Na Mukhsin Mambo
………………………………………………………………
Waziri wa
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Dr. Titus Kamani, amesema ili kwenda na
kasi ya maboresho ya wizara hiyo, inahitajika dhana ya uwajibikaji na
uwazi sambamba na kujitolea kwa nguvu zote katika kufanya kazi.
Waziri Kamani,
ameyasema hayo leo katika mkutano wa kwanza uliowakutanisha wafanyakazi
wote wa wizara hiyo, wakiwemo wastaafu wa mwaka jana katika ofisi za
wizara hiyo zilizopo Temeke jijini Dar es Salaam.
Amesema kama
kuna mtu ambaye ni kikwazo katika kukwamisha shughuli za wizara, ni bora
akawapisha mapema na kwamba kila mtumishi kwa nafasi yake, anatakiwa
kuifanya kazi kwa uwazi na akaitaka wizara kufanya kazi na vyombo vya
habari kwani ndio njia pekee ya kuwafanya watanzania wajue wizara
inafanya nini.
“Wewe upo
ofisini, halafu unaogopa ogopa vyombo vya habari, kwani unatatizo gani,
kuweni wazi mambo yenu yawe hadharani, watanzania wa Mbeya wayajue,
Rufiji mpaka Pemba, hakuna kufichaficha jambo katika wizara yangu.”
Alisistiza Dk Kamani.
Amesema wizara
ya maendeleo ya mifugo na uvuvi ndio moyo wa taifa kwani huwajumuisha
watanzania wengi wenye maisha ya kawaida, lakini amesikitishwa kwa jinsi
ambavyo wizara hiyo imekuwa ikichukuliwa na baadhi ya watu kama ni
wizara ya yenye migogoro na kuleta hasara maeneo mengine.
“N’gombe hawa
wamekua wakiingia kwenye hifadhi, wanapigwa risasi, wanaaribu mashamba
ya watu na kuleta njaa kwa wananchi, ngombe hawa wamekuwa wakiambiwa
wanaleta uharibifu wa mazingira kwa wananchi kwa sababu ya kuhamahama,
kama ngombe hawa ungepatikana utaratibu mzuri wa kuwatunza, kuwahifadhi
basi, taifa hili lingeingiza kipato kikubwa ikiwemo kuuza nyama hadi nje
ya nchi, maziwa na kuboresha afya za watanzania” alisema Dk Kamani.
Dk. Kamani,
amesema anafahamu Wizara yake ina changamoto nyingi katika kutekeleza
majukumu yake, ikiwemo bajeti kuwa ndogo, lakini kwa kutumia taaluma
yake pamoja na ushirikiano wa wafanyakazi wote wa wizara hiyo, anaamini
wizara hiyo badala ya kuonekana ni laana kwa watanzania, itakuwa ni
wizara yenye neema kwa watanzania, yenye kueneza ajira na kipato kwa
sababu hakuna jambo lisilowezekana kama kila mmoja atafanya kazi kwa
dhamira moja.
Akizungumzia juu
ya ranchi za taifa, waziri Kamani amesema ana nia ya dhati ya kuona
ranchi za taifa zinafufuka na kutengeneza uchumi imara wa taifa,
kuzalisha Ngombe wenye ubora ambao watatoa mazao ya mifugo
yatakayoliingizia taifa hili kipato kikubwa.
Akizungumzia
sekta ya uvuvi, Waziri Kamani, amesema sekta hiyo ni tabu tupu, amesema
leo tunaambiwa kuna uvuvi haramu, nyavu zisizokidhi viwango, huku wavuvi
wakiendelea kuwa masikini, katika nchi yenye bahari, maziwa na mito
mikubwa kila kona, ameuliza ni kweli wanahitaji bajeti kubwa ya
kushughulika na mambo hayo?.
“Tunahitaji
utashi wa kuwasadia wavuvi wetu, kwa kutoa elimu na kufanya mazungumzo
nao ya mara kwa mara, kuwatembelea maeneo yao ya kazi na kubaini
matatizo yao kisha kuyafanyia kazi” Alibainisha Dk Kamani.
Kuhusu zao la
kuku, Waziri Kamani amesema sasa hivi kuna tatizo la mayai feki na
chanjo feki, alihoji ni kweli kwamba wafanyakazi wa wizara hiyo haiwajui
wahusika au kuna baadhi ya watumishi ndio miradi yao? ambapo aliagiza
wizara kubaini wanaofanya biashara hiyo feki ambayo inaleta madhara hasa
wakazi wa mjini ambao ni watumiaji wakubwa wa bidhaa hizo.
Awali, kaimu
katibu mkuu wa wizara hiyo Dk Yohana Budeba alipongeza uteuzi wa Dk
Kamani, kuingia katika wizara hiyo kwakuwa ajira yake ya kwanza mwaka
1982 alikuwa chini ya wizara hiyo kama afisa Mifugo wa kata ya Kisongo
wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha, hivyo changamoto nyingi anazifahamu, ni
mwenzao na anaamini watashirikiana vyema katika kukabiliana nazo.
No comments:
Post a Comment