Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Naibu Rais wa Afrika Kusini Cyril
Ramaphosa (kulia) na Bw. Bw. Deng Alor Kuol wakifurahia wakati Rais
Salva Kiir Mayardiy wa Sudan ya Kusini (wa pili kushoto) na Makamu waRais wa zamani wa Sudan Dkt Riek Machar Teny (wa pili kulia) wakipeanamikono na kubadilishana nyaraka baada ya kutia saini mkatana wamakubaliano ya kukiunganisha upya chama cha SPLM cha Sudani Kusinikatika hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha Jumatano Januari 21, 2015usiku.PICHA NA IKULU
………………………………………………………………………………
MKATABA wa kujenga tena umoja na
kukiunganisha upya Chama Tawala cha Sudan Kusini cha Sudan People’s
Liberation Movement (SPLM) ulitiwa saini usiku wa jana, Jumatano,
Januari 22, 2015, katika sherehe ya kufana iliyofanyika katika Ukumbi wa
Mikutano wa Hoteli ya Ngurdoto, Wilaya ya Arumeru, Mkoa wa Arusha.
Mkataba huo unaojulikana kama Agreement on the Re-unification of
Sudan People’s Liberation Movement umepongezwa kuwa ni hatua muhimu
katika kulitoa taifa changa la Sudan Kusini katika hali ya machafuko,
vita vya wenyewe kwa wenyewe, kutoelewana na kutoaminiana, mambo ambayo
yameligubika taifa hilo tokea mwishoni mwa 2013 wakati kutokuelewana
kulipozuka ndani ya SPLM na hatimaye katika Serikali ya nchi hiyo.
Baada ya siku nzima ya mawasiliano na majadiliano baina ya pande
zinazovutana ndani ya chama hicho pamoja na viongozi wa nchi jirani na
rafiki na Sudan Kusini, viongozi watatu wa vikundi vinavyopingana ndani
ya SPLM walitia saini Mkataba huo muhimu sana.
Viongozi waliotia saini ni Mheshimiwa Salva Kiir Mayardit, Rais
wa Sudan Kusini ambaye pia ni Mwenyekiti wa SPLM na anayeongoza kundi
linalojulikana kama SPLM in Government (SPLM-IG), Mheshimiwa Dkt. Riek
Machar ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa SPLM na pia aliyekuwa Makamu
wa Rais wa Sudan Kusini anayeongoza kundi la SPLM in Opposition
(SPLM-IO) na Dkt. Deng Alor Kuol ambaye anaongoza kundi la SPLM Leaders-
Former Detainees (SPLM Leaders – FD).
Sherehe hiyo ilishuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho ndicho kimesimamia mazungumzo
yaliyozaa Mkataba huo. Rais Kikwete pia ndiye mdhamini mkuu wa Mkataba
huo.
Wengine walioshuhudia tukio hilo muhimu ni Rais wa Uganda,
Mheshimiwa Jenerali Yoweri Kaguta Museveni; Rais Uhuru Muigai Kenyatta
wa Kenya; Naibu wa Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini Mheshimiwa Cyril
Ramaphosa, Makamu Mwenyekiti wa zamani wa CCM Mheshimiwa John Samwel
Malecela ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti wa mazungumzo yaliyozaa Mkataba
huo na Katibu Mkuu wa CCM Mheshimiwa Abdulrahman Kinana ambaye alikuwa
mwezeshaji wa mazungumzo.
Mazungumzo yaliyozaa Mkataba huo yalianza mwishoni mwa mwaka
jana baada ya Rais Kikwete na Chama cha CCM kuombwa na Rais Kiir
Mayardit kukubali chama hicho tawala cha Tanzania kutumia uzoefu na
ujuzi wake wa miaka mingi wa uongozi na siasa kujaribu kuleta suluhu
ndani ya SPLM.
Mazungumzo hayo ya kutafuta suluhu ambayo yamefanyika kwa awamu
mbili, ya kwanza yakiwa yamefanyika Oktoba mwaka jana na pili yakiwa
yameanza mwanzoni mwa mwezi huu, Januari 2015, yameongeza thamani kwenye
mazungumzo mengine yanayofanyika Addis Ababa, Ethiopia chini ya
usimamizi wa taasisi ya IGAD na yanayojadili jinsi ya kurejesha amani
nchini humo.
Viongozi wa SPLM wanaamini kuwa kwa sababu mgogoro wa kisiasa
nchini mwao ulianzia ndani ya chama hicho na kwa sababu SPLM ndicho
chombo pekee ambacho kinawaunganisha wananchi wote wa Sudan Kusini, basi
busara inaelekeza kuwa suluhu ianze kutafutwa ndani ya chama hicho.
Mkataba wa jana, kimsingi, unalenga kuweka mazingira ya kujenga
utulivu, maelewano, amani na umoja wa kudumu ndani ya chama hicho na
nchini humo kwa kuhakikisha kuwa utekelezaji wa mambo ya msingi
yaliyokubaliwa kuhusu shughuli za siasa, uongozi na oganisheni ya chama
hicho yanafanyika bila kukawia.
Mkataba huo pia unalenga kuhakikisha kuwa chama cha SPLM
kinabuni na kutekeleza sera za kuondokana na ukabila, makundi yenye
mitazamo finyu na mwenendo wa kijeshi katika siasa za Sudan Kusini.
Aidha, Mkataba huo unalenga kuhakikisha kuwa chama cha SPLM
kinafanya mageuzi ya kuanza kujenga utamaduni wa kuvumiliana na ujenzi
wa misingi ya demokrasia.
Mkataba huo pia unataka watu wote ambao walishiriki katika
mauaji na umwagaji damu katika vita vya wenyewe kwa wenyewe wasiruhusiwe
kugombea wala kushika nafasi ya uongozi wa umma ndani ya chama hicho.
Pia viongozi wote wa Sudan Kusini wanatakiwa, chini ya Mkataba
huo, kuwaomba radhi wananchi wa nchi hiyo ya Sudan Kusini kwa kuruhusu
nchi hiyo kuingia katika machafuko ya umwagaji damu mkubwa.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
22 Januari,2015
No comments:
Post a Comment