UMOJA wa Jamii ya Watu kutoka
nchini India Bengali wa Dar es Salaam (Bango Sangho) wametoa huduma za
afya bure kwa watoto wa chini ya miaka mitano eneo la Kibugumu lililopo
Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Zaidi ya watoto 100 wamepatiwa
huduma mbalimbali za afya ikiwemo huduma za vipimo na ushauri, huduma za
afya ya kinywa na meno na pia kufanyiwa ukaguzi na ushauri wa lishe
suala ambalo limekuwa na changamoto kubwa kwa familia.
Akizungumza na waandishi wa habari
katika eneo la tukio, Mratibu wa huduma hizo, Dk. Ali Mzige ambaye ni
daktari wa watoto amesema Bango Sangho wameamua kuendesha zoezi hilo ili
kuwasaidia baadhi ya familia ambazo zimekuwa zikipata changamoto kwa
magonjwa anuai yanayowashambulia watoto.
Alisema zoezi hilo limeendeshwa
bure chini ya uratibu wa Umoja wa Jamii ya Watu wa India, Bengali ikiwa
ni utaratibu wao wa kujitolea kusaidia jamii katika masuala mbalimbali
yanayowakabilia. Alisema mbali ya huduma za vipimo ushauri na huduma za
kliniki wazazi pia walipewa ushauri stahiki wa kiafya kwa watoto wao ili
kukabiliana na magonjwa nyemelezi yanayowaathiri watoto.
Akifafanua zaidi juu ya zoezi
hilo, Dk. Mzige alisema idadi kubwa ya watoto waliopatiwa huduma eneo
hilo wamebainika kuwa na upungugu wa wekundu wa damu pamoja na upungufu
wa uzito jamboa ambalo linaathiri hali ya ukuaji wao kiafya.
Alisema waliobainika kuwa na
matatizo makubwa kiafya wamepewa rufaa kwenda hospitali za juu kwa
msaada zaidi wa kiafya. Alisema pamoja na mambo mengine wanawashauri
wazazi kuwatairi mapema iwezekanavyo watoto wa kiume ili kuzuia
uwezekano wa kupata maambukizi kwenye njia ya mkojo.
“…Kwa watoto wa kike tunawashauri
mama zao wawasafishe mara kwa mara wanapojisaidia…wengine wanafunga
pampasi lakini inakaa muda mrefu inakuwa na unyevu jamboa ambalo
linaweza kumsababishia mtoto kupata UTI…maambukizi kwenye njia ya mkojo
kwa hiyo hili ni suala ambalo wazazi tunawaelekeza ili kupunguza
maambukizi ya magonjwa kwa watoto,” alifafanua Dk. Mzige.
Aidha alisema mtoto anapopata
maambukizi ya mara kwa mara yanamuathiri katika ongezeko la uzito na
kukosa hamu ya kula jambo ambalo ni hatari kiafya kwa watoto wengi.
Miongoni mwa madaktari waliokuwa wakitoa huduma hizo ni pamoja na
wataalamu wa afya ya kinywa na meno, madaktari wataalamu wa watoto
pamoja na wataalamu wa vipimo vya maabara.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Bango Sangho Dar es Salaam, Amit Nandi alisema wameamua kutoa huduma
hilo eneo la nje ya Dar es Salaam ili kutoa fursa kwa wananchi wenye
kipato cha chini kupata huduma za afya bure na karibu jambo ambalo
litasaidia kupunguza gharama na mzigo kwao.
Alisema huduma hizo za afya
huzitoa kila mwaka bure kwa jamii ikiwa ni mchango wao kwa jamii ya
kawaida ili nayo iweze kupata huduma za afya ambazo zimekuwa changamoto
hasa maeneo ya vijijini na nje ya miji. Jamii ya Bango Sangho pia
wamesaidia ujenzi wa shule ya msingi na awali ya Kibugumu ikiwa ni
mchango kwa jamii.
No comments:
Post a Comment