Na Anna Nkinda – Maelezo, aliyekuwa Nachingwea
Wanawake nchini wametakiwa
kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika
uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji utakaofanyika
mwishoni mwa mwaka huu ili waweze kuingia katika ngazi ya maamuzi.
Mwito huo umetolewa jana na Mjumbe
wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia
wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wanachama wa
chama hicho wa wilaya ya Nachingwea waliofika kumpokea mara baada ya
kuwasili wilayani humo.
Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema ili jambo linalowahusu wanawake
liweze kufanyiwa kazi ni lazima wawepo wanawake wenzao wa kuwapigania
na hayo yote yatawezekana kama watajitokeza kuwania nafasi za uongozi.
“Ni vizuri wanawake tukakaa kwa
pamoja na kuangalia maslahi yetu kama wanawake, katika hili hatuwezi
kushinda kama siku ya uchaguzi tutakaa majumbani tu na kutegemea watu
wengine watuchagulie viongozi ni lazima siku hiyo tuende kupiga kura”,
alisema Mama Kikwete.
Alisema CCM imeweza kutekeleza
Ilani yake ya mwaka 2005/15 kwa waliyoyapanga na wasiyo yapanga hivyo
basi wanachama wa chama hicho wanakila sababu ya kutembea kifua mbele na
kutoa mfano kwa mambo yasiyokuwa katika Ilani hiyo ni ujenzi wa Chuo
Kikuu cha Dodoma (UDOM) ambacho hadi sasa kimeshatoa wahitimu wa fani
mbalimbali.
Kuhusu mapendekezo ya Katiba mpya
MNEC huyo alisema haikuwa katika Ilani ya Chama hicho lakini kwa kuwa
Mwenyekiti wake Rais Dkt. Kikwete ni msikivu aliweza kusikia maoni ya
wananchi na kuyafanyia kazi na hapo ndipo mchakato wa kuipata katiba
mpya na iliyo bora ukaanza.
Mama Kikwete alisisitiza, “Siku si
nyingi rasimu ya katiba iliyopendekezwa itapelekwa kwa wananchi kwa
ajili ya kuipigia kura , wakati huo ukifika angalieni maslahi ya Taifa
na siyo maslahi yenu binafsi na mpige kura ya ndiyo ili tupate
katiba bora”.
Mama Kikwete alikuwa wilayani humo
kwa ajili ya kuhudhuria kikao cha kamati ya siasa mkoa , wilaya na
makatibu wa CCM kata wilaya ya Nachingwea ambacho kilichojadili mambo
mbalimbali yanayohusu chama hicho.
No comments:
Post a Comment