WAKAZI
wa Kata Kibeberu na Magole, Kata ya Kitunda, Manispaa ya Ilala, Mkoa wa
Dar es Salaam wamemlalamikia mkandarasi wa ujenzi wa daraja la Magole
kwa kushindwa kukamisha ujenzi wa daraja hilo hadi sasa.Aidha
wakazi hao wamesema pamoja na daraja hilo kuchelewa kukamilika pia kwa
mtazamo wao wanaamini kuwa lipo chini ya viwango ambavyo vinatakiwa.Mjumbe
wa Kamati ya Ujenzi wa daraja hilo Samir Ibrahim alisema daraja hilo
lnatakiwa kukamilika ifikapo Februari mwaka huu lakini hadi sasa hakuna
dalili za kukamilika kwake.
Ibrahim alisema pamoja na kuchelewa kukamilika kwa daraja
hilo pia wamejaribu kutoa ushauri kuwa urefu wa daraja hilo hautaweza
kuhimili maji mengi ambayo yanapita hasa wakati wa mvua.
Mjumbe huyo alisema jambo lingine ambalo linawatia shaka kwa
kutodumu kwa daraja la Magole ni pamoja na aina ya nondo zinazotumika ni
ishara tosha kuwa haliwezi kudumu kwa muda mrefu.
“Mimi ni mjumbe wa kamati ya ujenzi lakini
kusema ukweli hali ya ujenzi wa daraja hili naitilia shaka sana
sidhani kuwa litadumu na ukiangalia mto huo ni mkubwa sana unahitaji
daraja la viwango,” alisema.
Ibrahim alisema pamoja na jitihada zao za kutoa taarifa za
hali ya daraja hilo kukosa ubora hakuna juhudi zozote ambazo
zimechukuliwa na Serikali kufuatilia.
Kwa upande wake Aisha Athuman alisema iwapo daraja hilo la
Magole halitakamilika kwa wakati ni wazi kuwa watoto na mama wajawazito
wataathirika kwa kiwango kikubwa.
Athman alisema daraja hilo likipitisha maji watoto hawaendi shule jambo ambalo linawaathiri kitaaluma.
“Unajua hapa njia ya kuendea shule ya Msingi Magole ni moja
tu hivyo iwapo hali ya daraja kutokamilika ka wakati itaendelea ni
dhahiri kuwa madhara yataongezeka,” alisema Athuman.
Akizungumzia adha hiyo Mwendesha Boda Boda Mbonamengi Charles
alisema kinachoonekana ni Serikali kuwasahau wakazi wa pembezoni hali
ambayo inafifisha maendeleo.
Charles alisema kutokana na kutokamilika kwa daraja hilo mambo mengi ya maendeleo yamekuwa yakikwama kutokana kero ya eneo hilo.
Aidha Mkazi huyo alihoji kuwepo kwa vifusi kwa muda mrefu
ambavyo vimewekwa barabarani bila kusambazwa huku wakiwa wameahidi kwa
muda mrefu kuwa vitasambazwa.
Diwani wa Kata ya Kitunda Daniel Julias alipotakiwa kuelezea
tatizo hilo la daraja kuchelewa alisema sababu kubwa ni ukosefu wa
fedha.
Alisema mkataba kati ya Manispaa na Mkandarasi wa ujenzi wa
daraja hilo unatarajiwa kuisha mwezi Februari hivyo anachoamini ni kuwa
wakati huo ukifika hatua zingine zitachuliwa.
Diwani huyo alisema suala la vifusi kutosambazwa linatokana na maagizo yake kuwa visubiri daraja litakapo kamilika.
Julias aliwataka wakazi wa Magole kuwa wavumilivu kwani
Serikali yao inafanya kila jitihada kuhakikisha kuwa changamoto
mbalibali zinatatuliwa kwa wakati.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment