Wanasema
uchungu wa mwana aujuae mzazi! Na kutokana na uchungu huo wa mama, ni
vigumu kumshawishi akae meza moja na mtu aliyemuua mwanae kwa makusudi
tena kwa kumpiga hadi kuhakikisha anakata roho.
Lakini imekuwa tofauti na jambo lililowaacha mdomo wazi umati wa watu
uliohudhuria kushuhudia kunyongwa kwa mwanaume aliyemuua kijana mwenye
umri wa miaka 18 nchini Iran ambako hukumu ya kunyongwa hadharani ni
kawaida kwa mtu aliyepatikana na hatia ya kuua kwa kukusudia, pale
ambapo mama mzazi wa marehemu alipoingilia na kumfungua kitanzi muuaji
huyo sekunde ya mwisho.
Kwa
mujibu wa The Guardian, mwanaume huyo aliyejulikana kwa jina la Balal
alikuwa tayari amefungwa kitambaa cheusi na kuvalishwa kitanzi akisubiri
amri ya kitanzi kufyatuliwa, ghafla mama huyo alimzaba kibao usoni na
kuanza kumfungua kitanzi akisaidiana na mumewe!
“Mimi ni mtu wa imani.” Alisema mama
huyo aliyefahamika kwa jina la Samereh Alinejad. “Nilipata ndoto ambayo
mwanangu alikuwa ananiambia kuwa yuko katika sehemu nzuri na yenye
amani…baada ya hapo, ndugu zangu wote, hata mama yangu, wakaanza
kunihimiza nimsamehe muuaji huyu.”
Balal alihukumiwa kunyongwa hadi kufa
baada ya kupatikana na hatia ya kumpiga vibaya Abdollah Hosseinzadeh
(18) hadi kumuua katika ugomvi uliotokea mtaani kati yao mwaka 2007.