Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amefanya uteuzi wa wakuu wapya wanne wa Mikoa, amewahamisha wengine sita na ameamua kuwa wengine watatu watapangiwa kazi nyingine.
Taarifa iliyotolewa mjini Dodoma
jioni ya leo, Jumatano, Novemba 5, 2014 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi
Ombeni Sefue inasema kuwa, Wakuu wapya wa Mikoa ni Bi. Halima Omari
Dendego ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dkt. Ibrahim Hamisi
Msengi ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Bi. Amina Juma Masenza
ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Bwana John Mongella Vianney
ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.
Taarifa inasema kuwa
kabla ya uteuzi wake Bi. Dendego alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dkt.
Msengi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Bi. Masenza alikuwa Mkuu wa
Wilaya ya Ilemela na Bwana Mongella alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha.
Taarifa hiyo inasema
kuwa Wakuu hao wapya wa Mikoa wataapishwa kesho, Alhamisi, Novemba 6,
2014 saa saba mchana, Ikulu, Dar es Salaam.
Aidha, taarifa hiyo
imesema kuwa Wakuu wa Mikoa ambao watapangiwa kazi nyingine ni Kanali
(Mst) Fabian Massawe wa Kagera, Dkt. Christine Ishengoma wa Iringa na
Kanali Joseph Simbakalia wa Mtwara.
Wakuu wa Mikoa ambao
wamehamishwa vituo vya kazi ni Bwana Magesa S. Mulongo ambaye anakwenda
Mkoa wa Mwanza kutoka Arusha, Dkt. Rehema Nchimbi ambaye anakwenda Mkoa
wa Njombe kutoka Dodoma, Bwana Ludovick John Mwananzila anakwenda Tabora
kutoka Lindi, Kepteni (Mst) Anseri Msangi anayekwenda Mkoa wa Mara
kutoka Njombe na Mhandisi Everist Ndikilo ambaye anakwenda Arusha kutoka
Mwanza.
Wengine waliohamishwa ni
Luteni (Mst) Chiku A.S. Galawa ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma
kutoka Tanga, Dkt. Rajab Rutengwe ambaye anakwenda Mkoa wa Tanga kutoka
Katavi, Bi Fatma Mwasa ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita kutoka
Tabora na Bwana Magalula S. Magalula ambaye anahamishiwa Lindi kutoka
Geita.
Taarifa hiyo imesema
kuwa Wakuu wa Mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Kilimanjaro, Manyara,
Mbeya,Morogoro, Pwani, Rukwa, Shinyanga, Ruvuma, Singida na Simiyu
watabakia kwenye vituo vyao vya sasa.
Aidha, Rais Kikwete amefanya uteuzi wa Wakuu wapya wa Wilaya, kuhamisha baadhi yao na kutengua uteuzi wa baadhi.
Taarifa kamili itatolewa na Waziri Mkuu baada ya kuwa wamepangiwa vituo vya kazi.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
05 Novemba,2014
No comments:
Post a Comment