…………………………………………………………….
Na: Genofeva Matemu – Maelezo, Mbeya
Tarehe 22/01/2015
Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi imeshauriwa kupeleka vijana wa
wilaya hiyo katika Vituo vya Vijana kupata mafunzo mbalimbali ili kuweza
kupata mbinu mbadala za kiujasiriamali.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Kituo cha Vijana Sasanda Bw.
Laurean Masele wakati wa semina ya Ujasiriamali, Stadi za Maisha, Ujuzi
na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana hivi karibuni katika Wilaya ya Mbozi
Mkoa wa Mbeya.
Bw. Masele amesema kuwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo inasimamia Kituo cha Vijana Sasanda Mbeya kinachotoa mafunzo ya
ujasiriamali katika fani za Kilimo na Ufugaji, Kituo cha Vijana cha
Ilonga Morogoro kinachotoa mafunzo katika fani ya teknolojia ya habari
na mawasiliano na Kituo cha Vijana cha Marangu Moshi kinachotoa mafunzo
ya uthubutu/ujasiri kwa vijana.
Aidha Bw. Masele amesema kuwa moto uliowashwa na Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuhamasisha vijana mbinu za
kiujasiriamali unalenga kuwajengea vijana ujasiri wa kuthubutu na
kufikia malengo waliyojiwekea.
Akizungumza wakati wa kufungua semina hiyo Kaimu Mkurugenzi
Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Bw. Elisey Ngowi amewataka
vijana kuzingatia elimu inayotolewa na kuifanyia kazi kwani vijana bado
wanauwezo mkubwa wa kufikiri hivyo kutumia akili nyingi na nguvu nyingi
kufanya mambo mbalimbali kwa maendeleo ya Wilaya hiyo.
Kwa upande wake kijana Yohana Chaula kutoka kikundi cha Bodoboda
B. Mloo Wilaya ya Mbozi amesema kuwa kundi la vijana wasiokua na ajira
kwa sasa linazidi kuongezeka hivyo kuiomba Wizara inayosimamia masuala
ya Vijana kuongeza fungu katika Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ili vijana
wote nchini waweze kunufaika na Mfuko huo.
Naye mwakakikundi wa kikundi cha Umoja wa Vijana Wilaya ya Mbozi
Bw. Chemli Ndema ameushukuru ujumbe kutoka Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo kufika Wilaya ya Mbozi na kutoa elimu ya ujuzi kwa
vijana kwani elimu aliyoipata katika semina hiyo imemtoa katika giza
nene na kukiri kuwa atakuwa chachu ya maendeleo na kiongozi bora katika
jamii.
No comments:
Post a Comment