………………………………………………………………
Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar, akiwa Mascut-Oman 22/01/2015
Watanzania wanaoshiriki katika Maonesho Kimataifa ya Sanaa,
Ubunifu na Utamaduni yanayoendelea nchini Oman wametakiwa kuitumia vyema
fursa ya kimataifa walioipata kwa kufuata vyema Miongozo waliyopewa ili
ziara yao iweze kuleta Tija.
Miongozo hiyo ni pamoja na Mashirikiano miongoni mwao,kujituma
kwa bidii na kutumia lugha nzuri katika Maonesho hayo kwa kuzingatia
kuwa Wananchi wengi wa Omani wanaelewa vyema Lugha ya Kiswahili.
Wito huo umetolewa na Balozi wa Tanzania nchini Oman Mh. Ali
Ahmed Saleh wakati alipokuwa akitoa nasaha zake kwa Washiriki wa
Maonesho hayo Ofisini kwake Mascut nchini Oman.
Amesema Tanzania ni nchi inayoongoza kuwa na Mahusino mema na
Oman hivyo Washiriki hao wanapaswa wafanye kazi zao kwa bidii na
kuzingatia kanuni na Maadili ya Oman.
Balozi Saleh ameongeza kuwa kufuata kanuni na sheria za Oman
kutawafanya Wajasiriamali hao wa Tanzania kufanyakazi zao kwa utulivu
bila ya kupata usumbufu jambo ambalo litazidi kuimarisha mahusiano mema
kati ya Tanzania na Oman.
Amebainisha kuwa Ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete aliyoifanya mwaka jana nchini humo imezidi
kuyaweka pazuri mahusiano na kwamba Washiriki hao wanapaswa wayatunze na
kuyalinda.
“Ndugu zangu Tanzania ina nafasi ya kipekee nchi
Oman,tunaheshimiwa sana kuliko nchi yoyote hasa baada ya ziara ya Rais
Kikwete, naomba Mahusiano haya muyaendeleze kwa kufanya kazi zenu kwa
bidii na kuchunga maneno yenu maana hawa Waoman wanakijua vyema
Kiswahili Mkiwasema Wanafahamu” Alinasihi Balozi Saleh.
Ameongeza kuwa Raia wa Oman wanautamaduni wa Kumsifu na
Kumtukuza Mfalme wao Sultan Qabus kwa mengi mazuri aliyowafanyia hivyo
Watanzania hao wanapaswa kulifahamu hilo na kulichukulia Tahadhari.
Balozi Saleh amesema Mashirikiano miongoni mwao ni Jambo muhimu
na kwamba wote wamekuja kwa Niaba ya Jamhuri ya Tanzania na Sio Bara au
Visiwani.
“Kitu kingine Mufahamu kuwa hapa Tunaiwakilisha Tanzania kwa
hiyo Uzanzibari na Ubara usiwepo maana mukiupa nafasi
utamusumbua,Tusimameni katika Jina moja tu la Utanzania ambalo ndio
uwakilishi wetu kimataifa” Alisema Balozi.
Aidha ametoa Wito kwa Wajasiriamali ambao hawakupata fursa ya
kushiriki Maonesho hayo kutokata tama na kuamini kuwa ipo siku nao
watapata nafasi ya kushiriki Maonesho ya kimataifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Msafara wa Watanzania Wanaoshiriki
Maonesho hayo Bi Khadija Batashy alimshukuru Balozi Saleh na Wasaidizi
wake kwa Mapokezi mazuri na Nasaha alizozitoa.
Aidha Bi Khadija alimuahidi Balozi huyo kuzifanyia kazi nasaha
hizo ikiwemo kujituma, kuzidisha mashirikiano na kutumia lugha nzuri ili
kuwavutia wateja katika Maonesho hayo.
Awali Mkuu wa Utawala katika Ofisi ya Ubalozi Bw. Abdallah
Kilima wakati akimkaribisha Balozi aliishukuru nchi ya Mascut kwa kuzidi
kuongeza njanja za kuimarisha mashirikiano ikiwa ni pamoja na Mwaliko
wa Maonesho hayo.
Kilima aliwataka Washiriki hao kuwa kitu kimoja na kusaidiana
kwa hali na mali jambo ambalo litaipatia sifa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Maonesho hayo ya muda wa mwezi mmoja ya Sanaa, Ubunifu na
Utamaduni yanayofanyika Jimbo la Al-Amerat mjini Mascut, huanza kila
ifikapo saa 10 za jioni na kufungwa saa 04 usiku kwa majira ya nchi ya
Omani ambapo Washiriki huonesha bidhaa za nchi zao na Watu kunua bidhaa
hizo.
No comments:
Post a Comment