Mkurugenzi
wa Takwimu za Jamii na sensa ya Watu na Makazi Bw. Ephraimu Kwesigabo
akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu
mfumuko wa bei nchini..
…………………………………………………
Na Aron Msigwa – MAELEZO, Dar es salaam.
Ofisi
ya Taifa ya Takwimu imesema kuwa hali ya mfumuko wa bei nchini
imeendelea kuwa katika kiwango kisichobadilika katika kipindi cha mwezi
Januari na Februari mwaka huu kutokana na kupungua kwa kasi ya upandaji
wa bei za bidhaa na huduma mbalimbali.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Takwimu
za Jamii na sensa ya Watu na Makazi Bw. Ephraimu Kwesigabo amesema kuwa
mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwezi Februari 2014 umeendelea kubaki katika
kiwango cha asilimia 6.0 kama ilivyokuwa mwezi Januari mwaka huu.
Amesema
kuwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwezi Februari
2014 imebakia kuwa sawa na ile iliyokuwepo mwezi Januari huku kukiwa na
ongezeko dogo la upandaji wa bei kwenye baadhi ya bidhaa na huduma
mwezi kwa mwezi Februari 2014 ikilinganishwa na bei za mwezi Februari
mwaka jana.
Ameeleza
kuwa mfumuko wa bei za bidhaa za vyakula na migahawa kwa mwezi Februari
umeongezeka hadi asilimia 6.9 kutoka asilimia 6.6 za mwezi Januari
mwaka huu huku bidhaa zisizo za vyakula kasi ya ongezeko la bei
ikipungua hadi asilimia 6.3 mwezi Februari 2014 kutoka asilimia 6.7 za
mwezi Januari mwaka jana.
Amefafanua
kuwa mwenendo wa bei za bidhaa za vyakula kama samaki, mbogamboga,
ulezi na matunda zimeonyesha kuongezeka kwa kiwanga kikubwa kwa mwezi
Februar ikilinganishwa na bei za bidhaa hizo kwa mwaka uliopita huku bei
za bidhaa zisizo za vyakula za vitambaa vya suti za wanaume, kodi za
pango la kuishi, mkaa, na nauli za bajaji zikionyesha ongezeko.
Kwa
upande wa mfumuko wa bei unaopimwa kwa kipimo cha mwezi,ameeleza kuwa
kumekuwa na ongezeko kwa asilimia 1.4 ikilinganishwa na ongezeko la
asilimia 1.8 kwa Januari mwaka huu, huku fahirisi za bei za taifa
zikiongezeka hadi kufikia 148.62 kati ya Februari mwaka uliopita na
Februari mwaka huu.
Amezitaja
bidhaa zilizochangia ongezeko la fahirisi za bei nchini kuwa ni pamoja
na dagaa,samaki wakavu, mbogamboga na viazi mviringo huku bidha zisizo
za vyakula zikiwa pombe za kienyeji, vitambaavya suruali, viatu vya
wazi vya plastic, mafuta ya dizeli na Petroli pamoja na huduma za
unyoaji na usafi wa nywele.
Aidha
kufuatia hali hiyo ya mfumuko wa bei Bw. Kwesigabo ameeleza kuwa
uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma za
jamii kwa mwezi Februari umeonyesha kupungua na kufikia shilingi 67 na
senti 29.
“Kupungua
kwa thamani ya Shilingi kunamaanisha kwamba, kama mtu alikuwa na uwezo
wa kununua bidhaa kwa Shilingi 100 mwaka jana, basi kwa mwaka huu
itampasa aongeze zaidi ili aweze kununua kitu kama kile kile, kwa mfano
badala ya shilingi 100 inabidi atumie Shilingi 132”
Kuhusu
ulinganifu mfumuko wa bei wa Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika
Mashariki amesema kuwa una mwelekeo unaofanana na kueleza kuwa mfumuko
wa bei nchini Kenya umepungua kidogo na kufikia asilimia 6.86 kwa mwezi
Februari kutoka asilimia 7.21 za mwezi Januari , huku Uganda ikiwa na
asilimia 6.7 kwa mwezi uliopita kutoka asilimia 6.9 za mwezi Januari.
No comments:
Post a Comment