Shirikisho la Mpira wa Miguu
Afrika (CAF) limefanyia marekebisho kanuni zake za michuano ya ngazi ya
klabu kwa upande wa malazi ambapo sasa timu zitachagua na kujilipia
zenyewe hoteli zinapokuwa kwenye mechi za ugenini.
Kabla ya marekebisho ya kanuni
hiyo, timu ngeni ilikuwa ikilipiwa hoteli na timu mwenyeji kwa msafara
usiozidi watu 25. CAF ilikuwa imepitisha hoteli maalumu katika kila nchi
ambapo mwenyeji alitakiwa kuziweka timu ngeni.
Kwa marekebisho hayo, Chama cha
Mpira wa Miguu cha nchi mwenyeji kitakuwa na wajibu wa kuitafutia hoteli
timu ngeni iwapo tu kitaombwa kufanya hivyo, lakini jukumu la kulipia
malazi litakuwa la timu yenyewe.
Mwaka huu Tanzania inawakilishwa
na timu mbili za Azam na Yanga katika michuano ya CAF. Azam inacheza
Ligi ya Mabingwa (CL) ambapo itaanzia nyumbani Februari 15 mwaka huu kwa
kuikaribisha El Merreikh ya Sudan kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini
Dar es Salaam.
Nayo Yanga itacheza michuano ya
Kombe la Shirikisho (CC), na imepangiwa kucheza mechi ya kwanza nyumbani
dhidi ya BDF IX ya Botswana. Mechi hiyo itafanyika Februari 14 mwaka
huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment