Takwimu hizo zimetolewa leo mkoani Njombe na Afisa Mawasiliano
Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Luhende Singu wakati akitoa
taarifa za maendeleo ya zoezi la utoaji wa huduma za afya kwa wananchi
chini ya ufadhili wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Amesema kuwa kati ya wagonjwa hao, 13 wamepatiwa huduma ya
upasuaji kutoka kwa madaktari bingwa pia huduma hizo zinaendelea
kutolewa katika Hospitali ya Kibena mkoani humo.
“Tunawashukuru sana wananchi wa Mkoa wa Njombe kwa kuitikia wito
wetu, leo ni siku ya tatu lakini tumeshawapatia matibabu jumla ya
wananchi 267 kati ya hao wagonjwa 13 wamepatiwa huduma ya upasuaji,
tunawasihi waendelee kuja kwakua bado tuna siku mbili za kuendelea
kuwapatia huduma za afya”alisema Singu.
Amefafanua kuwa asilimia kubwa ya wagonjwa waliopatiwa matibabu
mkoani hapo ni wanawake ambao wengi wao wanasumbuliwa na magonjwa ya
moyo pamoja na mfumo wa mkojo.
Lengo wa mpango huu wa kutumia madaktari bingwa kutoka Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili na Hospitali za Rufaa za Kanda ni kuhakikisha kuwa
huduma za matibabu kutoka kwa madaktari bingwa zinawafikia wanachama
wa Mfuko huo na Watanzania kwa ujumla popote walipo.
Mpaka sasa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umepeleka huduma ya
madaktari bingwa katika Mikoa 14 ikiwa na lengo la kuhakikisha huduma
bora za matibabu zinatolewa kwa usawa.
Singu ametoa wito kwa wananchi wa mkoani Njombe kuendelea
kujitokeza kwa wingi kujipatia matibabu kwa kuwa huduma hizo zinatolewa
kwa gharama nafuu.
No comments:
Post a Comment