Jumla ya Vijiji 10 katika Wilaya za Kongwa, Mlele na Uyui
vimeunganishiwa umeme kupitia Mradi wa makontena ya kuzalisha umeme
kutokana na jua.
Mradi huo unatekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Nishati na
Madini, ambapo upo katika hatua ya majaribio na unalenga kuvipatia umeme
vijiji vilivyo mbali na mfumo wa gridi ya Taifa.
Wizara ya Nishati na Madini wiki hii, ilisaini makubaliano ya
kukamilika kwa awamu ya kwanza ya Mradi na Kampuni ya Elektro-Merl ya
nchini Austria ambayo ndiyo ilileta na kufunga makontena 14 ya umeme wa
jua pamoja na mfumo wa usambazaji umeme kwa nyumba zilizoko katika
vijiji husika.
Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo, Mwakilishi
kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Styden Rwebangira alisema
wananchi waliounganishiwa umeme huo wa jua, watapata huduma hiyo bure
kwa kipindi cha miaka miwili ya mwanzo ambayo ni ya matazamio.
Alisema kuwa, baada ya miaka miwili, kuanzia tarehe waliyosaini
makubaliano, wananchi wa vijiji husika wataanza kuchangia fedha kidogo
kwa ajili ya ununuzi wa vifaa mbalimbali kama betri na paneli
vinavyotumika katika mradi huo, ambavyo vina ukomo wa kutumika.
“Vifaa hivi vina gharama kubwa sana, hivyo inabidi kuwa na
utaratibu wa kukusanya fedha za kutosha ili kuweza kununua vifaa vingine
pindi vilivyopo vinapofikia ukomo wake wa kutumika. Hivyo kila
mwananchi anayetumia huduma hii inabidi achangie gharama,” alisema
Mhandisi Rwebangira.
Aidha, aliongeza kuwa, ili kuhakikisha mradi unatoa matokeo
yaliyotarajiwa, inabidi uendeshwe na mtu au kampuni yenye utaalamu wa
masuala ya umeme, mitambo ya umeme jua pamoja na uzoefu na ufahamu wa
kutosha kuhusu mitambo ya aina hiyo.
“Hivyo, kila baada ya miaka miwili, ukiacha kipindi cha
majaribio ambapo mradi utakuwa chini ya Wizara, atachaguliwa mtaalamu au
kampuni kupitia njia ya ushindani ambaye atalipwa kwa utaratibu
utakaokubaliwa katika mkataba,” alisema Rwebangira.
Kwa upande wake, Ofisa wa Wizara aliyefika kushuhudia utiaji
saini makubaliano ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi, Paul
Kiwele alisema Wizara ilifanya tathmini ya kuchagua vijiji kwa ajili ya
majaribio ya mradi huo ambapo vigezo mbalimbali vilitumika.
Kiwele alivitaja vigezo hivyo kuwa ni pamoja na Kijiji husika
kuwa mbali na gridi ya Taifa, kutokuwa katika mpango wa kufikiwa na
miradi ya umeme ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco) hivi karibuni.
Alitaja vigezo vingine kuwa ni nyumba za Kijiji husika kuwa
karibu pamoja na uwepo wa matumizi ya kiwango cha umeme utakaozalishwa.
“Aidha, kwa kuwa mradi huu ni wa majaribio, ililengwa kupata
mikoa mitatu tofauti ili uzoefu utakaopatikana utumike katika
uendelezaji teknolojia hii katika maeneo mengine ya nchi,” alisema.
Naye, Mtaalam kutoka Kampuni ya Elektro Merl, Mhandisi Hannes
Merl akizungumzia mkataba uliosainiwa na Wizara pamoja na Kampuni yake,
Januari mwaka jana kuhusu utekelezaji wa mradi husika, alisema mbali na
kufunga makontena 14 ya umeme wa jua pamoja na mfumo wa usambazaji
umeme, mkataba pia ulihusisha ufungaji wa waya, taa, swichi na soketi
moja kwa kila nyumba iliyofikiwa.
Mhandisi Merl alisema kila kontena lina uwezo wa kuzalisha kWp
13.75 ambapo kila nyumba ya makazi na huduma za biashara zimetengewa W
250 na taasisi za kijamii zimetengewa W 500.
Aliongeza kuwa, wananchi wanaweza kuunganisha mashine ndogo
ndogo za kusaga, kuchomelea, kuranda na kuchana mbao pamoja na
nyinginezo kutoka katika makontena hayo hivyo kunufaika na shughuli za
kiuchumi.
Pia, Mhandisi Merl alisema mradi umetoa jokofu kwa kila zahanati
na vituo vya afya vilivyopo katika vijiji vinavyonufaika na mradi huu.
Aidha, alisema kuwa mradi umefunga taa za mitaani kwa kila kijiji
kitakachonufaika na mradi husika.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi katika vijiji vilivyonufaika
na mradi huo wa makontena ya umeme wa jua, waliishukuru na kuipongeza
Serikali kwa wazo zuri la kuwapelekea wananchi hao umeme wa jua ili nao
waweze kunufaika kwa namna mbalimbali kutokana na uwepo wa nishati hiyo
muhimu.
“Ninaishukuru sana Wizara ya Nishati na Madini kuona matatizo
yetu na kusikia kilio chetu. Imekuwa kama ndoto. Umeme huu umeniwezesha
kuendesha biashara ya saluni kwa njia ya kisasa kabisa. Situmii tena
Mkasi kunyoa wateja wangu kama hapo awali. Sasa ninatumia mashine za
kunyolea na ninapata wateja wengi, hivyo kuboresha kipato changu na
maisha yangu kwa ujumla,” alisema Lazaro Kutamika, mkazi wa Kijiji cha
Lobilo, Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma.
Wizara ya Nishati na Madini imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali
katika jitihada za kuwafikishia wananchi huduma ya umeme. Kwa kupitia
mradi huo wa makontena ya kuzalisha umeme kutokana na jua, Serikali
inafanya majaribio ya kuvipatia umeme vijiji vilivyo mbali na mfumo wa
gridi ya Taifa kwa kutumia teknolojia husika.
Vijiji vilivyonufaika na mradi huo kwa awamu ya kwanza ni pamoja na Lobilo, Leganga, Ngutoto na Silale vya mkoa wa Dodoma. Vingine ni Tura, Loya na Lutende vilivyoko mkoa wa Tabora. Aidha, kwa mkoa wa Katavi, vijiji vilivyonufaika ni Nsenkwa, Mapili na Ilunde.
No comments:
Post a Comment