari
bingwa katika Mikoa 14 ikiwa na lengo la kuhakikisha huduma bora za
matibabu zinatolewa kwa usawa.Singu ametoa wito kwa wananchi wa mkoani
Njombe kuendelea kujitokeza kwa wingi kujipatia matibabu kwa kuwa huduma
hizo zinatolewa kwa gharama nafuu.
No comments:
Post a Comment