Mwalimu Julius Nyerere (kushoto) na Sheikh Abeid Amani Karume
(kulia) wakibadilishana Hati za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Aprili, 1964.
Na Emmanuel J. Shilatu.
Ni miaka 52 imetimia tangu jahazi lililowabeba Watanganyika na
Wazanzibar liweke historia ya kung’oa nanga mara baada ya Jamhuri
Muungano wa Tanzania kuzaliwa rasmi mnamo April 26,1964. Hii ilitokana
na ujasiri, ushupavu na nia ya dhati waliyokuwa nayo waasisi wa Muungano
huu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Tanganyika) na Abeid Aman Karume
(Zanzibar).
Hatua hiyo ilifikiwa kutokana na mtiririko wa kimazingira na
mahusiano ambayo yalishabihiana kama sio kufanana kabisa kwa pande zote
mbili (Tanganyika na Zanzibar). Zipo sababu za kijiografia, kisayansi,
kitamaduni na kihistoria zilizochangia huu muungano wetu.
Kutokana na sababu za kijiografia na kisayansi inaaminika kabisa
kwamba Visiwa vya Zanzibar (Pemba na Unguja) vilikuwa vimeungana na hata
kushikamana kwa pamoja pembezoni mwa pwani ya ardhi ya Tanganyika.
Hivyo tangu awali tulikuwa ni kitu kimoja, tulio katika ardhi moja na ya
pamoja.
Pia kuna historia (isiyo na shaka) ya muingiliano wa kiutamaduni
baina ya Wakazi wa Tanganyika na Zanzibar ambapo hali nzima ya kuoa ama
kuolewa ilizidi kushamiri baina yao.
Halikadhalika harakati za kudai ukombozi wa uhuru wetu ili tuweze
kujitawala wenyewe kutoka kwa dudu la wakoloni nazo zilichangia
kutuunganisha. Inaaminika (na ndiyo ilivyo) ya kuwa asilimia kubwa ya
Wazanzibar walishiriki kwenye harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika
kutoka kwa Mwingereza ambapo kutokana na nia, ushupavu na nguvu ya
pamoja walifanikiwa kupata Uhuru wa Tanganyika mnamo Desemba 9, 1961.
Lakini pia licha ya asilimia kubwa ya Wazanzibar kushiriki katika
mchakato wa Mapinduzi ya Zanzibar lakini pia kulikuwepo na asilimia
kubwa ya mchango wa ushiriki kutoka kwa Watanganyika. Hatimaye matunda
yake yalionekana ya mapinduzi matukufu yaliyofikia kilele katika uwanja
wa Gombani Pemba yaliyofanyika Jamhuri 12, 1964, baada ya kuchoshwa na
hila na ghiliba za Waarabu uliotamalaki visiwani humo kwa zaidi ya karne
mbili na hatimaye waliwaacha wazalendo watwana katika ardhi yao.
Pia tusisahau lengo na nia ya dhati aliyokuwa nayo Mwalimu Nyerere
ya kutaka kuiunganisha Afrika mzima kwa hatua lakini jitihada zake
zilianza kuzaa matunda ambayo hayatakaa yatokee tena Afrika kwa
kuiunganisha Tanganyika na Zanzibar.
Mnamo April 22, 1964, Maraisi wa nchi hizi mbili ambazo sasa
zinaunda Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (wa Jamhuri ya
Tanganyika) na Abeid Amani Karume (wa Jamhuri ya watu wa Zanzibar )
walitia sahihi Mkataba wa kimataifa wa kuunganisha nchi zao,
unaojulikana kama “Hati ya Muungano” (Articles of union) na hivyo kuunda
Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ama United Republic of
Tanganyika and Zanzibar (URTZ) ambao ni muungano sahihi kabisa kisheria
na unaotambulika Kikatiba.
No comments:
Post a Comment