……………………………………………………………………………………….
Na: Genofeva Matemu – Maelezo, Mbeya
Vijana wa Mkoa wa Mbeya Wilaya ya
Mbeya Vijijini wametakiwa kutokuwa na tafsiri hasi kuhusu Mfuko wa
Maendeleo ya Vijana kuwa ni takrima inayotolewa na serikali kwa vijana
hivyo kuchezea fedha hizo na kushindwa kurejesha mkopo watakaouomba
kupitia mfuko huo.
Hayo yamesemwa na Mwezeshaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo Bibi Ester Riwa wakati wa semina iliyotolewa kwa
Vijana wa Mbeya Vijijini kuhusu Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, Stadi za
Maisha, Ujuzi na Ujasiriamali jana Mkoani Mbeya.
Bibi Riwa amesema kuwa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana unahudumia
vijana wote nchini bila kuangalia itikadi za kisiasa ukiwa na lengo la
kuwakomboa vijana na kuinua vipaji vya vijana nchi nzima.
“Vijana ni taifa la leo na kesho likiwezeshwa taifa zima
limewezeshwa, Wizara yenye dhamana na Vijana inalenga kuwafikia vijana
wote nchini bila kuangalia itikadi za kisiasa kwani vijana wote ni wetu
na tunatamani kuona vijana wanajiendeleza kufikia ndoto walizonazo”
amesema Bibi Riwa.
Aidha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbeya Vijijini Bibi Upendo
Sanga amesema kuwa ni bahati ya pekee kutembelewa na ugeni kutoka Wizara
ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo hivyo kuwaomba vijana wa Wilaya
yake kuzingatia elimu watakayoipata na kusambaza elimu hiyo kwa vijana
wengine wa Wilaya yake ambao hawakuweza kufika katika semina hiyo.
Bibi Sanga ameiomba Wizara yenye dhamana na Vijana kuendeleza
programu ya kuwaelimisha vijana mara kwa mara na kuwahamasisha vijana
kujiunga katika vikundi kwani ni raisi kusaidia vijana wakiwa katika
vikundi kuliko kumsaidia kijana mmojammoja.
Akichangia wakati wa semina hiyo kijana Evans Bembeja kutoka
Shirika la Efao linalojishughulisha na kilimo cha mbogamboga amesema
kuwa vijana wengi hawaangalii mbele wamekua kwenye mwamko wa kisiasa
wakiamini kuwa siasa ndio sehemu ya kupata pesa za haraka hivyo kuachana
na fursa nyingine kama vile kilimo na ufugaji.
No comments:
Post a Comment