Akizungumza
na waandishi wa habari huku akionyesha moja ya gazeti lililowahi
kuripoti kampeni hizo kwa picha Philip Mangula amelaani kampeni alizodai
zinadhalilisha watoto zinazofanywa na CHADEMA huku akionyesha mmoja wa
watoto ambaye alipigwa picha huku akionyesha sare zake za shule ambazo
zimechakaa na kuchanika na mmoja wa wapiga debe wa chama hicho akisema
kutangaza umasikini wa mtu ni kumdhalilisha
………………………………………………………………………………………..
*Asema Chadema wanalia kilio cha mamba
*Ni kwa kukimbiwa na wananchi kwa kudhuru watu.
*Asema hatapanda jukwaani, ataratibu tu kampeni
*Asisitiza anayegombea Kalenga si Mgimwa ni CCM
NA BASHIR NKOROMO, IRINGA
MRATIBU wa Kampeni za CCM katika
uchaguzi mdogo jimbo la Kalenga, Iringa Vijijini, Makamu Mwenyekiti wa
CCM (Bara), Philip Mangula amesema, madai ya Chadema kwamba CCM
imepeleka mamluki katika jimbo hilo ni kilio cha mamba, baada ya chama
hicho kukimbiwa kutokana na vitendo vyake vya kudhuru watu ikiwemo
kuwatoboa macho kwa bisibisi na kuwamwagia tindikali.
Hivi
karibuni Chadema wanadaiwa kumtoboa jicho kwa bisibisi Alphonce John
wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani mjini Kahama, na pia
wanadaiwa kumpa ulemavu wa kudumu kwenye sura Mussa Tesha baada ya
kumwagia Tindikali wakati wa uchaguzi mdogo uliofanyika Igunga 2012.
Mangula
amesema mbali na vitendo vya kutoboa macho na kumwagia watu tindikali,
ambavyo Chadema inadaiwa kufanya, pia chama hicho kimeogofya wananchi
kwenda kwenye mikutano yake, kutokana na kujiwekea histoa mbaya ya watu
kuuawa katika mikutano yake kadhaa ambapo sasa wamefikia watu zaidi ya
wanane tangu chama hicho kuanzishwa.
Makamu
Mwenyekiti huyo wa CCM Bara, ametoa ufafanuzi huo baada ya mwandishi
mmoja wa habari kutaka kujua CCM ilikuwa na maoni gani kuhusu tuhuma
ambazo zimetolewa na Chadema, kwenye mkutano wake na waandishi, leo,
Machi 3, 2013 ikisema kwamba CCM imeingiza watatu iliowaita majambazi,
kutoka mikoani kwa nia ya kufanya fujo jimboni Kalenga nyakati za
kampeni.
Mangula
ambaye amewasili mjini Iringa, leo, Machi 3, 2013, akiwa tayari kuingia
katika jimbo la Kalenga, ambako alisema atapiga kambi hadi Machi 16,
mwaka huu uchaguzi ukapofanyika na CCM kuibuka Kidededea, alisema, CCM
haina sababu ya kuingiza waovu jimboni kwa kuwa siyo jadi yake na
inatambua thamani ya amani kuwepo katika eneo lolote.
“CCM
inatambua umuhimu wa amani mahala popote, na kwa bahati nzuri mimi
binafsi ninao uzoefu na mifano mingi kuhusu madhara ya kutoweka amani
hivyo kama kiongozi na mratibu wa kampeni za CCM katika jimbo hili la
Kalenga siwezi kuruhusu CCM kufanya mambo ya kijinga kiasi hicho”,
alisema Mangula na kuongeza;
“Wakati
Chadema wanajaribu kujikosha kwa wananchi kwa kulia machozi ya mamba,
sisi tumeshajua kwamba chama hicho kimeingiza mamluki kumi kutoka nje ya
Iringa ikiwemo Tarime na Temeke, na kuwatawanya katika kata
mbalimbali. Na hili sisi tunalisema
kwa ushahidi wa kutosha, tunawajua mamluki hao na hata majina yao
tunayo…tunasubiri kuchukua hatua za kisheria kabla ya kuwataja”.
Katika
hatua nyingine, Mangula alilaani hatua ya Chadema kutumia ufukara wa
mtoto mmoja na familia yake, kuombea kura kwa wananchi katika kampeni
zake zinazoendelea za kumnadi mgombea wa chama hicho katika jimbo la
Kalenga, akisema kwamba hatua hiyo, mbali na kwamba siyo sahihi katika
siasa lakini ni kumfadhililisha mtoto huyo umasikini wake.
“Hawa
Chadema hawana utu kabisa, inawezekanaje Meneja wa kampeni wa chama
hicho anambeba mtoto wa mtu na kumnadi kwa wananchi kwamba amevaa sare
chakavu za shule na kwamba ni kiongozi wa CCM. Hili jambo
limetusikitisha sana kwa sababu ni kuivunjia heshima CCM na pia
kumdhalililisha mtoto huyu kwa umasikini wake”, alisema Mangula
alionyesha picha iliyochapishwa kwenye gazeti la Tanzania Daima, Meneja
wa kampeni za Chadema akiwa amembeba mtoto aliyevaa nguo chakavu za
shule.
Mangula aliwataka wana-CCM katika
jimbo la Kalenga kutokuwa na hofu yoyote, wakati wa kampeni na siku ya
kupiga kura kwa sababu anaamini ulinzi wa serikali upo wa kutosha.
Akizungumza na baadhi ya viongozi
wa CCM mkoa wa Iringa, Mangula aliwataka kutumia muda wa kampeni
kuwajulisha wana-CCM na wananchi kwa jumla kwamba wanayemnadi kushinga
ubunge si Godfrey Mgimwa, bali ni CCM ndiyo inayowania kiti hicho.
No comments:
Post a Comment