Rais
mpya wa Madagascar Hery Rajaonarimampianina akiapishwa rasmi rais wa
nchi hiyo mjini Antananarivo kufuatia ushindi mkubwa alioupata katika
uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo mwezi Desemba 2013.
Rais mpya wa Madagascar Hery Rajaonarimampianina akisani kiapo chake
tayari kuanza kazi ya kuwatumikia wananchi wa Madagascar mbele ya Jaji
Mkuu wan chi hiyo Jean –Michael Rasolonjatovo (kushoto) wakati wa
sherehe za kumuapisha rais huyo zilizofanyika mjini Antananarivo.
Rais
mpya wa Madagascar Hery Rajaonarimampianina akizungumza na wananchi wa
Madagascar waliofurika ndani ya uwanja wa Antananarivo mara baada ya
kuapishwa kuwa rais mpya wa nchi hiyo mjini.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mh. Bernard Membe
akimuwakilisha Rais Jakaya Kikwete katika sherehe za kumuapisha rais
mpya wa Madagascar akiwa kwenye jukwaa kuu pamoja na viongozi wengine wa
nchi za Afrika waliohudhuria sherehe hizo mjini Antananarivo.Wengine
wanaoonekana kutoka kulia ni Rais mstaafu wa Msumbiji Joachim Chisano,
Rais wa Zambia Ipikefunye Pohamba na aliyekuwa rais wa Madagascar Andry
Raojolina. Viongozi
mbalimbali na wanachi waliohudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais mpya
wa Madagascar Hery Rajaonarimampianina mjini Antananarivo
Gwaride maalum la jeshi la Madagascar wakati wa sherehe za kuapishwa kwa rais mpya wa nchi hiyo Hery Rajaonarimampianina.
Rais mpya wa Madagascar Hery Rajaonarimampianina akikagua gwaride la majeshi ya Madagascar baada ya kuapishwa.
Rais mpya wa Madagascar Hery Rajaonarimampianina akiwasili Ikulu ya nchi hiyo mjini Antananarivo.
……………………………………………………………………………………………
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
Antananarivo, Madagascar.
Tanzania
imesema kuwa itaendelea kushirikiana na Madagascar katika masuala
mbalimbali na kuhakikisha kuwa vikwazo ilivyowekewa nchi hiyo na
jumuiya za kimataifa vinaondolewa kufuatia nchi hiyo kurejesha utawala
wa kidemokrasia.
Akizungumza
katika mahojiano maalum mjini Antananarivo, Madagascar, Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mh. Benard Membe amesema kuwa
sasa serikali ya Madagascar imefungua ukurasa mpya wa ushirikiano sio tu
na Tanzania bali nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa
Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya za kimataifa.
Waziri
Membe ambaye alikuwa amemwakilisha Rais Jakaya Kikwete katika sherehe
za kuapishwa kwa rais mpya wa Madagascar Bw. Hery Rajaonarimampianina
zilizofanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo Antananarivo jana amesema
kuwa Tanzania imefurahishwa na hatua hiyo na kuongeza kuwa huo ni
ushindi mkubwa kwa SADC.
Amesema
kuwa mwaka 2009 Madagascar iliingia katika machafuko yaliyosababisha
serikali halali iliyokuwepo madarakani ya Rais Mark Ravalomanana
kupinduliwa na kufafanua kuwa Tanzania ikiwa Mwenyekiti wa Kitengo cha
Amani na Usalama cha nchi za jumuiya ya SADC (TROIKA) imekuwa mstari wa
mbele kuhakikisha kuwa amani ya kudumu inapatikana nchini humo.
“Kiongozi
mpya wa Madagascar aliyepatikana na kuapishwa ni ushindi kwa Tanzania
kwa sababu Rais Jakaya Kikwete amejihusisha sana na upatikanaji wa
kiongozi huyo, kama tunakumbuka rais Kikwete alimuita nchini Tanzania
kwa mazungumzo rais aliyekuwa madarakani Bw. Andry Rajoelina mara nne,
mazungumzo haya yamezaa matunda tunayoyaona leo” amesema Mh. Membe.
Amefafanua
kuwa yapo mambo makubwa ambayo Tanzania imeyafanya kufanikisha
kupatikana kwa amani ya kudumu nchini Madagascar ikiwemo upatikanaji wa
katiba ambayo ilikamilika mwezi wa 8 mwaka 2013 ,kufanikiwa
kuwashawishi Andry Rajoelina na Mark Ravalomanana waliokuwa mahasimu
kutoshiriki kugombea katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.
Amesema
Tanzania imefurahishwa na kitendo cha rais Andry Rajoelina aliyeingia
madarakani kwa kufanya mapinduzi kukubali kuachia madaraka na kuachia
utawala wa demokrasia utawale nchini humo.
Ameeleza
kuwa Tanzania sasa iko tayari kushirikiana na Madagascar na kama mjumbe
wa SADC itahakikisha kuwa vikwazo ilivyowekewa nchi hiyo vinaondolewa
pia kuhakikisha kuwa kiongozi huyo mpya anashiriki mkutano wa wakuu wa
nchi za Afrika utakaoanza tarehe 30 mwezi huu.
“Tulimwahidi
rais aliyekuwa madarakani Bw. Andry Rajolina kuwa atakapotekeleza hayo
tunayoyataka ikiwemo kuanzisha mchakato wa katiba, kuruhusu utawala wa
demokrasia, na kuruhusu uchaguzi ili kupata rais mpya sisi tutakuwa
mstari wa mbele kushawishi nchi za SADC na nchi za AU kuwaruhusu
kushiriki mikutano yote ili waweze kuijenga nchi yao na jambo hilo
tutalifanya ” amesisitiza Mh.Membe.
Katika
houtuba yake mara baada ya kuapishwa rais Rajaonarimampianina amesema
kuwa utawala wake unaanza ukurasa mpya wa kuijenga upya nchi hiyo
iliyokuwa imegawanyika kisiasa na kusababisha chumi wake kudorora huku
akiueleza umati mkubwa wa watu waliohudhuria sherehe za kuapishwa kwake
kuwa ataongeza mapambano dhidi ya rushwa na kuleta amani, utulivu na
maridhiano kwa mustakabali wa taifa hilo.
Madagascar
ambayo sasa inaingia katika utawala mpya wa rais Hery
Rajaonarimampianina ambaye hapo awali alikuwa Waziri wa Fedha wa nchi
hiyo iliingia katika machafuko yaliyosababisha kuondolewa kwa utawala wa
rais Mark Ravalomanana aliyekimbilia uhamishoni nchini Afrika Kusini.
Hery
Rajaonarimampianina akiungwa mkono na rais aliyepita Andry Rajoulina
anakuwa rais wa 4 wa nchi hiyo kufuatia ushindi mkubwa alioupata
katika uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo mwezi Desemba 2013
uliompatia asilimia 53.3 dhidi ya mpinzani wake Bw. Jean Louis
Robinson aliyepata asilimia 46.5.
No comments:
Post a Comment