Na:Henry Mdimu
JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA KAZI NA AJIRA
TAMKO LA SERIKALI KUHUSU KUSITISHA
UTARATIBU WA KUKODISHA WAFANYAKAZI UNAOFANYWA NA BAADHI YA WAKALA BINAFSI WA HUDUMA
ZA AJIRA
1. Wizara
ya Kazi na Ajira imekua ikipokea malalamiko
toka kwa wadau mbalimbali kuhusu utaratibu wa udalali wa kukodisha
wafanyakazi katika makampuni unaofanywa na baadhi ya Wakala Binafsi wa Huduma
za Ajira nchini.
2. Wizara
imefanya uchunguzi wa kina kuhusu suala hili na kubaini kuwa utaratibu wa
kukodisha wafanyakazi unaofanywa na baadhi ya Wakala Binafsi wa Huduma za Ajira
ni kinyume cha Sheria ya Huduma za Ajira Na. 9 ya Mwaka 1999 [Sura 243 kama ilivyorejewa Mwaka 2002].
Kwa mujibu wa Kifungu 4 cha Sheria
hii, majukumu ya msingi ya Wakala wa Huduma za Ajira ni kuwaandaa na
kuwaunganisha Watafuta Kazi na Waajiri kwa kutoa mafunzo na ushauri elekezi kwa watafuta kazi, kutafuta fursa za ajira na kutoa taarifa za
soko la ajira. Hivyo, Mawakala hawapaswi
kuwa waajiri wa wafanyakazi waliowatafutia kazi kwa niaba ya Waajiri wengine.
3. Aidha,
uchunguzi umebaini kwamba utaratibu huu
ni ujanja unaotumiwa na baadhi ya Waajiri na Mawakala kwa lengo la kukwepa kodi
na kujipatia faida kwa kukwepa kutoa haki za msingi za wafanyakazi kwa mujibu
wa Sheria za Kazi. Baadhi ya makampuni yanayokodisha wafanyakazi yamefanyiwa
uhakiki na TRA na kubainika kukwepa kodi ya mapato ya ajira (PAYE) na na kodi ya mapato ya kampuni kinyume na
Kifungu cha 7 cha Sheria ya Kodi ya
Mapato ya Mwaka 2004 [Sura 332 kama ilivyorejewa Mwaka 2008].
4.Uchunguzi
huu umebaini athari mbalimbali kwa
wafanyakazi wanaoajiriwa kwa utaratibu huu. Athari hizo ni pamoja na:
·
Wafanyakazi
kukosa haki ya hifadhi ya jamii kama vile likizo ya uzazi na matibabu
kinyume na Sheria mbalimbali za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii;
·
Uwepo
wa ubaguzi katika malipo ya mishahara kwa kazi ya aina moja kinyume na
kifungu cha 7(10) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na.6 ya mwaka
2004 ambacho kinamtaka mwajiri kuchukua hatua stahiki kwa kuhakikisha kuwa
wafanyakazi bila kujali jinsia zao wanalipwa mishahara linganifu na ya haki kwa
kazi yenye uzito na thamani sawa;
·
Kukosa
fursa za kujiendeleza kielimu na mafunzo;
·
Kukosekana
kwa usalama na uhakika wa ajira ;
·
Wafanyakazi
kulipwa mishahara ya kima cha chini kinyume na sekta wanayofanyia kazi.
5. Kwa
taarifa hii, Wizara ya Kazi na Ajira imeamua kusitisha mara moja utaratibu wa Mawakala kuwaajiri wafanyakazi wanaowatafutia kazi. Aidha, Mawakala na Kampuni husika waliopo
katika utaratibu huu kwa sasa wanapaswa kuwahamisha wafanyakazi waliokodishwa kutoka kwa Wakala kwenda kwa Kampuni husika. Waajiri na Wakala
wanatakiwa kukamilisha zoezi hili ndani ya kipindi cha mwezi mmoja na
kuwasilisha taarifa za utekelezaji kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Kazi na Ajira kabla
au ifikapo tarehe 28/02/2014.
6. Uchunguzi
zaidi unaendelea kubaini kama kuna wafanyakazi wa Kigeni wanaohusishwa katika
utaratibu wa kukodishwa ili hatua zinazotahili ziweze kuchukuliwa ikiwa ni
pamoja na kuwataka waombe vibali vya ajira kwa mujibu wa Sheria ya Uhamiaji Na.7 ya mwaka 1995 na Sheria ya Huduma za Ajira Na.9 ya mwaka 1999. Wageni watakao kidhi
vigezo wataajiriwa na kampuni walipokodishwa; ambazo kwa wakati huo zitakua
ndiyo mwajiri wao.
7. Wizara
ya Kazi na Ajira inawaelekeza Wakala wa Huduma za Ajira nchini kwamba, kwa
utaratibu wa sasa watapaswa kuwasilisha barua za maombi ya usajili wa Uwakala kwa KAMISHNA WA KAZI kwa mujibu
wa Sheria ya Huduma za Ajira Na. 9 ya mwaka 1999 [Sura 243 kama
ilivyorejewa Mwaka 2002] ili waweze kufanya shughuli za Uwakala wa Huduma za
Ajira kisheria. Maombi haya yawasilishwe ndani ya kipindi cha mwezi mmoja tangu
kutolewa kwa tangazo hili. Baada ya muda huo Wakala asiye na kibali cha
Kamishna wa Kazi hatoruhusiwa kuendesha shuguli za huduma za ajira nchini.
Aidha, Mawakala watakaopata leseni ya Kamishna
wa Kazi yatakua yakitangazwa ili yatambuliwe na Umma.
8. Nasisitiza,
maelekezo haya yatatolewa kwa Makampuni na Wakala waliohusishwa katika uchunguzi kwa ajili ya
utekelezaji.
IMETOLEWA
NA
GAUDENTIA MUGOSI KABAKA (MB)
WAZIRI WA KAZI NA AJIRA
No comments:
Post a Comment